AN-NUUR 
Na.175 Rajab 1419, Novemba 13 - 19, 1998 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
JIFUNZE KUUNGANISHA KOMPYUTA (V)
Hassan Omar

  
 

KUITAYARISHA LAN 

Ukishakuwa na vifaa vinavyohitajika, yaani NIC, nyaya za LAN, na hub (kama inahitajika), fuata hatua zifuatazo kwa kila kompyuta iliyomo kwenye LAN yako ili ukamilishe kazi ya kuitengeneza LAN yako. 
 

1. Ingiza NIC kwenye kompyuta: 

Izime kompyuta yako na ifungue gamba lake la juu na uifunue ili uweze kuona ndani yake. Kwenye motherboard tafuta upenyo (slot) wa aina ya PCI au ISA (kutegemeana na aina ya NIC yako) ulio kuwa haujachomekwa kitu chochote. Ichomeke NIC yako kwenye upenyo huo na ifunge vizuri kwa screw yake. Baada ya hapo unaweza kuifunika kompyuta yako. Rudia hatua hii kwa kila kompyuta iliyo kwenye LAN yako. 
 

2. Unganisha waya: 

Kwanza tafuta sehemu nzuri ya kuiweka hub yako. Vizuri zaidi iwe katikati ili iwe rahisi kuiunganisha na kila kompyuta iliyo kwenye LAN yako. Jambo jengine muhimu ni kuwa hub inahitaji umeme, kwa hivyo iweke mahali ambapo itakuwa rahisi kuichomeka plagi yake ya umeme kwenye soketi ya umeme. Ichomeke plagi hiyo kwenye soketi ya umeme. 

Ichomeke ncha moja ya waya wa LAN wa aina ya UTP kwenye NIC iliyomo kwenye kompyuta yako na ncha nyengine ichomeke kwenye port yoyote ile ya hub kama inavyoonekana kwenye Picha 3. Rudia hatua hii kwa kila kompyuta. 

Picha 3: Namna ya kuunganisha waya wa UTP wenye plagi za RJ-45

Kama unatumia nyaya za aina ya coax, chomeka T-junction ya aina ya BNC kwenye pini ya aina ya BNC iliyo kwenye NIC, na T-junction nyengine kwenye pini ya aina ya BNC iliyo kwenye hub. Kwenye pini moja ya T-junction iliyoungwa na NIC, chomeka 50-ohm terminator, na kwenye pini nyengine chomeka ncha moja ya waya wa aina ya coax kama inavyoonekana kwenye Picha 4. Ncha nyengine ya waya huo wa coax ichomeke kwenye pini moja ya T-junction iliyochomekwa kwenye hub. Pini iliyobaki ya T-junction iliyo kwenye hub ichomeke waya wa coax unaokwenda kwenye T-junction iliyochomekwa kwenye NIC iliyo kwenye kompyuta nyengine. 

Picha 4: Namna ya kuunganisha waya za aina ya coax zenye plagi za aina ya BNC

Kama LAN yako ina kompyuta mbili tu, huna haja ya kutumia hub – unaweza kuchomeka waya wa coax kutoka kwenye T-junction iliyo kwenye NIC ya kompyuta moja, na ukauunganisha moja kwa moja na T-junction iliyo kwenye NIC ya kompyuta ya pili. Ncha za T-junction zilizo kwenye kompyuta zote mbili ni lazima zichomekewe 50-ohm terminator. 
 

3. Ingiza driver ya NIC kwenye kompyuta: 

Washa kompyuta yako kama kawaida . Mara tu Windows 95 (au Windows 98) itakapoanza, itagundua kuwa kompyuta imewekewa NIC mpya na itakutaka uingize diskette yenye driver ya NIC hiyo. Driver ya NIC ni programu maalum ya kuifanya kompyuta iweze kuitumia NIC hiyo. Ukishaingiza diskette yenye driver ya NIC yako (diskette hiyo unapewa unaponunua NIC), Windows 95 ikiweza kuiona driver inayohitajika itakujuilisha hivyo na utahitajika kubonyeza Next. 

Kama Windows 95 haikuiona driver, bonyeza Browse kwenye kidirisha cha Device Driver Wizard ili uweze kuielekeza Windows 95 mahali ambapo panaweza kuwepo driver ya NIC hiyo. Ni muhimu kujua jina la kampuni iliyotengeneza NIC yako pamoja na modeli yake. Kwa maelekezo zaidi, soma kijitabu au maandishi yaliyokuja na NIC yako. 

Windows 95 ikifanikiwa kuiona driver ya NIC yako, itainakili kutoka kwenye diskette au mahali pengine popote ulipoielekeza na itakutaka uingize CD au diskette zenye Windows 95 ili imalizie kuyanakili mafaili mengine yanayohitajika kwa ajili ya LAN yako. Windows 95 inaweza kuchanganyikiwa isijue wapi hasa pa kuyapata mafaili hayo, kwa hivyo fuata maelekezo na uionyeshe Windows 95 mahali sahihi yalipo mafaili ya Windows 95 – inaweza kuwa kwenye CD, au kwenye diskette (A:\) au kwenye jalada, kwa mfano C:\WIN95, ambalo ndani yake umeyanakili mafaili yote kutoka kwenye CD au diskette za Windows 95. 

Kwenye kidirisha kitakachotokezea au kwa kubonyeza Start -> Settings -> Control Panel -> Network -> Identification, utahitaji kuipa kila kompyuta jina tafauti kwenye sehemu ya "Computer Name" – kwa mfano kompyuta moja unaweza kuipa jina "mypc1", na nyengine ukaipa jina "mypc2", n.k. Lakini kwenye sehemu ya "Workgroup", utahitaji kujaza jina sawa kwa kompyuta zote. Kwa mfano unaweza kutumia jina "WORKGROUP" kwenye kompyuta zote. Baada ya kujaza taarifa hizo, ianzishe tena (restart) kompyuta yako. 
 

4. Chagua password ya kuingilia kwenye LAN yako: 

Mara ya kwanza utakapoiwasha kompyuta yako, kitatokezea kidirisha cha kukutaka ujaze jina lako (user name), na password ya kuingilia kwenye Microsoft Networking, yaani kwenye LAN yako. Ingiza jina lolote lile, sio lazima jina lako hasa, na kwa urahisi zaidi wa kukumbuka, unaweza kutumia jina la kompyuta yako kama ulivyoliweka kwenye hatua ya 3 hapo juu. 

Kama hupendi udhia wa kukumbuka password yako, unaweza usijaze chochote kwenye mstari wa password. Lakini ukipenda kuweka password basi tumia neno ambalo ni rahisi kulikumbuka, na utatakiwa uliandike tena kwa uthibitisho. Kama umeweka password au hukuweka password ni muhimu kubonyeza OK, yaani sio ubonyeze Cancel tu. Kama hukubonyeza OK hutaweza kupata huduma za Microsoft Networking. Kwa maneno mengine, ukibonyeza Cancel utaweza kuingia kwenye kompyuta yako tu lakini utakuwa hukuingia kwenye LAN yako. 
 

5. Wezesha majalada na printa kutumika kwenye LAN yako: 

Kwa kutumia Windows Explorer, bonyeza kifungo cha kulia cha mouse juu ya Network Neighborhood, na uchague Properties -> File and Print Sharing. Kama unataka baadhi ya majalada yaliyomo kwenye kompyuta hiyo yaweze kusomwa kutoka kwenye kompyuta nyengine, bonyeza kifungo cha kushoto cha mouse ili uweke tiki kwenye kisanduku chenye maneno "I want to be able to give others access to my files", kama inavyoonekana kwenye Picha 5. 

Picha 5: Kuwezesha mafaili na printa kutumiwa na kompyuta nyengine.

Na kama kompyuta hiyo imeungwa na printa na ungependa watumiaji wa kompyuta nyengine zilizo kwenye LAN yako waweze kuitumia printa hiyo, utahitaji kuweka tiki kwenye kisanduku chenye maneno "I want to be able to allow others to print to my printer(s)". Kama kompyuta yako haikuungwa na printa usiweke tiki kwenye kisanduku hicho. Baada ya kuweka tiki kama unavyopenda, bonyeza OK, kisha bonyeza tena OK, na utahitajika kuianzisha tena (restart) kompyuta yako kabla ya kuweza kuyachagua majalada unayotaka yaweze kusomwa kutoka kwenye kompyuta nyengine. 

Baada ya kuianzisha tena kompyuta yako, tumia Windows Explorer au My Computer, na ubonyeze kifungo cha kulia cha mouse juu ya kila "drive" au jalada (directory) au faili (file) unalotaka liweze kusomwa kutoka kwenye kompyuta nyengine. Chagua "Sharing…" , kisha bonyeza mouse kwenye kifungo cha radio (radio button) cha "Shared As" na ujaze sehemu ya "Share Name" na "Comment". 

Kwa mfano, kama unataka drive C: iweze kusomwa kutoka kwenye kompyuta nyengine zilizomo kwenye LAN yako, jaza "C-Drive" kwenye sehemu ya "Share Name", na jaza maneno "C-Drive on mypc1" kwenye kisanduku cha Comment. Ukifanya hivyo, drive C: ya kompyuta yako na majalada yote yaliyomo ndani yake yataweza kusomwa kutoka kwenye kompyuta nyengine. 

Kwenye sehemu ya Access Type, unaweza kuchagua ama jalada linalohusika liweze kusomwa tu (Read-Only) bila ya mtumiaji wa kompyuta nyengine kuweza kulibadilisha, au hata kulifuta; au unaweza kuwapa watumiaji wa kompyuta nyengine uwezo wa kusoma na pia wa kubadilisha mafaili yaliyo kwenye jalada fulani kwa kuchagua "Full". Ukichagua sehemu ya "Depends on Password", utalazimika kuweka password kwenye sehemu ya Read-Only Password na pia kwenye sehemu ya Full Access Password. 

Mtumiaji wa kompyuta nyengine atalazimika kuandika neno uliloliweka kwenye Read-Only Password ili aweze kupata uwezo wa kulisoma jalada linalohusika. Kama haijui password hataweza kusoma mafaili yaliyo kwenye jalada hilo. Na ili aweze kuwa na uwezo wa kusoma na pia kuyabadilisha mafaili yaliyo kwenye jalada husika, basi itabidi akiulizwa password aandike neno uliloliweka kwenye Full Access Password. Hii ni njia nzuri ya kuhakikisha usalama wa mafaili yaliyomo kwenye kompyuta yako. 

Kuruhusu watumiaji wa kompyuta nyengine waweze kuitumia printa iliyounganishwa na kompyuta yako bonyeza Start -> Settings -> Printers na kwenye kidirisha kitakachotokezea, ibonyezee kifungo cha kulia cha mouse printa yako itakayoonekana na uchague "Sharing…". Bonyeza sehemu ya Shared As na ujaze jina la printa, kwa mfano "HPLaserjet6P", kwenye sehemu ya "Share Name". Kwenye sehemu ya Comment unaweza kujaza maneno kama, "Printer on mypc1". Unaweza pia kuweka password ukitaka, au unaweza usiweke chochote kwenye mstari wa password. 

Hatua ya 3, 4 na 5 zilizotajwa hapo juu, ni lazima zifanywe kwa kila kompyuta iliyo kwenye LAN. 
 

6. LAN yako iko tayari – itumie! 

Unaweza kutumia Desktop au Windows Explorer kuingia kwenye Network Neighborhood. Ukiifungua Network Neighborhood utaweza kuona orodha ya majina ya kompyuta zote zilizomo kwenye LAN yako. Ukiibonyeza mouse mara mbili (double-click) juu ya jina la kompyuta yoyote ile, utaweza kuona orodha ya majalada na printa unazoweza kuzitumia kwenye kompyuta hiyo. 

Majalada ya kompyuta nyengine utakayoweza kuyaona utaweza kuyatumia kama kawaida. Kwa mfano, unaweza kuingiza programu kwenye kompyuta yako kutoka kwenye CD iliyo kwenye CD-ROM drive ya kompyuta nyengine kama CD-ROM drive hiyo imefanywa iweze kusomwa na kompyuta nyengine kama ilivyoelezwa kwenye hatua ya 5. 

Kuweza kuitumia printa iliyounganishwa na moja kati ya kompyuta zilizo kwenye LAN yako, ingia kwenye Start -> Settings -> Printers -> Add Printer na uchague Next, kisha Network Printer –> Next -> Browse -> Entire Network. Ukifanya hivyo utaweza kuziona printa zote zilizo kwenye LAN yako na utaichagua unayoitaka. Ukishakamilisha hatua hizo, kwenye programu yoyote ile utakayohitaji kuchapa kitu kwenye printa unaweza ukaichagua printa hiyo uliyoiongeza kwenye kompyuta yako. 

Mwanzoni tumetaja kwamba unaweza kuzifanya kompyuta zilizo kwenye LAN yako ziweze kutumia modem moja tu. Hiyo inawezekana kabisa lakini kwa bahati mbaya, Windows 95 yenyewe peke yake haina uwezo wa kuzifanya kompyuta zilizo kwenye LAN zitumie modem moja. Lakini kuna programu ya bure inayoitwa WinGate unaweza kuitumia na kwa urahisi kabisa ukazifanya kompyuta zaidi ya moja kwenye LAN yako, zitumie modem moja na line moja ya simu kwa wakati mmoja. Maelezo na taarifa zote zinazohusiana na WinGate zinapatikana kwenye anuani ifuatayo ya World Wide Web: http://www.deerfield.com/wingate/pricing.htm. 

Ziko pia programu nyengine za namna hiyo, kwa mfano SyGate inayopatikana kwenye anuani ifuatayo ya World Wide Web: http://www.sygate.com/prod01.htm. Bei ya SyGate ni US$49 kama unataka kompyuta tatu ziweze kutumia modem moja kwa wakati mmoja; US$99 kwa kompyuta sita; na US$199 kwa idadi yoyote ile ya kompyuta zilizo kwenye LAN yako. 
 

HITIMISHO 

Ukikamilisha hatua sita zilizotajwa hapo juu utakuwa tayari umeitengeneza LAN ya aina ya peer-to-peer kwa kutumia Windows 95 au Windows 98. LAN ya namna hiyo inaweza kukusaidia kukata gharama nyingi. Kwa mfano, kwenye ofisi ndogo yenye kompyuta zaidi ya moja, inaweza kutumika printa moja tu badala ya kununua printa kwa kila kompyuta. Inaweza pia kutumika modem moja tu kwa ajili ya ofisi nzima na hivyo kutohitajika line zaidi ya moja za simu na modem zaidi ya moja za kutumiwa na kompyuta mbali mbali. Kompyuta moja inaweza kutengwa ikawa inahifadhi mafaili yanayotumiwa na watumiaji mbali mbali badala ya kuyaweka mafaili hayo hayo katika kila kompyuta na kupoteza nafasi za hard disk bure. 

Mwisho tunapenda kueleza kwamba, ingawa Windows 95 inaweza kutumika kutengenezea LAN za aina ya peer-to-peer, kabla ya kutolewa Windows 95 zilikuwepo tayari programu-mama za utando (network operating system), kama vile LANtastic, zenye uwezo wa kutayarishia LAN za aina hiyo. LANtastic ina sifa nyingi zaidi ya Windows 95 kwa kutengenezea LAN za aina ya peer-to-peer. Kwa mfano, yenyewe tayari inao uwezo wa kuzifanya kompyuta zilizo kwenye LAN kutumia modem moja tu wakati Windows 95 haina uwezo huo. Lakini kama tulivyowahi kusema, kama cha bure kinaweza kukidhi haja, kuna haja gani ya kutumia cha kununua? Lakini usisahau misemo ya Kiswahili: "Bure yaua!" na "Ukitaka uzuri, sharti uzurike!" 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Maoni  
Kuvuja kwa mitihani: Tuweni wakweli kwa nchi yetu  

Katibu wa Baraza Kuu  azikwa Dar  
Na Mwandishi Wetu  

Ubabe wa madhalimu kuzimwa:  
Na Mwandishi Wetu  

MACHO YA SHUTUMA  
Na Abu Halima Sa Changwa  

Wazo mpachiko (Programmed mind)  
Na Abu Halima Sa Changwa  

Ta'azia: Abbas Shaaban Kilima 1938-1998  

Wasemavyo Wanaharakati  

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 4  
Na Nandenga wa Mkomidachi  

Siri ya Miujiza  
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa  

Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo  
Na Ustaadh Kupa Pazi Said  

Ifahamu Madrasat Ghazal Muslim - Moro  
Na Mussa Ally, Morogoro  

Pamoja na sala, tusimamishe zakah  
Na Abubakari S. Marwillo  

Aina za maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu  
Na. Ramla  

Israi na Miiraji ni miujiza  
Mwandishi: Maalim Bassaleh  

Pamoja na ahadi ya Serikali kuzifuta: kesi za mihadhara zaendelea mahakamani  
Na Muhibu Said  

Waislamu Uluguruni  Moro wazama kwenye matambiko  

Imarisheni miradi ya elimu -  Prof.  Mikidadi  
Na Mwandishi Wetu, Dodoma  

Teknologia: Jifunze Kuunganisha Kompyuta (5)  
Na Hassan Omar  

Mafunzo ya Qur'an  
Shetani anawaogopesha wenye mali kutoa  

Chakula na lishe  
[Kansa ya tumbo]  

Matangazo  
 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita