|
|
| Msiwageuze
watoto ombaomba
KWA kipindi cha kama miezi miwili iliyopita karibu kila siku nikipita maeneo ya katikati ya Jiji, Kariakoo na vitongoji vingine maarufu hapa Jijini nakutana na vijana wadogo wanaomba michango kwa watu mbalimbali wanaopita njia hasa wale wanaowahisi ni Waislamu. Juzi baada ya kukutana na kijana mmoja ambaye nilishakutana naye siku za nyuma nikaamua kumhoji mara baada ya kuniomba mchango. Mazungumzo yetu yalikuwa hivi: Mtoto: Dada Assalaam Alaykum. Shikamoo naomba mchango wa madrasa. Baada ya kuitikia salamu yake niliendelea kumhoji. Swali: Umejuaje kama mimi Muislamu? Jibu: Umevaa baibui na ushungi hivyo bila shaka ni Muislamu. Swali: Mimi nitafahamu vipi kama wewe kweli ni Muislamu na huo mchango ni wa madrasa? Jibu: Mimi ni Muislamu haki ya Mungu vile. Huoni nimevaa barakashia, jina langu hili hapa (aoanyesha jina kwenye fomu ya michango aliyokuwa nayo). Swali: Chuo chenu kiko wapi? Jibu: Temeke kwa (nimesahau jina alilolitaja). Swali: Saa hizi saa tatu asubuhi wewe skuli unaenda saa ngapi na mchango unakusanya saa ngapi na wakati huo huo chuo unasoma saa ngapi? Jibu: Nimeshamaliza darasa la saba. Chuoni tunaenda jioni. Swali: Si juzi tu tumekutana Posta ya Zamani ukaniambia upo la tano hivyo unaingia jioni skuli? Au sio? Leo umeshamaliza? Jibu: Sio mimi kweli tena labda umenifananisha tupo wengi Wallah vile. Swali: Kwanini walimu wenu hawachangishi hiyo michango wenyewe? Jibu: Hata wao wanachangisha lakini sisi ndo tunakuja mjini kwa sababu nauli yetu "fisi" tu (50) na tunapata pesa kibao. Swali: Unafikiri kwa nini nyie mnapata pesa nyingi kuliko walimu wenu? Jibu: Tunatembea sana, watu wanatuonea huruma hivyo watugea pesa japo jiti tu (100) siku za Ijumaa kwa Wahindi unapata pesa kibao. Swali: Mmeanza lini kuchangisha pesa hizo na mnadhani mtapata kiasi gani pia mnategemea kumaliza lini? Jibu: Tumeanza siku hizi hizi, hata sijui tutamaliza lini, tukimaliza Ustaadh huwa anatuambia hayatuhusu sisi tuchangishe tu. Swali: Wazazi wako wanafahamu kama unafanya zoezi hili la uchangishaji? Jibu: Mwalimu wa chuo mwenyewe babangu mdogo. Dada wewe Paparrazi nini. Mbona maswali mengi? Swali: Nikikwambia siwezi kukupa pesa zangu kwani mimi siamini kama hizi pesa kweli walimu wenu wanazitumia kuendeleza madrasa utasemaje? Jibu: Siwezi kukulazimisha, pesa si yako! Wewe si Muislamu ("ndio") na mimi si Muislamu bassi haiwi kwa watu wawili Waislamu kuacha kuaminiana. Toa tu dada utaikuta amali yako kwa Mwenyezi Mungu. Swali: Hivi unadhani watu watawatafautishaje na ombaomba? Jibu: Mimi sio kilema, wala sio kipofu, na ninakaa kwetu pia ninayo fomu hii hapa ya kujaza ambayo ombaomba hawana. (Mwisho. Sikuwa na Cassette wala sikuandika hivyo nimenukuu kwa kadri Allah (sw) alivyonijalia kukumbuka). Kwa kumuonea huruma ya kumpotezea muda wake nikampa kiasi cha pesa na kumruhusu aondoke. Ndugu zangu katika Uislamu hawa watoto ambao wanalelewa katika mazingira haya tunategemea baadaye waje kuwa kitu gani? Nyie walimu wa chuo (madrasa) hamuoni mnaudhalilsha, ufedhehesha na kuudunisha Uislamu na Waislamu. Hawa watoto walivyo tu huzuni tosha kabla hawaja nyanyua mdomo kuomba mchango. Sijui mtu anayesoma Madrasa Temeke anafikaje Posta akiwa pekupeku. Ni wachafu na kwa haraka haraka unaweza kudhani ni vibaka fulani. Hivi kuna uhusiano gani kati ya uchafu au kuwa rough na Uislamu. Au Waislamu wanatakiwa uwa wasafi siku ya Ijumaa an siku za Eid? Wazazi mnaowapeleka watoto wenu madrasa ili wakafundishwe kuwa ombaomba si bora muwafundishe wenyewe japo mara mbili kwa wiki au dufu ni kitu muhimu sana hivyo ni lazima watoto waende madrasa. Hivi mzazi unaweza kumuachia mwanao aende skuli peku, hajachana nywele na akiwa uniform chafu? Mbona chuoni vitu hivi hamvijali? Waislamu tuache kujidhalilisha, Uislamu ni dini ya usafi sio dini ya kanzu zenye viraka. Tusikubali kudhalilishwa kwa kuhakikisha tunapiga vita juhudi zozote zile za Uislamu hasa kwa walimu wa madrasa wanaowageuza watoto (Waislamu) kuwa ombaomba. Kwa mtaji huu hatutafika popote. "Ee Allah tujaalie tuweze kuurejesha Uislamu katika nafasi yake hapa
duniani"
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Waislamu wasisitiza: Nyumba ya Waziri
Mkuu ni ya Waislamu
Kuchomwa nyumba za wananchi
Maoni Yetu:
Nguruwe marufuku Kinondoni – Tume
Watanzania waanzisha Baraza la Waislamu
Marekani
Wanawake Hai wamtaka Rais azungumzie
mauaji ya Mwembechai
‘Serikali haiwezi kuzuia rushwa’
Makala ya Kimataifa
Afghanistan washindi dhidi
ya uvamizi karne zote
MAKALA:
Tujikwamue na janga la utwaghuti
MAONI:
MAKALA:
Tufuate Uislamu kwa vitendo
na siyo kwa maneno -2
Tusihalalishe mauaji ya
raia kwa kisingizio cha ‘wananchi wenye hasira’
Historia ya sayansi na tiba
Msiwageuze watoto ombaomba
MAKALA YA JAMII:
Sensa ya majaribio: Wananchi watofautiana
na serikali
Uislamu ulivyoingia Zanzibar -3 Mwembechai wageuka Hame,
Bado walindwa na polisi
Waislamu Moro waendelea kusaidia
wagonjwa
Mjadala wa Katiba ya Shirikisho
kuzinduliwa Dar Jumapili
Walimu wa dini Tanga wapokea
Baiskeli
Mafundisho ya Quran
Chakula na Lishe
|