AN-NUUR  Na.174 Rajab 1419, Novemba 6 - 12, 1998 
 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kesi ya Waislamu Mwembechai:

Mashahidi washindwa  
 

  • Mwendesha Mashitaka adai hana mawasiliano na ofisi
SERIKALI haijathibitisha mahakamani ukweli wa tuhuma yake dhidi ya Waislamu kumi miongoni mwa Waislamu kadhaa inayowashitaki kwamba walihusika na ghasia za Mwembechai hapo Februari 29, mwaka huu, ambapo Waislamu wawili waliuliwa na polisi kwa risasi na wengine wengi kujeruhiwa. 

Kuchelewa kuthibitishwa tuhuma hizo kumetokana na mashahidi wa upande wa serikali kutofika mahakamani Jumanne ya Novemba 3, 1998, siku ambayo mashahidi hao walitaraajiwa kutao ushahidi wao tangu kesi hiyo ifunguliwe mahakamani. 

Kesi hiyo yenye namba 407/98 inayosikilizwa katika mahakama ya Kivukoni, Jijini na Hakimu wa mahakama hiyo Bw. Gabrieli Mivumbe ilifunguliwa na serikali mapema Februari 30, mwaka huu, 

Watuhumiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Rutemba Shabani, Idd Selemani, Ismaeli Hamisi, Jafari Mohammed, Omari Hemed, Hassan Habibu, Hamisi Nassoro, Aly Daudi, Juma Ali na Nurdin Abbas. 

Akitoa sababu za mashahidi hao (wa serikali) kutofika mahakamani siku hiyo, Mwendesha Mashitaka wa serikali, Bi. Pili Mande alisema hiyo imetokana na yeye muda mrefu kutokuwa na mawasiliano na ofisi yake ili kujua kulikoni. 

Kwa hali hiyo, Mwendesha Mashitaka huyo aliiomba mahakama impe muda zaidi aweze kuwasiliana na ofisi yake. 

Awali, Wakili anayewatetea watuhumiwa (Waislamu) Bw. Twaha Taslima aliiomba mahakama hiyo iwafutie wateja wake mashitaka yanayowakabili kwa muda mrefu sasa. 

Bw. Taslima aliiambia mahakama hiyo kuwa haki ya wateja wake kufutiwa shauri hilo imekwishatolewa na kifungu No. 205 cha sheria ya makosa ya jinai kinachoruhusu mtuhumiwa kufutiwa mashitaka endapo kesi yake itafikisha muda wa zaidi ya miezi sita mahakamani bila ushahidi wa kumtia hatia kutolewa. 

Wakili Taslima alitoa hoja kwamba ombi lake hilo (la kufutwa kesi kwa wateja wake) limezingatia kuchelewa kwa mlalamikaji (serikali) kuleta mashahidi wake mahakamani, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa wateja wake kusumbuliwa na kupata matatizo kwa muda mrefu bila tuhuma walizoshitakiwa kuthibitishwa. 

"Kwa hali hiyo, Mheshimiwa Hakimu naiomba mahakama yako tukufu iwaondolee wateja wangu shauri hilo ili waondokane na mzigo huu wa kusumbuliwa", alisema Wakili Taslima. 

Hata hivyo, Hakimu wa mahakama hiyo, Bw. Gabrieli Mivumbe alipinga ombi hilo kwa maelezo kwamba mahakama yake haijaziona kuwa ni za msingi sababu za kufuta kesi hiyo zilizotolewa na Wakili Taslima kwa vile upelelezi wake umekwishakamilika. 

Hakimu Mivumbe aliongeza kuwa anazo kumbukumbu kwamba mashahidi wa upande wa Serikali waliwahi kufika mahakamani na mahakama yake ikashindwa kusikiliza kesi hiyo kwa kuridhika na sababu zilizotolewa na Wakili wa watuhumiwa aliyetangulia, Bw. Abdul Mwengela za kutofika mahakamani siku hiyo. 

"Ama sababu ya tatu ya kupinga hoja za Wakili Taslima za kuomba mahakama yangu ifute shauri hilo ni kwamba kesi hii bado ina umuhimu mkubwa kwa kijamii (public interest)", alisema Hakimu Mivumbe. 

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 2, mwaka huu ambapo mashahidi hao (wa serikali) wanatarajiwa kutoa ushahidi wao. 

Wakati huo huo, kesi nyingine No. 184/98 kama hiyo itaendelea kusikilizwa tena katika mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu Jijini. 

Waislamu wanaotuhumiwa katika kesi hiyo kufanya ghasia baada ya onyo la polisi na kumjeruhi askari (Simon Nyakoro) hapo Mwembechai ni pamoja na Hatamu Saidi, Hamidu Mohammed, Hussein Mohammed, Ali Kassim na Kivuele Mawazo Abdallah. 

Wengine ni Abdallah Juma Bakari, Ramadhani, Hamza Amani Ali na Abdulrahman Juma Saidi. 


Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza
 

WANAFUNZI wa shule kadhaa za sekondari Mjini Mwanza wametoa kilio chao kwamba wananyimwa fursa ya kwenda kuabudu siku ya Ijumaa. Baada ya juhudi zao kukwamishwa mara kadhaa na wakuu wa shule zao, wanafunzi hao walilazimika kulipeleka tatizo hilo kwa uongozi wa Bakwata mkoa. 

Wakiwa katika mahafali ya kidato cha nne Oktoba 11, mwaka huu wanafunzi Waislamu wa shule za Nganza, Nsumba na Nyegezi walitoa kilio chao kwa Sheikh wa Mkoa Sheikh Farej wakati wakisoma risala yao kwa mgeni rasmi. 

Kufuatia risala hiyo uongozi wa Bakwata umemuomba Afisa Elimu wa Mkoa aingilie kati suala hili ili wanafunzi Waislamu wapate haki yao ya kufanya ibada kama ambavyo wenzao hupewa haki hiyo za Jumamosi na Jumapili. 

Katika barua yao Na. BKT/GVT/98/109 ya Oktoba 13, Bakwata imebainisha kwamba itakuwa ni kuwadhulumu wanafunzi hao kwani swala ndiyo nguzo kuu ya Uislamu. 

Wakati huo huo wanafunzi wa shule za wavulana na wasichana Bwiru, wametakiwa kuishi maisha yao yote kwa mujibu wa maagizo ya Mwenyezi Mungu. 

Nasaha hizo zilitolewa na Sheikh Omar Mbalamwezi aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwaaga wenzao wanaomaliza kidato cha nne. 

Sheikh Mbalamwezi aliwakumbusha wanafunzi umuhimu wa elimu na kwamba isomwe kwa ajili ya Allah na itumike kumfikisha mwanaadamu kwenye lengo la kuumbwa kwake. 

Katika risala yao wanafunzi wa Bwiru Girls wameyataja mafanikio ya wanafunzi Waislamu shuleni kwao kwamba ni pamoja na kupatiwa sehemu ya kuswalia, kupatikana kwa gazeti la AN-NUUR na kuwa na kipindi cha dini ambapo huelimishana wenyewe kwa wenyewe. 

Wanafunzi wa Bwiru Boys wameeleza kwamba wao bado hawana sehemu rasmi ya kuswalia. 


Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga

SHULE ya sekondari ya Jumuiya ya mjini Tanga imefungiwa na Manispaa ya Tanga tangu Oktoba 21, 1998 kwa madai ya kuwa ni chafu. 

Wiki iliyopita wanafunzi wa kidato cha nne wanaotarajia kufanya mtihani wao wa taifa walimua kuishambulia shule kwa mawe na wakasababisha uharibifu kidogo. 

Wapinzani wa Bakwata miongoni mwa Waislamu wanalaumu uongozi wa shule kwa kukosa maadili mazuri na kwa upande mwingine wamemlalamikia Sheikh Mkuu. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
 TAHARIRI  
Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha 

Serikali yakumbushwa kujiunga OIC 
Na Mwandishi wetu 

Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi 

Wafungwa waomba Futari na Vikoi 

Macho ya shutuma 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Hoja pofu 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Tafuteni ufalme wa kisiasa 

Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 

'Vichupi' vya nini Kimiti? 
Na. Said Rajab 

Mjadala wa Katiba na haki za Waislamu 
Na Masoud Mohammed Mbogo 

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 3 
Na Nandenga wa Mkomidachi 

Waliochukuliwa utumwa Uarabuni 
Na Hassan Omar 

Madrasatul Maamury Islamiya 

Teknologia: Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4) 
Na Hassan Omar 

Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito 

TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' 

Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa  

Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza 

Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga 

Mafunzo ya Qur'an  
Shetani anawaogopesha wenye mali kutoa 

Barua za wasomaji  

Masomo ya dini ya Kiislam  

Chakula na lishe 

Mashairi 

Matangazo 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita