|
|
| Maoni
Serikali inaWhite Paper:
Wananchi mna nini?
KATIKA makusudio ya kuunda Katiba huzaliwa serikali na vyombo vyake na namna ya kuendesha hiyo serikali, kama iwe ya kidemokrasia, kifalme n.k. Ingekuwa mazingira ya awali ingekuwa leo wananchi wakae wajadili wanataka serikali gani. Lakini leo tayari serikali ipo. Nayo imekuja na maoni yake ndio hii "White Paper". Ukitafakari sana mfano wa hii; mfano wake ni sawa na mtoto kusema tuwe na baba wa aina gani wakati mtoto mwenyewe ni zao la baba. Lakini pamoja na hayo leo tuna serikali na tusikae kana kwamba haipo. Bali serikali ipo naKatiba ipo ila inahitaji marekebisho. Lakini inarekebishwa na nani ? Hili ndio suala. Wenye Katiba ni wananchi; serikali ikichukua jukumu la kuirekebisha inamuwakilisha nani ? Ipo hoja kwamba "White Paper" ni zao la Bunge na Bunge linawawakilisha wananchi. Lakini Wabunge hawakuchaguliwa kuweka katiba mpya; bali kuongoza kwa katiba iliyopo. Hawakutumwa kuandika Katiba mpya wala kuiweka viraka. Kazi hiyo hawakutumwa na kama walitumwa kwanini sasa wananchi watakiwe kutoa maoni, kama ni kutoa maoni, basi wananchi wapewe jukwaa lao sahihi na kamili. Pamoja na kwamba katiba hii iliyopo inaonekana kuwa na upungufu mkubwa, lakini ina vifungu vingi tu vizuri ambavyo vingelinda haki, uhuru na usalama wa wananchi. Lakini vimekuwa vikivunjwa na vyombo vya dola na viongozi wake na kila wananchi wanapolalamika, serikali imeonekana kutowajali. Leo inawataka walete vifungu vipya ! Hapa ndipo penye wasiwasi. Mjomba kapewa hela ya dawa ya mgonjwa haikufika. Mgonjwa katutoka. Kapewa hela ya sanda kala. Leo baada ya kuanua tanga anataka kupewa usimamizi wa mirathi ! Hapana; ya tatu haramu. Lazima apatikane msimamizi mwingine. Huyu ni Bunge la Katiba. Huyu ndiye atajua shangazi apate nini, mjane asalie na kitu gani, halikadhalika haki ya watoto. Hatuwezi kupandia mgongoni kwako. Baba yetu, shangazi yetu, mjomba wetu, sawa lakini watu wana wasiwasi. Watu wanauliwa wazi wazi pale Mwembechai kwa amri ya "piga yule", "mwongeze". Wananchi wanasema walioua wafikishwe mahakamani hutaki. Wananchi wanasema, Tume ya uchunguzi iundwe ili ijulikane kama watu hawa walistahiki kuuliwa hutaki. Yote hayo hutaki. Wakati Katiba ya nchi inasema: "Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake; kwa mujibu wa sheria Kf. 14". Kwa kifungu hicho ni hitajio la sheria na wajibu muuaji yeyote afikishwe mahakamani aeleze sababu za msingi za kuhalalisha kutoa uhai wa mwananchi. Ndio maana wananchi wanasema walioua Mwembechai wafikishwe mahakamani. Hutaki ! Kisha unawaambia leteni maoni yenu juu ya namna nitakavyolinda uhai wenu ! Katiba iliyopo inalinda na kuheshimu utu na heshima ya wanawake na kila mtu. Leo wanawake wanasema tumenyanyaswa, tumedhalilishwa, tumevuliwa nguo na kupekuliwa na wanaume. Wanadai Tume iundwe, wahusika wapelekwe mahakamani. Kilio chao hakisikilizwi wala kuonekana ila wanatakiwa waione "White Paper" na watoe maoni yao jinsi utakavyoboreshwa utu wao, heshima yao na kuondoa unyanyasaji wa wanawake ! Walioamrisha "ua" ndio wale wale walishika misahafu na kuapa kuilinda Katiba ya nchi. Hapo ndipo wasiwasi wetu ulipo. Tutoe maoni yetu huko yatafika ? Dawa haikufika mgonjwa kafa. Hatuna ugomvi wala uhasama. Ni baba yetu sawa, na yule aliyekufa ni ndugu yetu. Lakini hatuwezi kumpa usimamizi wa kugawa mirathi aliyehini hela ya sanda. Hakuna ugomvi katika sera ya kugawa maeneo ya kuchimba madini kwa wawekezaji Wazungu. Lakini hii haijumuishi kuwafukia wananchi uliowakuta ndani ya machimbo. Wananchi walilalamika hapa kwamba katika maeneo fulani fulani ndugu zao wamefukiwa. Sio kwa mafuriko kama kule Miererani lakini katika zoezi la