|
|
LICHA ya kupita zaidi ya miezi minane tangu zilipotokea vurugu Msikiti wa Msikiti wa Mwembechai kukabidhiwa wadhamini wa Msikiti huo, mahudhurio ya waumini waswalio Msikitini hapo bado ni madogo ukilinganisha na ukubwa wa Msikiti huo na ilivyokuwa hapo awali kabla ya vurugu hizo. Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa habari hizi umeweza kuonyesha kuwa waumini wengi bado wana hofu kuswali ndani ya Msikiti huo kutokana na kuwepo kwa askari polisi maeneo ya Msikiti huo ambao hawaeleweki wako hapo kwa ajili gani. Mwandishi wa habari hizi aliweza kushuhudia waumini wakiswali swala ya alfajiri na zile za mchana wakiwa hawazidi safu mbili hali inayotia ukiwa Msikiti huo uliokuwa na waumini wengi na maarufu kutokana na mihadhara iliyokuwa ikiendeshwa Msikitini hapo na wahadhiri maarufu ambao kwa sasa hawapo kutokana na Msikiti kukabidhiwa kwa wazee wa Msikiti wajiitao wadhamini. Nyakati ambazo waumini huwa wengi kiasi cha kufikia safu tatu hadi nne ni siku ya Ijumaa, lakini vipindi vingine vyote mahudhurio huwa hafifu kiasi cha kuutia ukiwa Msikiti huo. Uhaba huo wa mahudhurio ya waumini ndani ya Msikiti huo yamefanya hata ukarabati uliofanyiwa Msikiti huo kuwa bure kwani ndege wameshaanza kujenga viota na kutapanya vinyesi vyao juu ya mazulia pamoja na sehemu za kutokea au kuelekea sehemu ya kutawadhia. Msikiti huo ulikabidhiwa wadhamini wa Msikiti huo wakiongozwa na Sheikh
Ramadhani Gumbo mnamo mwezi wa tatu mara baada ya "vurugu" zilizosababisha
Waislamu wapataao wanne kuuawa na polisi, wengine kwa mamia wakisekwa rumande
kwa madai ya kuvuruga amani, kuharibu mali na kuendesha mihadhara ya kashfa.
Na Rajab Rajab - Morogoro WAISLAMU mkoani hapa wanaendelea na zoezi lao la kuitafsiri Qur-an kwa vitendo kama kuwatembelea wagonjwa hospitalini, kuwasaidia dawa pamoja na kuwaombea dua kwa Mweneyezi Mungu na kuwafariji kwa kuwapa maneno mazuri ya Mwenyezi Mungu. Mapema wiki hii wakiwa katika kipindi chao cha tano tangu waanze kutembelea wagonjwa katika hospitali ya Mkoa, Waislamu hao waliweza kufanya usafi katika maeneo ya hospitali hiyo, kugawa dawa kwa baadhi ya magonjwa waliokuwa hawana uwezo pamoja na kugawa matunda kwa wagonjwa wote. Akiongoza msafara wa Waislamu hao, Ustadh Shaaban Jigaya amewataka Waislamu wote mkoani hapa kujiunga na wenzao katika shughuli hiyo kwani ina ujira mkubwa sana mbele ya Mweneyezi Mungu na pia Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (s.a.w) alikuwa akifanya kazi hii. "Ndugu zangu Waislamu tuliokusanyika hapa kwa ajili ya kuwafariji wenzetu naomba kila mtu awe muhamasishaji juu ya jambo hili kwani hata Mtume wetu alifanya tena yeye alikuwa akipita majumbani na kuwajulia hali watu", alisema Ustadh huyo. Aidha, Manesi na wagonjwa waliozungumza na gazeti hili wameonyesha kufurahishwa kwao na uamuzi uliochukuliwa na Waislamu wa mkoa huu na kutaka uigwe na watu wengine wakiwemo matajiri na taasisi mbalimbali za dini. "Tunashukuru sana na nyinyi mmeamua kutusaidia kwani muda mrefu mmetuachia peke yetu", alisikika akisema nesi mmoja wa wodi namba tisa (9) ambaye hakupenda kutaja jina lake wakati akitoa pongezi zake kwa Waislamu hao. Nao wagonjwa waliokuwa katika hospitali hiyo wakiwemo wafungwa wameeleza kufurahishwa kwao na uamuzi wa busara uliochukuliwa na Waislamu wa kwenda kuwajulia hali na kujaribu kutatua matatizo yaliyokuwa nje ya uwezo wa baadhi ya wagonjwa waliokuwa hospitalini hapo. "Tumefarijika kama Waislamu kuanza tabia ya kututembelea, kutufariji na kutatua baadhi ya matatizo yetu kwani muda mwingi tumekuwa tukiwaona Wakristo wakija na kutugawia ivitabu vyao vya Biblia na kutuhubiria idini yao", alisema Mzee Shomary Khamisi aliyekuwa wodi mbili ambaye ni mgonjwa wa muda mrefu hospitalini hapo. Aidha, Waislamu hao wameomba uongozi wa hospitali hiyo kutoa ushirikiano wa karibu sana kwa Waislamu ili kuweza kutimiza azma yao ya kuwafariji wagonjwa waliokuwa hospitalini hapo ambapo wengine hawana ndugu hawapati huduma muhimu. Ombi hilo limekuja kufuatia kushindwa kwa Waislamu hao kukamilisha azma yao ya usafi hospitalini hapo walipotaka kuchimba mashimo ya kutupia taka taka na kushindwa kwa wahusika kuwapatia eneo la kuchimba na badala yake makawa wanatupiana mpira wao kwa wao na mwisho ikaonekana mpaka awepo Katibu Mkuu wa hospitali hiyo au kikao cha viongozi wa hospitali hiyo kikae na kuona wapi pakuchimba shimo la taka. Wakati danadana hiyo ikiendelea baina ya wahusika, gazeti hili lilishuhudia
takataka mbali mbali zikiwa zinatupwa ovyo pembeni mwa wodi aidha na wagonjwa
au manesi kufuatia kukosekana kwa mashimo ya kuhifadhia taka au mapipa
maalum.
Na Mohamed Othman MJADALA wa kuijadili katiba iliyopo na kutoa upungufu wake unatazamiwa kuzinduliwa Jumapili Oktoba 11, mwaka huu katika kituo cha Radio binafsi cha Radio Free Africa cha Jijini kuanzia saa 7 hadi saa 8 mchana. Akiongea na Mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu juzi, Mwenyekiti wa taasisi isiyo ya kiserikali inayoandaa mapendekezo ya Katiba Mpya ya Tanzania (AFORD), Senator Miselya, alisema kipindi hicho kinatazamiwa kuanza kuwashirikisha watu binafsi, taasisi na vikundi mbalimbali vya dini katika mjadala huo unaotazamiwa kuvutia wengi. Katika kipindi hicho, kutakuwa na kuichambua katiba hii ya sasa ya Tanzania na baadaye kuichambua White Paper kisha kutoa majibu yake kwa kusoma mapendekezo ya Katiba Mpya ya Serikali ya Shirikisho (serikali tatu) yaliyoandaliwa na taasisi hiyo ya AFORD ambayo yalichapishwa katika magazeti mbalimbali hapa nchini likiwemo AN-NUUR. Senetor Miselya ambaye ndiye atakayefungua mjadala huo, aliwataja baadhi ya washiriki katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na Jaji Mark Boman, Monica Muhoja, Prof. Shivji, Ruth na Wakili Fatma. Kutoka katika taasisi za Kiislamu Mwenyekiti huyo wa AFORD aliwataja Othman Matata ambaye ni Mwanasheria na mhadhiri maarufu wa dini ya Kiislamu, Sheikh Abbas Kilima Katibu Mkuu wa BARAZA KUU nchini, Sheikh Aboubakar Mwilima na taasisi nyingine ambazo bado anafanya juhudi kuweza kuwasiliana nazo ili ziweze kuwemo katika mjadala huo. Mjadala huo umelenga zaidi katika kuichambua katiba ya sasa na kutoa upungufu uliomo katika katiba hiyo ambao kwa kiasi kikubwa umedaiwa kuchangia katika kuwakandamiza wananchi. Kutakuwa na majadiliano kuhusu Mapendekezo ya Katiba Mpya ambayo kwa kiasi kikubwa yanataka Tanzania iwe na Serikali tatu (Tanganyika na Zanzibar). Na ile ya Muungano iwe ya Shirikisho. Yamezitaka serikali hizo chini ya Shirikisho kuwa ni ile ya Tanganyika na Zanzibar zote kila moja ikiongozwa na Waziri Mkuu wake ambaye atachaguliwa kwa kura za wananchi. Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa AFORD, mjadala huo utadumu kwa muda
wa miezi sita kuanzia Jumapili wiki hii na utaendelea kuwaalika watu na
taasisi mbalimbali ili nao waweze kutoa michango yao katika kufanikisha
upatikanaji wa Katiba Mpya ya Tanzania ambayo itakidhi mahitaji halisi
ya wananchi wote.
Na Abu Said Walimu wa somo la Maarifa ya Kiislamu wasiopungua kumi wamefaidika na sadaka ya baskeli kumi kutoka kwa mfadhili ambaye hakupenda kutajwa jina lake. Baskeli hizo zilikabidhiwa kweneye tafrija fupi iliyofanyika tarehe 29 mwezi wa tisa kwenye makao makuu ya taasisi ya "Thakafat Al Islamiya" yaliyopo kwenye mskiti ujulikanao kama MV9 ulioko barabara ya tisa. Taasisi ya Thakafat Al-Ilslamiya katika siku za karibuni imekuwa msitari wa mbele katika kutoa walimu wa dini kwa shule za msingi, sekondari na vyuo. Kati ya walimu hao kumi waliokabidhiwa baiskeli hizo, wawili ni wa kike ambao viongozi wa taasisi walimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa wamejiunga karibuni wakitokea masomoni. Sherehe ya makabidhiano ya baskeli hizo yalishuhudiwa na kiongozi mkuu wa Thakafat, Sharif Hussein Hashim. Katika maelezo yake Sharif Hussein amesema, katika muda mfupi ujaoo watakutana na bodi za shule ambazo zimekuwa sugu kuruhusu uvaaji wa Hijaab, pamoja na kuwa idadi kubwa ya walipa karo wao ni waislamu. Juhudi za namna hii huenda zikaifaidisha pia mikoa ya Arusha na Dar
es Salaam ambako Thakafat Al-Islamiya ina matawi yake.
|
YALIYOMO
TAHARIRI Tutaendelea kudhalilishwa mpaka lini ? Waislamu wasisitiza: Nyumba ya Waziri
Mkuu ni ya Waislamu
Kuchomwa nyumba za wananchi
Maoni Yetu:
Nguruwe marufuku Kinondoni – Tume
Watanzania waanzisha Baraza la Waislamu
Marekani
Wanawake Hai wamtaka Rais azungumzie
mauaji ya Mwembechai
‘Serikali haiwezi kuzuia rushwa’
Makala ya Kimataifa
Afghanistan washindi dhidi
ya uvamizi karne zote
MAKALA:
Tujikwamue na janga la utwaghuti
MAONI:
MAKALA:
Tufuate Uislamu kwa vitendo
na siyo kwa maneno -2
Tusihalalishe mauaji ya
raia kwa kisingizio cha ‘wananchi wenye hasira’
Historia ya sayansi na tiba
Msiwageuze watoto ombaomba
MAKALA YA JAMII:
Sensa ya majaribio: Wananchi watofautiana
na serikali
Uislamu ulivyoingia Zanzibar -3 Mwembechai wageuka Hame,
Bado walindwa na polisi
Waislamu Moro waendelea kusaidia
wagonjwa
Mjadala wa Katiba ya Shirikisho
kuzinduliwa Dar Jumapili
Walimu wa dini Tanga wapokea
Baiskeli
Mafundisho ya Quran
Chakula na Lishe
|