|
|
| Fitna
ya Bakwata
IMEELEZWA kwamba Ijumaa Oktoba 16, askari Polisi wapatao kumi na nne waliovaa sare waliuzingira msikiti mkuu wa Ijumaa mjini Same kwa kile kilichodaiwa kutuliza fujo na kulinda amani. Pamoja nao walikuwepo askari wengine wanne wasio na sare pamoja na mkuu wa Kituo, Bw. Shomari ambao waliswali pamoja na waumini. Waumini ambao walifurika katika msikiti huo tayari kwa swala ya Ijumaa walishangaa kuona askari wakiwasili katika eneo hilo na kujibana katika sehemu tofauti tofauti. Pamoja na hali hiyo Ibada iliendelea kama kawaida na hatimaye Polisi hao kutawanyika bila kusema wala kufanya lolote. Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba askari hao walifika msikitini hapo kutokana na taarifa waliyopelekewa na Ofisi ya Bakwata kwamba pangetokea vurugu kutokana na maswala ya uchaguzi wa uongozi wa Msikiti. Uchunguzi zaidi umebaini kwamba mtu ambaye alijitaja kama Mwenyekiti wa Bakwata, Wilaya ya Same Oktoba 12, 1998 alimuandikia barua Mkuu wa Wilaya akidai kwamba kungekuwa na tukio la kuvunjika kwa amani ambalo lingesababishwa na baadhi ya waumini. Mwenyekiti huyo akiinakili barua hiyo No. BWS/ML/F.7/9/7 kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya alidai kwamba baadhi ya waumini walikuwa wamepanga kufanya uchaguzi wa msikiti kinyume cha katiba ya Bakwata. Kufuatia tukio hili la aina yake msikitini hapo, waumini wamekuwa na hisia na maoni tofuati. Hata hivyo takriban waumini wote walioongea na Mwandishi wa Habari hizi walisema kwamba kwa lolote ambalo lingetokea Polisi wasingekuwa wakulaumiwa kwani wao walikuwa wakitekeleza wajibu wao kwa mujibu wa taratibu zao za kazi. Kwa upande mwingine lawama kubwa imekuwa ikielekezwa kwa uongozi wa Bakwata kwa madai kwamba badala ya kujishughulisha na mambo ya kuwaletea maendeleo Waislamu pamoja na kujenga umoja na upendo miongoni mwao imekuwa ikiwafitinisha Waislamu na Serikali na kuleta faraka miongoni mwa Waislamu. Hata hivyo mama mmoja mtu mzima ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, aliongea kwa uchungu akidai kwamba wa kulaumiwa ni Waislamu wa Same wenyewe na wala si viongozi wa Bakwata. Akifafanua mama huyo alisema, miaka nenda miaka rudi, Waislamu wamekuwa na viongozi ambao ni mahiri sana kwa farka na fitna, halikadhalika weledi wa kuvunja hata zile juhudi ndogo wanazofanya Waislamu kujiletea maendeleo. Mama huyo aliyeonekana kuwa na majonzi alidai kwamba toka miaka ya 1970s wamekuwa wakiletwa waalimu na masheikh ili kuwa maimamu na kuwasomesha waumini waijue dini yao, lakini hakuna anayedumu. Alidai kuwa wamekuwa wakijengewa fitna na kufukuzwa huku maendeleo waliyoyaanzisha yakiachwa yaporomoke. Alisema kwamba pamoja na kwamba ni wengi wameshafukuzwa kwa fitna za viongozi lakini yeye binafsi waliomgusa sana kufukuzwa kwao ni watatu. Amewataja Masheikh hao kwa majina ya Sheikh Ramadhani Saiboko, Ustadh Thabit Othman na Ustaadh Atwaa Abdallah. Akifafanua alisema kwamba hawa ni Masheikh ambao lau si kwa fitna za viongozi wangeleta maendeleo makubwa sana. Alipotakiwa kufafanua juu ya dai la fitna ya viongozi mama huyo alitoa mfano wa Ustadh Thabit Othman ambaye alidai kwamba alifukuzwa kwa madai kwamba si ‘Rijali". Akitoa maelezo zaidi alisema kwamba Ustadh Othman alikuwa ndiye Khatibu wa kwanza kusoma khutba ya Ijumaa kwa Kiswahili Msikitini kwao. Hata hivyo akadai kwamba siku moja wakastukia wanatangaziwa na kiongozi mmoja wa Bakwata ambaye alimtaja kwa jina la Mwedadi Kiluvia; kwamba Imamu huyo anafukuzwa kwa vile si rijali jambo ambalo halikuwa kweli. "Viongozi wa namna hiyo ndio hao hao viongozi wa Waislamu wa Same toka miaka hiyo ya 1970 hadi leo. Sasa wa kulaumiwa nani kama sio Waislamu wenyewe wanaowafuga"; alihoji mama huyo kwa uchungu. Utafiti wa gazeti hili umebaini kwamba kwa vile Ustadh Thabit alikuwa hajaoa na kwa mujibu wa Uislamu alikuwa ametulizana.; baadhi ya viongozi wa Bakwata walimjengea dhana kwamba ana upungufu. Utafiti zaidi umebaini kwamba alipewa pesa msichana mmoja, Muuza Bar, ili amtie mtihanini Ustadh huyo. Alichofanya binti huyo ni kuingia ndani ya chumba cha Ustadh bila hodi na kufanya vitimbwi ambavyo vilimfanya Ustadh akikimbie chumba amwache binti huyo ndani. Binti huyo ambaye imeelezwa bado anaishi mjini Same akiwa mtu mzima na heshima zake sasa aliporejesha salamu kwa waliomtuma, ndipo likatolewa tangazo mbele ya mkutano wa Waislamu kwamba anafukuzwa kwa vile sio rijali. Katika kulifuatilia suala hili AN-NUUR ilifahamishwa kwamba Ustadh Thabit alijieleza kwa baadhi ya wazee kwamba yeye hajaoa kwavile masikini na yatima hivyo anafunga mara kwa mara kama Mtume (s.a.w.) alivyoagiza akisubiri Mwenyezi Mungu amjaalie cha kuolea. AN-NUUR imefahamishwa kwamba Mzee Ali Mshanga (marehemu sasa) alijitolea kumlipia mahari pamoja na gharama nyingine, akaoe. Kwa shani yake Allah imeelezwa kwamba mtoto aliyezaliwa akawa nakala halisi (photocopy) ya Ustadh Thabit jambo lililowafedhehesha sana viongozi wa Bakwata waliomfukuza uimamu. Nikutokana na maelezo haya mama huyo aliyeomba asitiriwe jina lake anasema kwamba wakulaumiwa si viongozi wenye fitna bali Waislamu wanaowafuga toka zama hizo mpaka leo. Kuhusiana na tukio hili la askari kuuzingira msikiti AN-NUUR iliwasiliana kwa simu na ofisi ya Kamanda wa Polisi mjini Same, hata hivyo msemaji ambaye hakutaja jina lake wala cheo chake alisema kwamba habari hizi aulizwe R.P.C . mjini Moshi. Hata hivyo juhudi za kumpata R.P.C. kwa njia ya simu hazikuweza kufanikiwa. Kwa upande mwingine AN-NUUR imegundua kwamba chanzo cha mgogoro wa sasa ni Bakwata kutaka kuweka uongozi wa msikiti bila ya kufuata katiba yake yenyewe. Hata hivyo juhudi za kuwapata viongozi wa Bakwata Mkoani Kilimanjaro
na Wilayani Same hazikuweza kufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wanawake Dodoma wataka mtoto aliyepigwa risasi akatibiwe nje Kesi za Mwembechai zaanza kusikilizwa Dondoo za saikolojia: Tuonavyo mambo Waraka wa Baraza Kuu kuhusu Parole Inawezekana kufanyika mdahalo kati
ya Waislamu na wasio Waislamu?
Teknologia
Serikali ihamie Dodoma kwanza !
Mahafali ya AMSIR Iringa
Bihawana Sekondari wafungua Ijumaa Vijana Shinyanga watakiwa
kuwa mfano mwema
Vyeo visiwasahaulishe majukumu
yenu- Sheikh Abri
Jiandaeni na kifo – Sheikh
Abdallah
Semina zawazindua wanawake
Bukoba
Waislamu wanaomaliza Kidato
cha Nne Tanga waaswa
Ndugu Kamuhabwa ndiye mwenye
chuki na AN-NUUR
'Ukombozi wa mwanamke si kugeuzwa
biashara huria'
Polisi walinda amani katika
muhadhara wa Wakristo
Mazengo wapewa uwanja wa
kujenga Msikiti
'Ajiengua Chuoni Z'bar kwa
kutoruhusiwa kuvaa hijab'
Shairi
|