|
|
|
Picha inayotolewa hapa ni kama vile Uislamu ulikuja kumdhalilisha Mwafrika kwa kumfanya kama bidhaa ambayo inaweza kuuzwa na kununuliwa na si kuleta maendeleo ya aina yoyote kwa Mwafrika. Madai haya yamejengwa kwa makusudi kwa nia ya kuupaka matope Uislamu mbele za watu ili kuonyesha haufai na dini ya hatari kuifuata. Ni kwa malengo haya haya ndio leo hii hatuna tena utumwa, zimezuka propaganda za siasa kali, imani kali n.k. Na hii ni kwa sababu kuna ukweli usiopingika kwamba Ukristo ulileta ukoloni hapa Afrika na sehemu nyingine duniani kama India na Latin Amerika. Hoja ya Bwana Charles Kamuhabwa AN-NUUR Na. 169, pia zinaendeleza madai haya, japo yeye amehoji masuala mengi yakiwemo hata usahihi wa Qur’an, na kuuawa kwa Khalifa wa tatu baada ya kutawafu Mtume (saw), Sayeedna Uthman bin Affan (r.a.), mimi ningependa tu kuchukua hoja yake juu ya Waarabu (Waislamu) waliokuwa wa kwanza kufika Afrika Mashariki wameacha athari zipi kwa Waislamu kielimu, kiuchumi na kiafya, mbali ya kupeleka mamilioni utumwani ambao hatujui vizazi vyao vimepotelea wapi. Anatoa changamoto Bwana Charles kwa AN-NUUR na wanaoliunga mkono wamuelezee maendeleo ya kujivunia ambayo Waarabu wametuachia Afrika Mashariki mbali ya masoko ya watumwa na kuandika kombe. Anasema haoni angalau Msikiti uliojengwa na Waarabu, mbali ya shule na madaraja au barabara. Kimsingi binafsi, sishangai madai hayo kwa sababu hizi ni fikra ambazo zimejengwa tangu utotoni na mashuleni alikopitia. Hata hivyo ni bora nimkumbushe kwamba elimu ili iwe na manufaa kwa mwanaadamu lazima imuelimishe. Lazima imfanye atafakari mambo kwa upana bila kusukumwa na utashi au mapenzi yake ya moyoni. Awe na uwezo wa kupima mambo juu chini, mbele nyuma, ukweli na uhalisi wake. Sijui kama amesahau somo la Historia hata shule za msingi vile alivyofundishwa Waafrika walivyojitahidi kupigana na wakoloni wa Kireno, Wajerumani na hata Waingereza. Hao akina Abushiri, Mkwawa na Milambo na vita vya Maji maji amesahau vilikuwa vinapingana na utawala dhalimu wa mkoloni – Mreno, Mjerumani, Mwingereza na si Mwarabu. Hizo kodi zilizokuwa zikidaiwa na wakoloni anazozitetea ndizo zilizotumiwa kama vigezo vya kupinga utawala wa mkoloni. Msumbuji – FRELIMO walipigana na Mreno, Zimbabwe ZANU na ZAPU walipigana na Mwingereza, Kenya – MAU – MAU- Mwingereza, Afrika Kusini – Makaburu, hakuna hata sehemu moja ya Afrika ambayo Mwafrika alipigana kupinga utawala dhalimu wa Mwarabu, japokuwa yeye ndiye wa kwanza kuingia bara hili. Leo hii tunashuhudia Waarabu wengi tu ambao ni wazaliwa wa nchi hii, wengine utawakuta vijijini kabisa na wanaongea lugha za kienyeji za sehemu wanazoishi, nenda Shinyanga kuna kijiji kinaitwa Maskat, hii ni kwa sababu ya wingi wa Waarabu katika eneo lile. Hata ukienda huko Uarabuni nchi kama Oman mji wa Maskat utakuwa na Waarabu wa huko wanaongea Kiswahili kama cha Tanzania, bila shaka hii ni kwa sababu wameishi huku kwa miaka mingi tu. Kwa vigezo hivi tunaweza kabisa kusema Waarabu walikuwa na tabia nzuri tofauti na Wazungu ndiyo maana wakakubalika na hivyo kuishi kwa amani na Waafrika. Tofauti na Wazungu ambao karibu wote walirejea kwao baada ya utawala wa kikoloni kung’olewa Afrika. Bwana Charles anapohoji maendeleo ya kiuchumi, kielimu na kiafya katika miji ya Mwambao, nadhani kama yeye ni mwenyeji wa Mtwara atumie muda wake atembelee sehemu zilizokaliwa na Waarabu azitazame kwa makini, bila shaka atapata picha ya miji ya kizamani sana. Picha hii ndiyo inayomfanya ahoji maendeleo ya sehemu hizo kwa kuwa anazitazama kwa kulinganisha na miji iliyojengwa na Wazungu na hata kuendelezwa na serikali zetu baada ya uhuru. Historia halisi ya nchi hii inaonyesha kuwa miji ya Bagamoyo, Ujiji, Kilwa, Tabora, Mafia, Pangani n.k. ilikuwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi kabla ya kuingia Wazungu. Watu walikuwa wanafanya biashara toka Buganda, Bunyoro kupitia Tabora hadi Bagamoyo ambako bidhaa zilikuwa zinasafirishwa hadi bara Arabu. Msafara mwingine ulikuwa unatoka Ujiji kuja Tabora hadi Kilwa na mpaka Msumbiji na si sababu ya biashara hizi ndizo mila na lugha ya Kiswahili ikaibuka. Huko Unguja athari za maendeleo hadi leo ni zao la karafuu na minazi ambayo yote yaliletwa na Mwarabu. Kuhusu elimu bila shaka Bw. Charles ana imani kuwa mtu mwenye elimu ni yule anayeongea na kuandika Kiingereza kwa ufasaha. Kwa maoni hayo hata yule Muitaliano aliyezaliwa kwao akasoma hadi Chuo Kikuu hana elimu kwa Charles kwa sababu hajui hata kuomba maji kwa Kiingereza. Mjapani, Mrusi, Mjerumani, Mhispania, Mreno, Mdenish wote watakuwa wameelimika tu pale watakapoweza kuongea Kiingereza. Hii ni kwa sababu leo hii unaweza kumchukua mtoto wa Kiislamu wa miaka 10 (kumi) tu akaweza kusoma Qur’an, sasa sijui sisi tungepata vipi uwezo wa kusoma Qur’an bila kusomeshwa na Mwarabu. Masheikh wote wa Tanzania wangeweza vipi kuswalisha, kufungisha ndoa, kuzika na kufundisha bila ya kusoma Kiarabu. Bw. Charles namuomba afungue Radio ya Taifa (RTD) siku ya Ijumaa asikilize swala ya Ijumaa halafu atueleze endapo mtu asiyekuwa na elimu anaweza kuswalisha na kutoa khutba kama ile. Kuhusu mamilioni kama anavyodai ambao walipelekwa utumwani Arabuni wako wapi leo ? Namuomba atafute kaseti ya mpira ya timu ya Saudi Arabia aone wachezaji wa timu hiyo ni Wazungu, Waarabu au Waafrika. Kama kweli anafuatilia vitabu vya Tarekh (historia) ya Kiislamu ajiulize swahaba Bilal bin Rabbah (r.a.) maisha yake kabla na baada ya Uislamu yalikuwaje. Baada ya hapo namuomba Bw. Charles na yeyote mwenye fikra kama zake asome historia ya biashara ya Trans-Atlantic Slave Trade. Pia afuatilie historia ya watu kama Marcus Garvery, Dr. Martin Luther King, Malcom X walikuwa wanadai nini na maisha yao yaliishia vipi ? Kwa Amani na kwa shari ? Amsome hata Mchungaji Jessey Jackson na Bwana Luis Farrakhan wote wanapigania nini. Mwanamuziki Bob Marley alipoimba kuhusu Babylon System alikuwa anawazungumzia Waarabu au Wazungu ? Na ni nini asili ya muziki wa Rap huko Amerika ? Sasa ningependa kunukuu sheria za utumwa ya Virginia huko Amerika namba 1668, kama ilivyonakiliwa na Bw. Leonard E. Barrett katika kitabu chake cha Soul Force, halafu kila msomaji atatafuta tafsiri yake mwenyewe: It cannot be presumed that prepensed malice (which alone makes murder a felony) should indunce a man destroy his own estate. Since the slave was property, a part of the estate, and not a person, killing him brought no moral or legal judgement. If any slave resists his master (or other by his master’s order correcting him) and by extrenuty of the correction should chance to die, that his death shall not be accompted a felony…. If any negroe or other slaves shall presume to lift up his hand in opposition against nay Christian, shall for every offence … have and receive thirty lashes on his bare back well laid on … Kuhusu sababu ya kuuana wao kwa wao baada ya Mtume (s.a.w.) namuomba
Bw. Charles asome vitabu vya Tarekh au asome AN-NUUR Tuisheni kidato
cha (IV) kuanzia toleo namba 169, na Insha-Allah atauona ukweli.
|
YALIYOMO
TAHARIRI Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha Serikali
yakumbushwa kujiunga OIC
Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi Wafungwa waomba Futari na Vikoi Macho
ya shutuma
Hoja
pofu
Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 'Vichupi'
vya nini Kimiti?
Mjadala
wa Katiba na haki za Waislamu
Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 3
Waliochukuliwa
utumwa Uarabuni
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4)
Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga Mafunzo
ya Qur'an
|