|
|
| Teknologia:
Jifunze kuunganisha
Kompyuta
Na Hassan Omar KUNA njia kadhaa za kuweza kuunganisha kompyuta mbili au zaidi kulingana na haja inayotakikana. Kwenye makala hii tutaieleza njia ya rahisi ya kuunganisha kompyuta mbili ili mtumiaji wa kompyuta moja awe na uwezo wa kusoma na kunakili majalada yaliyomo kwenye kompyuta ya pili iliyounganishwa nayo. KOMPYUTA nyingi za zamani hazina kitu kinachoitwa CD-ROM drive. Hiyo ni ile sehemu unayoingizia CD (Compact Disk). Ukosefu huo ni maarufu kwa kompyuta za mikononi, yaani laptop, zilizonunuliwa miaka ya nyuma kidogo. Mtu anapotaka kuweka programu mpya kwenye kompyuta hizo mara nyingi anakabiliwa na tatizo moja. Tatizo lenyewe ni kuwa programu nyingi siku hizi zinawekwa kwenye CD. Na kama kompyuta haina CD-ROM drive, bila shaka haitaweza kuzisoma CD hizo, na kwa hivyo programu hizo zinashindikana kuwekwa kwenye kompyuta hizo. Makala hii inakusudia kueleza njia rahisi ya kukabiliana na tatizo kama hilo. Mtumiaji wa kompyuta pia anaweza kuwa na haja ya kunakili majalada kadhaa kutoka kwenye kompyuta moja kuingia kwenye kompyuta nyengine. Kama majadala hayo ni makubwa sana, kuyanakili kwenye diskette kutoka kwenye kompyuta moja na kuyaingiza kwenye kompyuta ya pili ni kazi inayochukua muda mrefu sana. Kama jalada ni kubwa zaidi ya nafasi iliyomo kwenye diskette, bila ya kutumia mbinu za kulibana jalada hilo au kulikata vipande vidogo vidogo, inashindikana kabisa kuliingiza kwenye kompyuta ya pili. Haja kama hii hutokezea kwa mfano mtu anaponunua kompyuta mpya na kutaka kuyahamisha majalada yaliyomo kwenye kompyuta ya zamani kuingia kwenye kompyuta mpya. Au anapotaka kuyahamisha majalada yaliyomo kwenye kompyuta ya aina ya laptop kuingia kwenye kompyuta ya kawaida ya mezani, yaani ya aina ya desktop. Inatarajiwa kuwa msomaji wa makala hii ataelewa jinsi ya kukabiliana na haja kama hiyo. Ikiwa unazo kompyuta mbili zinazotumia
Windows 95, unaweza kuziunganisha kompyuta hiyo kwa kutumia
programu iliyomo kwenye Windows 95, inayoitwa Direct
Cable Connection. Lakini kabla ya kuweza kuitumia programu hiyo
inabidi uwe na vifaa vinavyohitajika.
VIFAA VINAVYOHITAJIKA Kifaa pekee utakachokihitaji ni waya. Unaweza kutumia waya za aina mbili. Aina ya kwanza na inayopendelewa ni waya unaojuilikana kama parallel cable DB25 Male/Male. Huo ni waya unaochomekeka nyuma ya kompyuta sehemu ile ile unayochomeka waya wa printer. Waya huo una plagi mbili zilizo sawa sawa, moja kila ncha, na kila plagi ina pini 25. Unaweza kuununua waya wa namna hiyo kwenye maduka ya vifaa vya kompyuta na bei yake ni kama Sh. 5,000 kwa waya wa urefu wa futi 3. Kama hukubahatika kupata parallel cable, unaweza pia kutumia waya unaojuilikana kama null-modem serial cable Female/Female. Waya huu huchomekwa nyuma ya kompyuta ama kwenye sehemu inayowekwa mouse, au sehemu ya kuchomekwa modem ya nje. Kutegemeana na sehemu hiyo ilivyo, unaweza ama kuhitaji waya wa DB9, wenye plagi ya tundu 9 kila ncha, au DB25, wenye plagi ya tundu 25 kila ncha. Null-modem serial cable bei yake ni nafuu kidogo ukilinganisha na parallel cable, lakini ukiunganisha kompyuta kwa kutumia serial cable, unapopeleka majalada kutoka kwenye kompyuta moja kuingia kwenye kompyuta nyengine, majadala hayo hayaendi kwa kasi kubwa ukilinganisha na parallel cable. Kompyuta nyingi huwa na sehemu mbili
za kuchomekwa serial cable zinazojuilikana kama communication
ports na kupewa majina COM1 na COM2.
Kwenye COM1, mara nyingi huchomekwa mouse,
na kwenye COM2 unaweza kuchomeka modem ya nje.
Kama kompyuta ina communication port moja tu inayotumiwa
na mouse, basi mtu anapotaka kuunganisha kompyuta mbili za
namna hiyo ni lazima atumie parallel cable.
KUUNGANISHA KOMPYUTA MBILI Ukishakuwa na waya unaofaa, hatua ya kwanza ni kuuchomeka waya huo nyuma ya kompyuta zako mbili. Ukishaziunga kompyuta hizo, washa kompyuta zako kama kawaida. Kama unapowasha kompyuta zako kinatokeza kidirisha cha kukutaka uingize jina na password yako, ni lazima ufanye hivyo na kisha ubonyeze OK. Hatua ya pili ni kuyatayarisha majalada ya kompyuta moja ili yaweze kusomeka kutoka kwenye kompyuta ya pili. Kwa mfano, kama ninazo kompyuta mbili: Kompyuta A na Kompyuta B, (majina hasa ya kompyuta na Workgroup zao zinawekwa kwenye Start -> Settings -> Control Panel -> Network -> Identification) na Kompyuta A haina CD-ROM drive wakati Kompyuta B inayo CD-ROM drive, ikiwa nina haja ya kuweka programu kwenye Kompyuta A kwa kutumia CD iliyo kwenye CD-ROM drive ya Kompyuta B, basi itabidi niifanye CD-ROM drive ya Kompyuta B iweze kusomwa kutoka kwenye Kompyuta A. Hatua za kufuata ni kama ifuatavyo: 1. Ukiwa kwenye Kompyuta B, tumia My Computer au Windows Explorer, kuweza kuiona CD-ROM drive na ubonyeze juu yake kifungo cha kulia cha mouse. 2. Kwenye kidirisha kitakachojitokeza, chagua Properties, na kisha uingie kwenye sehemu ya Sharing. Kwenye sehemu hiyo, bonyeza mouse kwenye sehemu ya Shared As na ujaze sehemu ya Share Name na Comment kama unavyopenda. Picha 1 inaonyesha mfano wa jalada litakalotambulika kwa jina la F kutoka kwenye kompyuta ya pili. 3. Rudia hatua zilizotajwa hapo juu kwa kila jalada unalotaka liweze kusomwa kutoka kwenye kompyuta ya pili. Hatua inayofuata ni kuitayarisha Direct Cable Connection. KUITAYARISHA DIRECT CABLE CONNECTION Kama tulivyoeleza hapo juu, programu inayoitwa Direct Cable Connection ndiyo inayotumika kwenye Windows 95 kuunganisha kompyuta mbili kwa namna tuliyoileza hapo juu. Hatua za kuitayarisha programu hiyo ni kama zifuatazo. Ili kurahisisha maelezo haya, tutatumia mfano wa Kompyuta A na Kompyuta B kama tulivyozitaja hapo juu. Yaani Kompyuta A ndiyo yenye haja ya kusoma majalada ya Kompyuta B. 1. Ukiwa kwenye Kompyuta B bonyeza Start, kisha Programs, kisha Accessories, kisha Direct Cable Connection. Kama Direct Cable Connection haionekani, basi programu hiyo haikuwekwa kwenye kompyuta hiyo. Itabidi uiweke kwa kutumia diskette au CD za Windows 95 kwa kupitia Start -> Settings -> Control Panel -> Add/Remove Programs -> Windows Setup. Hakikisha Communications imechaguliwa, yaani kuna tiki kwenye kisanduku chake, na kwa kubonyeza Details, hakikisha pia Direct Cable Connection imechaguliwa. Baada ya hapo bonyeza OK na ufuate maagizo utakayopewa na kompyuta. 2. Ukishaianzisha Direct Cable Connection utapata kidirisha cha kukutaka uitayarishe programu hiyo. Kompyuta B utaifanya kama ni Host kwa kubonyeza sehemu ya Host kama inavyoonekana kwenye Picha 2. Ukibonyeza Next utapata mahali pa kuchagua port unayoitumia kulingana na aina ya waya ulioutumia. Kama umetumia parallel cable, port ya kuitumia itakuwa ni LPT1, na kama ni serial cable basi itakuwa ama ni COM1 au COM2 kutegemeana na kompyuta yako ilivyo. Cha muhimu ni kuwa ni lazima utumie port hiyo hiyo kwenye kompyuta zote mbili. Ukishachagua port bonyeza Next na hapo utakuwa umeshakamilisha kuifanya Kompyuta B kuwa Host. Usibonyeze Finish kwanza, mpaka utakapoifanya Kompyuta A kuwa Guest kwa kuanzisha Direct Cable Connection na kufuata taratibu kama zilivyoelezwa hapo juu isipokuwa kwenye kidirisha kinachoonyeshwa kwenye Picha 2 itabidi ubonyeze sehemu ya Guest. 3. Ukishafika hatua ya kubonyeza Finish, bonyeza Finish kwenye kidirisha cha Kompyuta B, kisha bonyeza Finish kwenye kidirisha cha Kompyuta A, na baada ya muda mfupi utaona kidirisha kitakachokuonesha kuwa kompyuta zako zimeunganishwa. Pia utaona kutoka kwenye Kompyuta A majadala yote ya Komputa B unayoweza kuyasoma. Unaweza pia kutoka kwenye Kompyuta A kuanzisha programu utakazoziona kwenye Kompyuta B. Kama kuna tatizo lolote, utapata taarifa ya kuwepo tatizo hilo na utaweza kulitatua tatizo hilo kwa kufuata maelezo yaliyo kwenye Help. |
YALIYOMO
TAHARIRI Serikali iwahurumie wananchi wake KUCHOMWA MOTO NYUMBA ZA WANANCHI:
Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda
Mishikaki ya nguruwe Moshi yachomwa
mbele ya Msikiti
MAONI YETU:
Upimaji huu mpya ni wa nini
TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia
lengo
Makala:
Goda Muslim School, Manzese
Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu
Historia ya mgogoro wa Nzasa
DUMT watoa msaada kwa walioathirika
Nzasa
UCHOMAJI NYUMBA NZASA: Wafadhili
wana mchango gani?
Mafundisho ya Quran
|