|
|
| Tahariri
Kuangukia makaa hakuna nafuu kwa aliye kikaangoni NI vyema mtu unapoamua kufanya jambo ukalifanya kikamilifu ili kuepuka kujichanganya na kuwachanganya watu. Uking’ang’ania jambo lishike vizuri na sio kurukaruka kama panzi. Ipo historia na ushahidi wa Waislamu kudhulumiwa katika elimu, ajira na fursa za kushiriki katika sehemu mbalimbali za uongozi na utendaji wa Serikali yetu. Watu binafsi, taasisi na mabaraza ya Kiislamu yamekuwa kwa namna tofauti wakipigania kuondoka kwa dhulma hizi. Njia za Khotuba; mihadhara, uandishi wa makala na hata vitabu, zimekuwa zikitumiwa kuwasilisha hisia na madai ya Waislamu kwa mamlaka husika. Mfano ni Kitabu cha Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe. Ipo kadhia ya Mwembechai watu wameuliwa; wanawake wamedhalilishwa na wengine wametiwa vilema. Watu binafsi, jumuia za wananchi na zile za dini zimelizungumzia sana suala hili, lakini Tume haijaundwa wala waliohusika na mauaji hawajafikishwa mahakamani. Madhila yote haya Chama Tawala hakijafanya jambo lolote labda hili la Parole ambalo hata hivyo hatujui litaundwa vipi tena. Lakini hata likija kuundwa ovyo ovyo bado tunampongeza Mhe. Rais kwa kuiona dosari. Yapo matatizo ya wananchi wote kwa ujumla - kukithiri kwa rushwa, huduma mbovu za afya, maji na elimu; huku wakizidi kukamuliwa kodi. Vitendo vya polisi dhidi ya raia bila kujali sheria; Wafanyakazi kutolipwa mafao yao, sheria za kuzidi kuwakamua zaidi wananchi fedha kama ile ya "Tanzania Parking System."; kuchomewa moto nyumba wananchi wa Nzasa n.k. Yote haya ni matatizo yanayowakabili wananchi. Hata hivyo sisi tunadhani njia ya kuyamaliza matatizo haya na mengine sio kuwazuia watu kutoa maoni yao juu ya "White Paper". Hiyo itakuwa sawa na kuongeza dhulma. Kudhulumiwa halafu unaongeza dhulma kwa kujinyima haki yako ya kutoa maoni na kupiga kura. Kwa uzoefu, kutokutoa maoni au kutokupiga kura hakusadii kitu. Watu wamepiga kura na kura zao hawakuziona, sikwambii kutokupiga kabisa. Tunapozungumzia mazingira yetu ya Tanzania, unaposema siupi kura upande fulani, tafsiri ya kwanza ni kwamba huenda upo upande wenye afadhali. Lakini upigie upande gani wakati dhulma inaendelea dhidi ya wananchi na hatuoni ila maneno matupu. Juzi hapa wananchi wameuliwa Mwembechai, watoto wamedhulumiwa, wanawake wamenyanyaswa, nyumba za Ibada zimenajisiwa kinyume kabisa na sheria zote za kimataifa. Wazee vikongwe wameteswa magerezani kwa dhulma tu. Wananchi wamepiga kelele iundwe Tume japo kwa maslahi ya kisiasa, Chama Tawala na Serikali yake vimekataa. Vyama vinavyoitwa vya upinzani havipo kwenye madaraka kwamba vikishadidia kuundwa kwa Tume vitahatarisha maslahi yao ya kisiasa, lakini vimeshindwa hata kutoka nje ya Bunge kuonyesha hisia zao juu ya kadhia hii. Mwaka 1993 ulizuliwa uzushi juu ya Islam in Africa; uzushi uliokaribia kuilipua nchi kwa jinsi ulivyoshabikiwa na vyombo vya habari pamoja na wanasiasa. Hakikuwepo hata chama kimoja cha siasa ambacho kilitumia busara zake kuinusuru nchi na janga ambalo lingeletwa na uzushi ule wa "Nunda la Vichwa Viwili". Uzushi ule uliandamana na suala la OIC, bila ya kuzingatia ukweli na maslahi ya jambo lenyewe vyama vikatoa kauli nzito za kupinga Zanzibar kuingia O.I.C. Yote haya yanadhihirisha jambo moja muhimu. Waislamu hatuna mtetezi, hatuna msemaji. Kama ni kujitetea tujitetee wenyewe. Ingekuwa yupo wa kututetea basi ingekuwa CCM. Na hii ni kutokana na historia yake kwamba toka TANU Waislamu walishiriki uasisi wake na kujitolea mali zao na nafsi zao kuijenga na kuipa nguvu. Lakini imetufanya hivi. Vyama vingine vya siasa hamna kitu. Tunashindwa hata kuelewa vina agenda gani, baada ya ruzuku. Wananchi wana uchungu mkubwa wa kutaka Serikali nzuri yenye kujali watu; hata hivyo ni muhimu kuwa makini wasije toka kikaangoni wakaangukia makaa ya moto. Ni muhimu tuitumie vyema fursa hii ya Marekebisho ya Katiba kuhakikisha kwamba katiba ya nchi inatoa fursa kwa Waislamu kujitetea wenyewe. |
YALIYOMO
Wanawake Dodoma wataka mtoto aliyepigwa risasi akatibiwe nje Kesi za Mwembechai zaanza kusikilizwa Dondoo za saikolojia: Tuonavyo mambo Waraka wa Baraza Kuu kuhusu Parole Inawezekana kufanyika mdahalo kati
ya Waislamu na wasio Waislamu?
Teknologia
Serikali ihamie Dodoma kwanza !
Mahafali ya AMSIR Iringa
Bihawana Sekondari wafungua Ijumaa Vijana Shinyanga watakiwa
kuwa mfano mwema
Vyeo visiwasahaulishe majukumu
yenu- Sheikh Abri
Jiandaeni na kifo – Sheikh
Abdallah
Semina zawazindua wanawake
Bukoba
Waislamu wanaomaliza Kidato
cha Nne Tanga waaswa
Ndugu Kamuhabwa ndiye mwenye
chuki na AN-NUUR
'Ukombozi wa mwanamke si kugeuzwa
biashara huria'
Polisi walinda amani katika
muhadhara wa Wakristo
Mazengo wapewa uwanja wa
kujenga Msikiti
'Ajiengua Chuoni Z'bar kwa
kutoruhusiwa kuvaa hijab'
Shairi
|