|
|
| Sheikh
Khalifa Suleiman afariki dunia
MKOA wa Kilimanjaro na Waislamu wote kwa ujumla wamefikwa na msiba kwa kuondokewa na mmoja wa Maulamaa wake, Sheikh Khalifa Suleiman. Sheikh Khalifa Suleiman alifariki alfajiri ya Jummosi Desemba 19, 1998 katika hospitali ya KCMC na alizikwa siku hiyo hiyo nyumbani kwake Usangi Kighare. Sheikh Khalifa alizaliwa mwaka 1943 huko Usangi Kighare. Alipata elimu yake ya msingi huko huko Usangi kabla ya kujiunga na vyuo mbalimbali kusoma elimu ya dini. Sheikh wake wa awali alikuwa Sheikh Omar Mzimu kabla ya kujiunga na Chuo cha Ufundi Kirongwe. Sheikh wake aliyefuatia alikuwa Sheikh Rajabu Hussein, kisha Sheikh Jabir wa Gonja. Miongoni mwa Masheikh wakubwa wakubwa aliosoma kwao ni Al-Marhumu Sheikh Amir wa Tanga, Sheikh Mohamed Mkanga na Sheikh Hemed bin Juma bin Hemed. Sheikh Khalifa ni miongoni mwa Masheikh wachache waliotoa mchango mkubwa sana katika kueneza elimu ya Uislamu mkoani Kilimanjaro. Atakumbukwa sana kwa darsa zake za tafsiri ya Qur’an alizokuwa akiziendesha katika Msikiti wa Kilaweni na Kighare. Aidha, wengi watamkumbuka kwa mawaidha na nasaha zake mbalimbali alizokuwa anazirikodi katika kanda na kuzisambaza kwa wasikilizaji. Waislamu wa Misikiti ya Kilaweni na Kighare pamoja na wale wa pembezoni, wamekuwa waathirika wa aina yake kwa kulikosa darsa rasmi la tafsiri ya Qur’an katika mwezi wa Ramadhani ambalo Sheikh Khalifa amekuwa akiliendesha kila mwaka. Mwaka huu hakuwahi kulianza kwani alifariki alfajiri ya kuamkia Ramadhani Mosi. Mwenyezi Mungu amrehemu Sheikh Khalifa Suleiman. Innalillah Wainailaihi
Rajiun.
Sheikh wa wilaya ya Lushoto afariki SHEIKH wa wilaya ya Lushoto, Sheikh Sufian Mzimbiri amefariki dunia Desemba 3, 1998 baada ya kuugua kwa karibu miezi minne na kuzikwa kijijini kwake Desemba 4, 1998. Sheikh Sufian Mzimbiri amefariki akiwa na umri wa miaka 81, ameacha wajane wawili, watoto 17 na wajukuu 64. Amekuwa Sheikh wa wilaya hiyo kwa miaka 34 tangu ateuliwe na aliyekuwa Sheikh wa wilaya Sheikh Seif Daraja mwaka 1964 ambaye aliamua kupumzika kutokana na kudhoofu afya yake kutokana na umri mkubwa. Miongoni mwa juhudi kubwa alizofanya Sheikh Sufian ni kuanzisha madrasa za watoto na watu wazima wilaya nzima pamoja na kuanzisha elimu ya pamoja kwa walimu wa madrasa kwa wilaya nzima ya Lushoto. Miongoni mwa wanafunzi wake ambao kwa sasa ni Masheikh wakutumainiwa wilayani humo ni Sheikh Kassim Shekimo, Sheikh Rashidi Mzimbiri, Sheikh Hassan pamoja na Sheikh Abbasi Athumani. Sheikh Sufian Mzimbiri kabla ya kifo chake aliwateuwa Masheikh wa majimbo makuu matatu ambayo ni Lushoto, Mlalo na Bumbuli na viongozi wa tarafa nane ambazo ni Lushoto, Mlola, Mtae, Soni, Bumbuli, Mlalo, Mgwashi na Umba. Sheikh Sufian alimteua Sheikh Abbasi Athumani kuchukua nafasi yake baada
ya kuona afya yake imedhoofu.
|
YALIYOMO
Tahariri
Baada ya wanafunzi Wakristo kusherehekea Krismasi: Wanafunzi Waislamu kuikosa Id el Fitr Hoi hoi zatawala ziara ya Mwinyi Mwanza Waislamu Tunduma waswali ndani ya kilabu cha ulanzi MARADHI YA KISAIKOLOJIA: FROTTEURISM Barabara za Tabora zimepitwa na wakati Jicho la
Uzalendo: Nihiari yetu kuendelea kujidanganya!
Kuanza na kwisha mwezi wa Ramadhani Taarifa ya Kamati juu ya yaliyotokea Mwembechai Maazimio ya kongamano la wanawake wa Kiislamu Waislamu kijijini Kidunda Moro wahitaji mwalimu Waislamu Mtwara wadai jengo la Wakfu kwa CCM Wakati Makanisa yakimeremeta: Msikiti wageuka gofu Sanya Juu Sheikh Khalifa Suleiman afariki dunia Sheikh wa wilaya ya Lushoto afariki Ijue Madrasat Riyaadhwa ya mjini Dodoma Mwinyi apongeza juhudi za kulea yatima Mwanza Tuhuma za kupindua uongozi wa Bakwata: Sheikh Hamim Boza akanusha kuhusika Kuongezeka kwa ajali za barabarani Njia ya
uzimani ni nyembamba, waionao ni wachache - 4
Saggaf awataka watoto wahifadhi Qur'an Waislamu watakiwa kujitolea kupigania dini yao Kesi nyingine Mwembechai yaahirishwa Sayansi
na Teknolojia
Chakula
na lishe
|