AN-NUUR 
Na.182 Ramadhan 1419, Januari 1 - 7, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Barua
 
Makamba kutoa zawadi ya nguruwe ni kejeli

Ndugu Mhariri 

MUNGU anasema: Mmeharamishiwa nyamafu na damu na nyama ya nguruwe, na kinyama kilichochinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. (5:3) 

Kada Makamba alinukuliwa na gazeti la Msema Kweli Toleo Na. 040, Jumapili Desemba 6-12, 1998 hivi: "Makamba atoa zawadi ya nguruwe kwa shule". 

Licha ya Mwandishi wa gazeti hilo kushangaa kwa kitendo hicho cha kada huyu kutoa nguruwe ambayo imeharamishwa na Mungu ni kudhihirisha yale Waislamu waliyokuwa na shaka nayo kuhusu Uislamu wake wakati anafanya mambo kinyume, sio kwa bahati mbaya, ila ni kwa jeuri na kibri ya utawala wa dunia. 

Waislamu siku zote tumelalamika kuhusu kuzagaa kwa nguruwe na mabucha ya nyama ya nguruwe bila mafanikio, leo katudhihirishia kwamba kufuga nguruwe ni sera maalum. Vipi shule ambayo haifugi wewe uamue kutoa nguruwe halafu uhimize Waislamu kupeleka watoto wao waje. Siku wakipangiwa kusafisha zizi nani alaumiwe? 

Waislamu tumepata madhila mengi juu ya huyu Bwana tangu awe mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam. Mtume (s.a.w.) anasema Muislamu wa kweli ni yule ambaye Waislamu wenzake wanasalimika na ulimi wake na vitendo vyake. 

Yeye alikuwa mtu wa kwanza kuwatuhumu Waislamu kuiba bia wakati wa vurugu za Mwembechai, kasema tumekamata silaha Msikitini, kumbe ni vigingi vya jukwaa si hilo tu wakati anafungua Bia mpya aliwahi kusema kuwa Watanzania kunyweni Bia hii kwa wingi ili serikali ipate kodi kwa wingi. 

NASAHA: Ndugu Luteni amedai mtu asitawaliwe na dini bali yeye aitawale dini; watu wanasema ukistajaabu ya Musa utaona ya Firauni, lakini mimi nasema "ukistaajabu ya Firauni utaona ya Musa, kwanza yeye sio kiongozi wa dini yoyote wala si kiongozi wa taasisi ya dini kwa hiyo fatwa yake inamrejea yeye mwenyewe. 

Kama ni umaarufu wengi wameutafuta, lakini dunia wameiacha, uhai ni kama mvua, leo mafuriko kesho ukame, yeye adai tusitumie kigezo cha dini kujenga tofauti zetu.  

Je, mbona hawaambii chama tawala wasitumie chama kujenga tofauti na vyama vingine mbona amekuwa mstari wa mbele kuviponda vyama vya upinzani. Je, yeye haoni anazidisha tofauti? Je, mbona kama ni msuluhishi mzuri mbona haendi kuchangia vyama upinzani. 

Je, umoja unaletwa kwa kulazimishwa matakwa yako katika dini. Mungu anasema: "Na wanapokuwa na walioamini husema tumeamini na wanapokuwa peke yao kwa mashetani wao husema "Hakika sisi tu pamoja nanyi tunawacheza shere tu" (2:14) 

Usifikiri Mungu ameghafirika na yale wanayoyafanya watu madhalimu Hakika Yeye anawangojea siku yatakapotoka macho. 

Haki iko juu wala haikaliwi Mungu ndiye Mjuzi, mtambuzi, mwenye nguvu, mshindi, mfalme wa wafalme. Kwake hakuna kugeuka geuka haramu ni haramu na halali ni halali. 

Milango ya toba iko wazi hasa mwezi huu wa Ramadhani kwa yule mwenye kutaka. 

Abu Hafsa, 
Box 16617, 
Dar es Salaam. 


Kama Bakwata ndio hii mimi pia siitaki!

Ndugu Mhariri 

NIMESIKITISHWA sana na taarifa iliyotangazwa na Bakwata kuhusu Mufti kutangaza mwezi wa Ramadhani. Hili si la makosa, bali sababu zilizotolewa na vishindo vyake ndivyo vilivyonishangaza. 

Msemaji alisema, nanukuu "hatutafuata mwezi utakaoandana Saudia wala London bali nchini na sehemu nyingine za Afrika Mashariki". 

Hivi Sheikh kama huyu anawagawa Waislamu kwa misingi ya mipaka iliyowekwa na makafiri ndiye atakiwae kuwaongoza Waislamu? 

Na Baraza kama hili lenye Masheikh kama hawa ndilo litakalo kuwaongoza na kuwasimamia Waislamu? 

Hii ina maana kuwa Baraza hili pia haliwatambui wala kuwaonea uchungu wale Waislamu waliouliwa kikatili kule Sudan, Bosnia na Kossovo kwa kuwa wako nje ya mipaka ya Afrika Mashariki. 

Lakini pia si kweli kuwa Baraza hili linawatambua na kuwakubali wale Waislamu walio ndani ya nchi hii. Mbona mauaji ya Mwembechai halikutoa kauli za vishindo kama hivi za mwezi ili kuwatetea wale waliouliwa? 

Huku ni kuwagawa Waislamu kwa kisingizio cha mipaka ya wakoloni. Mwisho watakuja kutuambia tusiende Makkah kuhiji maana ipo nje ya mipaka ya Afrika Mashariki. 

Capt. Ahmad Abdallah Al-Amoudi, 
Box 5316, 
Tanga. 
 


Tupambane na wanaodhulumu

Ndugu Mhariri 

MWENYEZI Mungu ni mwenye huruma na ni mkali wa kuadhibu na Mwenyezi Mungu hapendi dhulma kundi moja la waja wake kudhulumu, kunyonya au kunyanyasa kwa namna yoyote ile kundi lingine.  

Ukisoma katika vitabu vyake vitukufu, Torati, Zaburi, Injili na Qur’an utaona ni namna gani Mwenyezi Mungu anavyokemea tabia ya dhulma na maonezi na jinsi anavyotoa mwongozo kwa wanaodhulumiwa namna ya kupigania haki zao. 

Kwa hiyo, msimamo huu wa Mwenyezi Mungu umekuwa ukiwaudhi watawala wengi kwa sababu hawapendi kutenda haki kwa jamii wanazoziongoza.  

Kwa hiyo, wale waja wema wanao mtii Mwenyezi Mungu na kuhubiri haya maneno matukufu ya Mwenyezi Mungu wamekuwa wakiteswa, kuwekwa magerezani na hata kuuawa kwa sababu tu ya kuhubiri haki itokayo kwa Allah (s.w.) ambayo ni hatari kwa maslahi ya watawala. Tukisoma katika surat Qasas aya ya 4: 

"Hakika Firauni alitakaburi (alijitukuza) katika ardhi na akawafanya watu wa huko makundi mbalimbali, akalidhoofisha kundi moja miongoni mwao akiwachinja watoto wao wanaume na kuwaacha hai watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa miongoni mwa waharibifu". (28:4) 

Katika kuisherehesha aya hii, mfasiri mkubwa wa Qur’an amefafanua kuhusu kuchinja. 

Anasema kuna kumchinja mtu "kihisiy" na "kimaanawiy" anasema kuchinja kihisiy ni kama Firauni alivyokuwa akifanya kutenganisha kichwa na kiwiliwili na kuchinja kimaanawiy ni kunyima mtu elimu, ajira na huduma mbalimbali za kijamii, matokeo yake watu wanakufa kwa maradhi, utampiamlo huku ni kuchinja kimaanawiy na hata kuchoma nyumba au kubomoa huku ni kuchinja pia. 

Kwa hiyo, Nabii Musa (a.s.) alivyopambana na Firauni kwa sababu ya tabia ya kuchinja watu kihisiy na kuwadhalilisha, basi nasi leo Waislamu tunajukumu hilo zito la kupambana na wanao chinja kimaanawiy ili haki idumu katika ardhi. 

Pia wafuasi wa Nabii Isa (a.s) waliteswa, mfano Yohana wa Zebedayo aliteswa na kuuawa kwa sababu ya kuhubiri Injili halisi ya Nabii Isa (a.s) iliyojaa haki ambayo ni hatari kwa maslahi ya watawala na Yohana Mbatizaji alifungwa gerezani na kukatwa kichwa (kuchinjwa kihisiy) kwa sababu ya kudai haki za kijamii jambo lililowaudhi watawala. 

H.B. Sultan, 
Kibaha Picha ya Ndege - PWANI. 


Askofu aliruka jambo muhimu

Ndugu Mhariri 

NAOMBA nimpongeze Askofu Norbert Mtega, Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Katoliki Songea aliamua kutumia jukwaa la Krismasi kuwapa Watanzania picha halisi ya nchi yao. 

Akihutubia katika sherehe hizo Desemba 25, 1998 alitaja mambo mazito matatu yanayoikabili Tanzania. 

Kwanza, alisema (viongozi) waliolilia kukabidhiwa dhamana za uongozi hawana malengo ya kuwasaidia wananchi bali malengo mengine. 

Pili, alisema nchini Tanzania haki sasa haipatikani tena kwa misingi ya usawa.  

Na tatu, alisema Tanzania sasa ni nchi yenye matabaka na akakemea viongozi. 

Aliyoyasema Askofu Norbert siku zote Waislamu wamekuwa wakiyasema lakini wanaposema Waislamu hugeuka na kuitwa "uchochezi". 

Askofu aliorodhesha matabaka (6) na kuyataja kuwa ni vyeo, ukabila, mikoa, uwezo wa kifedha, kisiasa na ubara na visiwani. 

Kwa bahati mbaya kwa upande wa hali halisi na bahati nzuri kwa upande wa Askofu akaliruka tabaka "muhimu" ambalo ni "udini". 

Kwa yeyote anayetaka kuzungumzia amani ya kweli anajua ubaguzi wa kidini ndio mzizi wa fitna wa taifa hili. Hivi sasa hali imeanza kuwa mbaya kiasi kwamba maagizo ya watu wa dini moja kwa vyombo vya dola hupelekea watu wa dini nyingine kuuawa hadharani. 

Kilele cha wasiwasi ni pale Makadinali hutokeza na kunukuu vifungu vya Biblia kuhalalisha mauaji ya watu hao wa dini nyingine. 

Mwisho napenda kuitahadharisha serikali isije ikamtia ndani Askofu wa jimbo kuu la Katoliki Songea kwa madai ya uchochezi kwani aliyoyasema ni kweli. 

Maulidi S. Lameck, 
Kimara, 
Dar es Salaam. 



AN-NUUR mnabagua 

Ndugu Mhariri 

NI jambo la kusikitisha kuona barua zangu nyingi zinazoandika hazichapishwi. 

Naomba Ndugu Mhariri unijibu kama barua zangu zinafika au hazifiki. 

Naomba unieleze ni kwa nini hazichapishwi. Naomba unieleze ni upi utaratibu niufuate ili barua zangu ziweze kuchapishwa. 

Natarajia utanijibu kupitia gazeti hili la AN-NUUR. 

Siraju Mwanga, 
Box 8708. 
MOSHI. 

KWANZA hatubagui. Barua zinazotufikia ni nyingi kuliko uwezo wa gazeti. Tuma barua fupi zenye maudhui iliyo hai. 

MHARIRI 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Kingunge, kweli upo uonevu na dhulma

Wananchi wahoji kuhusu polisi aliyeua Arusha

Matokeo ya Darasa la Saba yacheleweshwa kusherehekea sikukuu ya Krismasi: Wananchi wahoji je, nchi hii ina dini moja tu?

Njaa yaikumba Kilwa

Dondoo za Saikolojia
Na. Abu Halima Sachangwa

Kona ya Wacha Mungu
Mavuno yangu yasiwe...

Jicho la Uzalendo: Bhabhoo! Muungwana huyoo!
Na Sompo wa Kahambwe

Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897)

Mafunzo kuhusu funga ya Ramadhani
Imetayarishwa na Africa Muslims Agency

Marekani ni mtetezi au adui wa haki?: Umoja wa Mataifa upo upande gani?
Na Abu Salim

Dawa ya ukimwi ni mwenendo mwema
Na Habiba Swedi, Arusha

Mwalimu Maif: Mwanamke aliyetumia maisha yake kufundisha Qur'an

Ijue  Madrasa Hudaa Arusha

Wazazi waaswa kutoshabikia maovu

Mzee maarufu afariki Moro

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? (jibu) 
Na Ally Said

Mapinduzi, Muungano kwa manufaa ya nani?

Fufueni EAMWS - Sheikh Amana
Na Habiba Swedi

Msiitupie lawama serikali - Dk. Omar

Baada ya kuvunjiwa nyumba, kuchomewa vyakula na Serikali: Nzasa sasa wafuturu Maembe
Na Q. Mtaita

Acheni mifumo mibovu, fuateni Qur'an - Sheikh Kilemile

Sayansi na Teknolojia 
[Kuunganisha Kompyuta kwa Kutumia Modem

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Saumu na lishe ya mama anayenyonyesha] 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita