AN-NUUR
Na.155 Rabi' Awal 1419, Juni 26-Julai 3, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Aliyoyazungumza Mhe. Kitwana Kondo Bungeni 

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. 

Mheshimiwa Spika, kwa kuanza naomba na mimi niseme kwamba naunga mkono hoja ya Waziri Mkuu. (Makofi) 

Baada ya kusema hayo, Mheshimiwa Spika. Nabii Muhammad S.A.W. anasema, "Alhaki Habiba llah, albatil yaaduallwah". Maana yake msema; kweli ni mpenzi wa Mungu, na mwongo ni adui wa Mungu. Waswahili wanasema, "kweli thawabu, kweli sababu". Ukisema kweli utapata thawabu kwa Mungu, lakini utamwudhi yule unayemwambia kweli. (Kicheko/Makofi) 

Mheshimiwa Spika, mimi nina nia ya kuiambia Serikali yangu kweli, ili niwe Mpenzi wa Mungu na nipate thawabu; na ninaamini ya kwamba haitanitafutia sababu. (Kicheko/Makofi) 

Mheshimiwa Spika, mwaka 1170, huko Uingereza kulikuwa na Mfalme Henry II. Yeye alikuwa hampendi sana Archbishop wake wa Cantibery, jina lake Thomas Abecket. Sababu ya uadui wao ni kwamba yule Archibishop alikuwa akimtaka Mfalme atekeleze mambo yake kwa kufuata maadili ya Kikatoliki. Mfalme hakutaka. Siku moja Mfalme akawaita wasaidizi wake akawaambia, na nanukuu. "Who will lget rid me of this mad monk". Siku ile ile baadhi ya wafuasi wake walikwenda Cantibury, wakamkuta Thomas Abacket yuko kanisani. Wakamfuata wakamwua. Walifanya vile kwa kumpendeza mzee. (Kicheko/Makofi) 

Mheshimiwa Spika, mwaka 1648 huko huko Uingereza, Oliver Cromwell aliipindua Serikali ya King Charles I, na baadaye akamtuhumu kwa uhaini. Kabla ya kusikilizwa kesi yake, Oliver Cromwell aliwaita majaji na akawaambia, na ninanukuu. "During his trial, you may wish to hear his defence. You will then convict him of treason and sentence him to death". Majaji wakafanya hivyo hivyo. King Charles I akawa convicted of treason and sentenced to death, na tarehe 30/1/1649 akakatwa kichwa. Kwa nini? Kwa sababu ya kumpendeza mzee. (Kicheko/Makofi). 

Mheshimiwa Spika, sasa nikurudishe nyumbani. Hivi karibuni huko Arumeru, watu wa Wilaya ile wameongezewa kodi. Wamasai wamefanya ghasia wame-riot, wameharibu mali, wamechoma nyumba ya Mwenyekiti wao, waliolipa kodi hiyo wakawapiga. Hakuna kilichotokea. Serikali haikufanya kitu. Karibuni hivi hivi., wamewakamata watu 18 wakasema hawa majambazi. Polisi waliposema tupeni, wakasema hatuwapi; na mkija tutawaua. Tutawapiga mpaka tuwatoe vilema. Serikali haikufanya kitu. Mwisho, tarehe 6 Mheshimiwa Waziri Mkuu amekwenda huko Arumeru, akakutana nao. Pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenda kule, hao watu walikuwa karibu watoke kwenye mkutano. Ikabidi wabembelezwe na Mwenyekiti kwa lugha ya Kimasai wakakaa. (Kicheko/Makofi) 

Sasa,Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema mengi. Lakini niseme machache tu, na haya nimeyapata kutoka kwenye magazeti. "Bwana Sumaye aliwakumbusha wananchi kuwa kamwe Serikali haitakuwa tayari kupambana nao, wala kusuguana nao kuhusu suala lolote. Alisema, wananchi wana haki ya kujua na kujadiliana na viongozi juu ya tatizo lolote linalojitokeza katika jamii hii, ili kulitafutia ufumbuzi". Ni maneno mazuri, ya taadhima. Na baada ya hapo akasema kwamba atahakikisha kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri anaondolewa. Siku mbili baadaye, Halmashauri imekaa, Mwenyekiti kaondolewa. Ni kama yale ya Cromwell na Henry II. (Makofi) 

Mheshimiwa Spika, sasa naomba ni contrst haya maneno ya Waziri Mkuu ya tarehe 13 Februari, baada ya ghasia ya Mwembechai. Katika maneno mengi aliyosema Waziri Mkuu, na mengi ni lazima niseme kwamba ni maneno ambayo yanapendeza kwa kiongozi kusema. Kwa sababu hakuna mtu asiyetaka amani katika nchi hii. Lakini nataka niseme machache. Waziri Mkuu amesema hivi, "Hao waliokamatwa watashitakiwa, na wakipatikana na hatia lazima waadhibiwe vikali sana. Hapatakuwa tena na huruma ya Serikali katika jambo hili. Huruma zilizotolewa huko nyuma zinatosha, na bahati mbaya hazikubadili hali hiyo". Hayo ndiyo maneno ya Waziri Mkuu aliyoyasema siku ya tarehe 13 Juni hapa Bungeni. (Makofi). 

Mheshimiwa Spika, Marehemu Archbishop Edgar Maranta wa Dar es Salaam alikuwa akisema, "When God closes the door, he somewhere opens the window". Haya sikusema mie, ni Marehemu Edgar Maranta – Archbishop wa Dar es Salaam. Ikajaalia Mungu akafungua dirisha, Rais Mkapa kwa uadilifu wake akawatoa wanawake wote waliokamatwa, wazee wote waliokamatwa, na vitoto vidogo vile vya miaka 12 mpaka 15, ambao kwa sheria ilikuwa wawekwe katika mahabusu ya watoto, lakini kwa jazba na over-zealousness ya Polisi kwa kutekeleza agizo, wakapelekwa Keko. Lakini Rais aliwatoa wote, na akaagiza ya kwamba wanafunzi wote watolewe. (Makofi) 

Sasa Mheshimiwa Spika, mimi nataka niulize. Hakuna kiongozi zaidi ya Rais. Analosema yeye ndilo. Juu yake yeye ni Mungu. Mmoja katika hawa wanafunzi, jina lake Chuki Athumani kapigwa risasi tarehe 13, kapelekwa Muhimbili hakutolewa. Chuki Athumani amekaa Muhimbili toka tarehe 13 ya mwezi wa pili mpaka tarehe 17 ya mwezi wa sita. Amepooza ana pingu kwa muda wa miezi minne. Amri ya Rais hapa ilikuwaje? Kwa nini mtoto huyu asitolewe? Hilo la kwanza. 

Mheshimiwa Spika, Chuki Athumani hakupata dawa kwa muda wote huo, ninayo karatasi yake hapa. Admitted on 13/2/98 at 7.00 p.m. Seen by Doctor on call (Dr. Kirigiti)who found penetration wound below the left clavical and wrote a note to general surgeon to review the patient. General surgeon reviewed the patient and noted weakness of lower limbs same day, and wrote a note to Chest surgeon. Chest surgeon saw the patient on 14/2/98 at 11.00 a.m., and found that the bullet had passed through the body and exit on posteria and weakness of sijui LL nini, subcurtenous emphisma and wrote a note to Neuro surgeon. Neuro surgeon saw the partient on 18/2/98 and ordered N/S which was done on 18th February, 1998, CT N/S finding fracture of Tz vetebra and fracture fragment compressing the spinal code, tarehe 18, hakuna dawa mpaka tarehe 17 June. 

Sasa, Mheshimiwa Spika, na Serikali wanajua, na tuliyasema ya kwamba jamani kuna maneno kuwa hawa watu wanauawa kwa hila. Sasa nataka nipate maelezo, kwa nini huyu kijana kawekwa ndani muda wote huo bila ya kutibiwa, na pingu? Mtu kapooza mwili mzima kuanzia kiuno kwenda chini. Pingu ya nini? Lakini kafungwa pingu. Baadaye walipoona kwenye miguu haina maana yoyote kuifunga pingu, wakabadilisha pingu ikawekwa mkononi. Sasa nataka nipate maelezo mimi na wengi wengine. (Makofi). 

La pili, Mheshimiwa Spika, kuna kijana Mohamed Omar. Huyu kafia mahabusu, na mara baada ya kufa kulikuwa na maneno "mgonjwa, mgonjwa", ugonjwa wenyewe haujulikani. Na mara baada ya kufa huyu, Polisi wameshikilia haraka haraka azikwe. Taratibu tunazoambiwa ni kuwa mtu anayekufa mahabusu, kuna na inquest. Sasa huyu kwa nini asifanyiwe inquest? Kuna kitu gani kinachofichwa? Naomba na hilo nalo liangaliwe, na siliombi pake yangu, wengi wanaliomba. (Makofi) 

Mheshimiwa Spika, Serikali isijivune kwamba sasa tumempeleka MOI tunamlipia kila siku Sh. 40,000. Michango mingi imeshachangwa na Waislamu na wasiokuwa Waislamu juu ya Chuki. Serikali ikishindwa, wenzake wako tayari kumtibia Dar es Salaam na kumpeleka nje. Kwa hiyo, Serikali kwa makosa yake isiseme sasa sisi tumesha mmaliza huyu, tutamweka kwenye chumba cha Sh. 40,000 (Makofi). 

Mwisho, Mheshimiwa Spika, nataka niseme moja kwamba mwaka 1995 kulikuwa na maneno ya nani umchague na nani usimchague, kwa Marais. Waislamu waliambiwa kwamba mchagueni Mkapa kwa sababu ni Rais mwadilifu. Uadilifu wake umethibitika, hapendelei. Anapenda wote wananchi Watanzania. Hata Gazeti la Mtanzania juzi juzi wamesema kwamba Mkapa anasikiliza kilio chaWaislamu. Sasa sisi tunamwombea Mungu katika shughuli zake. Ila nina moja ninalotaka kusema. Nimesema mara moja na narudia tena, kwamba nchi hii yetu wote. Kuna baadhi yetu hawawahitaji Wakristo katika shughuli zao, kuna baadhi yetu hatahitaji Waislamu. Rais anawahitaji wote. Rais anawahitaji Waislamu, anawahitaji Wakristo. (Makofi) 

Tafadhali naomba, Mheshimiwa Spika, kwamba tusimkaangie mbuyu. Naishia hapo hapo. Wanaojua Kiswahili, maneno yanayofuata wanayajua. (Makofi). 

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi). 

 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Kitwana Kondo anguruma bungeni : Uadilifu wa serikali watiliwa mashaka 
Na wandishi wetu 

Mtawa asema ni haki Waislamu kukosoa Ukristo 

Hakuna haki bila ya wajibu 

Mabadiliko ya Katiba 

Aliyoyazungumza Mhe. Kitwana Kondo Bungeni 

Waislamu amkeni: Msikiti wa Mwembechai umefanywa Masjid dhirara 

Post Card zinadhalilisha Zanzibar 

MAKALA: Serikali ichunguze nini? 
Na Tatu A. Rajab,  

Waandishi tusidhalilishe taaluma 

MAKALA: Serikali ifafanue kashfa ni nini? 

Madai ya kunyimwa elimu ni hisia sahihi 
Na Ustadh A.S. Fundi 

Kampeni za kudhibiti ukimwi 

Waandishi kashfa mnayosema ni ipi? 
NA M.A.KAZUKAMWE  

Acheni kufungamanisha ushirikina na nyota 
Na Masoud Mohamed Said 

Uvutaji wa sigara na madhara yake kiafya 
Na. Anaphy A. Said  

Matibabu ya mwanafunzi aliyepigwa risasi 

Warejeshwa rumande kwa kukosa wadhamini 

Bakwata Handeni yataka mihadhara iendelee 

Mgogoro wa kiwanja kati ya Wakatoliki na Waislamu 

Vijana Masjid Aqswa waunda umoja 

Barua 

Mashairi 

Masomo 

Lishe 

 

 
 Maoni yoyote kuhusu ukarasa huu yapelekwe kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita