AN-NUUR 
Na.171 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 16 - 22, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
MAONI YETU: 

Je; ni halali kuchoma Kidungu cha mtu? 

  • Naye akichoma hekalu je?
KUFUATIA kuchomwa nyumba za wananchi wa Nzasa, kauli nyingi zimetolewa na viongozi wa serikali. Wapo waliodai kwamba kuchomwa kwa nyumba hizo ni sawa na kufinywa tu. Lakini wapo waliodai kwamba si nyumba bali vidungu – yaani nyumba za kuhamia ndege au za kujihifadhi wakati wa kilimo. 

Kwa kauli hizi utata hakuna juu ya wananchi kuchomewa nyumba na nani kachoma. Lakini vipi mlalamikaji awe mshitaki, mwendesha mashitaka, hakimu, shahidi na mtoa adhabu! Pengine hapa wananchi wangetaka wapewe darsa; nini maana ya utawala wa Haki na Sheria. 

Tulikuwa na mashamba ya Taifa ya mkonge, ngano, kahawa, mpunga, mifugo n.k. Ilikuwepo GAPEX, R.T.C, KAMATA, UDA, UFI, Tanganyika Packers, viwanda kadhaa vya nguo na vingine vingi pamoja na mashirika ya umma. Nchi ilikuwa imenawiri. Leo baadhi ya watu wameifilisi nchi. Wametufikisha mahala wafadhili wanatushikia viuno kutupa amri. Wapo walionunua vivuko na ndege mbovu. Tume ya Warioba imetoa taarifa yake watu wakadai wahusika waadabishwe. Lakini kigugumizi kikaingia. Kumbe uwezo upo wa kuchukua hatua tena kwa operesheni ! Au ni kwa hawa tu wanyonge wa Nzasa ! Tungeelewa kama wananchi hawa wangevamiwa na maharamia wa Kisomali waliotishia amani huko Arusha hivi karibuni ! Lakini serikali yenyewe ! 

Huko nyuma nchi za Ulaya zilitulaumu kwamba nchi yetu haina demokrasia ya kweli kutokana na kuwa na chama kimoja cha siasa. Lakini mkoloni ana uso gani wa kutulaumu wakati alitutawala kwa mabavu? Kwa haya serikali iliyowafanyia wananchi wa Nzasa; itakuwa na uso gani wa kuwakemea wanaowaponda kwa mawe vibaka. Yawezekana isionekane tatizo sana kuchomwa moto kibaka anayepora kofia, heleni na mikufu. Je, siku wananchi wakipata bahati ya kuwapata wale ‘vibaka’ wa kweli wa nchi hii. Je, tutasemaje wananchi wakifundishika kuchoma hekalu la mvamizi wa kiwanja cha michezo ! 

Kuna hii kauli kwamba vilivyochomwa ni vidungu – vidungu vya muda shambani. Kama vilivyochomwa ni vidungasegu wananchi hawa waonyeshwe basi nyumba zao. Mbona vitanda vyao bado viko nje ! Mbona watoto na vikongwe bado wanakesha nje kwenye baridi. Vipi vilivyochomwa viwe ‘viota’ watu hawa wasirejee kwenye nyumba zao wakae nje na watoto wao kwa zaidi ya siku 14 sasa ! 

Tatizo hapa ni tafsiri. Ukitazama mahekalu ya wakubwa wanaotamka maneno haya, kweli vile vya Nzasa ni vibanda vya kulindia ndege. Lakini alaumiwe nani ? Miaka 37 ya kujitawala bado wananchi wanaishi kwenye viota?  

Je, hivi kilichowaponza watu wa Nzasa ni kuwa na nyumba za aina hiyo ? Mbona ndio hizi hizi tunazoombea msaada kwenye El-nino. Tukisema nyumba 2000 zimezolewa na mafuriko ndio hizo sio zile za Mbezi Beach na fedha tunapata kutoka kwa wafadhili. 

Hivi tumefikia mahali mahekalu ya Oysterbay na Mbezi ndio kigezo cha nyumba za wananchi ! Ikumbukwe kwamba si wote wanaojua inakouzwa almasi, dhahabu ya nchi yetu na nyara mbalimbali za serikali. Wala si wote wanaojua deni tunalowalipa wafadhili sasa na riba yake lilifanyia kazi gani. Wengi hatujui hayo kama ambavyo hatujui fedha na mali za mashirika ya Umma zilizamia wapi hata yakafilisika. Kwa hali hiyo ni lazima wengine wawe na vidunda. 

Lakini je, ni halali kuchoma kidungu cha mtu ? Na kama kufinya ndio huku, kuchoma moto ndio kupi ? 
  
Juu  
 

YALIYOMO 
 

 TAHARIRI 
Serikali iwahurumie wananchi wake 

KUCHOMWA MOTO NYUMBA ZA WANANCHI: Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda 
Na Mwandishi Wetu, Nzasa 

Mishikaki ya nguruwe Moshi yachomwa mbele ya Msikiti 
Na Mwandishi Wetu 

MAONI YETU: 
Je; ni halali kuchoma Kidungu cha mtu? 

Upimaji huu mpya ni wa nini 
Na Mwandishi Wetu 

TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI 

Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia lengo 
Na Bi. Zuhura Tajiri, Shinyanga 
 
Teknologia:
Jifunze kuunganisha Kompyuta
Na Hassan Omar

Makala:
Nani atakayewahoji Waheshimiwa hawa

Goda Muslim School, Manzese
Na Mwandishi Wetu

Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

Historia ya mgogoro wa Nzasa
Na Mwandishi Wetu

DUMT watoa msaada kwa walioathirika Nzasa
Na Mwandishi Wetu

UCHOMAJI NYUMBA NZASA: Wafadhili wana mchango gani?
Na Mwandishi Wetu

Mafundisho ya Quran 
Kutoa pasipo masimango 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe  

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita