|
|
|
Tunaifanyia mzaha Hijab mashuleni ? Ndugu Mhariri IMEKUWA jambo la kawaida kabisa kukutana na wanafunzi wa shule za sekondari za Kiislamu hasa za Al-Haramain na Kinondoni wakiwa nje ya majengo ya shule huku hijab zao zikiwa zimelegezwa vichwani mwao ama wengine huvua kabisa na kuzitia mikobani mwao. Na hizo zinazosingiziwa kuwa hijab huwa vitambaa tu ambavyo vingine havifuniki hata kifua pamoja na chuo cha Al-Haramain kubuni hijab mpya tunazowaona nazo, wanafunzi wake bado wamekuwa na tabia ya kuzilegeza vichwani mwao pindi wavukapo majengo ya shule. Kwa hali iliyopo katika shule hizo mbili kubwa za Kiislamu nchini ndipo yanapozuka maneno toka kwa baadhi ya wanafunzi wa shule ‘zinazoitwa’ za serikali kuwa ‘ si afadhali ya mimi nisiyevaa kabisa’ na wale wasiolipenda vazi hilo katika mashule hayo hudai ‘ nyie nini kujifungafunga maguo wakati hata katika hayo mashule yenu "hijab" yanadharauliwa". Kwanini tumekuwa hodari wa kutetea vazi hilo katika sekondari za serikali, huku katika shule zetu wenyewe tunazoziita "Islamic College" na "Muslim School" tukishuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili, hivi tunategemea nini kutoka kwa wanafunzi kama wa Al-Haramain, ambayo mwalimu mmoja wa shule hiyo alifikia hata kuandikwa kwenye gazeti kama Sanifu KUWA "Mwalimu Al-Haramain gwiji wa ufuska". Wote tunajua kuna wanafunzi wa kweli katika shule hizo, lakini wengine wanayapaka matope majina ya shule hizo. Hapo ndipo tunapowahimiza wanafunzi wa Kiislamu wa shule za sekondari za serikali wavae hijab, kwa msemo "Rights are not given, they are taken". Tukiambiwa kuwa kwa kuwa kuvaa hijab ni haki yetu tusiiombe bali tuichukue, lakini hatuambiwi kama wanafunzi wa "Muslim School" na "Islamic College" hawaitaki hiyo haki yao ya kuvaa vazi hilo. Kwanini tusianze na "Muslim Schools" zetu kisha ndipo tumalizie na shule za serikali. Mwapwani Mohamed,
Ndugu Mhariri BARUA ya ndugu yetu mwananchi mkereketwa wa Tanga iliyotoka katika gazeti lako la Septemba 18 – 24, 1998 inayohusu kichwa cha habari hapo juu ina haki zote za kuungwa mkono na kila mpenda haki. Imekuwa ni mazoea ya viongozi wetu kila wanapotembelea mkoa wetu hawana jipya la kutueleza, isipokuwa dharau na kejeli ambazo ni kweli zinazidi kututia wasiwasi kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa agenda ya siri. Ni vema kama kweli viongozi wetu wana nia njema na mkoa wetu huu wa Tanga, wangetufahamisha kwanza uvivu wetu ni nini ili tujirekebishe badala ya kututukana. Au kule kufa kwa Bandari, mashamba ya mkonge, uwanja wa ndege, shughuli za reli, kutokujengwa barabara ya Tanga hadi Mombasa, na Tanga hadi Pangani n.k. ndizo hoja zinazopelekea kuitwa watu wa Tanga ni wavivu? Na kwa sera hiyo hiyo ndio inayopelekea kuletewa waliosomea vita kuja kutumaliza tunapokwenda kuvua samaki baharini? Hivyo tungependa viongozi watueleze maana ya uvivu na namna ya maendeleo. Tunawaomba viongozi watuelekeze badala ya kututukana, Wapendao haki,
Kulikoni TAMSA Ndugu Mhariri NAPENDA kutoa malalamiko yangu kuhusu Tanzania Muslim Students Association (TAMSA) wengi wa wanafunzi wa Kiislamu nchini hatuelewi nini madhumuni ya kuwepo kwake na wengine hatujapata hata kuisikia kabisa. Natoa wito kwa TAMSA ijisambaze na kujitangaza kwa manufaa ya wanafunzi Waislamu Tanzania na Uislamu. Wakati TAMSA imelala usingizi wenzao MSAUD na TAMPRO wanatia matumaini. TAMSA mmh! M. Mohammed,
Wasichana tunanyanyaswa shuleni Kigogo Ndugu Mhariri TUMEZOEA kuona hapa shuleni petu masomo kadhaa yakifundishwa kwa maelezo na kwa vitendo. Kuna hata baadhi siku hukatishwa vipindi na badala yake tukaja na vitu kama mchele ilikufahamishwa pia kwa vitendo jinsi ya kupika katika somo la sayansi kimu. Vile vile tunafundishwa kwa ufasaha mambo ya vipimo vya tungamo katika somo la Sayansi, lakini mwalimu hatosheki hadi ahakikishe somo hilo amelifundisha kwa vitendo. Bila shaka nia na madhumuni ya walimu hao nikumuweka mwanafunzi katika uwazi zaidi wa kufahamu. Kama hivyo ndivyo, je, inakuwaje mwalimu wa Dini ya Kiislamu shuleni hapa asiwe na ruhusa wala uhuru wa kuwafundisha wanafunzi wa Kiislamu kwa vitendo mambo yanayostahiki kufanya hivyo. Tumefikiwa kuvuliwa mitandio yetu ndani ya kipindi cha dini. Mitandio ambayo tuliamriwa na mwalimu wa dini kwa ajili ya kufahamishwa kwa vitendo, vipi mwanamke wa Kiislamu anatakiwa avae, Waislamu oneni udhalilifu huu. Mwalimu Mkuu anaingia katika somo la dini kwa jazba na matusi juu ya Uislamu na kutunyang’anya mitandio yetu. Mitandio ambayo hatuvai ila kwenye kipindi cha dini tu, tukitoka ndio basi. Tuna wasiwasi hapo baadaye kuwa hata ambacho tunataka kufundishwa sharti itabidi kichunguzwe kwanza, kama kina maslahi kwa Uislamu kiruhusiwe. Mtume (saw) amesema: "Ukiona uovu uondowe kwa mkono wako, la huwezi basi kwa mdomo wako, la huwezi basi uchukie ndani ya moyo wako, lakini huo ndio udhaifu wa imani (kuchukia). Mwanafunzi muathirika,
Ndugu Mhariri NAPENDA kutoa dukuduku langu kuhusu kichwa habari hapo juu. Rais kaongeza wizara sio vibaya ni moja ya kazi yake, lakini sisi walipa kodi hatuna manufaa na wingi wa wizara wakati dawa hospitalini hakuna, watoto wa masikini hawaendi shul sababu ada kubwa badala ya kuunda wizara, pesa hizo zingetumika kutoa ruzuku ya afya, elimu n.k. Rais atuhurumie kutubebesha miwizara isio na kazi kama wizara ya wanawake na watoto kazi yake nin? Wizara ya wanawake na watoto ni mwanamke gani wanaemsaidia wakati maji tabu, kuni tabu, matibabu hakuna n.k. Kuhusu watoto sasa hawasomi kabisa ada kubwa wizara inafanya nini? Wizara ya Elimu kwa nini ziwe mbili, Elimu ya Juu na chini hapa Tanzania! Sisi walipa kodi tunaomba utuhurumie tupate dawa, maji, barabara n.k. Yasini Sauka,
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Waislamu wasisitiza: Nyumba ya Waziri
Mkuu ni ya Waislamu
Kuchomwa nyumba za wananchi
Maoni Yetu:
Nguruwe marufuku Kinondoni – Tume
Watanzania waanzisha Baraza la Waislamu
Marekani
Wanawake Hai wamtaka Rais azungumzie
mauaji ya Mwembechai
‘Serikali haiwezi kuzuia rushwa’
Makala ya Kimataifa
Afghanistan washindi dhidi
ya uvamizi karne zote
MAKALA:
Tujikwamue na janga la utwaghuti
MAONI:
MAKALA:
Tufuate Uislamu kwa vitendo
na siyo kwa maneno -2
Tusihalalishe mauaji ya
raia kwa kisingizio cha ‘wananchi wenye hasira’
Historia ya sayansi na tiba
Msiwageuze watoto ombaomba
MAKALA YA JAMII:
Sensa ya majaribio: Wananchi watofautiana
na serikali
Uislamu ulivyoingia Zanzibar -3 Mwembechai wageuka Hame,
Bado walindwa na polisi
Waislamu Moro waendelea kusaidia
wagonjwa
Mjadala wa Katiba ya Shirikisho
kuzinduliwa Dar Jumapili
Walimu wa dini Tanga wapokea
Baiskeli
Mafundisho ya Quran
Chakula na Lishe
|