kuwafukuza katika eneo lililogawiwa mwekezaji. Serikali ilipuuza kwamba hakukuwa na tukio kama hilo. Lakini si mfukue basi ili waonekane waongo ? Leo huyo anayelalamika kwamba ndugu yake kafukiwa na kufukua marufuku; imani kwamba maoni yake yatafika itatoka wapi ? Wananchi ni jukumu lao kulipa kodi, lakini vipi leo iwe ‘uhaini’ nikihoji ilivyotumika ? Hawa wananchi wa Arumeru, Tanga na kwingineko wanaonekana ‘wahaini’ kwa kuhoji matumizi ya kodi zao. Vipi wasidhani kwamba wataonekana ‘wahaini’ kama watadai kuongezwe kipengele ndani ya Katiba cha kuwawajibisha viongozi wanaohini kodi zao ? Vipi wasidhani kwamba maoni kama hayo hayatofika kunakohusika ! Katiba ya nchi inawapa wananchi haki ya kuwakilishwa. Kuwapora haki hiyo ni uvunjaji wa Katiba. Hata kama ujenzi wa ukuta kuzunguka Mnazi Mmoja wananchi wangefurahi, lakini wawakilishi wao wangekuwepo, wangejadili lipi litangulie. Wangejadili umuhimu wa kuongeza vitanda katika hospitali ya Mwananyamala wagonjwa wasilale chini kabla ya kujenga ukuta. Pengine wangejadili na kutoa kipaumbele kununua "gloves" kwanza za wauguzi (manesi) na pengine wangetizama kwanza uboreshaji huduma za afya, maji safi na kusafisha mifereji michafu ili kupunguza milipuko ya kipindupindu. Wananchi hawa walionyimwa uwakilishi wao wa halali, kuwa na madiwani wao; kitu gani kitawahamasisha kuamini kwamba maoni yao yatasikilizwa ? Katika suala la Nzasa/Kazimzumbwi, iwe vyovyote iwavyo na iwe kwamba haja ilikuwepo wananchi wale kuondoka, bado haki ya kujadiliana nao namna ya kuondoka ilikuwepo. Ndio maana walipeleka maombi yao kutaka kukutana na viongozi mbalimbali. Wajadiliane, wasikilizwe sio wapewe agizo na waamriwe tu. Na lengo halikuwa kugoma kuondoka, lakini wakiondoka waende wapi, wataanzaje maisha mapya, vipi mazao yao, n.k. Fursa hiyo hawakupewa, wakamwagiwa petroli nyumba zao na kupigwa kiberiti. Vyote vilivyomo ndani vikaungua pamoja na kaniki za wake zao. Leo na kesho wewe huyo huyo unakuja na "White Paper" unawataka wakupe maoni yao namna utakavyolinda heshima yao, mali yao na uhai wao ! Jana umewaona wao mijusi, na nyumba zao vidunda hawana wanalostahiki ila kukatwa mkia. Leo wao wakupe maoni yao jinsi utakavyolinda ubinadamu wao, utu wao na mali yao ! Tunayasema yote haya sio kujenga chuki, lakini ni mjomba wetu tunayemnyima haki ya kusimamia mirathi. Mchango wa sanda hakufikisha, ndugu tumechanga upya . Tumezika. Hatumkatai; bado yeye mjomba wetu na katika kikao cha kugawa mirathi naye yumo tutakaa naye, lakini hatumkabidhi mali agawe. Tupeni jukwaa wananchi katika vikundi na taasisi zetu mbalimbali – NGOs, taasisi za kidini, vyama vya siasa, Kamaka, AFORD (Seneta Miselya) n.k wapewe fursa kusimamisha majukwaa yao watoe maoni na mapendekezo yao; na wasilazimishwe kupitia "White Paper". Serikali itambue haki yao hii. Waachiwe haki yao na uhuru wao wa kusimamisha majukwaa ya kutoa maoni yao. Utaratibu huu ni lazima mwishowe jukwaa la majumuisho yote lipatikane. Iwepo sekretarieti sio hii ya serikali; ya kupokea maoni kwa niaba ya Bunge la Katiba hadi hapo litakapoundwa. Serikali ipeleke maoni yake (White Paper) huko na wengine nao wapeleke mapendekezo yao huko. Lakini leo na kesho isijesemwa Bunge hili ndio limekaa kama Bunge la Katiba. Hawakutumwa kazi hiyo. Wananchi wapewe fursa na haki yao kutoa maoni juu ya kuundwa kwa Bunge la Katiba. Katika suala la kuhamia Dodoma mkusanya maoni alikuwa serikali na mtoa majumuisho ya maoni ya wananchi alikuwa serikali. Ikasemwa wananchi wengi wameona umuhimu wa kwenda Dodoma, lakini wana hofu gharama. Zaidi ya miaka 20 sasa makao hayajahama na mamilioni ya fedha yashaangamia. Wasipuuze wananchi kuandaa maoni yao vya kutosha kwa kadri ya hali wanavyoona wao. Bora wakusanye maoni yao wapiganie maoni yao kupuuzwa. Kukaa kimya si dawa. Pale wananchi wanapodhulumiwa pengine Katiba haisemi anayedhulumu afanywe nini. Wananchi wanahisi hawawakilishwi na kutetewa kikamilifu kwa vile labda Wabunge wamekuwa wawakilishi na watetezi wa misimamo ya maslahi ya vyama vyao. Labda moja ya sababu inayowafanya Wabunge wasiwe karibu na wapiga kura wao ila wanaporudi kuomba tena kura ni kwa vile wananchi wakishachagua, Katiba haiwaelezi ‘wachomoe’ vipi kura zao. Zamani demokrasia ilikuwa nzuri. Wananchi walikuwa wakiwafukuza waganga wa mvua kiangazi kinavyozidi. Leo Mbunge akishaingia Bungeni basi, haendi kwa wananchi ila kuhamasisha kodi au kutembeza "White Paper". Katika hali hii ambapo madeni ya serikali yamezidi pato la nchi likizamishwa katika kulipa riba za I.M.F huku huduma za kijamii na kiuchumi zikizidi kudidimia. Katika hali hii ambapo nchi imegeuzwa soko na jaa la bidhaa za kila mwekezaji na mzalishaji toka Ulaya na Asia. Katika hali hii ambapo mafao ya wafanyakazi imekuwa ni tatizo, ajira za waalimu wa skuli za msingi na mishahara yao imekuwa ni ‘bidhaa adimu’ ya kutolewa kwenye duka la kaya. Katika hali hii ambapo Utamaduni wa Mtanzania haujulikani kama ni wa kuvaa lubega ‘mini sketi’, wanaume kuvaa hereni na vidani, ndombolo au charanga. Katika hali hii ambapo wauguzi na madaktari wanaowahudumia wagonjwa na akina mama wanaojifungua hawana ‘gloves’ wala vifaa vingine muhimu, lakini maafisa serikalini, wabunge hata wale wa majimbo ya mijini kwenye barabara za lami hupewa magari mazito mazito ya gharama kubwa yenye kufaa barabara za vijijini. Katika hali hii ambapo pamoja na ukimwi kuchukua ushuru wa roho za watu kila uchao lakini wengine huhamasisha zinaa salama. Katika hali hii ambapo nchi nzima katika sehemu ya Muungano, imegeuzwa hoteli ya Kitalii. Ama mwananchi atakuwa mhudumu (weita) akimsubiri mtalii, kumchezea ngoma; amuuzie huduma yoyote na ‘mapenzi huria’ akimfurahisha mtalii. Kama wapo watu wenye mfumo wa maisha, itikadi. sera na mipango yenye kutuepusha na yote haya ni lazima wapewe fursa. Kila mtu apewe fursa atoe ‘modeli’ yake. Kama akitokea mtu kwa mfano akisema kwamba kila mwezi Desemba atachinja kondoo mweusi njia panda, ili kuondoa mabalaa, ajali zipungue barabara ya ‘Morogoro Road’ apewe fursa. Wananchi wataamua katika kura Ikiwa kitatokea chama cha siasa ambacho kinaamini kuwa namna pekee ya kuleta haki na ustawi katika nchi yetu ni kuleta ufalme wa Mwenyezi Mungu duniani kama alivyopendekeza mwanachuoni mkubwa wa Kanisa Katoliki, St. Augustine, chama hicho lazima kipewe fursa na uhuru wa kuzieleza sera zake kwa wananchi ili wananchi wakishawishika wakipe idhini ya kuongoza nchi. Halikadhalika endapo kitatokea chama kitakachokuwa na
msimamo kama ule wa Montesquieu (1689 - 1755) ambao unatofautiana sana
na ule wa St. Augustine, Katiba yetu lazima itoe uhuru na haki kwa chama
hicho kuelezea sera zake.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wasomi watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga Akina mama watakiwa kushikamana na dini yao Maoni
Dondoo
za Saikolojia: Hoja kengeza
Makala ya mtangazaji
Makala
Tanzania
tuna sera gani kuhusu kanda
Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 2
Teknologia
Makala na habari
Mwinyimkuu
kufanya sensa ya waumini Magomeni
Wazazi
Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab
Tuwaige
Wangazija, 'tutafanikiwa'
Serikali
imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim
Muhadhara
waunguruma Geita
Fuateni
Sharia ya Allah - Sheikh
Wanawake wa Kiislamu Mburahati wahimizwa kutafuta elimu Mafunzo
ya Qur'an
Chakula na lishe
|