|
|
| TAHARIRI:
Serikali iwahurumie wananchi wake
Awali, walikuwa chini ya miembe angalau wakipoa jua la mchana,wakisubiri kupigwa baridi ya usiku maana hata shuka hawana baada ya kuunguzwa pamoja na nyumba zao, lakini sasa hata kwenye kivuli cha miembe wamefukuzwa wapo ‘jangwani’. Serikali imedai kwamba watu hawa waliochomewa nyumba ni wavamizi wa msitu na hivyo wanafukuzwa. Lakini wananchi hawa wanasisitiza kwamba wao hawana tatizo na suala la kuhifadhi msitu, wala kuwahamisha kwa nguvu waliovamia kama wapo. Wao wanasema hawajavamia msitu na eneo lao lipo mbali sana na mpaka wenyewe wa msitu. Lau serikali inadai kwamba wao wamo ndani, basi ziletwe ramani za eneo hilo pamoja na msitu wenyewe, watalaamu waonyeshe mipaka ya msitu ulipokomea. Katika baadhi ya matamshi ya viongozi wa serikali, imeelezwa kwamba zilizochomwa moto si nyumba bali vibanda vya muda vya wachoma mkaa, wapasua mbao na wakulima. Yawezekana kulikuwa na vibanda vya aina hiyo katika jumla ya nyumba zilizochomwa. Lakini tutasema nini juu ya wananchi ambao kwa siku 14 wapo nje wakishinda juani na kulala chini wakipigwa na baridi usiku kucha huku wakiwa hawana chakula cha uhakika. Haiwezi kuwa wananchi hawa kwamba walichomewa ni kibanda cha kuamia ndege. Ingekuwa hivyo wangesharudi makwao. Kubaki kwao hapo siku zote hizi ni kwamba hawana pa kwenda. Watakwenda wapi wakati hapo ndio kwao ? Hayo ndiyo makazi na mashamba waliyorithishwa na babu zao ! Waende wapi wakati sehemu zote zinazowazunguka ni makazi na mashamba ya watu wengine ! Yawezekana serikali ikawa imeona kwamba eneo hilo ni muhimu liwe sehemu ya hifadhi, au hata kama toka awali lilikuwa hivyo. Lakini angalau basi ubinadamu ufanyike katika kuweka mradi mwingine utakaoiongezea serikali mapato. Izingatiwe kwamba japo hawa wanaoondolewa hawana uwezo sawa na na muhisani mhifadhi mazingira, lakini ni binadamu hawa sawa na wale wanaodai kwamba nyumba zao ni "viota" vya ndege. Wana roho sawa na binadamu wengine na hawana manyoya ya kuwakinga na jua au baridi. Serikali ina maguvu ya kufanya operesheni yoyote itakayo lakini na iwaonee huruma wananchi hawa. Hata kama wanaharibu msitu, tusiongeze janga kwa kuwaua kwa njaa, baridi na jua. Hawa hawahitaji ramani wala mhandisi, waonyeshwe eneo watapigilia fito na kuzungusha nyasi, waishi na watoto wao. Lakini kabla viazi havijachipua watakavyopanda katika maeneo hayo mapya waruhusiwe kuvuna mihogo yao. Hii ikiwa ni wiki ya kupunguza majanga kama azimio la Umoja wa Mataifa linavyosema, tuanze na Nzasa. Mpaka serikali itakapotoa ushahidi wake ukawawekwa kwenye mizani wananchi hawa wana haki ya kulipwa fidia kama sheria ya Misitu (Cap. 389 K.f. 6(1) ( c ) inavyoelekeza lau imeona eneo lao la Nzasa linafaa kuwa Msitu. |
YALIYOMO
TAHARIRI Serikali iwahurumie wananchi wake KUCHOMWA MOTO NYUMBA ZA WANANCHI:
Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda
Mishikaki ya nguruwe Moshi yachomwa
mbele ya Msikiti
MAONI YETU:
Upimaji huu mpya ni wa nini
TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia
lengo
Makala:
Goda Muslim School, Manzese
Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu
Historia ya mgogoro wa Nzasa
DUMT watoa msaada kwa walioathirika
Nzasa
UCHOMAJI NYUMBA NZASA: Wafadhili
wana mchango gani?
Mafundisho ya Quran
|