AN-NUUR 
Na.180 Shaaban 28 - Ramadhan 1419, Desemba 18 - 24, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Wasomi Waislamu wawajibike
 
Na Mwandishi Wetu
 
 

ELIMU katika maisha ya mwanaadamu inaweza kufananishwa na dira kwa msafiri; kasoro yoyote itakayokuwa katika dira hii itaathiri safari nzima. Kutokana na msingi huu ndiyo maana jambo la mwanza Allah alilowapa Mitume wake ni elimu, ambayo iliwapelekea wao na ummah zao kumwabudu Allah kwa namna inavyostahiki. Elimu ni vazi la akili, mtu mwenye elimu akili yake imehifadhika. Elimu ndiyo inayomjenga binaadamu. 

Lengo la elimu ni kumbadilisha msomi au msomaji kitabia na kiutendaji katika maisha yake. Hivyo inatarajiwa aliyeelimika atende kwa ufanisi zaidi kuliko yule asiyeelimika. Ndiyo kwa kufanya hivyo Mwenyezi Mungu atawainua daraja wasomi kama alivyoeleza ndani ya Qur’an (58:11) "Enyi mlioamini! Mnapoambiwa (katika mikutano) wafanyieni wasaa wenzenu katika (nafasi) za kukaa, wafanyieni nafasi na Mwenyezi Mungu atakufanyieni nafasi (duniani na akhera) na (hata) ikisemwa "simameni", ondokeni muwapishe wenzenu, basi ondokeni. Mwenyezi Mungu atawainua wale walioamini miongoni mwenu, na waliopewa ilimu watapata daraja zaidi. Na Mwenyezi Mungu anayo habari ya mnayoyatenda yote". 

Nabii Yusuf aliinuliwa daraja na Mwenyezi Mungu kwa sababu alitumia elimu yake kuondoa matatizo katika jamii yake. Jamii ya Nabii Yusuf ilikuwa na viongozi wasiowajali wananchi wao. Alipoona hivyo yeye kama msomi aliomba kazi ya kuendesha uchumi wa nchi: Qur’an (12:55) Akasema (Yusuf) Nifanye mtazamaji wa hazina za nchi (yote) hakika mimi ni mlinzi mzuri na mjuzi hodari". 

Alipochukua kazi ya kuendesha uchumi wa nchi, Nabii Yusuf alitumia elimu yake katika kuwaelimisha watu wa jamii yake namna bora ya kuhifadhi chakula. Lilipotokea baa la njaa katika eneo lile watu wote walikimbilia Misri kuhemea. Nabii Yusuf alisimamia kwa uadilifu sana kazi ya ugawaji wa chakula. Qur’an (12:59) "Na alipowatilia chakula chao alisema: (Mkinijia mara ya pili) nijieni na ndugu yenu kwa baba. Je! Hamuoni ya kwamba mimi ninatimiza kipimo, nani ni mbora wa wakaribishao? Basi nitakukaribisheni nyote kwa uzuri". 

Tumeona jinsi Nabii Yusuf kama msomi alivyoshughulikia matatizo ya watu wa jamii yake. Na kisha Mwenyezi Mungu akampa cheo baada ya kushughulika kwa bidii kuondoa matatizo ya watu wake. Qur’an (12:56): "Basi namna hii tukampa Yusuf cheo katika nchi hiyo ya (Misri); anakaa humo popote anapopenda. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupuuzi malipo ya wafanyao mema. 

Sisi wasomi Waislamu kama warithi wa Mitume tunapata changamoto gani kutokana na kisa cha msomi mwenzetu huyu Nabii Yusuf? Au tumerundika madigrii vichwani mwetu mfano wa yule punda aliyebeba mzigo asijue ndani kuna nini? 

Kama sote tunavyoelewa jamii ya watu wowote wale inategemea sana wasomi wake katika kuleta maendeleo na ustawi wa jamii hiyo. Wasomi wa fani mbalimbali ndiyo mhimili wa kutafsiri. kushauri na kuielekeza jamii yao kuhusu matukio au matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii. 

Si busara kwa wasomi kujiweka mbali na jamii zao na hivyo kusababisha matabaka baina ya wasomi na wasiosoma. Jamii ina lengo moja, kwa hiyo wasomi watimize wajibu wao kama wasomi na wasiosoma vile vile wana sehemu yao katika kukamilisha lengo. Jambo la kushangaza wasomi Waislamu wamejiweka mbali na matatizo yanayoikabili jamii ya Kiislamu utadhani hayawahusu. 

Hawajiulizi kwa nini Makanisa na Mahekalu ya Wahindi yanaongozwa na wasomi kama wao, lakini Misikiti inaongozwa na watu wasiokuwa na elimu ya kutosha? Leo Msikiti unashindwa hata kuwa na wahasibu wa kudhibiti mapato na matumizi ya Msikiti wakati waumini wanatoa michango kila siku. 

Waislamu wanadhulumiwa viwanja vyao na nyumba zao za Wakfu wakati wanasheria Waislamu wapo! Wana faida gani hawa na jamii ya Kiislamu? Ila wakifa ndiyo wanakimbiziwa Misikitini kuja kuombewa na waumini! Waumini wanawapenda lakini wao hawajali mapenzi yao. 

Wachumi tunao wengi tu, lakini hata siku moja hawajakaa na waumini Misikitini kuwalekeza namna ya kubuni mipango ya uchumi ya Waislamu. Angalau wasaidie namna ya kuanzisha na kusimamia mifuko ya maendeleo ya Waislamu. Kina mama wakopeshwe mitaji ya kuanzishia biashara ndogo ndogo na kadhalika. Wachumi wetu ni mabingwa wa kulaumu tu bila ya kutoa ufumbuzi: "Waislamu wenyewe hawataki kujishughulisha". Wajishughulishe na nini? Nani atoe maelekezo ya kitaalamu? 

Wahasibu wapo pia; lakini hawataki kutumia taaluma zao kwa manufaa ya Waislamu wenzao. Misikiti inakosa watu wa kudhibiti mapato na matumizi. Michango yote ya waumini inaishia kwenye mifuko ya kanzu za watu; na hivyo kila tatizo linapotokea waumini wanachangishwa tena. Kumbe tungekuwa na wahasibu tu ambao wangeweza kuweka akaunti za Msikiti na mambo yangeenda sawa. 

Madaktari Waislamu hawajawahi hata siku moja kuwatembelea waumini Misikitini na kuwapima afya zao. Tunao madaktari bingwa, wengine Maprofesa lakini wanashindwa kubuni hospitali moja tu yenye kufuata maadili ya Kiislamu katika kutoa tiba. 

Wake zetu, mama zetu na dada zetu wanahudumiwa na wakunga wanaume katika mahospitali yenye mfumo wa kitwaghuti na madaktari Waislamu wapo tena wengine ni Matabligh wala hawajisikii vibaya. 

Hivi kuna ubaya gani kama waalimu nao wangeweka "notes" kwenye maktaba za Misikiti ili wanafunzi wanaoshindwa kulipia gharama ya ‘tuition’ nao wapate kusoma. Hii shughuli itaendeshwa na nani kama si walimu? Walimu ndiyo wanaotarajiwa kutoa mchango mkubwa kwa jamii ya Waislamu kuliko wanataaluma wengine wowote wale kwa sababu walimu ndiyo chimbuko la watalaam wa fani zote nyingine. 

Wahandisi na wasanifu majengo Waislamu wamekuwa si wabunifu ni watu wa kukopi tu michoro na majengo yenye mwelekeo wa Kiyahudi na kinasara. Wanashindwa hata kutambua kwamba Waislamu wana sanaa yao ya majengo inayokwenda sambamba na maadili yao. Utakuta majumba mengi ya Waislamu vyoo vyake vya kukaa wakati hivyo havikubaliki katika mila ya Kiislamu, vyoo vingi vinaelekea Kibla wakati ni makosa kwa Muislamu kujisaidia wakati ameeleka nyumba tukufu. Isitoshe nyumba nyingi za Waislamu hazikujengwa kwa madhumuni ya kuchunga maadili ya familia na maingialino yasiyo na adabu kati ya wanaume na wanawake. 

Lawama hizi wanastahili wahandisi majengo na wasanifu majengo Waislamu. Hawako karibu na jamii yao ya Kiislamu ndiyo maana wanashindwa kutoa ushauri kwa Waislamu kuhusu makazi ya Waislamu. 

Wanasosholojia wetu ndiyo hao tena mabingwa wa kumomonyoa maadili ya Waislamu badala ya kuwajenga. Hodari sana wa kuandika upuuzi magazetini. Jamii ya Kiislamu imekosa mwelekeo na watalaamu wa sayansi ya jamii wapo lakini hawafanyi lolote. 

Wanasahau wajibu na majukumu yao kwa ummah wa Kiislamu. 

Waislamu tunao mabingwa wa shariah Qur’an, Hadith na fani zote za Kiislamu. Lakini wako wapi na wanafanya nini kuunusuru ummah wa Kiislamu? Wamebaki kung’ang’ania utukufu tu Misikitini utadhani Uislamu unaishia Misikitini. Kuna sababu gani ya migogoro ya ndoa za Waislamu ipelekwe TAMWA au kwenye mahakama za kitwaghuti wakati wasomi wetu tunao? Hivi wanashindwa kabisa kuunda chombo cha kusimamia ndoa na mirathi ya Waislamu? 

Wanaotanabahi ni wale wenye akili tu ambao wanatumia elimu zao kwa malengo yaliyokusudiwa. Kinyume cha hapo huwa ni wasomi wajinga (educated fools). Je afanyae ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama kuogopa Akhera na kuwa asiyefanya hivyo? Sema: Je wanaweza kuwa sawa wanaojuwa na wale wasiojuwa?" Wanaotanabahi ni wale wenye akili tu. (39:9). 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri
Umaskini unachafua mazingira!

Mauaji ya Mwembechai: Spika wa Bunge aombwa atoe gharama za kuunda Tume

UWAWARU yafa Rufiji

UN yaidhinisha udhalimu wa Marekani

Qur’an yachomwa moto Shinyanga

Marekani yadhihirisha Ubeberu wake

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: SEXUAL SADISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Kitengo cha Zaka chazinduliwa Dar

Tume ya Jiji kubomoa Msikiti wa vipofu

Akheri ya zamani
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC. USA

UWAWARU yaleta nusura Ikwiriri

Tamko la Masjid NNUUR juu ya kuanzishwa kwa UWAWARU

Kuanzishwa kwa UWAWARU

Wasomi Waislamu wawajibike
Na Mwandishi Wetu

Albucasis  936 - 1013 (CE)

Ijue Uhuru madrasa - Morogoro

Madrasa Akhlaqil Islamiya yapiga hatua

MADRASATUL Husseiniyi Shadhily
Na Jamillah Nassoro
 
Hatimaye kesi ya kushambulia kituo nayo yafutwa

Changieni vyombo vya mihadhara - Sheikh Said

Misikiti yakosa maji ya kutawadhia

Bakwata Tanga haifuati katiba yake

Sheikh Mbukuzi ataka Waislamu watafute radhi za Allah

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 3
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache - 3
Na Yasin Valerian Massawe

Sheikh Omar Bashir afikishwa mahakamani

Mufti pekee kuidhinisha watu kufunga

Nguruwe wanaofugwa maeneo wanayoishi watu kusababisha magonjwa ya kuambikiza

200 wamesilimu

Sayansi na Teknolojia 
[Kuiweka Modem kwenye Kompyuta] 
 
Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Mlo wa Daku] 
 
Tangazo 
New Book: The untold story of the Muslim struggle against British Colonialism in Tanganyika. 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita