|
|
Waislamu
kijijini Kidunda Moro wahitaji mwalimu
Sheikh huyo Yusuf Issa (Sheikh Rule) ambaye amehamia kijijini hapo tangu mwaka 1994 akitokea Dar es Salaam, alianzisha madrasa katika Msikiti wa kijiji hicho, lakini alisimamisha kufundisha kwa madai ya kuhamia ndege hali inayopelekea kufa kwa madrasa hiyo ambapo watu wazima wapatao 77 walijitokeza kusoma. Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo umeonyesha kuwa mara Waislamu hao walipoona mwalimu wao (Sheikh Rule) ametingwa na shughuli nyingi wakaamua kujenga madrasa ya nyasi pembeni mwa nyumba ya Sheikh huyo wakati mwenyewe akiwa safarini Dar es Salaam. Sheikh Issa aliporejea kijijini hapo alishtushwa na hali ya kujengwa kibanda karibu na nyumba yake ndipo alipoamua kuwaita wazee na vijana hao na kudai kuwa amevamia. Hata hivyo, vijana walimueleza Sheikh huyo kuwa wameamua kujenga madrasa ile pale ili aweze kuwafundisha lakini Sheikh huyo kwa muda mrefu akawa hajaliafiki suala hilo kwa madai ya kupangiwa maisha yake. Uchunguzi umeendelea kuonyesha kuwa Sheikh huyo ambaye amefundisha vijana wa kijiji hicho kwa muda usiopungua miaka miwili alikuwa anamtegemea kijana mmoja kusaidia kufundisha ambapo naye imedaiwa na wanakijiji hao kuwa ameliwa na mamba wakati akivuka mto yeye na wenzake. Akiongea na mwandishi wa habari hizi, mmoja wa wanakijiji hicho ambaye alidai ni Mwenyekiti wa madrasa isiyo hai Bwana Saidi Mdumka amesema kuwa kijiji chao kina Waislamu wengi lakini hakuna Masheikh wa kufundisha ambapo hata Msikiti wao wa Ijumaa wameugeuza kuwa Msikiti wa kuswalia wakati wa Iddi tu. Naye kijana mmoja aliyejitambulisha kuwa ni Katibu wa madrasa hiyo Bwana Hassani Mwamila amesema kuwa katika kijiji chao chenye watu wazima wasiopungua 3,000 na watoto wasiopungua 2,000 kina majuzuu matatu ambayo yameanzia Fatiha (Alhamdu) na msahafu mmoja ulioanzia sura za katikati na karatasi nyingine zikiwa zimechanika. Uchunguzi umeendelea kuonyesha kuwa watu wengi wa kijiji hicho cha Kidunda
hawawezi hata kujiendeshea ibada hali iliyofanya Msikiti wao uliojengwa
kwa miti na kuezekwa na nyasi kuwa nyumba ya paka na wadudu wengineo kutokana
na kutotumiwa na Waislamu wa eneo hilo.
Waislamu Mtwara wadai jengo la Wakfu kwa CCM WAISLAMU kijiji cha Mahuta kata ya Mahuta mkoani Mtwara wamo katika harakati za kudai jengo lao la madrasa ambalo lilitolewa wakfu na Jumuiya ya Waislamu Aga Khan ambalo CCM imelikalia kwa muda mrefu na hatimaye kulikodisha jengo hilo kwa mfanyabiashara mmoja ambaye amefungua mashine ya kusaga. Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na baadhi ya wananchi wa Mahuta waliotembelea Jijini hivi karibuni, Jumuiya ya Aga Khan ilitoa Wakfu jengo hilo ambalo lilikuwa likitumika kama shule kwa Waislamu katika miaka ya sitini. Baada ya kutolewa wakfu, Sheikh maarufu kijijini hapo Sheikh Ali alihamishia madrasa yake katika jengo hilo na kuifanya madrasa hiyo kuzidi kuaminika kutokana na kupokea wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo nje ya nchi kama vile Msumbiji n.k. Wakati Sheikh Ali akiendelea kuendesha madrasa katika jengo hilo, serikali ya kijiji iliomba nafasi ya kuendesha masomo ya shule ya msingi katika jengo hilo la madrasa huku wakisubiri majengo yaliyokuwa yakijengwa kwa ajili ya shule ya msingi yakamilike. Waislamu walikubaliana na maombi ya serikali ya kijiji na hivyo jengo hilo likawa linatumika kwa zamu; masomo ya shule ya msingi yakawa yanaendeshwa asubuhi wakati masomo ya dini yakiendeshwa jioni. Hali iliendelea hivyo mpaka majengo ya shule yalipokamilika na kuhamiwa na kuwaachia Waislamu jengo lao. CCM ilipoanzishwa serikali ya kijiji ikaomba tena nafasi katika jengo hilo kwa ajili ya kutaka kuendeshea shughuli za chama huku wakisubiri majengo ya ofisi yakamilike. Kwa mara nyingine Waislamu walikubali, hata hivyo, shughuli za chama zilizokuwa zikiendeshwa katika jengo hilo la madrasa zilisababisha kero na bughudha kwa wana madrasa na kulazimika Sheikh Ali kuihamisha madrasa hiyo katika jengo lingine lililojengwa kwa ajili ya kuepuka kero hiyo. Majengo ya ofisi za CCM yalipokamilika shughuli za chama zikahamishiwa katika maofisi hayo. Imeelezwa kwamba hata baada ya kuhama katika jengo hilo la madrasa na kuhamia katika majengo yao, CCM haikurejesha jengo hilo tena kwa wenyewe Waislamu. Bali walichofanya ni kulikodisha kwa mfanyabiashara mmoja kijijini hapo ambaye amefungua mashine ya kusaga. Baada ya CCM kupokea kodi ya jengo hilo la Waislamu kutoka kwa mfanyabiashara huyo kwa miaka mingi, hivi karibuni Waislamu wa kijiji cha Mahuta ndio wamezindukana na kuanza kudai haki yao. Vikao viwili vikubwa vimeshakaliwa kuzungumzia uwezekano wa jengo hilo kurejeshwa kwa Waislamu lakini mpaka sasa Waislamu hawajafanikiwa. Wakati huo huo, imeelezwa kwamba kwa muda mrefu sasa tokea gazeti la
AN-NUUR kupunguzwa bei kwa mikoa ya kusini, gazeti hilo halijafika kijijini
Mahuta. Aidha imedaiwa kwamba kwa hivi sasa gazeti la AN-NUUR linaishia
mjini Newala.
Wakati Makanisa yakimeremeta: Msikiti wageuka gofu Sanya Juu HALI ya Misikiti wilayani Hai imeelezwa kwamba ni ya kusikitisha kutokana na uchakavu wake na kutokutunzwa. Hali hiyo imekuwa ni tofauti na Makanisa mapya kujengwa kila leo yale makongwe yamekuwa yakifanyiwa ukarabati ikiwa ni pamoja na kupakwa rangi. Hali hiyo ya kutoitunza na kuithamini Misikiti imeelezwa kwamba inatokana na ari ndogo, upeo mdogo na elimu ndogo waliyonao wengi wa Waislamu wa eneo hilo juu ya dini yao. Hali hiyo imekuwa ikitoa mchango mkubwa kwa Waislamu wengi kujishughulisha zaidi na mambo yao binafsi kuliko kuishughulikia dini yao. Kwa mujibu wa taarifa za wanaharakati mbalimbali waliotembelea eneo hilo hivi karibuni pamoja na kuwa Wakristo ni wengi ikilinganishwa na Waislamu lakini pia wana ari kubwa na hamasa za kimatendo kuishughulikia dini yao. Katika jitihada za hivi karibuni za kuwazindua Waislamu, Sheikh Kimaro wa Sanya Juu amewataka Waislamu kuunusuru Msikiti wa Fuka ambao upo katika hatari ya kuanguka. Akitoa taarifa hizi Sheikh wa Mtaa, Bashir A. Kimaro alisema kuwa Msikiti wa Fuka ambao una miaka ishirini na tano umefikia katika hali ya kukatisha tamaa na kuwaweka waumini wanaotumia Msikiti kuweza kuangukiwa; na idadi ya waumini wa Msikiti huo ni wachache sana na wameshindwa kuundeleza. Msikiti wa Fuka ambao una eneo la hekta mbili una malengo ya kuanzisha madrasa, zahanati na shule ya awali kwa watoto wadogo. Sheikh Kimaro amewaomba Waislamu wa mkoa wa Kilimanjaro na wale ambao wako nje ya mkoa, watume misaada yao hususan vifaa vya ujenzi ili Msikiti upate uhai wake. Akitilia uzito taarifa hizo kijana
Mussa Mohammed ambaye ni mwanafunzi wa sekondari aliyeko hapo likizoni
alisema hali ya hapo inawasikitisha sana kuwa na Msikiti mbovu kama huo,
na watoto hukosa kituo cha kuwalea, hali ambayo inapelekea watoto kukosa
malezi ya Kiislamu.
|
YALIYOMO
Tahariri
Baada ya wanafunzi Wakristo kusherehekea Krismasi: Wanafunzi Waislamu kuikosa Id el Fitr Hoi hoi zatawala ziara ya Mwinyi Mwanza Waislamu Tunduma waswali ndani ya kilabu cha ulanzi MARADHI YA KISAIKOLOJIA: FROTTEURISM Barabara za Tabora zimepitwa na wakati Jicho la
Uzalendo: Nihiari yetu kuendelea kujidanganya!
Kuanza na kwisha mwezi wa Ramadhani Taarifa ya Kamati juu ya yaliyotokea Mwembechai Maazimio ya kongamano la wanawake wa Kiislamu Waislamu kijijini Kidunda Moro wahitaji mwalimu Waislamu Mtwara wadai jengo la Wakfu kwa CCM Wakati Makanisa yakimeremeta: Msikiti wageuka gofu Sanya Juu Sheikh Khalifa Suleiman afariki dunia Sheikh wa wilaya ya Lushoto afariki Ijue Madrasat Riyaadhwa ya mjini Dodoma Mwinyi apongeza juhudi za kulea yatima Mwanza Tuhuma za kupindua uongozi wa Bakwata: Sheikh Hamim Boza akanusha kuhusika Kuongezeka kwa ajali za barabarani Njia ya
uzimani ni nyembamba, waionao ni wachache - 4
Saggaf awataka watoto wahifadhi Qur'an Waislamu watakiwa kujitolea kupigania dini yao Kesi nyingine Mwembechai yaahirishwa Sayansi
na Teknolojia
Chakula
na lishe
|