AN-NUUR 
Na.179 Shaaban  1419, Desemba 11 - 17, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Barua 
 

Uadilifu katika ndoa 

Ndugu Mhariri 

INGAWA nimechelewa kuisoma barua ya ndugu yetu Abdallah A. Abdallah wa Dar es Salaam, nakuomba unipe nafasi katika gazeti lako ili nimpongeze kwa sababu katika barua yake ile amegusa jambo zito linalosumbua ndoa nyingi - Uadilifu. 

Kama tunavyojua ndoa ni kitu kizito kwa watu wengi hasa vijana ambao wanaanza sasa kuingia katika ndoa. Na hapa ndipo ndoa nyingi zinapoharibika na wahusika wakashindwa kuona umuhimu wa kuoa, ama kuolewa kutokana na kushindwa kuvumiliana, kukosoana, kuelimishana na kusameheana. 

Vijana ambao wamepata misukosuko katika ndoa, wanahitaji ushauri mzuri kutoka kwa wazee au walezi, na miongozo mizuri ya kuwafanya wastahamiliane. 

Endapo yatatokea matatizo ya kutokuelewana na wazazi wakashindwa kuyaweka sawa kwa Uadilifu na badala yake wakaangalia upande mmoja kisha wakamuunga mkono kwa vile ni mtoto wao, tusitegemee kupata faida katika ndoa bali tutapata wazururaji na "machangudoa" ambao kwa maana hii au nyingine tutakua tunapenda kuwaona. 

Ushauri wangu kwa wazazi: Kwa sababu vijana wengi wa kike na wa kiume huwa hawajui ugumu wa ndoa, ni vyema kuwa nao karibu ili kuwaongoza na kuwafahamisha yale yote yanayotakiwa kama vile sisi wazee tulivyokuwa tunalelewa na wazee wetu. 

Kwa mfano, kama mtoto wa kike kajakushtakia basi msilikize, kisha mwite na mwanzake (mume wake) ili aeleze bayana. Hapo ndipo itapatikana suluhu kwani mume nae atapata nafasi ya kueleza yake. 

Ikishindikana, si vibaya wazee wa pande zote mbili mukakutana na kuwaweka sawa watoto wenu. Hii ni faida kubwa na tutapata rehema za Allah kwa kuzuia talaka zisizokuwa na lazima. 

Na tuepuke hasa kuwadekeza watoto wetu kwa kujifanya tunawapenda. Kumkumbatia mtoto wa kike kwa maneno aliokushtakia bila ya kufanya utafiti wa kina ili ukajua ukweli si kumpenda bali ni kumfanya awe jeuri akijua kwamba lolote atakalomfanyia mume wake ni sawa kwani mzazi wake anashindwa kumkosoa. Matokeo yake atamaliza waume, waume watamchoka na mzigo ubaki kuwa kwako. 

Kassim Abdallah Naaman, 
Box 125, 
Zanzibar. 



Kura tumewapa sasa zamu yenu kutudhalilisha 

Ndugu Mhariri 

KUMEKUWA na tabia iliyojengeka katika hii awamu ya tatu ya uongozi wa nchi hii ambapo viongozi wa Kiislamu hapa nchini wamekuwa hawana raha kutokana na kamata kamata ya serikali na kuwekwa kizuizini. 

Madai yanayoandamana na kamata kamata hii ni kwamba wanahusishwa na mihadhara inayodaiwa kuwa ya kashfa na kuchochea vurugu za kidini. 

Ni jambo la kusikitisha vipi viongozi wa Kiislamu wanakimbizwa mitaani na kukamatwa kama vibaka! 

Jambo la kujiuliza ni kwamba hali hii kwa Waislamu itaendelea mpaka lini? Au ndio agenda iliyoandaliwa ili kuwashughulisha Waislamu wasizungumzie lolote la maendeleo yao ila matatizo tu? 

Waislamu lazima tutambue kuwa hii ni agenda tuliyoandaliwa ii itushughulishe na kwa ajili hiyo tuwe macho. Tusiwe legelegele namna hii. 

Serikali ambayo inajinadi ni ya ukweli na uwazi, utawala wa sheria bila kujali cheo cha mtu au dini yake leo hii ndio inawafanyia Waislamu namna hii kuwadhalilisha kwa dhulma bila ya makosa yaliyothibitika kisheria, jamani huu ndio utawala wa sheria? Ukweli na Uwazi? 

Kumbe kelele zote zilizokuwa zinapigwa wakati wa uchaguzi lengo lilikuwa kupata kura zetu kisha kutudhalilisha. 

Shamsi, 
Dar es Salaam. 



Hongereni akina mama Zanzibar 

Ndugu Mhariri 

NAPENDA niwapongeze wanawake Waislamu Zanzibar kwa juhudi zao wanazofanya katika harakati za Uislamu. 

Binafsi nimeshuhudia darsa zao, mihadhara yao na ziara mbalimbali wazifanyazo mijini na mashambani kwa ajili ya kuwahamasisha wanawake waishi Kiislamu. 

Naamini kama wanaume nao watatekeleza wajibu wao kama wafanyavyo wanawake, Zanzibar isingeendelea kuporomoka kimaadili kwa kiwango hiki. 

Seif Hamad Suleiman, 
Zanzibar. 



Macho ya shutuma 

Ndugu Mhariri 

Macho ya shutuma , vile vile Wazo mpachiko (Programmed mind) na Abu Halima Sa Changwa zimechemsha bonga za wengi! Twampongeza! 

Tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu amzidishie ilmu na hikma, afya njema na umri tawil ili aendelee kuzirutubisha akili na kuichanganua mioyo ya nduguze, Waislamu zaidi, kwa mengi mengineyo. Inshaalllah. 

Nikimalizia na shukrani zangu kwa wote wanaochangia kulifanikisha gazeti hili lenye ukweli na kupigania haki. 

Bi. F. Salim (al-Khanjary), 
Dar es Salaam. 



Waislamu wa Mafia washangaza ulimwengu 

Ndugu Mhariri 

NAOMBA nafasi katika lako hilo la wanyonge. Kama kichwa cha habari kinavyosomeka hapo juu, katika siku za hivi karibuni huko wilayani Mafia, katika kijiji cha Kirongwe kitongoji cha Bugudadi alifariki mwanamke, mwanzo alikuwa Muislamu na baadaye akaingia katika Ukristo (karitadi). 

Chakushangaza baada ya kifo chake jamaa wa marehemu waliwaambia Waislamu waliohudhuria mazishini kuwa ndugu yao atazikwa Kiislamu, kwani mmoja wa jamaa wa marehemu, baada ya kifo cha huyo ndugu yao, eti alimsilimisha tena marehemu kwa kumwagia maji pamoja na kuchoma moto kitabu chake cha Biblia, na kwa kufanya hivyo eti marehemu huyo ana haki ya kuzikwa Kiislamu. 

Na chakushangaza zaidi alisaliwa ndani ya Msikiti uliopo hapo kitongojini Bugudadi. 
 

S,M. Awadh, 
Dar es Salaam. 



Nusra ina mtazamo gani kuhusu Ukimwi? 

Ndugu Mhariri 

KWANZA kabisa napenda kutoa shukrani zangu pamoja na pongezi kuhusu kuanzishwa kitengo cha Nusra kupitia gazeti hili la AN-NUUR. 

Kwa kweli umuhimu wa kitengo hiki ni mkubwa mno kwa sababu unaunda umoja wa Kiislamu kwa kuwakutanisha Waislamu kutoka sehemu mbalimbali kwa kutumia mtandamo wa INTERNET. Vile vile kitengo hiki kinasaidia kukamilisha lengo la ndoa katika nyanja za upendo, huruma, uzazi pamoja na ushirikiano. 

Kinachonifanya nisukumwe kuandika barua yangu kuhusiana na kitengo cha Nusra ni madhara ambayo yanapatikana baada ya kuwakutanisha Waislamu kwa ajili ya Nusra itokeapo mmojawapo amekwisha ambukizwa virusi vya HIV. 

Hivyo basi, kitengo cha Nusra lazima kiangalie suala la ukimwi, kwa sababu ukimwi ni kifo kwa kuwa hauna dawa. Mimi napenda kushauri kuhusu suala la kuchunguza ukimwi ni suala nyeti, kwani itasaidia kupata jamii ambayo itaendeleza Uislamu hadi kufikia hukumu zake. 
 

Ustaadha Zawadi Salim, 
Popatlal Secondary School, 
Box 5007, Tanga. 

Uchunguzi wa kina hufanyika kabla ya kuwakutanisha wawili - Mtangazaji (Nusra) 



Mh. Alhaj Jumbe unamfafanulia nani 

Ndugu Mhariri 

NIMESIKITISHWA sana na habari iliyojitokeza kwenye gazeti moja la kila siku kwamba Mh. Alhaj Aboud Jumbe katoa ufafanuzi kwamba haendelezi udini. 

Ufafanuzi huo ameutoa kufuatia tuhuma zilizoelekezwa kwake kwamba kwa kuanzisha taasisi ya kidini ya Muslim World Congress analeta udini. 

Kwanza nani anapewa ufafanuzi, kipi cha kuogopa hata ufafanuzi utolewe? Kwani ni Alhaj Jumbe pekee ambaye anajishughulisha na mambo ya dini yake. Huko kwa Wakatoliki hawapo. 

Na hata Mzee wetu akitoa huo ufafanuzi haitawazuia wenye "donge" na chuki zao kuendelea kuhoji. 

 Jummi M. Omary, 
Tanga. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Maoni
Waislamu tunakusudiwa kufanywa watumwa wa nani?

Wananchi waingiwa na hofu kuhusu silaha

Serikali yagwaya kwa wafugaji nguruwe 
Na Muhibu Said

Hakuna njama za kupindua Bakwata - Sheikh Yahya

MARADHI YA KISAIKOLOJIA:: VOYEURISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Tathmini: Miaka 37 ya uhuru wa Tanganyika
Na Maalim Mwalimu

Adabu katika swala

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo: Batendi hakumuelewa Mkomidachi
Na Ally Said

Muhammad (s.a.w.) katika Unabii wa Isaya  (a.s.)
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa, Korogwe

Ijue SUA Madrasa Moro
Na Mussa Ally, Morogoro

Kiteto wakosa darsa kwa kupinga Ramli

Ustadh ayeyuka na saruji ya Msikiti mjini Arusha

Akina mama Muheza waungana kufanya Daawa
Na B. Mwakangwale

Wanafunzi Waislamu Mbeya wapata uongozi
Na B.  Mwakangwale

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 2
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzima ni nyembamba,  waionao ni wachache - 2
Na Yasin Valerian Massawe

Waandishi andikeni ukweli - Kamati
Na Mwandishi Wetu

Sheikh Jongo  aichachamalia Uwawaru
Na Badru Kimwaga

Waamriwa kurejesha Mali ya Mirathi
Na Njuki  A.

Waislamu Mlimba Moro mashakani
Na Q. Mataita

Sayansi na Teknolojia 
[Ielewe Modem yako] 
 
Mafundisho ya Quran

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Futari ya Tende] 
 
Tangazo
Vitabu na Mihutasari ya Maarifa ya Uislamu
 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita