|
|
|
UNAPOMTAJIA Muislamu yeyote wa mjini Tanga jina la Mwalim Maif, kwa haraka sana atatambua mtu uliyemkusudia si mwingine bali ni mwalimu maarufu wa Qur’an anayeongoza madrasa inayotoa mafundisho ya dini ya Kiislamu iitwayo Taalim iliyopo barabara ya 19 mjini Tanga. Umaarufu wa mwalimu huyo unatokana na kuwa mwalimu pekee mwanamke anayefundisha Qur’an na kufahamika kwa miaka mingi mjini hapa kuliko mwanamke mwingine yeyote. Hivi sasa mwalimu Maif ana umri wa miaka 74. Na anaeleza kuwa alianza kufundisha Qur’an kabla ya kuolewa kwake wakati akiishi na wazazi wake. Akiwa mzaliwa wa kijiji cha Tongoni kilichopo kilometa kadhaa nje kidogo ya Manispaa ya Tanga katika barabara inayoelekea wilaya ya Pangani, mwalimu Maif alilieleza gazeti hili kuwa alipata elimu yake ya kidini kutoka kwa Sheikh Toba wa huko Tongoni ambapo alianza kusomeshwa akiwa na umri wa miaka 5. "Nakumbuka ni mwaka 1952 nilipoamua kuanzisha madrasa kamili ya kufundisha Qur’an. Wakati huo nilikuwa nikiishi mjini baada ya kuolewa", alieleza mwalimu Maif akionyesha kuwa na kumbukumbu za kutosha za historia yake. Kwa mujibu wa maelezo ya mwalimu huyo, madrasa yake ambayo aliipa jina la madrasa Taalim ilianzia barabara ya 13 kisha ikaenda barabara ya 12 kabla ya kuhamia barabara ya 10 na hatimaye barabara ya 19 ilipo hadi hivi sasa. Anakumbuka madrasa yake ilianza ikiwa takriban na watoto 200 ambapo idadi hiyo iliongezeka na kufikia watoto 500 katika miaka tofauti. Hata hivyo hivi sasa madrasa hiyo ina wanafunzi chini ya 200. Mwalimu Maifu alitaja sababu ya kupungua kwa wanafunzi kwenye madrasa yake kuwa ni uwezo mdogo wa kufundisha alionao kwa hivi sasa kutokana na utu uzima na pia ni mgonjwa wa miguu na anasumbuliwa na shinikizo la damu linalomtokea mara kwa mara. Kutokana na hali hiyo ametoa madaraka kwa mtoto wake wa kiume anayeitwa Salim Rashid el-Mazrui kumsaidia kuendesha madrasa hiyo akishirikiana na Ustadh Bwana ambaye ni miongoni mwa wanafunzi wa awali wa madrasa hiyo. Maustadh wote wawili tayari ni watu wazima wenye wake na watoto. Wakati hivi sasa Ustadh Mbwana anasoma elimu ya juu ya kidini kwa Sheikh Jumaa Heka ambaye ni Imamu wa Msikiti wa Ijumaa wa mjini hapa na ambaye amepata elimu yake kutoka kwa Mufti, Sheikh Hemed bin Jumaa bin Hemed, Ustadh Salim el-Mazrui naye alisoma kwa Sheikh Abdallah Ayoub ndugu yake marehemu Sheikh Mohammad bin Ayoub wa Jumuiya ya TAMTA ya mjini Tanga na pia alisomeshwa na Sheikh Abdallah Farsy aliyekuwa Chifu Kadhi wa Kenya. Hivi sasa ni marehemu. Pamoja na majukumu mengi ya madrasa kutwaliwa na Maustadh hao, mwalimu Maifu bado anaendelea kufundisha pale anapojisikia kufundisha. Hata hivyo ameeleza kazi kubwa ambayo inamkabili hivi sasa ni kutoa mihadhara au mawaidha ya kuwalingania wanawake. "Nikiwa kama mwanamke msomi wa Kiislamu nimeona ninalo jukumu kubwa la kuwaelimisha hata wanawake wenzangu na sio watoto tu", alisisitiza mwalimu Maifu. Mara kadhaa katika siku za Ijumaa mwalimu Maifu amekuwa akitokeza kwenye kipindi cha Kiislamu cha televisheni ya BSC inayorusha matangazo yake mjini hapa akitoa mawaidha yanayohusiana na masuala ya wanawake. Mwalimu Maifu pia amekuwa akishirikishwa katika hafla nyingi za kidini hasa zinazowahusu wanawake ambapo hupewa nafasi ya kutoa nasaha zake. Alishawahi kualikwa kufuturu katika Ikulu ya mjini hapa katika hafla iliyoandaliwa na Makamu wa Rais Dk Omar Ali Juma. Pia amekuwa na uhusiano mzuri na wahadhiri wanawake wa Kiislamu wa hapa nchini. Masheikh mbalimbali wanaozuru mji wa Tanga hufika kwenye madrasa yake kumsalimia. Katika nasaha zake kwa Waislamu, mwalimu Maifu aliwalalamikia Waislamu wenye uwezo wa kifedha pamoja na mashirika ya misaada ya Kiislamu kutojitokeza kusaidia madrasa ndogo ndogo za hapa nchini. Amesema madrasa yake pamoja na kuwa na historia ndefu ya kufundisha Qur’an haina hadhi inayostahiki kutokana na kutokuwa na uwezo wa kifedha wa kuiendeleza na kuajiri walimu. Ametoa wito kwa mashirika ya Kiislamu na Waislamu wenye uwezo kusaidia kuinua madrasa yake ambayo amedai anaiendesha kwenye upenyu wa nyumba yake na ikionyesha kila dalili ya kufifia kwa sasa. Kwa watakaopenda kusaidia madrasa yake anuani ya mwalimu Maifu ni S.L.P.
2060, Simu ni 44011, Tanga.
Ijue Madrasa Hudaa Arusha AL-MADRASATUL - Hudaa ipo katika mtaa wa Sokoni I kwenye kitongoji cha Migungani mkoani Arusha. Imeanzishwa mwaka 1995 chini ya uongozi wa Maalim Hussein S. Ijunje ambaye hivi sasa ndiye Mudir wa Madrasa hiyo. Idadi ya wanafunzi madrasani hapo ni 170, inao waalimu watatu waliobobea katika ufundishaji ambao ni pamoja na Maalim Idrisa J. Kibwana, Maalim Juma bin Swalehe na Maalim Hussein S. Ijunje. Inatoa mafunzo kwa utaratibu maalum, ambapo darsa la akina mama linaanza baada ya Salatil Dhuhur, darsa la watoto huwa ni baada ya Salatil Asr, watoto hao huwa ni wenye umri kuanzia miaka 7-15. Lipo pia darsa maalum la akina baba na vijana, hili huanza baada ya Salatil Inshai hadi saa 4:00 usiku. Awali, mafunzo hayo yalikuwa yakifanyika ndani ya Msikiti wa Ijumaa (Masjid Hudaa) lakini hivi sasa waumini wa kitongoji cha Migungani wamekamilisha jengo ambalo wamelijengaa kwa nguvu zao, ambalo litatumika kama darsa maalum. Hata hivyo, kutokana na kero wanayoipata waumini hao ya watoto wao wadogo kusoma katika shule za watoto wadogo (chekechea) ambazo hazifundishi kimaadili ya dini ya Allah, wamefanikiwa kulitumia darsa hilo nyakati za asubuhi kwa madhumuni hayo. Kama ilivyo kwa madrasa nyingi mkoani hapa, madrasa hii inakabiliwa na matatizo mbalimbali lakini kubwa zaidi ni vifaa vya kufundishia kama vile chaki na madaftari, majuzuu, misahafu na mikeka. Hivyo, waalimu wa madrasatul Hudaa wanawaomba Waislamu popote pale linaposomwa gazeti hili, kutoa misaada yao ili kuboresha madrasa hiyo. Aidha, wametoa wito wa ushirikiano miongoni mwa Waislamu bila kujali tofauti za itikadi zao, na kuwasisitizia pia kuwa makini dhidi ya mbinu mbalimbali toka kwa maadui wa dini ya Allah. Wamewakumbusha pia wazazi wa Kiislamu kuwa na muamala mzuri katika suala
zima la malezi ya watoto ili kupata jamii nzuri ya Waislamu wa kesho.
|
YALIYOMO
Tahariri Kingunge, kweli upo uonevu na dhulma Wananchi wahoji kuhusu polisi aliyeua Arusha Dondoo za Saikolojia
Kona ya Wacha Mungu
Jicho la Uzalendo: Bhabhoo! Muungwana
huyoo!
Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) Mafunzo kuhusu funga ya Ramadhani
Marekani ni mtetezi au adui wa haki?:
Umoja wa Mataifa upo upande gani?
Dawa ya ukimwi ni mwenendo mwema
Mwalimu Maif: Mwanamke aliyetumia maisha yake kufundisha Qur'an Wazazi waaswa kutoshabikia maovu Je, hivi tuendelee kushika amri za
Mungu tena? (jibu)
Mapinduzi, Muungano kwa manufaa ya nani? Fufueni EAMWS - Sheikh Amana
Msiitupie lawama serikali - Dk. Omar Baada ya kuvunjiwa nyumba,
kuchomewa vyakula na Serikali: Nzasa sasa wafuturu Maembe
Acheni mifumo mibovu, fuateni Qur'an - Sheikh Kilemile Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|