AN-NUUR  Na.174 Rajab 1419, Novemba 6 - 12, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Barua
 
 
Ujumbe rasmi kwa Waislamu wa Tanzania

Ndugu Waislamu 

WAKATI umefika kwa Waislamu kuzinduka wote pamoja. Waungane kwa kalimat "Laa Ilaha Illa Llah wa Anna Muhammadan Rasulu Laah". 

Tusahau ikhtilafu za kimadhehebu, za kikabila na za rangi kwani sasa tunapigwa vita baridi na tumeghafilika, tumo usingizini na hata tukiamka hatuna silaha yoyote ya kujitetea. Tukiamka tumo vitani tukipigana sisi wenyewe kwa wenyewe. Twapigana kimadhehebu, kiakida, kikabila na rangi. Tumesahau kuwa Mwenyezi Mungu ametuamuru kushikamana na kuungana. 

Mwenyezi Mungu ametuamuru tushikamane kwa dini ya Allah (s.w.) na wala tusifarakiane kabisa. Na tushikamane kidini, wala si kwa misingi ya kabila, rangi au madhehebu. Tuache fikra ya ukabila ambayo ndiyo mbaya sana, Taasubi aliyotukataza Mtume (s.a.w.) kwa kusema kuwa: Mwenye kulingania Taasubi si katika sisi kwani Taasubi ni mbaya, yanuka. 

Mambo hayo matatu au manne tuliyoyataja hapo juu ndiyo yanayotudhoofisha sisi Waislamu. Tumedhoofika mpaka tumekuwa tunachezewa na kila mtu. Tumekuwa madhalili hata ingawa tupo wengi, na hatukukosa mali wala uwezo. Kila mmoja wetu anatizama nafsi yake na familia yake tu, na hii ni hatari kubwa sana. Mtume (s.a.w.) amesema: 

"Mtu ambaye hajishughulishi na mambo ya Waislamu basi yeye si katika wao". (Waislamu). 

Mwenyezi Mungu (s.w.) naye amesema katika Qur’an: 

"Basi waandalieni nguvu mziwezazo (silaha) na mafarasi yaliyofungwa tayari tayari ili kuweza kuwaogopesha maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu". 

Tufahamu kuwa vita hivi baridi tunapigwa katika magazeti na maredio siku zote. Magazeti na maredio yatangaza mabaya tu ya Waislamu na Uislamu na madogo yakakuzwa, huku mema yetu yakifichwa. 

Uislamu hauna mabaya, ila mbaya wanayo wao makafiri na yao huyaficha maovu makubwa makubwa. Wakristo wamefika hadi ya kututukania muongozi wetu mpendwa Nabii Muhammad (s.a.w.) na sisi kimya. Au labda ndivyo Makanisa yanavyowafunza kuutukana na kuukashifu uongozi wa dini ya Kiislamu ? 

Je, ni kweli kuwa Waislamu hawawezi kuwa na gazeti kubwa linaloweza kurudisha matusi na fedheha za uongo na uchafu unaopakwa ndani ya Uislamu na Waislamu ? Gazeti ambalo litaweza kuuzwa nchini Kenya, Uganda na Tanzania ? 

Gazeti ni mojawapo ya silaha na pia ni ulimi wa Ummah wa Kiislamu. Gazeti ambalo lingeweza kuleta umoja wa Waislamu wa Afrika ya Mashariki yote. Ikiwa wapo watu au mtu mmoja tu, akaweza kumiliki na kuendesha Redio na kituo cha televisheni, kweli Waislamu sote hatuwezi kuwa na vitu kama hivyo vya Redio na televisheni ? 

Ndugu Waislamu, vita baridi vya wakati huu ni sisi kuwa na mambo matatu tu kwanza : 

Mashule pamoja na madrasa zetu za uhakika na tena zenye mfumo wa kisasa kiufundishaji. 

Gazeti kama ulimi wetu sisi Waislamu wa Afrika Mashariki. 

Redio na Televisheni zenye kufunza dini na mengineyo (Brodcasting). 

Shime Ndugu Waislamu, na tuzinduke toka katika usingizi huu wa kughafilika. Tujue kwamba kwa kutojibu mashambulizi haya baridi tunayofanyiwa, tunakimbia vita, na kukimbia vita ni katika dhambi kubwa. Na tutaulizwa siku ya Qiyama. 

Na muakilishi maalum, 
Adnan Abdallah Mohammed. 



Uislamu hauruhusu majivuno! 

