|
|
|
JAPO kifungu cha 13(4) cha katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinapiga marufuku ubaguzi wa aina yoyote ile. Na japo kifungu cha 13(5) kinatoa ufafanuzi wa neno ubaguzi bado wapo Watanzania ambao wamebaguliwa na wanaendelea kubaguliwa na mamlaka mbali mbali hadi leo. Baadhi ya vigezo vinavyotumika katika ubaguzi ni dini, jinsia, kabila, rangi na mahali mtu anapotoka. Maeneo yaliyokithiri kwa ubaguzi ni elimu, mfumo wa mahakama na sheria, madaraka serikalini na katika mashirika ya umma n.k. Ni bahati mbaya kwamba mtu anapobaguliwa katika elimu athari ya ubaguzi huo inajitokeza katika nyanja nyingine zote za maisha yake kama vile madaraka, kupata haki, uchumi na uhuru wa mtu kutekeleza imani yake iwe ya dini au ya kisiasa. Kwa kujua hili wataalamu wengi wa elimu wamekuwa wakiionya serikali kuwa endapo hapatachukuliwa hatua za makusudi za kurekebisha hali ya uwiano mbaya iliyopo katika mashule, vyuo na vyuo vikuu basi kuna hatari kutokea kwa machafuko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi: (Taz. G.Malekela: Papers in Education and Development 1995:66). Akizungumzia uwiano mbaya uliopo katika mfumo wa elimu hapa Tanzania baina ya wanafunzi Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Bwana Joel Sanoff ameshangazwa na sera za elimu yetu ambazo hazizingatii kabisa tatizo la uwiano mbaya miongoni mwa watu wake: (Taz: Comperative Educational Review 1987 Vol. 31 No. 3 Pp. 335). Katika kutilia mkazo udhaifu wa sera zetu za elimu katika kurekebisha uwiano mbaya, Uk. wa 334 wa Jarida hili Bwana Joel anasema, sera za Tanzania zinalenga mikoa tu na wala siyo makundi mengine ya watu kama vile dini jinsia, rangi na matabaka. Msomi mwingine Bwana Abel Ishumi (Profesa) yeye amedokeza kwamba mfumo wa elimu wa Kikoloni ambao Tanzania imerithi utaleta athari kubwa sana katika suala zina la mgawanyo wa elimu na madaraka kwa Watanzania kwa siku za mbeleni. (Taz. Education and Social Change 1980:208). Miaka 37 sasa tangu Tanzania imepata uhuru, ndoto za watu wengi kuwa yangetokea marekebisho muhimu ya kisera yatakayoleta uwiano mzuri katika kupata elimu na hatimaye kugawana maradaka kwa uwiano muafaka (equity) zimetoweka. (Tazama kitabu cha Aboud Jumbe Mwinyi, the Partnership: 1994:122). Hata hivyo kuna matumaini mapya ambayo yameanza kujitokeza. Ni vigumu kufahamu kwa uhakika nguvu zilizoko nyuma ya matumaini haya ambazo zinaonekana kushinda hata hoja zilizotolewa na wasomi asili yake nini. Hata hivyo huenda vyama visivyo vya kiserikali (NGO) na mashirika ya misaada ya kimataifa yakawa na nafasi kubwa hapa ya kutoa shinikizo. Matumaini yenyewe ni kwamba moja ya makundi ya watu ambao wamekuwa wakibaguliwa katika mfumo wetu wa elimu kilio chao kimeanza kusikika. Hawa ni wanawake. Matumaini haya yaliwekwa wazi na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Mathew Luhanga tarehe 22/10/1998. Profesa Luhanga alikuwa akifungua kongamano la viongozi wa Juu wa Chuo Kikuu lililofanyika tarehe 22-23 Octoba, 1998. Kongamano hili lilikuwa juu ya kuwa makini katika masula ya kijinsia (Gender Sensitization). Katika hotuba yake Profesa Luhanga alisema kuwa, Chuo Kikuu kimeazimia kwa makusudi kabisa kurekebisha uwiano mbaya uliopo wa kijinsia kwa ujumla na hasa katika taasisi za elimu ya juu. Lengo letu (target) ni kufikia asilimia 50/50 kwa wanafunzi watakaoingia chuo kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2000. Hata hivyo Profesa alibainisha changamoto kuu inayowakabili Watanzania kuwa ni:- - Kujenga mfumo wa elimu ambao kila mtu anaweza kusonga mbele bila kujali jinsia yake mradi tu anao uwezo wa kiakili. Hatua hii ni njema kwa vile dhamira ni kuwapa wanawake haki kama raia wengine. Ni wazi kwamba matatizo ya wanawake kama vikundi vingine vyovyote vinavyobaguliwa yanahitaji mabadiliko makubwa ya kisera yenye mtazamo wa kitaifa zaidi kuliko ule wa kitaasisi. Hivyo basi wakati kila mwenye nia njema analazimika kuunga mkono hatua zozote zenye kuondoa ubaguzi, ni vyema pia kuwa huru kutoa maoni juu ya hatua bora zaidi za utekelezaji. Dhana ya 50/50 ifikapo mwaka 2000 baina ya wanaume na wanawake watakaoingia Chuo Kikuu inahitaji kutazamwa kwa makini. Kwanza si kweli kwamba kuingiza wanafunzi kwa kigezo hiki ni kutenda haki. Na pili chuo kikuu hakiwezi kwenda kwa dhana za usawa (equality) bali kinawajibika kujenga dhana ya uadilifu (equity) ambayo ndiyo inayotekelezeka:- Ubaya wa dhana ya usawa hapa ni kuwa:- (1) Unapoweka lengo la 50/50 maana yake ni kuwa idadi ya wanawake na wanaume iko sawa. Kitu ambacho siyo kweli. (2) Watanzania wanaume walio na sifa za kuingia chuoni ni sawa na ile ya wanawake au itakuwa sawa itakapofika mwaka 2000. Kitu ambacho pia ni uongo. (3) Kila mtu mwenye sifa ya kuingia chuo kikuu ataweza kufanya hivyo. Jambo hili siyo kweli kwani kadri tunavyokwenda mbele ndivyo mfumo wa elimu unavyozidi kubinafsishwa na hivyo aina na ubora wa elimu pamoja na kiwango chake utategemea zaidi uwezo wa mwananchi kifedha Kwa hali ilivyo sasa lengo hili la 50/50 halitaweza kufikiwa bila kuwanyima vijana wa kiume wenye sifa za kujiunga na chuo kikuu nafasi na kuwaleta chuoni wanafunzi wanawake wasiyo na sifa za kufanya hivyo. Kwa kuzingatia hili, Profesa Luhanga katika hotuba yake amegusia jambo hili kwa kusema, "our affirmative actions should not sacrifice academic standards, and this is one of the challenges we have to grapple with." Swali hapa ni kwa jinsi gani tutawaleta chuoni watu wasio na sifa bila kuathiri kiwango cha elimu. Katika hotuba ya Rais Mkapa Bungeni tarehe 04/11/98 kuhusu elimu alisema, "ni wazi kuwa hatuwezi kuwataka walio mbele wawasubiri wale walio nyuma.....". Mtaalam mmoja wa elimu Bwana Court. D anasema kuwa, "mafanikio ya haraka katika kurekebisha uwiano mbaya katika mfumo wa elimu ni lazima kuweka mikakati ya kudumu ya makusudi kabisa ya kuwabagua wale waliofaidika na mfumo wa kibaguzi na kuwapendelea wale walioathirika (Tazama Journal of Modern African Studies Vol: 14 pp.672 of 1976). Kwa ufupi Profesa anasema ongeza wanawake lakini ubora wa elimu ubakie pale pale. Raisi anasema wale walio nyuma wakimbie. Bwana Court anasema wale waliofaidi ubaguzi nao wabaguliwe. Ni wajibu wa viongozi wa Chuo Kikuu kuzichambua raia na hoja hizi. Ni vyema pia kubainisha ubaya wa nne wa dhana ya usawa (equality) miongoni mwa wanawake. Hili si jingine bali ni kujenga dhana kuwa wanawake ni watu dhaifu hivyo hawawezi kushindana iwe ni shuleni, siasa au uongozi, bali wanastahili kupendelewa. Dhana hii ni mbaya zaidi kwani itawajengea wanawake mazingira ya kudharauliwa na kusimangwa. Vidokezo vifuatavyo kuhusu hali ya wanawake kitaaluma vitasaidia kubainisha kazi iliyo mbele yetu ya kutimiza nia nzuri ya kuondoa dhuluma ya kubaguliwa kwa wanawake. 1.0 Matokeo ya mitihani ya wasichana kidato cha nne miaka ya 1995 na
1996.
Kwa ujumla kwa daraja la "O" na la 4 kila wanafunzi wasichana 100 waliofanya mtihani 85 wako katika daraja hili. Kwa hali ya kawaida hawa hawafikii sifa za kujiunga na kidato cha tano. Kwa mwaka wa 1996 wanafunzi wanawake 88 kati ya kila wanafunzi 100 waliofanya mtihani waliangukia madaraja ya Ona "4'. Katika masomo yale ya sayansi pamoja na hesabu hali yao pia ni ya kutisha. Tukiangalia kwa miaka hii miwili (1995 na 1996) asilimia za wanafunzi wakike walioangukia kwenye madaraja ya sifuri na nne ni kama ifuatavyo:- Hisabati 95.7% (1995) na 98.5% (1996)
Inatisha zaidi iwapo utafahamu idadi ya wale wasichana walioshindwa kabisa mitihani yao. Yaani waliopata "F. Hisabati 83.0% (1995) na 89.4% (1996)
Unapoambiwa kila wanafunzi 100 waliofanya mtihani wa hesabu (1996), wanafunzi 89 walishindwa, katika biolojia 79, kemia 77 na fizikia 61 walishindwa, halafu ukawa unatakiwa mwaka 2000 idadi yao iwe sawa na ile ya wanaume katika vitivo vya sayansi na uhandisi bila shaka unaweza kukadiria ugumu wa kazi iliyo mbele yako. Ni maoni yangu kuwa dhana ya 50/50 katika vyuo vikuu itatoa mchango mdogo sana katika kazi kubwa ya kuondoa ubaguzi kwa wanawake. Wanawake wanahitaji mfumo huria unaotiliwa nguvu na mfumo wa kisiasa na kiuchumi ambao umeondokana na vikwazo vya kijamii na kiutamaduni vinavyowabagua. Wale wanaoshindwa kwenda shule waende shule, wale waliopo shuleni wafaulu ili waingie vyuo vya elimu ya juu kwa ushindani na siyo kwa upendeleo. Hata hivyo ni jambo la kushukuru kuwa kilio cha wanawake ambao ni kundi lililokuwa likibaguliwa limepata wa kukijali. Kama nilivyokwisha kusema awali siyo wanawake tu wanaokumbana na tatizo la ubaguzi. Yapo makundi mengine ya watu. Kuna ubaguzi mkubwa wa kidini hapa Tanzania. Yapo mathehebu ya dini ambayo yameshajitangazia wazi kufaidika na mfumo wa utawala uliokuwepo tangu 1954 hadi 1995, bila shaka hadi hivi sasa. Lakini wapo ambao hata kwenye bodi za parole hawaonekani na wakubwa wanadai eti hawapo wenye sifa. Je ni lini kilio chao nao kitasikilizwa hata japo na taasisi za elimu ya juu tu? Waislamu wa Tanzania wamebaguliwa sana katika suala la elimu. Kama walivyo wanawake kuwa ni wachache miongoni mwa wanafunzi na pia miongoni mwa viongozi wa ngazi mbalimbali katika taasisi za elimu ya juu ndivyo walivyo Waislamu. Rejea Luhanga anaamini kuwa ubaguzi wa wanawake katika mfumo wa elimu ni kinyume na haki za binadamu na kuwa ubaguzi huu unalinyima taifa nguvu kazi ya wanawake, sijui ikiwa atashauriwa na kuuona ukweli kuhusu kubaguliwa kwa Waislamu atakuwa na lipi la kusema. Ni vyema ikafahamika kuwa wanawake Waislamu wanabaguliwa mara mbili. Wanabaguliwa kwanza kama wanawake na halafu kama Waislamu. Zipo tetesi kwamba imekuwa ni vigumu kwa wanawake wa Kiislamu kupata ufadhili wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayopitishia fedha zake Chuo Kikuu cha Dar es Salaama. Ugumu unaongezeka zaidi pale mhusika anapokuwa na mavazi ya Kiislamu. Watanzania wengine wanabaguliwa kutokana na makabila yao au mikoa wanayotoka. Pia ubaguzi unagusa kwa kiasi fulani tabaka la mtu. Hili linaweza kuonekana zaidi linapokuja suala la kwenda kusoma nje kwa fedha za Serikali. Mwisho kama wazo la kuondoa ubaguzi kwa wanawake ni zao la Watanzania
wenyewe basi ni vyema wigo ukapanuka ili kuhakikisha kuwa wote waliokuwa
wanabaguliwa ifikapo mwaka 2000 hawatabaguliwa tena. Kwangu mimi la msingi
ni kujenga mfumo ambao watu wote watakuwa huru kutoka hatua moja kuingia
nyingine.
|
YALIYOMO
TAHARIRI Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha Serikali
yakumbushwa kujiunga OIC
Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi Wafungwa waomba Futari na Vikoi Macho
ya shutuma
Hoja
pofu
Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 'Vichupi'
vya nini Kimiti?
Mjadala
wa Katiba na haki za Waislamu
Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 3
Waliochukuliwa
utumwa Uarabuni
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4)
Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga Mafunzo
ya Qur'an
|