|
|
|
TUKIO la Mwembechai lililenga katika yale waliyofanyiwa kina mama Msikitini, vituo vya polisi, magereza hadi kuimbishwa nyimbo za pambio (Yesu ni Mungu, mwokozi ni mwamba) huku wakiwa uchi mbele ya askari wa kiume. Ukiondoa gazeti la AN-NUUR, vyombo vya habari vyote vilivyobakia viliendesha propaganda na uzushi dhidi ya Waislamu aidha vingine viliamua kukaa kimya. Maneno ya uzushi yalijengwa kama watu waliohusika Mwembechai ni wahuni, wanaokashifu dini za watu wengine, n.k. Wale wazee, vijana na Masheikh waliokuwa ndani ya Msikiti au wale waliojaribu kulisemea tukio zima la Mwembechai walionekana eti ni wakorofi, wahuni, n.k, kuitwa wachochezi, wanajenga uhasama kati wananchi na serikali yao. Kwa kuzingatia hali hiyo sisi wanawake wa Kiislamu kupitia kamati hii hatukuwa na budi ila kujaribu kuongea na wananchi ili kuwaeleza ukweli wa mambo. Kwa hiyo tulikwenda Diamond Jubilee, lakini ukajengwa uzushi na kuendeshwa propaganda kwamba sisi wanawake wa Kiislamu tuliazimia kuandamana uchi, baadhi ya magazeti yaliripoti hivyo. Hii ilikuwa huzuni kubwa kwetu. Pia mkutano huo hakuandaliwa na sisi ila kuna watu nyuma yetu. Kutokana na propaganda hizo tukazuiliwa kukutana hapo Diamond Jubilee Hall. Tukarudi Msikitini Mwembechai pamoja na vitisho vilivyokuwepo siku ile ya Machi 29, 1998 maaskari wa wazi na siri ambao walizunguka Msikiti wote tukaita waandishi wa habari tukatoa matamko ya kulaani kuvunjwa kwa mkutano wetu wa Diamond Jubilee Hall. Baada ya matamko hayo katika mazingira magumu ya siku ile tulifanya mkutano wetu pale Msikitini na tulimaliza kwa amani kinyume na ilivyokuwa ikitangazwa. Tulikubaliana tuandae mkutano mwingine kama huo ili tueleze hisia zetu. Tulikwenda Magomeni Islamic Centre kwa ajili ya mkutano huo lakini Msikiti ulizingirwa na maaskari na hivyo hatukuweza kukutana tena hapo. Jaribio letu la kukutana kuzungumza na waandishi wa habari Press Centre pia lilizuiliwa. Katika mfululizo huu wa dhulma, ukandamizaji, uonevu, propaganda na uzushi, tukapata salamu kutoka mikoani wenzetu walituuliza tumeshindwa na kama tumeshindwa basi wao waje kutoka huko mikoani. Salamu zilitufariji mno. Kwa hiyo badala ya wao kuja sisi twende huko. Tulianzia hapa Sinza tukazungumza na ndugu zetu wa hapa Dar es Salaam na Pwani. Hata hivyo vyombo vya habari vikasusia kutangaza yale yaliyosemwa. Matarajio yetu wenzetu wa mikoani wangepata habari kupitia vyombo hivyo. Kwa hiyo tukaona kheri tuanze safari kuelekea mikoani tukutane na ndugu zetu huko kikanda. Lengo likiwa ni kutoa taarifa ya ukweli wa yaliyotokea Mwembechai. Hata hivyo, baadhi ya ndugu zetu wa mikoani hawakukubali utaratibu huu wa kikanda. Tulipofika Morogoro tuliwakuta wa Iringa, Dodoma na wengine waliotoka hapa Dar es Salaam. Hivyo tukalazimika kutembea mkoa kwa mkoa. Kila tulipofika mkoa mmoja tuliwakuta watu kutoka mikoa mingine tukapokea mialiko yao. Katika safari zetu; mada ikawa kuelezea yaliyotokea Mwembechai, na kwamba chanzo ni uchochezi wa Paroko hadi sisi kuvamiwa pale Msikitini, kurundikwa gerezani hadi kuimbishwa nyimbo za Kikristo, kurushwa kichura. Pia tulitaka tuwaeleze ndugu zetu pamoja na kuimbiwa huko hakukututoa kwenye Uislamu wetu, kwa hiyo tukawa tunawathitibishia Uislamu wetu. Tulitaka kuonyesha pia ilikuwa ni uzushi na fitna za vyombo vya habari kuwa tulitaka kuandamana uchi. Hiyo katika mizunguko yetu mada kuu ilikuwa umuhimu wa vazi la hijabu. Kila mkoa tulieleza kikamilifu mada ya hijab pamoja kuonyesha hijab yenyewe. Wenzetu wa mikoani wakatuitikia, tuliandamana na hijab zetu. Wengi walishona hijab. Suala lingine tulionyesha katika mizunguko yetu ni kuwa sisi sio watu wa kutumiwa kwa hiyo tuliwaalika wakuu wa mikoa, wabunge, vyombo vya habari ili washuhudie hilo. La mwisho, tulitaka kuweka msimamo kila mkoa tumezungumza na kutoa kauli ya pamoja kwamba yaliyotokea Mwembechai chanzo ni Paroko ambaye aliitikiwa na vyombo vya habari uzushi ukaenezwa dhidi ya Waislamu hadi uongozi kutoa amri nguvu za dola zituangukie bila kosa lolote. Pia tukaweka msimamo kwamba katika mazingira hayo ya uzushi, propaganda, Tume iundwe ili kuchunguza tukio zima hili na wahusika watakaobainika wachukuliwe hatua. Ama wale walioua wafikishwe mahakamani. Yote hayo kongamano hili ni shahidi; yote hayajafanyika.
|
YALIYOMO
Tahariri Hakuna Idd kwa wanafunzi Waislamu mwaka huu Baada ya wanafunzi Wakristo kusherehekea Krismasi: Wanafunzi Waislamu kuikosa Id el Fitr Hoi hoi zatawala ziara ya Mwinyi Mwanza Waislamu Tunduma waswali ndani ya kilabu cha ulanzi MARADHI YA KISAIKOLOJIA: FROTTEURISM Barabara za Tabora zimepitwa na wakati Jicho la
Uzalendo: Nihiari yetu kuendelea kujidanganya!
Kuanza na kwisha mwezi wa Ramadhani Taarifa ya Kamati juu ya yaliyotokea Mwembechai Maazimio ya kongamano la wanawake wa Kiislamu Waislamu kijijini Kidunda Moro wahitaji mwalimu Waislamu Mtwara wadai jengo la Wakfu kwa CCM Wakati Makanisa yakimeremeta: Msikiti wageuka gofu Sanya Juu Sheikh Khalifa Suleiman afariki dunia Sheikh wa wilaya ya Lushoto afariki Ijue Madrasat Riyaadhwa ya mjini Dodoma Mwinyi apongeza juhudi za kulea yatima Mwanza Tuhuma za kupindua uongozi wa Bakwata: Sheikh Hamim Boza akanusha kuhusika Kuongezeka kwa ajali za barabarani Njia ya
uzimani ni nyembamba, waionao ni wachache - 4
Saggaf awataka watoto wahifadhi Qur'an Waislamu watakiwa kujitolea kupigania dini yao Kesi nyingine Mwembechai yaahirishwa Sayansi
na Teknolojia
Chakula
na lishe
|