 Ndugu Mhariri 

NINAOMBA nichukue fursa hii adhimu kujaribu kufuta sumu mbaya ambayo hali ilivyo ni kuwa baadhi ya wasomi wa Kiislamu wangependa ienee. 

Ijumaa ya Septemba 25, mwaka huu nilisikia kupitia Sauti ya Tanzania Zanzibar mawaidha ya Sheikh mmoja ambaye anapenda kujinasibisha na lililokuwa jina la nchi yake ambayo kwa sasa inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Katika mawaidha hayo, Sheikh huyo alikuwa akiongelea kwa madaha na majivino makubwa juu ya kuwa Uislamu uliingia kwanza Afrika baada ya bara la Arabu kabla ya nchi nyingine yoyote na hivyo kujaribu kutaka kuifanya Afrika kuwa ni sehemu bora kuliko nyinginezo na vile vile kuwafanya Waafrika wajione kuwa ni bora kwa vile Uislamu uliingia kwanza katika bara hilo. 

Mimi sio mtaalamu wa masomo ya Kiislamu (Islamic Studies) wala historia (Tarekh) kwa ujumla. Lakini kwa hii hii elimu yangu ndogo niliyonayo ninathubutu kusema kwamba hakuna hata aya ya Qur’an (kwa mujibu wa nakala tulizonazo) wala Hadith sahihi ya Mtume (s.a.w.) ambayo inasema kuwa Waafrika wajivune kwa sababu hiyo iliyotajwa hapo juu na Sheikh huyo Mzaire. 

Ningependa kumkumbusha Sheikh huyo pamoja na watu (Waislamu) wengine wenye mawazo kama yake kuwa njia pekee ya kumfanya mtu kuwa bora mbele ya Allah (s.w.) kuliko mwingine ni kwa kuwa mcha Mungu tu na sio vinginevyo. 

Anasema Allah (s.w.): 

"Enyi watu ! Hakika ahishimiwaye (aliye bora) sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi katika nyinyi (49:13) 

 
Hassan Makame, 
Box 1542, 
Tanga. 


Utabiri wa kuibuka Uislamu

Ndugu Mhariri 

NIMEVUTIWA sana na makala ya Ndugu B.P. Nyangasa kuhusu utabiri wa kuibuka Uislamu ndani ya Biblia. AN-NUUR Na. 171. 

Kwanza kabisa nimtahadharishe ndugu yangu Nyangasa kama isemavyo Meth. 27:2 kwamba asijifu bali sifa zitoke kwa wale watakao soma makala zake na kuona ukweli uliyopo ndani yake. 

Pili, nampongeza kwa jinsi alivyoyaona mafundisho ya Mwanatheolojia mkongwe Paulo yanafaa kuwa utangulizi wa makala yake 1 Wakor. 2:10-15. Nakupongeza sana. 

Tatu, napenda kumuuliza Ndugu Nyangasa huyo Roho Mtakatifu kampata wapi. Namnukuu "Alhamdulil llaahi Rabbil Aalamin. Mimi nimejaaliwa neema hiyo adhimu na zingine. Mwisho wa kunukuu. 

Ndugu Nyangasa wewe na wahadhiri wenzako mmetufundisha Roho Mtakatifu ni Mjumbe atakayekuja baada ya Bwana Yesu kuondoka, na mnathibitisha kwamba ni Mwamedi (Muhammad) mimi nashindwa kuelewa huyu ni mtu au ni nguvu apewazo mtu baada ya kumwamini Yesu Kristo na kukiri kwamba Yeye ni mwana wa Mungu na alikufa siku ya tatu akafufuka. 

Katika gazeti la AN-NUUR toleo la 199 Uk. 15 ulisema tuangalie toleo Na. 60 ambalo ulithibitisha kwamba ukumalizia tafsiri ya Roho Mtakatifu. 

Naomba basi kwa msaada wako unisaidie kwa ufupi tu juu ya huyu Roho Mtakatifu. 

Baada ya hapo nitaomba ufafanuzi zaidi juu ya Uislamu ndani ya Biblia. Asante. 
 

Ni mimi mpenzi wa AN-NUUR, 
Jackson Urassa, 
Box 62848, 
Ubungo – Kibangu, 
Dar es Salaam. 


Tusome Maulidi ya Mtume (s.a.w.) kwa Kiswahili

Ndugu Mhariri 

NAOMBA nafasi kidogo katika gazeti lako la AN-NUUR ili nitoe malalamiko yetu sisi ambao ni Waislamu tusiyojua au kutambua lugha ya Kiarabu kwa tafsiri ya Kiswahili. 

