|
|
|
AKIMKABIDHI bendera ya Taifa kwa mwakilishi wa Tanzania katika michuano ya Dunia ya urembo mwaka huu, Bi. Basila Mwanukuzi, Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Mheshimiwa Paul Kimiti alisisitiza waandaji wa Tanzania lazima wazingatie vigezo vya kimataifa katika mashindano ya kumpata mrembo wa Tanzania kwa maana hiyo vazi la kuogelea maarufu kwa jina la ‘vichupi; haliepukiki. Waziri Kimiti alijenga hoja kwamba hakuna sababu ya kushiriki mashindano ya urembo ya dunia iwapo wawakilishi wetu hawaandaliwi kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa. Watakuwa wanashindwa tu. Kwa sababu hawa kauzoea kutoka kwenye halaiki ya watu na vazi la kuogelea (vichupi). Kwa mantiki hiyo, Mheshimiwa Waziri Kimiti aliwahamasisha waandaji wa "Miss Tanzania" na umma wa Watanzania kwa ujumla kulirejesha tena vazi hilo la aibu katika mashindano ya urembo ya "Miss Tanzania". Mheshimiwa Waziri Kimiti pia aliwasisitiza wazazi waache tabia ya kuwakataza mabinti zao kushiriki mashindano ya urembo kwa kudhani kufanya hivyo ni uhuni. Alisema wao waliosoma na waliopita pita nje wanaona ni jambo la kawaida. Lakini wenye upeo mdogo wa elimu na fikra duni ndiyo tatizo. Hata hivyo taratibu wataelewa shabaha na madhumuni hasa ya mashindano haya. Wafurukutwa wa mashindano haya wameipokea kauli ya Waziri Kimiti kama changamoto inayojenga mazingira mazuri ya kurejeshwa kwa vazi la ‘vichupi’ katika mashindano ya urembo. Wanadhani waziri ametoa hoja nzito na yenye mantiki kuhusiana na sababu za kurejeshwa kwa vazi hilo. Eti ! Kwa sababu mashindano ya kimataifa yanaruhusu ‘vichupi’ basi na sisi lazima turuhusu huku kwetu kama tunataka kushiriki mashindano ya dunia. Waziri hakujibu hoja kwanini tuendelee kushiriki mashindano ya aibu kama haya ? Kwani tukikataa kushiriki ‘Miss World’ tutakuwa tumekiuka katiba ya nchi au tutavunja tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu ? Kwa nini iwe lazima kushiriki mashindano ya dunia ili dada zetu wavae ‘vichupi’? Kwani ‘vichupi’ .Vilizuiliwa kwa sababu tulikuwa hatushiriki mashindano ya kimataifa ? Kushiriki mashindano ya dunia si pasipoti ya kuvalia ‘vichupi’ kwa sababu ‘vichupi’ vilipigwa marufuku kwa hoja za kimaadili. Wapinzani wa mashindano ya urembo wanatoa hoja madhubuti na yenye kueleweka kwanini mashindano haya yasipigwe marufuku ? Kwani yanamdhalilisha mwanamke; hoja ambayo hakuna anayeweza kuipinga. Ni dhulma kubwa sana kuwatumia wasichana kama vyombo vya kuwastarehesha wanaume wenye tabia mbaya ya ‘kukodolea’ macho maungo ya siri ya wanawake wasiowahusu. Vile vile ni udhalilishaji ulioje kuwatumia wasichana walio uchi katika matangazo ya biashara ! Kama huu si udhalilishaji wa wanawake basi udhalilishaji maana yake nini ? Halafu mashindano haya yanasaidia sana kuua utumaduni wetu na maadili ya taifa kwa ujumla. Mmomonyoko mkubwa wa maadili ulioikumba jamii yetu unachangiwa kwa kiasi fulani na mashindano ya namna hii. Hakuna hata taifa moja linaloshiriki haya likajivunia kuwa na maadili mema. Mashindano ya urembo ni moja ya vigezo vya kulitambua taifa lililooza kimaadili. Inakuwaje wasichana wadogo waliojipodoa vyema na kuvaa mavazi yanayodhihirisha sehemu zao za siri wanapopita kwa madaha mbele ya halaiki ya watu wakiwemo wahuni ? Nini makusudio kama si kuamsha hisia za ngono kwa wanaume ? Hili ndiyo jambo la kuvaliwa njuga na Waziri! Napenda kuwatahadharisha wazazi wenzangu msithubutu kuwaruhusu mabinti zenu kushiriki katika ujinga huu. Waipuuze kauli ya Waziri na wawaepushe kabisa mabinti zao na udhalilishaji na uhuni uliomo katika mashindano ya urembo. Ustaarabu gani wa wanawake kutembea uchi mbele ya wanaume ? Mzazi gani mwenye akili timamu yuko tayari kumwona binti yake akichunguzwa mpaka maungo yake ya siri na majaji wanaume ? Huku ndiyo kujenga taifa ? Eti ! Wao waliosoma na waliopita nje wanaona ni mambo ya kawaida ! Mambo ya kawaida kutembea uchi mbele za watu ! Kuna faida gani kuwa msomi kama unashindwa kuinusuru jamii yako na uchafu unaoletwa kutoka nje ? Tatizo la wasomi wetu walio wengi wanadhani wameelimika kuacha mila na utamaduni wao na kuiga wa Kimagharibi. Fikra zao na uwezo wao wa kufikiri umedhibitiwa na Umagharibi. Yaani Mheshimiwa Waziri anawatukana na kuwakejeli wanaowakataza mabinti zao kushiriki mashindano ya urembo kwa kuwaita wana upeo mdogo wa elimu na fikra duni ! Mashindano haya yamekuwa muhimu kama chanjo ya ‘polio’ mpaka wazazi washurutishwe kuwapeleka mabinti zao ! Sasa kina Kimiti wanataka kuturudisha nyuma tulikotoka. Ni vyema Watanzania wote waelewe kwamba sababu za kupigwa marufuku kwa vazi la ‘vichupi’ zilikuwepo, zipo na zitaendelea kuwepo daima. Kwenda na wakati na sera za ‘Globalisation’ haziondoi ukweli huu. Ikumbukwe tu kwamba mashindano ya urembo pamoja na vilabu vya usiku vilipigwa marufuku kwa mara ya kwanza mwaka 1968 kwa sababu ya uharibifu wao wa maadili ya jamii. Yamefufuliwa tena mwaka 1994 kwa visingizio vya kwenda na wakati na biashara ya uchumi wa soko huria. Kuruhusiwa kwa mashindano haya kunatokana na kushindwa kwetu kuhimili wimbi la mabadiliko kutoka nje. Lakini sababu za kuyapiga marufuku bado zingalipo. Simuelewi Waziri anaposema lazima tubadilike na twende na wakati, wakati ukweli wenyewe tumezidiwa nguvu na mila na utamaduni wa kigeni. Kwa nini Waziri hasemi: "Tumeshindwa kuyazuia", badala yake anatutaka wananchi tuyaenzi ya kuyapokea kwa ‘Slogans’ za kwenda na wakati ? Huku ni kwenda na wakati au kuburuzwa tusikotaka kwenda ? Ni kweli mfumo wa biashara unaotokana na uchumi wa soko huria unaambatana na mambo mengi ya ajabu ajabu kama hamko makini. Soko huria maana yake si kila biashara inaruhusiwa ili mradi kuna wateja tu. Kama biashara ina madhara kwa jamii inapigwa marufuku tu bila ya kuzingatia soko lake. Kama serikali zote duniani zimepiga marufuku biashara ya mihadarati kwanini biashara ya ukahaba au mashindano ya urembo zishindikane ? Serikali ina dhima ya kulinda mila, utamaduni, na maadili ya Taifa. Namalizia kwa kuwakumbusha tena wazazi wenzangu acheni kabisa kuwaruhusu
mabinti zenu kujiingiza katika mambo yasiyopendeza. Mashindano gani haya
hayanogi mpaka mabinti wabaki na ‘vichupi’ tu mbele ya wanaume ! Wanawake
wote wa Tanzania ni wazuri na warembo. Hawahitaji kuonyeshwa hadharani
wala kwenye vioo vya televisheni kuthibitisha hilo.
|
YALIYOMO
TAHARIRI Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha Serikali
yakumbushwa kujiunga OIC
Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi Wafungwa waomba Futari na Vikoi Macho
ya shutuma
Hoja
pofu
Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 'Vichupi'
vya nini Kimiti?
Mjadala
wa Katiba na haki za Waislamu
Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 3
Waliochukuliwa
utumwa Uarabuni
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4)
Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga Mafunzo
ya Qur'an
|