|
|
| Nani
atakayewahoji Waheshimiwa hawa?
Waamerika walio wanachama na wapenzi wa Republican halikadhalika na wale wa Chama Tawala Democratic, wanatafakari ni hatua zipi wachukue ili kumrudi Bill Clinton ambaye licha ya kujihusisha na ‘ngono haramu" ameliongopea Taifa hilo kwa miezi kadhaa kwamba yeye hakuwa na mahusiano ya kingono na Monica Lewinsky. Katika makala haya mtoa hoja binafsi angependa watanzania wajifunze utamaduni wa kuhoji kauli na matendo mbalimbali ya viongozi wao.... Izingatiwe kwamba hasira ya Waamerika dhidi ya Rais wao hivi sasa si kule kuiona ngono nje ya ndoa ni kosa la kimaadili kwani tangu hapo kwa mujibu wa Demokrasia yao, raia wa nchi hiyo ana uhuru "kutembea" apendavyo. Wao hasa wamekasirishwa na kule kuendelea kwake kusema uongo huku akiwa na dhamana nzito. Akiandika kuhusu mkasa huo, mwandishi maalum wa jarida la TIMES, Charles Krauthmmer, anaeleza, "hatimaye mwongo kabainika". Akiendelea mwandishi huyo anahoji katika makala yake kwa kusema ijaaliwe Kenn Starr hakuwa tayari kujiingiza katika mgogoro huu mgumu wa kutafuta vielelezo na ushahidi wa kimazingira, nani ambaye angekuwa na shaka juu ya "uaminifu" wa Clinton? Kwa hali hiyo Waamerika wengi hivi sasa wana mawazo tofauti tofauti na hasa wazo kwamba "Kama hakuwa mkweli kwa muda wote huo basi yapo mengi anayoyafanya kinyume cha utaratibu ambayo hatuyajui". Kwa sababu hiyo Waamerika huenda wakamrudi Rais huyo. Tukiweka kando kidogo sera za unafiki na ubeberu wa serikali ya Taifa hilo kubwa kwa mataifa mengine, Mkasa wa Bill na Monica umewajengea sifa fulani Waamerika. Ni vyema raia wa nchi nyingine kama hii yetu wakafungua macho sasa kuona kuwa Rais au kiongozi yeyote yule ni mwananchi sawa na wananchi wangine, ni mfanya kazi sawa na wafanyakazi wengine. Tofauti yake ni kule tu kupata ridhaa yao kupitia kura walizompigia kuwa msemaji au mwamuzi wa mwisho katika masuala ya kinchi kwa mujibu wa katiba. Hata hivyo naye kama ilivyo kwa raia yoyote yule hana uchochoo wa kuukwepa mkondo wa sheria inapobidi. Nimesema iwe mfano kwa nchi zetu hizi kwa sababu kumekuwa na kasumba ya kudhani nafasi ya urais au uongozi wowote wa juu wa serikali kana kwamba ni "dudu" la kuogofya, kamilifu, lisiloulizwa muda wa kuwepo kwake madarakani. Kwa fursa ya dhana hii potofu iliyojengwa na wengi, Rais na timu yake kudiriki kuwafanyia raia lolote watakalo na asitokee wa kuhoji. Katiba ambayo ingetarajiwa kuwa dira na mdhibiti wa mambo yote,huwa si lolote si chochote mbele ya wakubwa hao. Inaweza kusiginwa dhahiri shahiri kiutendaji na asiwepo wa kuhoji. Mahakama nazo kinyume na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba, zimekuwa kana kwamba kijakazi anayesubiri za bwanyeye. Linalozungumzwa na kiongozi serikalini huathiri utendaji wake, chambilecho cha Mrema "mahakama zifutwe". Tunaweza kurejea matukio kadhaa kulisemea jambo hilo. Imeshatokezea nchini hapa ngano kuchomwa kwa maelfu ya magunia licha ya kuwepo amri ya mahakama kusitisha zoezi hilo. Watanzania walihamasishwa wakahamasika kuwa ngano ile ni mbovu "ingehatarisha" afya zao, wakameza ndoano, kilichofuatia ngano kuchomwa chini ya usimamizi mkali wa jeshi. Hakuna aliyehoji. Si mahakama, mwenye ngano wala wananchi wengine. Sote hatukuona haja ya kuhoji yaliyofichwa katika suala lile hadi jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) "kugeuzwa" Halmashauri ya Jiji au polisi. Wakazi wa Ubungo hadi Kimara walibomolewa nyumba zao kwa idhilali kubwa huku ikidaiwa kwamba wakazi hao walishalipwa fidia toka mwaka 1972. Nadhani hata mkarandarasi alishangazwa na dai hilo, lakini kwa kuwa ni amri kutoka juu hata yeye alisita kufungua mdomo kwani angeliambiwa hayo ni mambo ya ndani ya nchi hana sababu ya kuyaingilia. Kwa watanzania wenyewe hakuna aliyethubutu kuhoji, na wale waliofikisha shauri hilo mahakamani waliambulia patupu. Hatujui hivi sasa mamia hao wako wapi. Wapo waliotoa hoja kuhalalisha unyama ule kwamba inapobidi "mkono wa chuma" kutumika ili "kuleta maendeleo" hatuna budi kufanya hivyo. Lakini ni maendeleo gani hayo tunayoambiwa; ni haya ya kushindwa hata kusambaza maji mijini, huduma mbovu za hospitali, elimu duni kwa vijana wetu, umeme wa mgao kila mwaka inapofikia kiangazi, au utitiri wa magari ya fahari kwa waheshimiwa wetu. Haya yalipofanyika Soweto chini ya ubaguzi wa rangi tulihamasishwa kuchangia ukombozi kusini mwa Afrika." Labda kwa moyo wa uzalendo kabisa niulize lini utaanza ujenzi wa barabara ile baada ya "mkono wa chuma" kuwaacha wengi wakiwa hawana hata mahali pa kujisetiri hivi sasa. Mwezi Februari mwaka huu, polisi walivunja katiba ya nchi na haki za binadamu kwa ujumla pale walipovamia jengo la ibada Msikiti wa Mwembechai wakadhalilisha wanawake, kuua na kujeruhi raia kadhaa; kisa, wanamtafuta Magezi na wenziwe wanaoendesha mihadhara ya kashfa dhidi ya dini nyingine. Wananchi walipolalamikia hatua hiyo ya kinyama viongozi walipuuza na wanaendelea kupuuza hadi hii leo. Wanachojiamini kikubwa ni ukweli kwamba kwani mtafanya nini? Wao ndio waliokamatia usukani. Limekuja hili la Nzasa watu kuchomewa nyumba zao kwa madai wamevamia msitu ulio chini ya hifadhi ya Taifa. Ni unyama usiosemeka. Ingawa haya ya Nzasa Wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam yanaingia katika rekodi ya matukio ya kuliza yaliyowahi kutokea nchi hii, lakini nini kitafuata kama si wananchi wale waliokuwa na makazi yao kusambaratika wasijue wapi wataishi kwa ndugu au jamaa. Na asiwepo mwenye kuwajali alie na moyo wa kusema hapana kama ilivyokuwa umasaini. Ni waswahili hao, ambao nadhani ni utamaduni wao kuishi kikondoo chini ya mazingira ya ukandamizaji! Wanamsemo wao usemao "yaliyopita si ndwele tugange yajayo". Haishangazi watu ni wasahaulifu kweli kweli kiasi upande wa kitenge, kanga, fulana, pilau au pesa kidogo zatosha kuwarubuni wanapohitajika. Labda linaloshangaza ni hii tabia ya viongozi kupata taabu ya kuyumbisha maneno. Inashangaza kwa sababu inachefua kuwasikia wakisema uongo hadharani kiasi cha kujidharaulisha wao wenyewe na Taifa kwa ujumla. Kwa lipi hasa wanalo hofia mpaka wautoe muhanga uheshimiwa wao ilihali wanaowaongoza idadi kubwa ndio hao wenzangu na mie. Zilipobomolewa nyumba za Ubungo na Kimara tuliambiwa wananchi wale walikataa kuhama licha ya kuwepo amri "halali" ya kuwataka wafanye hivyo. Lakini hatukuambiwa eneo lipi lilitengwa kwa ajili yao baada ya kuyahama makazi yao ya muda mrefu! Na kwa nini Halmashauri ya Jiji ilikuwa ikiendelea kugawa viwanja eneo hilo wakati ikifahamu kuwepo amri hiyo? Mwembechai, tuliambiwa kulikuwa na vurugu ambayo ingesababisha kuvunjika kwa amani ya nchi. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alitamba mbele ya waandishi wa habari "askari walikamata silaha msikitini ‘zilizothibitisha’ malengo mabaya waliyokuwa nayo vijana wale wakorofi". Ukweli ukajathibitika baadaye kuwa zile hazikuwa silaha kama ilivyodaiwa na mheshimiwa yule bali ni mambo zilizokuwa zikitumiwa na wahadhari kuwekea vipaza sauti! Hakuhojiwa Mheshimiwa kwa kauli yake, si na wananchi, wakuu wake wala vyombo vya habari. Waziri wa Mambo ya Ndani, ndani ya kikao cha Bunge la nchi hii alidai eti kilichowakasirisha polisi hadi kumpiga risasi mtoto Chuki ni kule kumkuta na makaratasi ya uchochezi. Mama wa mtoto huyo siku moja tu baada ya hotuba ya Waziri alikanusha dai hilo na kuonyesha upotofu wa kauli hiyo. Waziri hakuwa na la kusema baada ya majibu hayo. Nini kilifuatia ni tofauti kabisa na ilivyotokea kwa maseneta wa Baraza la Congress la Marekani dhidi ya Clinton. Waziri hakuhojiwa si na wabunge wala wananchi juu ya kusema kwake yasiyo sahihi katika kikao kizito kama kile! Hili la Nzasa linatia kichefuchefu zaidi kwa jinsi kauli za waheshimiwa zisivyo na haya, heshima wala huruma. Kulikoni kumwambia bi kizee wa miaka 65 aliyezaliwa pale Nzasa kwamba amevamia eneo lile! Kama ilivyokuwa kwa Mwembechai alitangulia
Mkuu wa Mkoa ambaye licha ya kuoneshwa nyaraka za mahakama alitoa vitisho
na kuahidi haya yaliyotokea. Ahadi imetimizwa, anasimama Waziri, tena mwanamama
kudai kuwa wananchi wale si wenyeji wa maeneo yale, wanatumiwa na wapasua
mbao na wachoma mkaa! Kweli Waziri anathubutu kutokusema ukweli kiasi hiki
tena mbele ya waandishi wa habari? Asiwepo mwenye moyo wa uzalendo
kusema sasa tumechoka kudanganywa kama watoto, viongozi wetu heshimuni
katiba na maadili ya uongozi, sio nyinyi mliotufunza "kusema kweli daima
fitina iwe mwiko?"
|
YALIYOMO
TAHARIRI
KUCHOMWA MOTO NYUMBA ZA WANANCHI:
Nzasa wamtaka Mkapa awaonyeshe pa kwenda
Mishikaki ya nguruwe Moshi yachomwa
mbele ya Msikiti
MAONI YETU:
Upimaji huu mpya ni wa nini
TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI Ndoa si lengo, ni wasila wa kufikia
lengo
Makala:
Goda Muslim School, Manzese
Utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu
Historia ya mgogoro wa Nzasa
DUMT watoa msaada kwa walioathirika
Nzasa
UCHOMAJI NYUMBA NZASA: Wafadhili
wana mchango gani?
Mafundisho ya Quran
|