Sehemu nyingi hapa kwetu nchini, mikoani, wilayani hata vijijini inapokuwa ikisomwa maulidi ya Mtume (s.a.w.) husomwa kwa lugha ya Kiarabu. 

Pamoja na hayo tujue kwamba kile kinachosomwa ni historia ya Mtume Muhammad (s.a.w.) nasaba yake aliyozaliwa, alivyokuwa, mwenendo wake, uongozi wake na jumla ya sifa zake zote. 

Kwa kuwa vitu vyote hivyo husomwa kwa lugha wasioijua waliohudhuria Maulidi hiyo, basi huanza mazungumzo yao na mambo mbalimbali katika sherehe hiyo pasina kuzingatia kuwa kinachofanyika pale ni kitu muhimu sana kwa Waislamu na wasio Waislamu. 

Madhara yanayopatikana pale Waislamu hukosa thawabu za kumtakia rehema Mtume (s.a.w.) pia hukosa faida ya kutokumuelewa vyema Mtume wao. 

Ninawaomba Masheikh na walimu wajaribu kuacha tabia ya kusoma Maulidi kwa Kiarabu, wasome kwa Kiswahili ili watu wengi waelewe hayo yanayosomwa. 

Nasiru Issa, 
Nguruka, 
Kigoma. 


Wenye kuhadaika na dunia wasiongoze Waislamu

Ndugu Mhariri 

  

IMEKUWA ni jambo la kawaida kwa kuigeuza Misikiti ya Mwenyezi Mungu kama sehemu ya kukidhia haja za kidunia ikiwemo kuitumia kama mashamba yao ya kuchuma mali kupitia migongo ya Waislamu, hivyo kuwa kero kwa Waislamu na Uislamu kwa ujumla. 

Aibu iliyotokea Ijumaa Septemba 19, 1998 katika Msikiti wa Majengo ni mfano tosha kwa aina ya kiongozi wanaotanguliza njaa zao mbele na kuaicha taqwa nyuma yao. 

Tatizo linalowakabili Masheikh wetu na viongozi wengine wa Taasisi mbalimbali za Kiislamu ni kule kugubikwa na maradhi ya ubinafsi, uchoyo na ujinga, vitu ambavyo vinachangia sana kwa kuwafanya wenzetu hawa wasiweze kufundishika wala kuelewa hali halisi ya Muislamu wa Tanzania. 

Masheikh hawa wanapandikiza fitna na chuki dhidi ya Waislamu Msikitini na kupandikiza mbegu ya ukabila na ubaguzi wa wazawa na wasio wazawa, lengo likiwa ni kupata kuungwa mkono ili waendelee kuhodhi madaraka Msikitini hata kama hawakubaliki kuongoza Waislamu. 

Basi Masheikh wa aina hii wako radhi kutumia mbinu mbalimbali hata zile za "kimafia" ili wabaki madarakani. 
 

Salma A. Madebe, 
Box 10190, 
Moshi. 


Je, hii ni haki?

Ndugu Mhariri 

KUMEZUKA mtindo hapa Pemba ambapo baadhi ya wazee huwaapisha watoto wao kwa kuwashikisha Msahafu ili wawe CCM. 

Kwa bahati mbaya watoto nao huogopa wakidhani kwamba watadhurika. 

Mashuhuri kwa vitendo hivi ni kijiji cha Mwembe kizuka, Mkungu, Mkoani Pemba. 

Ningependa kuwanasihi wazee hao wasiifanyie maskhara Qur’an ya Mwenyezi Mungu. 

 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI  
Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha 

Serikali yakumbushwa kujiunga OIC 
Na Mwandishi wetu 

Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi 

Wafungwa waomba Futari na Vikoi 

Macho ya shutuma 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Hoja pofu 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Tafuteni ufalme wa kisiasa 

Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 

'Vichupi' vya nini Kimiti? 
Na. Said Rajab 

Mjadala wa Katiba na haki za Waislamu 
Na Masoud Mohammed Mbogo 

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 3 
Na Nandenga wa Mkomidachi 

Waliochukuliwa utumwa Uarabuni 
Na Hassan Omar 

Madrasatul Maamury Islamiya 

Teknologia: Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4) 
Na Hassan Omar 

Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito 

TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' 

Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa  

Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza 

Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga 

Mafunzo ya Qur'an  
Shetani anawaogopesha wenye mali kutoa 

Barua za wasomaji  

Masomo ya dini ya Kiislam  

Chakula na lishe 

Mashairi 

Matangazo 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita