|
|
|
Na Mwandishi Wetu WAZEE wenye watoto wao vibaka utawajua tu. Siku akikurupushwa kibaka wengine wote watatoka kumfukuza lakini wao watapiga kimya ndani ya majumba yao. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Bw. Laurent Kabila amepiga kelele kwamba amevamiwa na majeshi toka Rwanda na Uganda yakiwasaidia waasi wanaompinga. Vyombo vya habari huru na baadhi ya nchi zimelisemea jambo hili, hao ni wale ambao hawana "vibaka" miongoni mwa "vijana wao". Si muda mrefu uliopita kurasa za magazeti yetu zilikuwa zikishehenezwa kwa taarifa za unaodaiwa ugaidi wa "Usama bin Laden". Kwa kawaida taarifa ambazo zilikuwa zikiwekwa ndani katika kurasa maalum za habari za kimataifa zikawa zinatokea kurasa za mbele. Kila mmoja akawa analaani kwa namna yake unaoitwa ugaidi wa Usama. Na hayo yalifanyika si kwamba vyombo vyetu vya habari vilikuwa na ushahidi wowote madhubuti kuonyesha wapi Usama aliua au kukodi watu kuua, bali ilikuwa kutegemea propaganda za Marekani. Pengine wengi wetu walidhani na hata kuamini kwamba ile ilikuwa juhudi ya vyombo vyetu vya habari katika kupasha habari, kuelimisha juu ya ubaya wa ugaidi hali kadhalika kuulaani. Haikupita muda Marekani ikiwa mlalamikaji ikajipa uhakimu, na askari magereza ikaipiga Sudan na Afghanistan. Kimya kikatanda hakuna aliyelaani. Ulimwengu leo unashuhudia mauaji ya kutisha huko Kossovo. Wananchi wa Kossovo wenye asili ya Albania kwa mamia na maelfu wanachinjwa na kuchomwa moto makazi yao katika kile kinachoonekana kama "Ethnic cleansing" kama ilivyokuwa Bosnia. Wengi wa wanaouliwa na kukatwakatwa viungo vyao na askari wa Serbia ni wanawake na watoto, wengi wameyakimbia makazi yao ambayo baadaye yamechomwa moto na askari wa Bw. Slobodan Milosovic ili kuhakikisha kwamba hawarejei. Watu hawa wanaofanyiwa mauaji ya maangamizi (genocide) huko Kossovo wanatajwa kuwa ni wenye asili ya Albania. Watu hawa ni mfano useme Wamakonde wenye asili ya Msumbiji, au wenyeji wa Mara (Wakurya) wenye asili ya Kenya. Bin Laden anashutumiwa kwamba ni gaidi na ugaidi hulaaniwa kwa sababu hupoteza maisha ya watu wasio na hatia na kuharibu mali. Japo mauaji haya ya raia wa Kossovo yamekemewa na vyombo vya habari vya kimataifa, NATO, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani na Uingereza, hatuoni vyombo vyetu vya habari vikiyakemea mauaji haya ya kutisha kama vilivyochemka na suala la Bin Laden! Je, Bin Laden tunao ushahidi, ameshaua watu wangapi na kuharibu mali kiasi gani ? Je, Milosovic ashaua raia wa Kossovo elfu ngapi na majumba kiasi gani ashayaangamiza ! Akinamama na watoto wangapi wapo mwituni bila chakula wala maji, huku wakikabiliwa na baridi kali ? Mbona hili hatulisemi kwa nguvu ? Haki gani tunatetea ? Ugaidi gani tunaoupiga vita ? Mauaji gani tunayolaani kama hatuoni haya ya raia wa Kossovo ? Au kwa vile anayeua ni Slobodan Milosovic aliyebarikiwa kwa Sakarament na sio Bin Laden ! Saddam Hussein alipoingia Kuwait, hakuwaua raia wa Kuwait ovyo wala kubomoa majumba yao au kuyachoma moto. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikusuasua, wala Marekani haikungoja ipewe kibali na Baraza hilo. Haraka haraka majeshi na zana za kivita zilimiminika Mashariki ya Kati. Iraq ikapondwapondwa na maelfu ya Wairaq kuuliwa kwa kisingizio cha kumwadhibu Saddam Hussein. Sasa huu mwendo wa kinyonga kwa suala hili la Milosovic unakujaje ! Si Marekani wala Baraza la Usalama lenye haraka ya kumwadhibu Solobodan Milosovic kana kwamba anapewa muda amalize kazi ya kuwafyeka wananchi wa Kossovo. Marekani ilipoipiga Afghanistan na Sudan haikusubiri kauli wala kibali cha Baraza la Usalama na ilikuwa na haraka ya kupambana na ugaidi unaoangamiza maisha ya watu na mali. Leo Milosovic anawaua raia wa Kossovo kwa maelfu – ugaidi na uuaji huu vipi ! Hakuna mwenye haraka ila mpaka Baraza la Usalama liamue na Baraza lenyewe limekuwa na kigugumizi pengine halijaelewa endapo wale wanaouliwa pale Kossovo nao ni binadamu au la ! Lakini Marekani na wababe wenzake katika Baraza la Usalama wakifanya hivyo haishangazi sana. Ila wengine ni kinyaa na aibu tupu. Majanga hutokea sehemu mbalimbali duniani. Mamia kwa maelfu ya watu hufa kwa baa la njaa na magonjwa ya kuambukizwa kama kipindupindu katika nchi za Afrika, Asia na Latin Amerika. Hatuoni nchi za Kiarabu zikipigana kikumbo kupeleka madawa na misaada mbalimbali. Tulikumbwa na janga la Elnino na kipindupindu, hatukuona ndege za Misri, Saudia, Algeria n.k. zikipanga foleni uwanja wa ndege wa Dar es Salaam kushusha misaada. Leo umelipuliwa ubalozi wa Marekani nchi zinapigana vikumbo kuwahi foleni ya kutoa mkono wa pole na misaada kwa waathiriwa. Hivi sasa maelfu ya wananchi wa Kossovo wako nje porini hawana chakula wala hema. Mbona hatuoni nchi hizi zikipigana vikumbo kuwapelekea msaada watu hawa ! Mbona hatuwasikii Misri, Saudia, Kuwait wakituma ujumbe mzito mzito Umoja wa Mataifa kutaka idhini maalum ya kupeleka ndege zao zilizosheheni madawa na vyakula kwa wananchi wa Kossovo! Pengine wanasubiri Marekani ianze kupeleka !Walijisemea wanasiasa kwamba huu ni wakati wa uwazi na ukweli. Na kweli, hakuna tena kufanya dhulma, kinyemela au kimya kimya. Wanaoonekana kiroja ni wale wanaoendelea kujipendekeza wakiwa na majoho yao. Na Faiza bint Abubakar WAAFGHANI wamekuwa wakiandamwa na watawala wa mataifa ya kigeni kwa karne nyingi. Wananchi hao wa eneo ambalo sasa linajulikana kama Afghanistan wamekuwa wazoefu wa kupambana na wavamizi toka nchi na mataifa ya nje. Na mara zote wamekuwa washindi dhidi ya wavamizi. Katika historia yao ya karne za awali wamekuwa wakipambana na wavamizi toka nchi za jirani, Persia ( Iran), India (ikiwemo Pakistan ya wakati huo), China na Russia. Mabeberu wa Kiingereza nao walipoingia na kutawala India wakaona haitoshi, lazima pia waitawale Afghanistan. Walishindwa kuingia kwa rai na ulaghai. Wakaamua kuvamia kwa kutumia nguvu za kijeshi. Mwaka 1839 watawala wa Kiingereza waliokuwepo India walidhani wamepata mwanya mzuri wa kuivamia Afghanistan. Mwanya huo ulitokana na vita vilivyotokea ndani ya Afghanistan baina ya Waafghani. Katika vita hivyo, wananchi walioshindwa walimuondoa mtawala wao aliyekuwa madarakani Shah Shoja na kumuweka Dost Mohammed. Bahati mbaya Waingereza hawakuelewa vizuri kiini cha ugomvi kati ya wananchi hao na mtawala pamoja na genge lake walioondolewa madarakani. Hawakujua utawala ulivyokuwa ukipuuza kufuata mwongozo wa Kiislamu. Waafghan wenyewe wamekuwa kwa karne hizo wakiongozwa na watawala wa Kiislamu katika majimbo. Na yule wa kitaifa alitakiwa kuwa hivyo. Na kila watawala hao walipo kengeuka wananchi walisimama kuwahoji na kuwarekebisha, ilipobidi waliwang’oa madarakani. Tofauti kubwa baina ya watawala waliofuta Uislamu na wale waliouacha ilionekana