|
|
|
MHESHIMIWA Alhaj Simae Pandu Makame ameutaka uongozi wa shule ya Jamhuri kuwa wabunifu na kuweka mikakati ya miradi ya uchumi ili kuinua kiwango cha taaluma kwa kujenga maabara, madarasa na kuajiri walimu wenye ujuzi zaidi. Mheshimiwa Makame aliyasema hayo kama mgeni rasmi katika sherehe ya kuwaaga vijana wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Jamhuri ya Mjini Dodoma, Oktoba 31, mwaka huu. Mheshimiwa Makame alisema makusanyo ya ada ambayo yanakaribia milioni 76 kwa mwaka yanatosha kuboreshwa shule baada ya kuondoa gharama za uendeshaji. Shule inaweza kukusanya mazao kwa bei rahisi katika kipindi cha mavuno, kisha kuyauza kwa bei nzuri baada ya miezi michache, alisema. Aliwahusia wanafunzi waagwa kuwa elimu waliyopata isiwe kikomo, bado wana safari ndefu na kipindi kigumu kuifikia elimu ya juu, pia aliwataka wahitimu hao watafute njia rahisi kujipatia riziki zao kwa kuvitumia vipaji walivyonavyo, na aliwataka wahitimu hao kuitumia elimu waliyoipata waiweke katika vitendo. Aliuomba uongozi wa shule kuwa na mwelekeo wa shule wa baadaye uwe wenye kuwafanya wanafunzi wajiajiri wenyewe pindi wamalizapo elimu za sekondari. Akiwanasihi wanafunzi wanaobaki, aliwaomba kuwa wavumilivu katika kutafuta elimu kwani bila usumbufu huwi mtukufu, vitu viwili haviendi kwa pamoja navyo ni elimu na starehe. Awali akimkaribisha mgeni rasmi Katibu wa Mkoa wa Bakwata na Meneja wa shule, Bwana Iddi Msafiri alimfahamisha Mh. Makame kuwa shule ina matatizo ya uhaba wa madarasa, ujenzi wa ukumbi wa maabara. Wakati huo huo, sherehe za mahafali ya shule ya Jamhuri zilichupa maadili ya Kiislamu. Shule ya Jamhuri inamilikiwa na Baraza Kuu la Waisalmu Tanzania (BAKWATA) kwa katiba ya Bakwata inaendesha shughuli zake kwa Qur’an na Sunnah. Kikundi cha ngoma maarufu kwa jina la Nindo Group toka Zuzu kilikesha hapo shuleni usiku wa kuamkia Oktoba 31, mwaka huu, makao makuu Taarabu, Makutopora J.K.T. Brass Band nao walitoa "burudani" katika taasisi ya Kiislamu siku hiyo. Mchanganyiko wa jinsi tofauti hivi vyote vilitafsiriwa vibaya na baadhi
ya wazazi waliofika hapo. Ngoma ya utamaduni ya shule nayo haikuwa mbali
siku hiyo, wakinengua na kupigiwa makofi kwa ishara kuwa kilichofanyika
hapo ni kizuri.
TELEVISHENI ya Zanzibar ni kituo pekee cha kutumia huduma hiyo kwa upande wa Zanzibar. Katika kuboresha huduma zake televisheni hiyo inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) hivi karibuni ilianzisha kipindi maalum cha wananchi kutoa maoni yao, kijulikanacho kama "Wasemavyo". Lengo na dhamira ya kipindi hicho lilikuwa ni zuri na lilifurahiwa na wananchi wengi kwa vile walihisi kwamba hivi sasa walau watapata uhuru wa kuyaelezea yale yanayowakera kupitia televisheni yetu ya umma. Lakini kuna watu kwa makusudi wamekuwa wakijaribu kuliharibu lengo zuri. Siwezi kusema kwamba mpango huo umepewa baraka na uongozi wa juu wa TVZ lakini hali inayojitokeza ni dhahiri kwamba viongozi hao nao kwa upande mwingine wameridhia hali hii. Katika siku za karibuni mwanafunzi mmoja wa sekondari ya Lumumba mjini hapa aliuliza suala ambalo alitaka afafanuliwe na TVZ wanaposema kipindi cha watu wazima wanakuwa wana maana gani ? Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo aliyelazimika kuuliza hivyo kwa sababu ameona kwamba vipindi hivyo huwa vinatizamwa na hata watoto wadogo, hivyo kulikuwa na haja ya kufafanua umri wa mtu mzima aliyekusudiwa na TVZ. Suala jingine aliloliuliza binti huyo ni kuhusu ngoma zenye asili ya Kizaire ambazo maarufu huitwa "Ndombolo" kama zinalingana na utamaduni wa Mzanzibari. Mimi binafsi nilihisi umuhimu wa majibu ya masuala haya ukizingatia kwamba bado suala la mtu mzima haliko bayana katika sheria zetu za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Kuna baadhi ya sheria ambazo zinamtambua mtu mzima kwamba ni yule aliyepindukia miaka 15, sheria nyingine zinamtambua mtu mzima kwamba ni yule aliyepindukia miaka 17 na nyingine miaka 21. Sheria zote hizo zinatumika hapa nchini na zinatambulika kihalali na mahakama kutegemea na kifungu cha sheria kilichovunjwa. Hivyo mtaona kwamba suala la kubainishwa mtu mzima ni suala la msingi kabisa. Ama kuhusu "ndombolo" muulizaji alikuwa na haki ya kutaka kujua ni kwa nini muziki huo uonyeshwe kwenye televisheni wakati unaenda kinyume na maadili ya wenye televisheni hiyo (Wazanzibari). lakini badala ya binti huyo kujibiwa kwa hoja muafaka bibie muendeshaji wa kipindi hicho Sharia Maulidi alianza kumshambulia kwa maneno mabaya muulizaji na katika njia za kuonyesha dharau zaidi kwa muulizaji bibi huyu alionyesha miziki mbalimbali ambayo wanenguaji wake walikuwa nusu uchi na kudai kwamba wao hawawezi kubabaishwa na mtu mmoja wakati walio wengi wanaipenda miziki hiyo. Bibie Sharifa hata hivyo alishindwa kutoa takwimu au ushahidi kwamba muziki huo unapendwa na watu wengi hapa visiwani. Hata hivyo ingelikuwa maneno ya Bi. Sharifa ni kweli bado hakuwa na haki ya kumdhalilisha muulizaji kiasi cha alivyofanya. Kutokana na jazba zilivyompanda bibie huyo alisahau hata kujibu suala la msingi la muulizaji juu ya mtu mzima aliyekusudiwa na TVZ na hivyo kutuacha hadi leo kutofahamu mtu mzima ni mwenye umri gani. Pengine jambo moja ni lazima wafanyakazi wa TVZ walielewe kwamba televisheni hiyo ni ya wananchi (Public TV) na wao ndio wanaoifanya iendelee kuwapo kutokana na kodi zao mbalimbali wanazotoa. Kwa maana hiyo kila mwananchi anayo haki ya kutoa mchango wake juu ya uendeshaji wa televisheni hiyo na pale anapoona baadhi ya vipindi haviendani na maadili ya Kizanzibari ana haki na wajibu wa kukosoa. TVZ kwa kipindi kirefu imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kutokana na jinsi inavyoendesha vipindi vyake ambavyo vingi havina maadili . Baadhi ya vipindi vinavyoonyeshwa na televisheni hiyo vimekuwa havitazamiki hata na hao wanaoitwa watu wazima seuze vijana na watoto. Katika kuonyesha kwamba kipindi hicho cha "Wasemavyo" hakina nia ya kuwasilisha au kusikiliza maoni ya wananchi bali kipo kwa maslahi ya watu wachache tu, Bwana mmoja mkazi wa maeneo ya Mji Mkongwe alimweleza mwandishi wa habari hizi kwamba yeye mwenyewe aliwahi kufika TVZ na kutaka kutoa maoni yake juu ya adhana ambazo zimekuwa zikionyeshwa katika televisheni hiyo. Bwana huyo ambaye malalamiko yake yalikuwa ni kwa nini katika kuonyeshwa adhana hizo Misikiti inayohusishwa ni ya Unguja tu na wala siyo ya Pemba, wakati Zanzibar imejengwa na visiwa vya Unguja na Pemba. Kwa mujibu wa maelezo ya Bwana huyo hakupewa nafasi ya kuuliza suala lake hilo na zaidi alijibiwa kwa maelezo yasiyo rasmi na baadhi ya watangazaji aliowakuta hapo kwamba hakukuwa na umuhimu wa kuonyeshwa Misikiti ya Pemba na kutakiwa yeye mwenyewe aeleze ni kwa nini alikuja kutetea Misikiti ya Pemba tu na sio ya Dar, Mwanza, Arusha, n.k. Bwana huyo alijibu kwamba suala lake lililenga kwa Misikiti ya Pemba kwa sababu televisheni inayotumika kuonyesha Misikiti hiyo ni ya Zanzibar na sio ya Tanzania, hivyo hakuna umuhimu wa kutetea kuonyeshwa kwa Misikiti ya Bara. Hata hivyo Bwana huyo aliondoka kituoni hapo kwa unyonge baada ya kupewa jibu la mdomo na watangazaji hao kwamba tunakujueni nyie wapinzani. Pengine jambo la kusikitisha zaidi ni kuhusishwa masuala yanayoulizwa
TVZ na upinzani. Wanaouliza ni Wazanzibari na Watanzania kwa jumla wala
hapana kipengele ambacho kinamkataza mpinzani kuuliza suala kupitia TVZ,
sasa unapokataa kulirusha hewani suala la muulizaji kwa sababu tu ya wasiwasi
wa kwamba ni mpinzani, jamii itashindwa kufahamu lengo halisi la kuwekwa
kipindi hicho cha "Wasemavyo" kama tulivyotangulia kusema awali TVZ ni
ya Wazanzibari wote bila kujali rangi zao, kabila au itikadi zao za kisiasa,
hivyo si busara kwa mtu, tena mlipa kodi kunyimwa haki yake ya kuuliza
suala na kupata ufafanuzi kwa sababu tu ni mpinzani.
|
YALIYOMO
TAHARIRI Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha Serikali
yakumbushwa kujiunga OIC
Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi Wafungwa waomba Futari na Vikoi Macho
ya shutuma
Hoja
pofu
Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 'Vichupi'
vya nini Kimiti?
Mjadala
wa Katiba na haki za Waislamu
Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 3
Waliochukuliwa
utumwa Uarabuni
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4)
Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga Mafunzo
ya Qur'an
|