|
|
| Kuanza
na kwisha mwezi wa Ramadhani
ALHAMDULILLAH. Tunaendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa kutuwezesha tana kukamilisha toleo Nambari 2. Toleo hilo lilihusu "Adabu katika Swala". Tuliweza kuona maasi ya swala katika Uislamu na vipi kichezewa au kupuuzwa tutatoka katika Uislamu. Pia tuliweza kutathmini swala yetu ya sunnah ya Taraweih na kuona hasara kubwa tunayoipata kutokana na haraka zetu za kumaliza mapema rakaa zinazotukabili. Tunamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.) atujalie utulivu na pia unyenyekevu wakati tunapokuwa mbele yake katika jitihada ya kusimamisha swala zetu. Kama tulivyoahidi katika toleo lililopita, Inshaallah katika toleo hili, tutaangalia kuhusu "Kuanza na Kwisha kwa mwezi wa Ramadhani". Tutaiangalia kwa ufupi mitazamo miwili inayotofautiana na maegemeo wanayotegemea. Hatimaye tutatoa nasaha katika suala hili na pia mambo mengineyo yenye kuleta mifarakano miongoni mwa Waislamu. Kuanza kwa Ramadhani Mwenyezi Mungu (s.w.) amejalia, vitu vingi katika dunia hii kuwa ni vyenye mwanzo na mwisho. Hivyo, ni vema tuzingatie mianzo na miisho ya hususan vitu vyenye kheri kubwa nasi ni funga ya Ramadhani. Hivyo, hatuna budi kuwa makini na funga hii ili tuweze kuelewa ni lini itaanza na lini itakwisha? Katika jambo hili la kuwa makini na kuanza kwa Funga ya Ramadhani, Abu-Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Allah ameagiza: "Hesabuni mwandamo wa Shaaban kwa ajili ya Ramadhani". (Tirmidh) Swaum ya Ramadhani inaanza kwa kuona mwezi baada ya siku 29 au 30 Shaaban kama tunavyofahamishwa katika hadithi nyinginezo: Ibn Umar (r.a.) ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: Msifunge mpaka muuone mwezi umeandama na msiache kufunga mpaka muuone mwezi (wa Shawwal) umeandama. Kama kuna mawingu (hamkuuona) hesabuni kamili (siku 30). Katika silimulizi nyingine amesema: Mwezi una masiku 29, kwa hiyo usifunge mpaka uone mwezi umeandama; kama kuna mawingu subiri na kamilisha idadi ya siku 30. (Bukhari na Muslim) Abu Hurairah (r.a.) ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: Funga kwa kuandama mwezi, na futuru kwa kuandama mwezi. Kama kuna mawingu, kamilisha siku 30 za Shaaban. (Bukhari na Muslim) Kutokana na hadithi tulizozinukuu, ni wazi kuwa kigezo pekee kwa watu kutumia ili kuanza ama kumaliza funga ya Ramadhani ni kuuona mwezi. Hivyo inafaa juhudi za kuuangalia mwezi ziwepo kwa umma wa Waislamu tangu mwandamo wa Shaaban kama tulivyokwishaona katika hadith tuliyoinukuu hapo mwanzoni kabisa. Je, ni lazima kila mfungaji aone mwezi? Mwezi wa Ramadhani akiuona mtu mmoja muadilifu inatosha na wengine waliobaki itawabidi wafunge. Hivyo ndivyo alivyoamrisha Mtume Muhammad (s.a.w.) kama tunavyojifunza katika hadithi zifuatazo: Ibn Abbas ameeleza kuwa Mwarabu wa Jangwani alikuja kwa Mtume (s.a.w.) akasema: Hakika nimeuona mwezi wa Ramadhani umeandama. Mtume (s.a.w.) akamuuliza: Unashuhudia kuwa hapana Mola ila Allah? "Ndio" alijibu, akamuuliza tena: Unashuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Allah? Akajibu: "Ndio". Akasema (Mtume): Ee Bilal! Watangazie watu kuwa hawana budi kufunga kesho. (Abu Daud, Tirmidh, Nisai, Ibn Majah). Ibn Omar ameeleza: Watu walioua mwezi. Kisha nikamfahamisha Mtume (s.a.w.): Hakika nimeuona. Kwa hiyo alifunga na aliwaamrisha watu wafunge. (Abu Daud, Darimi) Je, mwezi ukionekana sehemu moja, Waislamu wote ulimwenguni watalazimika kufunga? Waislamu wote wanakubaliana kutokana na hadithi tulizozinukuu hapo juu, kuwa mtu mmoja au watu wachache wakishuhudia kuandama kwa mwezi wa Ramadhani au mwezi wa Shawwal, Waislamu watalazimika kufunga au watalazimika kufuturu na kuswali Iddil-Fitr. Hitilafu kati ya Waislamu juu ya suala la watu wachache kushuhudia kuandama kwa mwezi wa Ramadhani au wa Shawwal ipo kwenye umbali; kwamba ni watu wa wapi wafunge watakaposikia habari za kuandama mwezi kutoka wapi? Juu ya suala hili Waislamu wamegawanyika katika makundi mawili yafuatayo: Kundi la kwanza ni wale wanaosema kuwa mwezi ukionekana katika mji mmoja au sehemu moja, basi Waislamu wengine popote walipo ulimwenguni watalazimika kufunga au kufungua. Haya pia ni maoni ya Imamu Hambali, Malik na Abu Hanifa. Hawa wamejiegemeza katika hadithi tulizozinukuu hapo juu kuhusu Mtume (s.a.w.) kuletewa taarifa ya kuandama kwa mwezi. Kundi la pili ni wale wanaojigemeza katika hadith ifuatayo: Kurayb ameeleza kuwa Umm Fadhl, bint wa Harith alimtuma (mtoto wake) Fadhl Syria (Sham) kwa Muawiya. Fadhl aliwasili Syria na akatekeleza yale aliyotumwa na mama yake. Alipokuwa pale Syria mwezi wa Ramadhani ulianza. (Amesema Fadhl): Niliouna mwezi wa Ramadhani ulipoandama siku ya Ijumaa. Kisha nilirudi Madina mwishoni mwa mwezi. "Abdullah bin Abbas (r.a.) aliniuliza juu ya kuandama kwa mwezi wa Ramadhani na akasema: Mliuona lini? Nijajibu: Tuliuona siku ya Ijumaa. Akauliza: Uliouna wewe mwenyewe? Nilijibu: Ndio, na watu pia waliuona na wakafunga na Muawiya pia alifunga; ndipo akasema: Lakini sisi tuliuona siku ya Jumamosi. Kwa hiyo tutaendelea kufunga mpaka tukamilishe 30 au tuuone mwezi (Shawwal baada ya 29 Shaaban). Nikauliza (Fadhl): Kuonekana kwa mwezi kwa Muawiya hakukutosha? Akajibu: Hapana, hivi ndivyo Mtume wa Allah alivyotuamrisha. (Muslim) Kutokana na Hadith hii, kama kuna masafa marefu kati ya mji mwezi ulipoonekana na mji watu walipopata taarifa juu ya kuonekana kwake haijuzu kwao kufuata mwandamo huo. Lakini endapo miji hiyo itakuwa imekaribiana, basi watu waliopata taarifa ya kuandama mwezi kutoka mji wa karibu watawajibika kufunga au kufungua. Mwana chuoni mashuhuri anayeshikilia rai hii ni Imamu Shafii. Kutokana na hitilafu hizi, imetokea kuwa Waislamu wote ulimwengu hawaanzi kufunga Ramadhani siku moja na kuswali Iddil-Fitr na Iddil-Hajj siku moja. Wale wanaoshikilia rai ya kwanza, wanaona kuwa si vyema umma mmoja wa Kiislamu kutofautiana katika matukio haya muhimu ambayo ni alama ya Dini. Isitoshe kutokana na maendeleo ya sayansi, mawasiliano ulimwenguni hivi leo yamerahisika mno. Ulimwengu mzima unaweza kupata habari kwa muda wa dakika chache juu ya mwandamo wa mwezi katika mji mmoja. Wale wanaoshikilia rai ya pili, wanaona kuwa si vyema kufunga au kufungua Ramadhani kwa kufuata habari ya kuandama kwa mwezi kutoka popote pale bila kujali masafa au matlai kati ya mji huo huo na pale habari ya kuandama mwezi ilipopokelewa. Kwani kijiografia sehemu mbalimbali za ulimwengu zinatofautiana sana. Kutoana na uchunguzi wa anga umepatikana ushahidi kuwa kuna kutofautiana katika kuona mwezi. Ambako katika mji mmoja kuna uwezekano mkubwa kabisa wa kuona mwezi endapo hapatakuwa na mawingu, katika mji mwingine ulio masafa ya mbali au matlai mengine, mwezi hauonekani kabisa siku hiyo hata kama hapatakuwa na mawingu. Kwa hiyo, hawa wenye mtazamo wa pili, pia kutokana na maendeleo hayo hayo ya sayansi, wanaona kuwa hadithi zilizowaamrisha watu kufunga kwa kupata habari ya kuandama mwezi kutoka kwa mtu mmoja au watu wachache, hazionyeshi kuwa wale walioleta habari za kuandama mwezi walitoka masafa marefu na pale alipokuwa Mtume (s.a.w.). Hii ndiyo mitazamo mawili inayohitilafiana na maegemeo wanayotegemea kama tulivyojaliwa kuyaeleza kwa ufupi sana. Hoja kwa kila upande bado ni nyingi. Si madhumuni ya makala hii kuonyesha kuwa mtazamo wa kundi fulani ndio sahihi. Bali ni madhumuni ya makala hii nii kuwazindua Waislamu ama kutoa changamoto kwa Waislamu kuwataka wawe ni wenye kuwa na elimu sahihi kwa kila jambo wanalolifanya au wawe ni wenye kutafuta kujua kikweli kweli kwanini wenzetu wanafanya tofauti na sisi? Hivyo, Waislamu wasigombane, wasidharauliane wala kubezana kwa jambo hili. Waislamu wa kweli ni wale wanaohuzunika pale wanapowaona wenzi wao wamepotea njia. Ni wale wanaotumia busara kuwaelekeza watu njia iliyo sahihi. Si wale wanaotumia nguvu, kebehi ama dharau. Allah (s.w.) anatufundisha utaratibu mzuri wa kulingania, pale alipomuelekeza Mtume (s.a.w.) kuwa: "Waite watu katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora". (16:125) Utaratibu unaotumika na wengi wetu katika kuyaendea mambo yaliyo na hitilafu baina yetu sio sahihi katika maadili ya Kiislamu. Tunafanya ushabiki katika mambo ya Uislamu sawasawa na tunavyofanya ushabiki katika mambo ya mipira, vyama vya siasa na mengineyo mengi katika mambo ya pumbao. Hali hii inajenga chuki kubwa baina yetu Waislamu. Chuki ambayo ni kubwa zaidi ya ile tunayostahili kuijenga kwa maadui wa Uislamu. Hali hii pia inapelekea kutokuwa na mazingira bora ya kuvumiliana ili kuweza kusoma ama kufundisha kutoka kwa mwenzio, aliye na fikra tofauti na yako. Lililo muhimu ni kila Muislamu, kwa lolote analolifanya, afahamu kwa nini analifanya? Vipi alifanye? Na limetoka wapi? Tusiwe ni wenye kuiga ama kuendeleza tu bila ya kuwa na elimu ya tunayoyafanya tutaangamia. Inshaallah, kama tulivyoahidi katika toleo Nambari 1 katika toleo lijalo, tutaangalia kuhusu "Vipi Tufunge". Vipi tufunge ni Swaum aliyoikusudia kwetu Mwenyezi Mungu (s.w) ili tuweze kufikia daraja ya kuwa na Taqwa. Kwa maoni, maswali au mapendekezo,
tafadhali tuandikie:
|
YALIYOMO
Tahariri Hakuna Idd kwa wanafunzi Waislamu mwaka huu Baada ya wanafunzi Wakristo kusherehekea Krismasi: Wanafunzi Waislamu kuikosa Id el Fitr Hoi hoi zatawala ziara ya Mwinyi Mwanza Waislamu Tunduma waswali ndani ya kilabu cha ulanzi MARADHI YA KISAIKOLOJIA: FROTTEURISM Barabara za Tabora zimepitwa na wakati Jicho la
Uzalendo: Nihiari yetu kuendelea kujidanganya!
Kuanza na kwisha mwezi wa Ramadhani Taarifa ya Kamati juu ya yaliyotokea Mwembechai Maazimio ya kongamano la wanawake wa Kiislamu Waislamu kijijini Kidunda Moro wahitaji mwalimu Waislamu Mtwara wadai jengo la Wakfu kwa CCM Wakati Makanisa yakimeremeta: Msikiti wageuka gofu Sanya Juu Sheikh Khalifa Suleiman afariki dunia Sheikh wa wilaya ya Lushoto afariki Ijue Madrasat Riyaadhwa ya mjini Dodoma Mwinyi apongeza juhudi za kulea yatima Mwanza Tuhuma za kupindua uongozi wa Bakwata: Sheikh Hamim Boza akanusha kuhusika Kuongezeka kwa ajali za barabarani Njia ya
uzimani ni nyembamba, waionao ni wachache - 4
Saggaf awataka watoto wahifadhi Qur'an Waislamu watakiwa kujitolea kupigania dini yao Kesi nyingine Mwembechai yaahirishwa Sayansi
na Teknolojia
Chakula
na lishe
|