kwenye majina ya vyeo. Mtawala aliyeongoza nje ya Uislamu mara nyingi alipenda kujiita kwa jina la cheo cha kimila kabla ya Uislamu -‘Shah’.Na wale walioongoza Kiislamu walitambulika zaidi kwa vyeo vya Amir. Hivyo, Waingereza walipovamia Afghanistan mwaka 1839 walitumia kisingizio cha kumrudisha madarakani Shah Shoja ambaye aliondolewa na wananchi waliomuweka Amir Dost Mohammed. Hivyo, Waingereza hawakujua kuwa walikuwa wanakwenda kupambana na Waislamu. Kiongozi wa watawala wa Kiingereza India, Lord Auckland akaamua kufanyike uvamizi dhidi ya Afghanistan na kumuamuru kiongozi wa majeshi Lord Palmerston kupeleka jeshi lipatao askari 5000. Uvamizi ulifanyika na Shah Shoja akarudishwa madarakani. Ufisadi wa watawala wa kigeni na ule usiokuwa wa Kiislamu ukaanza kufanyika. Wanawake wa Kiislamu ikawa walengwa wakuu wa mafisadi hao ambao inaonyesha siku zote chuki zao dhidi ya Uislamu hujidhihirisha haraka na zaidi kwa wanawake wa Kiislamu wanaovaa Hijab. Hivyo, ikatokea siku moja mnamo mwaka 1841, miaka miwili baada ya kuingia wavamizi hao, askari wao waliingia katika nyumba ya mmoja wa Maamir wa vitongoji vya Kabul, Amir Akbar Khan. Askari hao waliingia bila ya kupiga hodi mpaka uani! Huko wakawakuta kina mama wale wa Kiislamu ambao waliamua kuwa siku hiyo ndiyo mwisho wa mafisadi na vibaraka wao kuendelea na ufisadi wao dhidi ya misingi ya Kiislamu. Walianza kinamama wale kupambana na askari hao walioingia mle ndani kinyume cha adabu. Waandishi wa historia ya kisa hicho wanaeleza kuwa askari wale walitoka vipande vipande mle ndani na wengi waliuawa na kinamama hao. Vita hivyo vilipamba moto. Kinamama wengine wakajitokeza dhidi ya mafisadi na kupambana nao nyumba hadi nyumba. Kisha wananchi kwa ujumla wao – vijana, wazee na hawa watoto wa umri wa kuweza kutupa mawe waliingia kwenye vita hivyo. Waingereza walipoona wamechokoza ‘nyuki’ wakataka kujitutumua kwa kumwaga askari wake katika kila mji, matokeo yake ikawa vita kuenea nchi nzima na siyo Kabul peke yake. Ikashindikana kwa majeshi hayo ya Kiingereza hata pale yalipotaka kukimbia. Yalizingirwa katika eneo moja lililojulikana kama Bolan Pass. Hapo askari hao wavamizi waliangamizwa na kiongozi wao Sir Alexander Burnes aliuawa. Hapana aliyebaki ila askari mmoja aliyeweza kufika kambini India mnamo Januari 1842. Askari huyo alifikisha salam za onyo; kuwa Waafghan ni Waislamu na sio watu wa kuchezea. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Waislamu wasisitiza: Nyumba ya Waziri
Mkuu ni ya Waislamu
Kuchomwa nyumba za wananchi
Maoni Yetu:
Nguruwe marufuku Kinondoni – Tume
Watanzania waanzisha Baraza la Waislamu
Marekani
Wanawake Hai wamtaka Rais azungumzie
mauaji ya Mwembechai
‘Serikali haiwezi kuzuia rushwa’
Makala ya Kimataifa
Afghanistan washindi dhidi
ya uvamizi karne zote
MAKALA:
Tujikwamue na janga la utwaghuti
MAONI:
MAKALA:
Tufuate Uislamu kwa vitendo
na siyo kwa maneno -2
Tusihalalishe mauaji ya
raia kwa kisingizio cha ‘wananchi wenye hasira’
Historia ya sayansi na tiba
Msiwageuze watoto ombaomba
MAKALA YA JAMII:
Sensa ya majaribio: Wananchi watofautiana
na serikali
Uislamu ulivyoingia Zanzibar -3 Mwembechai wageuka Hame,
Bado walindwa na polisi
Waislamu Moro waendelea kusaidia
wagonjwa
Mjadala wa Katiba ya Shirikisho
kuzinduliwa Dar Jumapili
Walimu wa dini Tanga wapokea
Baiskeli
Mafundisho ya Quran
Chakula na Lishe
|