AN-NUUR 
Na.179 Shaaban  1419, Desemba 11 - 17, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Waandishi andikeni ukweli - Kamati 
Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya kutetea haki za Waislamu imekanusha taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba ina mpango wa kutafuta Msikiti utakaotumika kuwahamasisha Waislamu kulipiza kiasi kufuatia kukamatwa Sheikh wao juma moja lililopita. 

Akizungumza na gazeti hili katikati ya wiki hii, Kaimu Katibu wa Kamati hiyo Bw, Abdul Satar amesema kwamba habari zilizochapishwa na vyombo hivyo zinajaribu kujenga mazingira ya kuhalalisha dhulma dhidi ya Waislamu. 

Akifafanua kauli hiyo, alisema kwanza hao wanaokaririwa na vyombo vya habari kutoa kauli za vitisho ambao wamehusishwa na Kamati si watendaji wa kamati. 

"Mwandishi wa habari ile amemtaja mtu anayeitwa Kalanje kama mmoja wa wanakamati yetu, hili si kweli sisi hatumjui Bwana huyo", alisema Katibu huyo. 

Aidha, alimlaumu Mwandishi huyo kwa kuandika habari bila ya kuzifanyia uhakikisho. 

Mwanzoni mwa wiki hii baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kwamba kufuatia kukamatwa Sheikh Omar Bashir Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu ikiwaongoza wanaoitwa "wafuasi wa Ponda" imekuwa ikisaka Msikiti utakaotumika kujibu mapigo ya serikali dhidi ya Waislamu. 

Aidha, vyombo hivyo viliwakariri baadhi ya watu waliotoa vitisho hivyo na kuwanasibisha na kamati ya kutetea haki za Waislamu. 

"Waandishi wasiandike habari kwa chuki au kwa malengo ya kibiashara bila ya kuzingatia matokeo yake", alisisitiza Katibu wa kamati hiyo. 

Kamati hiyo imetoa wito kwa waandishi kujiepusha na uandishi wa chuki na fitna dhidi ya baadhi ya wananchi. 


Sheikh Jongo aichachamalia Uwawaru
Na Badru Kimwaga

UMOJA wa Waislamu na Wakristo wa Watu wa Rufiji (Uwawaru) umeelezwa kuwa ni kiini macho na wenye lengo la kuwafumba watu macho, hususan Waislamu wenyewe. 

Hayo yalielezwa na Imamu wa Msikiti wa Manyema ulioko Kariakoo Jijini, Sheikh Hamid Jongo alipohutubia mara baada ya swala ya Ijumaa hivi karibuni Msikitini hapo. 

Sheikh Jongo alisema, kuwa umoja huo uliodaiwa kujumuisha Waislamu na Wakristo si umoja kweli, kwani Waislamu hawawezi kuungana na Wakristo katika kuendesha mambo yao yakiwa mojawapo ni kumuabudu Mungu kutokana na kutofautiana kiimani na kudai pengine yeye kama kiongozi wa Kiislamu angeelewa iwapo umoja huo ungekuwa wa mambo ya kijamii tu na sio kiimani kama ulivyotambulishwa. 

Aliongeza kuwa, kwanza umoja huo hauna baraka za viongozi wa Kiislamu wakiwemo Bakwata na kaongeza kwamba Masheikh waliotumbukizwa katika kiza hicho, huenda si Waislamu ila imetumiwa jina la Kiislamu ili kuweza kutekeleza malengo yaliyokusudiwa na watu waliojiundia umoja huo. 

"Sheikh kama Doga yuko huko huko, tena Kibiti tu, lakini hana taarifa, unawezaje kuungana na watu wa nafsi tatu, wakati wewe una nafsi moja ... uongo huu na kiini macho, lipo lililokusudiwa na sio umoja wa Waislamu na Wakristo, kwanza nasikia mikutano yao inafanyiwa Kanisani... Waislamu jiulizeni hawa waliungana nao ni Waislamu kweli au .." alieleza Sheikh Jongo. 

Aliongeza kuwa wale wote walioungana katika umoja huo aliouita kiini macho watakuwa wameritadi kulingana na maelezo ya Mwenyezi Mungu. 

Pia alisema kwa kuwataka Waislamu ambao huenda wamejiingiza katika umoja huo, kwa kutaka fadhila za chakula, nguo na vijipesa, kujitoa mara moja na kuleta shahada mpya, la sivyo watakuwa wanajidanganya na watakuwa wanajichumia dhambi na wakikumbwa na mauti kwa muda huu, watakufa wangali si Waislamu. 

"Ikiwa mnawasilikiza viongozi wa kiserikali, ambao hawatakuongoza katika haki mbele ya Kiama, mimi kama kiongozi wenu, nawaamuru mara moja kujitoa katika umoja huo wa wizi na wenye malengo ya kudhoofisha Uislamu .. najua vijipesa ndivyo vilivyowashawishi ... je ni bora fedha au imani yako itakayokuokoa kiama... umoja gani wa watu wenye kuabudu Mungu wa nafsi tatu na Mungu mmoja...? Aliuliza Sheikh Jongo. 

Alimalizia kwa kutoa ushauri kuwa umoja uliokuwa unakusudiwa ulengwe kwenye taifa ili kuleta mshikamano, kwani tumeunganishwa na serikali yetu ya Tanzania na sio katika imani za watu wa Kiislamu na Wakristo, kwani watu hawa hawaingiani hata chembe kutokana na imani zao kupingana na ikiwa itaendelezwa umoja huo, atakutana na viongozi wa kidini kuweza kujua hatua za kuchukua, kwani ana hakika lengo haswa ni kuharibu imani za Waislamu na si vinginevyo. 



  
Waamriwa kurejesha Mali ya Mirathi
Na Njuki A.

SHEIKH wa kata ya Kikilo wilayani Kondoa amemwagiza Imamu wa Msikiti wa Ijumaa wa Ororimo na ndugu wa marehemu Asia Mohammed warejeshe mali za urithi walizojigawia kwani zoezi hilo limefanywa kinyume na sheria. 

Habari kutoka kijijini hapo zimeeleza kwamba Sheikh Abdallah Mussa Gora ametoa agizo hilo kufuatia kugundulika kwamba mali ya marehemu Asia Mohammed Msala iligawiwa kwa baadhi ya watu wasiostahiki kisheria huku wastahiki wengine wakiachwa. 

Mfano ilielezwa kwamba mtoto mmoja wa marehemu alinyimwa urithi kwa madai kwamba ni mtoto wa nje ya ndoa wakati mali inayorithiwa ni ya mama na si ya baba anayedaiwa kumzaa nje ya ndoa. 

Dosari nyingine ni kwamba Imamu naye alikatiwa sehemu ya urithi pamoja na walioitwa wanakamati ya mirathi wakati hawana fungu kisheria na wala hawakupewa kama hidaya, lakini lakushangaza zaidi ni kwamba Imamu alipata fedha nyingi zaidi kuliko walivyopata warithi wenyewe. 

Ni kutokana na dosari hizo Sheikh Abdallah Musa Gora aliagiza mirathi hiyo igawiwe upya. 


Waislamu Mlimba Moro  
mashakani 

Na Q. Mataita

HALI ya Waislamu Mlimba imeelezwa kuwa ni ya kusikitisha kutokana na Waislamu wachache walio katika eneo hilo kutokufahamu Uislamu wao. 

Akiongea na mwandishi wa habari hizi, mkazi mmoja wa eneo hilo amesema watu walio wengi katika eneo hilo ni Wakristo ambao wamekuwa wakifuga nguruwe holela, kuchinja na kuchoma mishikaki ya nguruwe katika maeneo ambayo kuna mchanganyiko wa Waislamu na Wakristo kama vile karibu na maeneo ya shule ambapo pia kuna kaangwa mihogo. 

Katika kukabiliana na hali hiyo, Waislamu wa Mlimba waliandika barua kwa Katibu Mtendaji wa Kijiji hicho wakimlalamikia ufugaji huo holela wa nguruwe pamoja na uchinjaji na uuzaji wake, barua hiyo ya Waislamu kwa Katibu Mtendaji iliandikwa mwanzoni mwa mwezi wa Agosti mwaka huu, lakini hadi kufikia mwanzoni mwa mwezi Novemba walikuwa hawajapewa majibu yoyote. 

Waliamua kuandika barua nyingine kukumbushia suala lao na kujibiwa kwa mdomo kuwa barua yao imepokelewa na kuahidiwa kuwa hadi itakapofika Desemba 8, mwaka huu suala hilo litakuwa limekwisha shughulikiwa na wahusika kupangiwa maeneo yao maalum kwa ajili ya shughuli zao hizo. 

Lakini imedaiwa kuwa hadi kufikia Desemba mwaka huu wahusika bado walikuwa wanendelea na shughuli zao na pia kulikuwa na ujenzi wa bucha mpya kwa ajili ya kuuzia nyama ya nguruwe. 



  
Vitabu na Mihutasari ya Maarifa ya Uislamu
Vitabu vya Maarifa ya Uislamu shule za Sekondari cha kwanza na cha pili vilivyotayarishwa na Islamic Propagation Centre vinapatikana Ofisi ya ANNUUR Kariakoo, D’ Salaam. 

Muhutasari (silabasi) wa elimu ya Dini Madrasa na shule za Msingi unapatikana pia. 

Halikadhalika Muhutasari (outlines) wa Maarifa ya Uislamu kwa Darsa za watu wazima na vitabu vyake vinapatikana. 

Kitabu cha kwanza na cha pili kwa ajili ya madrasa na shule za msingi viko mbioni kutoka. 

Islamic Propagation Centre
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Maoni
Waislamu tunakusudiwa kufanywa watumwa wa nani?

Wananchi waingiwa na hofu kuhusu silaha

Serikali yagwaya kwa wafugaji nguruwe 
Na Muhibu Said

Hakuna njama za kupindua Bakwata - Sheikh Yahya

MARADHI YA KISAIKOLOJIA:: VOYEURISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Tathmini: Miaka 37 ya uhuru wa Tanganyika
Na Maalim Mwalimu

Adabu katika swala

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo: Batendi hakumuelewa Mkomidachi
Na Ally Said

Muhammad (s.a.w.) katika Unabii wa Isaya  (a.s.)
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa, Korogwe

Ijue SUA Madrasa Moro
Na Mussa Ally, Morogoro

Kiteto wakosa darsa kwa kupinga Ramli

Ustadh ayeyuka na saruji ya Msikiti mjini Arusha

Akina mama Muheza waungana kufanya Daawa
Na B. Mwakangwale

Wanafunzi Waislamu Mbeya wapata uongozi
Na B.  Mwakangwale

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 2
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzima ni nyembamba,  waionao ni wachache - 2
Na Yasin Valerian Massawe

Waandishi andikeni ukweli - Kamati
Na Mwandishi Wetu

Sheikh Jongo  aichachamalia Uwawaru
Na Badru Kimwaga

Waamriwa kurejesha Mali ya Mirathi
Na Njuki  A.

Waislamu Mlimba Moro mashakani
Na Q. Mataita

Sayansi na Teknolojia 
[Ielewe Modem yako] 
 
Mafundisho ya Quran

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Futari ya Tende] 
 
Tangazo
Vitabu na Mihutasari ya Maarifa ya Uislamu
 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita