AN-NUUR 
Na.170 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 9 - 15, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
MAKALA
Marekani ni magaidi wa haki za binadamu

WASHINGTON licha ya kuingilia mambo ya ndani (ya Umoja wa Mataifa) inachukua nafasi muhimu katika (kuingilia) mambo ya kimataifa (ya Umoja wa Mataifa), Hiyo ni kauli ya Boutros Ghali katika kikao cha 48 cha Umoja wa Mataifa, akiuweka wazi bila kujua ubabe wa Marekani katika sura ya ulimwengu wa haki za binadamu, MUSSA ALLY anaeleza zaidi. 

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kabla ya Bw. Kofi Annan, aliwahi kuutoa wasiwasi ulimwengu wa wanyonge juu ya kitendawili cha nani mmiliki halisi na halali wa Umoja wa Mataifa, pale aliposema mbele ya kadamnasi ya vigogo wa dunia kwamba malengo na makuu ya kisiasa ya Umoja huo yanaoana kabisa na siasa za nje za Amerika! 

Kauli hiyo ya Boutros Boutros Ghali inadhihirisha ni kwa jinsi gani Katiba ya Umoja wa Mataifa ambayo ilitakiwa kutoa haki sawa kwa wanachama wake wote inavyovunjwa kwa makusudi kabisa. 

Kama vile haitoshi, Bw. Boutros Boutros Ghali alimdokeza mwandishi mmoja wa Kijerumani katika moja ya mikutano yake: "Kama Umoja wa Mataifa unahitaji kubeba jukumu zito la utatuzi wa matatizo kadhaa ya kimataifa yaliyochomoza kufuatia kipindi cha vita baridi, basi unalazimika kutegemea Amerika". 

Aidha, Bw. Ghali aliwahi kusema kuwa eti yeye naihitaji mno Marekani hali kadhalika chombo anachokiongoza Umoja wa Mataifa (nao pia kama nilivyoamini) unamhitaji Muamerika hivyo ni jambo lisiloepukika (kama sio la lazima) kuwa na uhusiano mzuri kati yao", alisema. 

Lakini kabla ya hatujakwenda mbali, hebu tuangalie moja ya malengo makuu halisi ya kuundwa umoja huo kwa mujibu wa Katiba yake iliyokubaliwa na kusainiwa na wanachama wake wote. 

"Kulinda amani na usalama wa mataifa kuchukua hatua zifaazo kwa minajili ya kufuta vitisho vya (uvunjikaji) amani, kusimamisha chokochoko.. (Hivyo) kuleta amani ya kweli inayofuatana na misingi halisi ya uadilifu na sheria za kimataifa". 

Na katika tamko la kimataifa la haki za binadamu lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Desemba 10, 1948, aidha, tunaona nafasi ya umoja huo kwa wanachama wake. 

Kwa mfano, katika ibara ya kwanza: ya tamko hilo kunawekwa wazi kuwa binadamu wote wamezaliwa huru na kwa usawa katika hadhi na haki 

Aidha, ibara ya pili inatufahamisha kwamba, kila mtu anastahili kupata haki na uhuru ulioelezwa katika tamko hili bila kujali tofauti za kiasili, rangi, jinsia, lugha, dini, siasa au maoni mengine, utaifa au asili ya kijamii, mahali pakuzaliwa au hali nyingine yoyote. 

Zaidi ya hapo hakuna ubaguzi utakaofanyika kwa sababu za kisiasa, mamlaka za kisheria au hadhi ya kimataifa ya nchi ambayo mtu anatoka, bila kujali kama hiyo ni nchi huru au bado inatawaliwa (mfano Palestina inayotaliwa na Waisraeli). 

Sasa hebu tugeuze macho yetu kwa Marekani na bakora yake (Umoja wa Mataifa). Bw. Parez de Culler aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliwahi kusema kuwa kura ya Veto (turufu) inayopigwa na madola matano yaliyojikweza (Amerika, Uingereza, Ufaransa, China na Russia) ni moja ya kizingiti kikubwa kabisa cha utatuzi wa matatizo ya kimataifa na msiba mkuu ulioifunika dunia. 

Mwandishi mmoja mashuhuri huko Ghuba aliwahi kusema kuwa turufu ya Amerika na "wapambe wake" ina aibu chafu mbili, mosi veto imefelisha jitihada za kurudisha haki katika sura ya ulimwengu na imefeli kuondoa ubatilifu uliopea. Na aibu ya pili ni wa ukiwa msafi unasukumwa na Baraza la Usalama uchukue jukumu chafu la kuibinya vilivyo haki na kutetea kwa nguvu zote batili. Jambo ambalo linakwenda kinyume na Katiba ya Umoja wa Mataifa ibara ya pili kipengele cha nne, "Wanachama wote wa Umoja wa Mataifa wajifunge (na njia za) kutumia vitisho au nguvu (ubabe) kwa nchi au uhuru wa kisiasa wa taifa jingine, ama njia yoyote iendayo kushoto mwa malengo (halisi) ya Umoja wa Mataifa". 

Licha ya kipengele hicho cha katiba ya umoja huo kuwa wazi kiasi hicho, pia tunaona kuna kujichanganya kwa katiba hiyo, kwani ni hiyo hiyo inayotoa mwanya wa ugandamizaji wa wanyonge kwa kura ya turufu. Wanachama wa umoja huo hasa wa nchi zinazonyanyasika pia wanachangia kwa upande mwingine. 

Tukiachana na dondoo hiyo fupi ya veto, na tutazame vitendo vya Amerika katika masiku ya usoni hasa baada ya balozi zake hapa Dar es Salaam na Nairobi, Kenya kuhujumiwa kwa mabomu. 

Marekani akisaidiwa na vyombo vyake au vyenye mualekeo wake wa habari wakasukuma moja kwa moja shutuma, tuhuma na propaganda dhidi ya Uislamu na Waislamu (hususan Waarabu) kwa mwavuli wa kupambana na ugaidi wa kimataifa. 

Marekani ikaendesha kamata kamata na upekupeku kwa Waislamu, nyumba na taasisi zao. Vyombo vya habari navyo vikadiriki hata kutoa hukumu kwa watuhumiwa, jambo ambalo ni kinyume cha tamko la kimataifa la haki za binadamu la Desemba 10, 1948 ibara ya 11 kipengele cha kwanza kinachosema: "Mtu yeyote anayeshitakiwa kwa kosa la jinai, atahesabiwa kuwa hana hatia mpaka pale itakapothibika kisheria mbele ya sheria kwenye mahakama ya wazi akiwa amejitetea". 

Baya zaidi serikali ya Marekani ikalazimisha watuhumiwa hao (Waislamu) wakahukumiwe kwa sheria za Kiamerika! Wewe ndiyo mlalamikaji (mshtaki) wewe huyo huyo polisi, tena wewe huyo huyo unataka uwe mwendesha mashitaka, shahidi (wa mlalamikaji) na hakimu! 

Wakati huo huo umekwisha tanguliza kauli za kibaguzi dhidi ya mtuhumiwa; ibara ya kumi ya tamko la kimataifa la haki za binadamu inatufumbua macho: "Kila mtu anastahili kusikilizwa kwa haki na usawa mbele ya vyombo vya sheria visivyo vya ubaguzi katika kuamua haki na wajibu wake na kwenye kusikilizwa kwa kosa la jinai analoshitakiwa". 

Sasa tunategemea nini pale nyani anapompelekea "Gendaheka" (dume la nyani) "Fursa" (hadhi) ya uhakimu? Na Profesa Kapteni alishatueleza; "We are not from the Ape’s" kwamba hatukutokana na manyani. 

Akikabiliwa na kashfa nzito ya "kunajisi Ikulu" na kulidanganya taifa, kiongozi Mkware Bill Clinton alijaribu kuondoa umakinifu wa Waamerika juu ya "segele" lake na Lewnsky badala yake akaishambulia Sudan na Afghanistan kwa kisingizio cha kuhujumu kambi za magaidi huku dunia ikitia "super glue" vinywani. 

Kwanini iwe hivyo? Swali hili lilishajibiwa na Bw. Boutros Ghali kabla ya tukio miaka kadhaa iliyopita kwa kutamka; "Baraza la Usalama linatenda kufuatana na maslahi ya wanachama wa kudumu na wala si juu ya msingi wa uadilifu". 

Ni lazima tufahamu suala hili kuwa Baraza la Usalama ni chombo cha kisiasa, kwani utekelezaji wa baadhi ya maazimio yake unazingatia misimamo ya madola (wababe) yaliyo wanachama wa Baraza la Usalama. 

Na ndiyo maana miongoni mwa maazimio yaliyopitishwa na Baraza hilo yanacheleweshwa au hayatekelezwi kabisa. (Rejea mazungumzo yake Bw. Boutros na CNN mapema mwaka 1995). 

Na hilo ndilo lililotokea barazani pale Sudan ilipopeleka madai yake juu ya Marekani kuishambulia nchi hiyo na kupuuza ibara ya 28 ya tamko la haki za binadamu la umoja wa mataifa inayosema; "Kila mtu anastahili utulivu katika jamii yake na kimataifa, ambapo haki na uhuru wake uliotolewa katika tamko hili utapatikana". 

Kwa kifupi tukiangalia mazingira ya matukio hayo mawili ya mabomu na jinsi yalivyoshughulikiwa tunapata darasa juu ya siasa za kimataifa za Amerika, Kenya na Tanzania. 

Aidha, tunapata darasa juu ya hali ya Uislamu na Waislamu wa Kenya na Tanzania, hususan vyombo vya kutetea haki zao na mitazamo ya viongozi wao. 

Kwa Tanzania, majibu yako wazi, lakini kwa Kenya hatuna budi kuwapongeza si tu viongozi wa taasisi zao za Kiislamu bali Waislamu wote, hasa kwa hatua yao ya mapema wiki hii kukataa mwaliko wa Amerika katika kile kilichoitwa na serikali ya Marekani kuwa eti ni "mazungumzo ya meza duara" kati ya Amerika na Waislamu wa Kenya! 

Kwa macho makavu bila ya aibu wala woga, Waislamu wa Kenya walitoa kauli kali dhidi ya magaidi hao wa haki za binadamu ulimwenguni na kuwaita kuwa ni maadui wa Uislamu duniani kote. 

Tunawapa hongera Waislamu wa Kenya kwa msimamo huo na tunawaambia wazi Waamerika kuwa Uislamu ni amani, isipokuwa ubalakala wa Kiamerika ndiyo ugaidi. 

 

 
Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI 
Tutaendelea kudhalilishwa mpaka lini ? 

Waislamu wasisitiza: Nyumba ya Waziri Mkuu ni ya Waislamu 
Na Mwandishi Wetu 

Kuchomwa nyumba za wananchi 
Na Mwandishi wetu 

Maoni Yetu: 
Maisha ya Mtanzania yanapokosa thamani 

Nguruwe marufuku Kinondoni – Tume 
Na Kassim Juma 

Watanzania waanzisha Baraza la Waislamu Marekani 
Na Mwandishi Wetu 

Wanawake Hai wamtaka Rais azungumzie mauaji ya Mwembechai 
Na Mwandishi Wetu 

‘Serikali haiwezi kuzuia rushwa’ 
Na Kassim Msuya 

Makala ya Kimataifa 
Nani gaidi: Slobodan Milosovic au Usama bin Laden 
Na Mwandishi Wetu 

Afghanistan washindi dhidi ya uvamizi karne zote 
Na Faiza bint Abubaka 

MAKALA: 
Demokrasia ya rushwa ! 
Na Mwapwani Mohamed 

Tujikwamue na janga la utwaghuti 
Na I. Kikong’ona 

MAONI: 
Nini Jihad na nani Mujahidina ? 

MAKALA: 
Marekani ni magaidi wa haki za binadamu 
Na MUSSA ALLY 

Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo kwa maneno -2 
Mwandishi: Maalim Ali Bassaleh 

Tusihalalishe mauaji ya raia kwa kisingizio cha ‘wananchi wenye hasira’ 
Na Mwandishi Wetu 

Historia ya sayansi na tiba 
Na Dk. Amur A.A. 

Msiwageuze watoto ombaomba 
Na H.E. Omar 

MAKALA YA JAMII: 
Profesa Malise Kaisi acha uzushi dhidi ya Mtume Muhammad 

Sensa ya majaribio: Wananchi watofautiana na serikali 
Na Rajab Rajab - Morogoro 

Uislamu ulivyoingia Zanzibar -3 

Mwembechai wageuka Hame, Bado walindwa na polisi 
Na Badru Kimwaga 

Waislamu Moro waendelea kusaidia wagonjwa 
Na Rajab Rajab - Morogoro 

Mjadala wa Katiba ya Shirikisho kuzinduliwa Dar Jumapili 
Na Mohamed Othman 

Walimu wa dini Tanga wapokea Baiskeli 
Na Abu Said 

Mafundisho ya Quran 
Kutoa katika njia ya Allah: Al-Baqarah aya  264 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Vitu vinavyoweza kuwemo katika vyakula 

 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita