AN-NUUR 
Na.181 Ramadhan 1419, Desemba 25 - 31, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Matajiri wahimizwa kutoa zaka

KITENGO cha zaka na sadaqa kijulikanacho kama Dar es Salaam Yemen Community For Charity and Culture, kimehimiza utoaji wa zaka kwa wale wote wenye kustahiki. 

Kitengo hicho kimesema iwapo nguzo ya zaka itatekelezwa vilivyo itapunguza umasikini miongoni mwa waumini kwani umasikini unapunguza amani. 

"Si Muislamu anayeshiba na kumwacha jirani yake na njaa", kimesema kitengo hicho katika moja ya makabrasha yake yanayohimiza utoaji wa zaka. 

Kuhimiza utekelezaji wa amri hiyo miongoni mwa waumini, kitengo hicho kimefafanua suala la zaka, viwango vyake, wakati wa kulipa, wanaostahiki kupewa na umuhimu na faida ya kutoa zaka. 

Katika hafla ya kugawa vifaa na zawadi mbalimbali iliyofanyika juma moja lililopita, kitengo cha zaka kilieleza hatua kadhaa inazokusudia kuzichukua ili kuboresha shughuli ya ukusanyaji wa zaka na kuzigawa kwa wanaostahiki. 

Mwenyekiti wa kitengo hicho Bw. Said al Jabri alizieleza hatua hizo kuwa ni pamoja na kubadilisha mfumo mzima wa ugawaji wa zaka. 

Alisema siku za nyuma waligawa zaka kwa kuzingatia makundi yaliyotajwa katika Qur’an, lakini walitoa pesa taslimu. Alisema mtindo huu haukuwa ukilenga kutatua tatizo la msingi la muhusika. Pesa hizo ziliweza kutumiwa kwa namna tofauti na hivyo kutotatua tatizo la umasikini. 

Bw. Abri alisema kuanzia sasa kitengo chake kitagawa zaka kwa wanaostahiki kwa kuangalia shughuli ya kudumu anayoweza kuifanya muhitaji ili zaka hiyo iwe kama mtaji wake. 

"Mtindo huu tunatarajia utaweza kuongeza idadi ya watoaji zaka kama sio kutufikisha katika hali ya kuisha kwa wanaostahiki kupewa zaka katika eneo letu", Hii imewahi kutokea wakati wa maswahaba. 

Kitengo cha zaka kilianzishwa rasmi mwanzoni mwa mwaka huu kikiwa na malengo ya kufuta umaskini miongoni mwa wananchi hususan Waislamu. 



Saggaf awataka watoto wahifadhi Qur’an 

WAISLAMU wametakiwa kuwapeleka watoto wao Madrasa ili wakajifunze Qur’an kwa kuhifadhi na kuielewa maana yake. 

Hayo yamesemwa na Mh. Hashim Saggaf katika tamasha la mashindano ya kuhifadhi Qur’an ambalo lilifanyika hivi karibuni katika shule ya Al-Hijra mjini Dodoma. 

Mheshimiwa Saggaf alikuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo ambayo yalidhaminiwa na shirika la Kiislamu la misaada la kimataifa (Internatinal Islamic Relief Organization). 

Mheshimiwa Saggaf aliwaeleza wazazi waliohudhuria tamasha hilo kuwa Qur’an ni kitabu kinachoonyesha miujiza yake Mwenyezi Mungu, kwa kubaki katika hali ya ukamilifu na usahihi wake tangu kiliposhuka na kitabaki hivyo hadi mwisho wa ulimwengu. 

Aidha, aliwaeleza wazazi kuwa pamoja na Qur’an kuwa katika hafadhi ya Allah (s.w.) na sisi Waislamu hawana budi kuienzi kwa kuihifadhi. 

Mheshimiwa Saggaf ambaye ni mbunge wa Dodoma Mjini aliwahimiza Waislamu juu ya kutafuta elimu ili waweze kuwa Makhalifa wa Allah (s.w.) hapa ulimwenguni. 

Pia aliwataka Waislamu wa Dodoma wawe na moyo wa kujitolea ili waweze kuleta maendeleo kwa kuwa na vituo vya kutoa huduma, kama mashule, zahanati na miradi mengine ya uchumi. 

Mashindano hayo ya Qur’an yaliwakusanya zaidi ya wanafunzi 36 kutika katika madrasa mbalimbali za hapa Dodoma, na kusimamiwa na mwakilishi wa I.I.R.O kwa mkoa wa Dodoma Ustadh Khatibu Mussa, akishirikiana na Mwenyekiti wa maandalizi Sheikh Abdullazizi wa Masjid Bilal. 

Akitoa taarifa fupi, Ustadh Khatibu alisema washindi watakaopatikana watakwenda Dar es Salaam kwa mashindano ya kitaifa, na huko watapatiwa zawadi kubwa zaidi. 

Jumla ya majaji wanne walishiriki kikamilifu ili kuwapata washindi halali, majaji hao walikuwa Sheikh Ahmed Saidi kutoka Masjid Manyema, Sheikh Mohamed Mafita kutoka Masjid Al-Hudaa, Ustadh Mohamed Saidi na Ustadh Al-Amin. 

Washindi 16 walipatikana waliohifadhi Qur’an kuanzia juzuu mbili hadi kumi na tano walipewa zawadi ikiwa ni pamoja na fedha taslim, vyeti, Radio, misahafu, kanzu na vitabu mbalimbali vya Kiislamu. 

Washindi waliohifadhi juzuu mbili walikuwa, Juma Hamisi, Issa Othmani Adam na Haji Binde. Juzuu tatu ni Abdallah Daruwesh, Shufaa Saidi na Abubakari Zuberi. 

Wengine waliohifadhi juzuu tano ni Mohamed Abdallah na Omari Issa. Juzuu sita ni Aisha Maulidi na Rahma Juma na Juzuu kumi ni Yasin Yusuf Kai, Hassani Hamisi na Mohamed Abbasi. Wakati washindi wa juzuu kumi na tano walikuwa Hamisi Juma na Omar Said. 

Wakati huo huo, Imam wa Masjid Nunge Sheikh Ahmed Zuberi amelishukuru shirika la Kiislamu la misaada la kimataifa kwa kudhamini mashindano ya kusoma Qur’an ya kuhifadhi katika mkoa wa Dodoma kwa mara ya pili mfululizo. 

Sheikh Zuberi alitoa shukrani hizo katika tamasha la ufunguzi wa mashindano hayo ya kusoma Qur’an. 

Sheikh Zuberi alisema hii ni fakhari kubwa kwa Waislamu wa Dodoma hasa wale washindi wote wawili waliopatikana mwaka jana (1997) walitokea Dodoma. 

Sheikh Zuberi alisema washindi hao walikuwa mabalozi si kwa Dodoma tu bali hata kitaifa huko Dar es Salaam, kwani walishinda na kuweza kupata zawadi ya kupatiwa tiketi za Makkah na Madina kwa kufanya ibada ya Umra, akiwataja mabalozi hao wa nchi kwa usomaji wa Qur’an kwa hifadhi aliwataja kuwa ni Hamisi Juma na Saidi Omari Saidi. 

Aidha, Sheikh Zuberi aliwasisitiza wazazi na walimu kuwa watoto wasome Qur’an kwa kuhifadhi na kuijua maana yake. Kwa kufanya hivyo ndiyo itakuwa njia pekee ya kuilinda Qur’an isipotoshwe na maadui. 


Waislamu watakiwa kujitolea kupigania dini yao

WAISLAMU wamekumbushwa wajibu wao wa kujitolea mali zao na nafsi zao ili kuipigania dini yao tukufu na kufikia kwa salama lengo lake kwa ujumla. 

Nasaha hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Utamaduni na Da’awah ya shirika la Kimataifa la World Muslim Congress, Sheikh Abubakar Mwilima katika kikao cha kubadilishana mawazo juu ya malengo ya shirika hilo baina ya kamati yake na Maimamu wa Jijini Dar es Salaam. 

Kikao hicho kilifanyika katika ofisi za shirika hilo zilizopo mtaa wa Uhuru, Kariakoo Jijini Dar es Salaam, Jumamosi ya Desemba 19, mwaka huu. 

Sheikh Mwilima alisema kuwa kiukweli wapo Waislamu nchini wenye uwezo ambao wanaweza kufanya mambo makubwa na muhimu kwa manufaa ya Uislamu na Waislamu. 

Alitoa mfano kwamba iwapo kila mkulima mmoja Muislamu wa Bukoba atajitolea sehemu ya mavuno yake ya zao la ndizi kwa ajili ya kuendeleza Uuislamu, yatosha kwa mchango wake huo kujenga mjini humo hospitali moja kubwa ya Kiislamu. 

Kwa hali hiyo, Sheikh Mwilima alisema inasikitisha kusikia kuwa hata mwalimu wa madrasa anayejitolea kuwasomesha watoto Uislamu analipwa kima cha kwanza cha mshahara wa kazi yake hiyo nzito shilingi 5,000 (elfu tano) wakati Waislamu wenye uwezo wapo. 

"Kwa kweli wapo Waislamu wengi tu wenye uwezo wa kufanya mambo makubwa bila ulazima wa kungoja msaada kutoka nje", alisema Sheikh Mwilima 
 


Kesi nyingine Mwembechai yaahirishwa 

KWA mara nyingine tena kesi ya tuhuma ya kufanya "ghasia" maeneo ya Mwembechai, Jijini Dar es Salaam iliyofunguliwa na serikali katika mahakama ya Kivukoni, Jijini dhidi ya Waislamu kumi imeahirishwa hadi Januari 29, mwakani, tarehe ambayo inatazamiwa tena kuanza kusikilizwa. 

Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa mahakamani hapo mapema Desemba 21, mwaka huu, ambapo mashahidi wa upande wa serikali walitarajiwa kutoa ushahidi wao. 

Hata hivyo, mahakama hiyo imeamua kuahirisha kesi hiyo kwa madai kwamba Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Bw. Gabriel Mirumbe yuko likizo ambapo anatarajiwa kumaliza likizo yake hapo Januari 20, mwakani. 

Kesi hiyo yenye nambari 407/98 awali ilifunguliwa mahakama ya mkazi ya Kisutu, jijini, mapema mwezi Machi, mwaka huu, ambapo baadaye ilihamishiwa katika mahakama ya Kivukoni, Jijini Dar es Salaam. 

Hii ni mara ya tatu kwa kesi hiyo kuahirishwa kuanza kusikilizwa tangu upelelezi wake ukamilike hapo Oktoba, mwaka huu. 

Awali, iliahirishwa mapema mwezi Novemba, mwaka huu, kwa madai kwamba mashahidi wa upande wa serikali waliotarajiwa kutoa ushahidi wao walishindwa kufika mahakamani. 

Pia mnamo Desemba 2, mwaka huu, iliahirishwa tena kwa madai kwamba Hakimu huyo anayesikiliza kesi hiyo, Bw. Gabriel Mirumbe anaumwa. 

Watuhumiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Rutemba Shaabani, Iddi Selemani, Ismaili Hamisi, Jafari Mohamed, Omari Hemedi, Hassani Habibu, Hamisi Nassoro, Ally Daudi, Juma Ally na Nurdin Abbas. 

Wakati huo huo, kesi nyingine nambari 184/98 ya tuhuma ya kufanya "ghasia" na kujeruhi inayowakabili Waislamu kumi na mmoja inatazamiwa kuanza kusikilizwa hapo Januari 25, mwakani katika mahakama ya Kisutu, Jijini Dar es Salaam. 

Aidha, kesi nyingine nambari 192/98 ya Mwembechai inayowakabili watu 12, wakiwemo Waislamu tisa na Wakristo watatu nayo pia inatazamiwa kuendelea kusikilizwa hapo Januari 26, mwakani pia katika mahakama ya Kisutu. 

Kesi hii imekwishasikilizwa mara moja mahakamani hapo mapema mwezi Novemba, mwaka huu. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Hakuna Idd kwa wanafunzi Waislamu mwaka huu 

Baada ya wanafunzi Wakristo kusherehekea Krismasi: Wanafunzi Waislamu kuikosa  Id el Fitr 

Hoi hoi zatawala ziara ya Mwinyi Mwanza 

Waislamu Tunduma waswali ndani ya kilabu cha ulanzi  

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: FROTTEURISM 

Barabara za Tabora zimepitwa na wakati 

Jicho la Uzalendo: Nihiari yetu kuendelea kujidanganya! 
Na Sompo wa Kahambwe 

Kuanza na kwisha mwezi wa Ramadhani 

Taarifa ya Kamati  juu ya yaliyotokea Mwembechai 

Hotuba ya Mwenyekiti wa Wanawake wa Kiislamu katika Kongamano lililofanyika Masjid Nnuur Sinza  19/12/1998 

Maazimio ya kongamano la wanawake wa Kiislamu 

Waislamu kijijini Kidunda Moro wahitaji mwalimu 

Waislamu Mtwara wadai jengo la Wakfu kwa CCM 

Wakati Makanisa yakimeremeta: Msikiti wageuka gofu Sanya Juu 

Sheikh Khalifa Suleiman afariki dunia 

Sheikh wa wilaya ya Lushoto afariki 

Ijue Madrasat Riyaadhwa ya mjini Dodoma 

Somo la Zaka 

Maiti ya Muislamu yasusiwa 

Mwinyi apongeza juhudi za kulea yatima Mwanza 

Tuhuma za kupindua uongozi wa Bakwata: Sheikh Hamim Boza akanusha kuhusika 

Kuongezeka kwa ajali za barabarani 

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache - 4 
Na Yasin Valerian Massawe 

Matajiri wahimizwa kutoa zaka 

Saggaf awataka watoto wahifadhi Qur'an 

Waislamu watakiwa kujitolea kupigania dini yao 

Kesi  nyingine Mwembechai yaahirishwa  

Sayansi na Teknolojia  
[Kuirekebisha Modem Yako]  

Masomo ya Dini ya Kiislamu  

Barua za Wasomaji  

Mashairi  

Chakula na lishe  
[Saumu na lishe ya mama mjamzito] 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita