|
|
|
WAZAZI nchini wametakiwa kutoshabikia uovu unaofanywa na watoto wao hususan ule wa utoaji mimba na vitendo vingine vyenye kuondoa maadili mazuri ya Uislamu nchini. Wito huo umetolewa hivi karibuni na mmoja wa Maulamaa wa Msikiti wa Uwanja wa Ndege mjini hapa Sheikh Imran Athumani wakati akiongea na waumini wa Msikiti huo kabla ya swala ya Ijumaa. "Kama mtu hataki mimba basi asifanye tendo la ndoa ambapo watu wanadiriki kutupa watoto majalalani, mtoni na hata chooni bila ya kujali mtoto yule angekuwa na nafasi gani katika umma huu wa Kiislamu", alisema Ulamaa huyo. Aliendelea kusema kuwa watu wengine wanaona aibu baada ya kupata mimba wanaamua kutoa na huku wengine wakisaidiana na wazazi wao. "Siku ya Kiama zitaletwa roho za watoto hao na kuulizwa kwanini ziliuawa na ndipo hapo Mwenyezi Mungu atakapotoa hukumu yake iumizayo ikiwa ni pamoja na kuwekwa katika moto wa Jahanamu". Naye Ustadh Abdallah Kombo akitoa hotuba katika swala ya Ijumaa Msikitini hapo alilaani tabia za Waislamu kugombana wenyewe na kupelekwa kesi zao kwenda kuhukumiwa na watu wasioujua Uislamu wao, hali ambayo imechangia kuporomosha na kuwagawa Waislamu na Uislamu wao. "Wakati mwezi wa Ramadhani umefika Waislamu lazima washikamane na kuondoa tofauti zao na lazima kuanzia sasa turejee katika hukumu na kuwaomba Waislamu waliokoseana waanze kusameheana na kufungua ukurasa mpya wa kuelekea katika ucha Mungu", alisema. Wakati huo huo, Waislamu wa mjini hapa mapema wiki iliyopita walifanya kongamano kubwa la kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo mada mbalimbali kuhusiana na mwezi huu zilitolewa na Waadhiri maarufu wa mjini hapa na mwisho kutolewa mapendekezo na maazimio ya kongamano hilo. Akisoma maazimio ya kongamano hilo, Ustadh Mbaraka Mcharagande alisema kuwa kila Muislamu mwanamke na mwanaume kuhakikisha kuwa anatekeleza ibada ya funga ya Ramadhani na kujitahidi kadri iwezekanavyo kulifahamu lengo halisi ya funga. Pia kufahamu nini maana ya ibada ya funga na nafasi yake katika maisha ya kila siku. Pendekezo lingine lililotolewa katika kongamano hilo ni Waislamu kusoma Qur’an vilivyo na kufahamu tafsiri yake aghalabu kila siku juzuu moja. Vile vile Waislamu wametakiwa kujiepusha na michezo isiyofaa wakati wa Ramadhani kama vile kucheza karata, bao, kusikiliza miziki ya ovyo na kuangalia maonyesho mabaya katika televisheni. MZEE maarufu wa Kiislamu mjini hapa Mzee Athumani Kibwana (70) amefariki dunia Jumapili Desemba 20, 1998 katika hospitali ya mkoa wa Morogoro kutokana na kuugua kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu. Mzee Athumani Kibwana aliyezaliwa mwaka 1928 alikuwa ni mmoja kati ya waze waliojitolea kushirikiana na vijana pamoja kufanya juhudi ya kuwaunganisha wazee wenzake katika suala zima la kuupigania Uislamu. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ndugu wa marehemu Mzee Majuto amesema kuwa Mzee Kibwana alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifua ambapo mara kadhaa alilazwa na kutolewa katika hospitali ya mkoa na alipolazwa tena mapema mwezi Desemba mwaka jana ndio ukawa mwisho wa safari yake. Mzee Kibwana wakati wa uhai wake aliweza kushirikiana kwa karibu sana na umoja wa vijana wa Kiislamu Morogoro (JUSHUMUDI) akiwa na wazee wenzake Mzee Hamza Mtingwa pamoja na Mohammed Kiombo ambapo licha ya umri aliokuwa nao lakini mzee huyo aliweza kupanda milima ya Tangeni na kuvuka mabonde kwa lengo la kutangaza Uislamu katika vijiji kadhaa vya mkoa wa Morogoro. Mzee Kibwana mwaka 1994 alikuwa ni mmoja kati ya Waislamu wengi aliyeshambuliwa na mabomu ya F.F.U katika Msikiti wa Uwanja wa Ndege na kufanya afya yake iathirike kwa kiasi kikubwa na kupelekea kuanza kuugua kifua. Katika salamu zao za rambirambi kwa familia ya marehemu kupitia idara yake ya habari imemuelezea marehemu Kibwana kwamba ni mzee aliyejitoa mhanga kwa kuweza kuwaunganisha vijana na wazee kuwa katika msimamo mmoja wa kuusimamisha Uislamu. Pia taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa marehemu atakumbukwa kutokana na fikra na hekima zake pamoja na kuwa mfano kwa wazee wengine hasa pale alipokubali kutembea kilometa nyingi kwa mguu kwa lengo la kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu yeye pamoja na Waislamu wengine. Mazishi ya marehemu mzee Athumani Kibwana mbali ya kuhudhuriwa na Waislamu wengi wa mjini hapa pia yalihudhuriwa na Imamu wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa Sheikh Mohammed Kairo. Marehemu alizikwa Jumatatu ya Desemba 21, mwaka jana katika makaburi
ya Kora. Ameacha mke, watoto na wajukuu kadhaa. Wainna Ilillah Wainna Rajiun.
|
YALIYOMO
Tahariri Kingunge, kweli upo uonevu na dhulma Wananchi wahoji kuhusu polisi aliyeua Arusha Dondoo za Saikolojia
Kona ya Wacha Mungu
Jicho la Uzalendo: Bhabhoo! Muungwana
huyoo!
Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) Mafunzo kuhusu funga ya Ramadhani
Marekani ni mtetezi au adui wa haki?:
Umoja wa Mataifa upo upande gani?
Dawa ya ukimwi ni mwenendo mwema
Mwalimu Maif: Mwanamke aliyetumia maisha yake kufundisha Qur'an Wazazi waaswa kutoshabikia maovu Je, hivi tuendelee kushika amri za
Mungu tena? (jibu)
Mapinduzi, Muungano kwa manufaa ya nani? Fufueni EAMWS - Sheikh Amana
Msiitupie lawama serikali - Dk. Omar Baada ya kuvunjiwa nyumba,
kuchomewa vyakula na Serikali: Nzasa sasa wafuturu Maembe
Acheni mifumo mibovu, fuateni Qur'an - Sheikh Kilemile Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|