AN-NUUR 
Na.171 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 16 - 22, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Kuchomwa moto nyumba za wananchi: 

Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda 

  • Bado wapo juani
  • Wafukuzwa chini ya miembe
  • Wakatazwa kung’oa mihogo yao
Na Mwandishi Wetu, Nzasa 

Wananchi waliochomewa nyumba zao katika kijiji cha Nzasa wamesema wanayaelekeza macho yao kwa. Rais Benjamin William Mkapa kwamba ndiye atajua wapi awapeleke. 

Wamesema kwamba wao ni wakazi wa Nzasa toka enzi na enzi kabla hata eneo la Kazimzumbwi kutangazwa kuwa ni msitu. 

Akiongea na mwandishi wa habari hizi chini ya mwembe alikojisitiri na wajukukuu zake, Mzee Khamis Issa Ulende (82) alisema kwamba wao ni wakazi wa eneo hilo toka wazazi wao, kwa hiyo suala la wao kuvamia msitu halipo.  

Alisema kilichowahamisha miaka ya 1970 ni operesheni ya vijiji vya ujamaa ambapo baadae walirejea kwenye asili yao.  

Mzee Khamis alisema kwamba toka mgogoro huu uibuke umepitia kwa viongozi wengi sana, hivyo wanayemsubiri ni Mheshimiwa Rais awaeleze waende wapi. 

Alisema wana wasiwasi ardhi yao imetolewa kwa Wazungu wa Sweden na hivyo wanamsubiri Mh. Rais awaone walivyo, halafu aamue ama kuwanunulia ardhi Nairobi, Sweden au popote atakapoona panawafaa. 

Alisisitiza kwamba ni muhimu Mh. Rais aende angalau awaone wazee kama ataamua kuwasaidiaa au la ni suala la baadae lakini muhimu awaone kwanza. 

Katika kufuatilia hilo, alisema kwamba wamefika Ikulu mara mbili ambapo mara ya kwanza waliambiwa ana mkutano na Mawaziri na walipokwenda tena Jumanne Oktoba 13, wakakuta yuko safarini. 

Kuhusu kauli ya baadhi ya viongozi wa serikali kwamba vilivyochomwa ni vidunda na sio nyumba, wazee mbalimbali walioongea na mwandishi wa habari hizi walisema: "Iwe vidunda au viota humo ndimo walimozaliwa na wazee wao na wao wamezaa na kujukuu humo humo". 

Naye Bibi Halima Mwinyimvua amelalama akiisihi serikali iwape hifadhi kwani watu wazima kama yeye wapo hatarini kufa kwa baridi ya usiku.  

"Mjukuu wangu nashinda juani nalala chini nikipigwa baridi usiku kucha na umri huu sijui mvua ikija itakuwaje", alilalamika bi kikongwe huyo ambaye alidai kwamba wakati Mjerumani anaondoka yeye ni mwali wa kuolewa. 

Kuhusu madai kwamba wamevamia msitu, Bibi Halima Mwinyimvua alisema kwamba yeye kazaliwa hapo na baba yake Marehemu Mwinyimvua Ngunduli kazikwa hapo hapo Nzasa. Hivi leo anapoambiwa aondoke aende wapi, alihoji. "Kote huko unaona mashamba ya watu, leo sisi nyumba zetu zimechomwa, mihogo yetu imekatwa tunaambiwa tuhame, tuhamie kwa nani", aliendelea kuhoji bibi huyo. 

Akizungumzia hasara waliyoipata wakati wa zoezi la uchomaji nyumba, alisema gunia zake mbili za mpunga zimeteketezwa, mahindi na vifaa vyote vya ndani. 

Pamoja na hayo, alisema kwamba ana muhogo mwingi sana shambani ambapo alikuwa akienda kuchuma kisamvu na kung’oa muhogo wa kupika. Lakini sasa anasema amepigwa marufuku kukanyaga shambani na mihogo yenyewe pamoja na midizi, mipapai na minazi inakatawakatwa. 

Pamoja na misaada kadhaa ya chakula wanayopewa na wananchi wema Bibi huyo amesema kwamba lililo muhimu sasa hivi ni serikali kuwaonyesha pa kwenda ili wakajenge tena hivyo vinavyodaiwa kuwa vidunda. 

Bw. John Joseph Swila ambaye alijitambulisha ni askari mstaafu wa JWTZ (No. MT 27012) amedai kwamba yeye amepoteza nyumba mbili, fedha taslimu shilingi 85,000 pamoja na vifaa vyote vya ndani. 

Bw. John anasema yeye ameshiriki operesheni nyingi akiwa jeshini, lakini hajashuhudia operesheni za kuangamiza mali za raia. "Mwenyewe hayuko unaiwasha moto nyumba yake bila kujua kilichopo ndani", alihoji Bw. John Joseph. 

Kutokana na hii nguvu kubwa inayotumika bila kujali sheria wala hisia za wananchi na shida zao, Bw. John alisema anahisi kwamba huenda eneo hilo limetolewa kwa wanaoitwa wafadhili. 

Kauli hiyo iliungwa mkono na wananchi wengi ambao wamekuwa wakidai kwamba walinzi wa misitu (Forest guards) wamekuwa wakiwabughudhi wananchi huku wakiwakejeli kwamba hawana fedha kama Anna. Imedaiwa huyo Anna ni Mzungu anayewalipa walinzi hao. 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI 
Serikali iwahurumie wananchi wake 

KUCHOMWA MOTO NYUMBA ZA WANANCHI: Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda 
Na Mwandishi Wetu, Nzasa 

Mishikaki ya nguruwe Moshi yachomwa mbele ya Msikiti 
Na Mwandishi Wetu 

MAONI YETU: 
Je; ni halali kuchoma Kidungu cha mtu? 

Upimaji huu mpya ni wa nini 
Na Mwandishi Wetu 

TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI 

Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia lengo 
Na Bi. Zuhura Tajiri, Shinyanga 
 
Teknologia:
Jifunze kuunganisha Kompyuta
Na Hassan Omar

Makala:
Nani atakayewahoji Waheshimiwa hawa

Goda Muslim School, Manzese
Na Mwandishi Wetu

Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

Historia ya mgogoro wa Nzasa
Na Mwandishi Wetu

DUMT watoa msaada kwa walioathirika Nzasa
Na Mwandishi Wetu

UCHOMAJI NYUMBA NZASA: Wafadhili wana mchango gani?
Na Mwandishi Wetu

Mafundisho ya Quran 
Kutoa pasipo masimango 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita