|
|
| Njia
bora zitakazotusaidia kuwalea watoto
Na Ust. Hashim Rusaganya, Mombasa MALEZI yaliyo bora kwa watoto limepewa uzito na nafasi pana katika Uislamu. Jukumu hili huanzia kwa mzazi mwenyewe na hatimaye kwa jamii ya Kiislamu kwa ujumla. Kwa hiyo ili mtoto ainukie kuwa mwema katika jamii yategemea sana malezi ya wazazi wake walivyomlea. Katika gazeti la ANNUUR toleo nambari 175 hadi toleo nambari 177, Ustadh Kupa Pazi Said alieleza kwa upana juu ya umuhimu wa kutoa elimu bora ya awali kwa watoto wadogo. Katika ufafanuzi wake amegusia maeneo muhimu ambayo ni chanzo cha kupata watoto wema. Mimi si lengo langu kurudia makala ile bali napenda kuwakumbusha Waislamu warejee tena makala hizo kwa ufafanuzi zaidi. Hata hivyo mimi nitagusia maeneo mengine ambayo naona oia ni muhimu kuyafahamu ili tuweze kuwalea watoto wetu malezi ambayo yatasaidia kupata kizazi bora kinachomugopa Allah (s.w.) na kusimamisha ufalme wake hapa duniani. Njia bora zitakazotusaidia kuwalea watoto wetu ni hizi zifuatazo: Kwanza: Ni kumchagua mke/mume mwema. Kuoa au kuolewa na mtu ambaye ni mwema. Kwa maana ya kwamba ni Muislamu wa vitendo anayefuata Uislamu bila kujali mazingira gani anayoishi huyu ni mtu mwema. Kupatikana kwa wazazi wema ni sababu ya kupatikana kizazi kizuri kinachomtambua Allah (s.w.). Wazazi hawa ni wazi kwamba wanafahamu wajibu wao na lengo lao la kuletwa hapa duniani. Watashirikiana katika kila hali kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata malezi bora kinyume na wazazi ambao hawakuchaguana kwa wema wa mtu na hivyo kujikuta malezi anaachiwa mzazi mmoja tu na hivyo mtoto kupotoka kimaadili. Pili: Baada ya kumlea mtoto malezi bora katika kipindi hiki, wazazi wana jukumu la kumtafutia au kumpatia elimu bora. Hivyo watampeleka mtoto wao kwa mwalimu mwema anayefahamu kazi yake kama zilivyoelezwa sifa hizo katika makala ya Ustadh Kupa. Kwa muhtasari tu, mwalimu mwema ataangaliwa kwa sifa zifuatazo: Awe na Ikhlas, awe na Taqwa (ucha Mungu), awe na elimu sahihi kwa mtazamo wa Uislamu, awe mpole na huruma kwa watoto, awe anafahamu jukumu lake kuhusu huyo mtoto aliyekabidhiwa. Pamoja na wazazi kumpeleka mtoto wao kwa mwalimu mwenye sifa hizi nzuri za kiucha Mungu lakini bado yapo mambo mengine ambayo yanaweza kuathiri tabia ya mtoto kuwa nzuri zaidi. Kwanza mtoto anaiga tabia kutoka kwa wazazi kwanza. Hivyo wazazi lazima wawe na tabia njema itakayomuathiri hata mtoto wao. Tunafahamishwa ndani ya Qur’an kuwa Nabii Ismail (a.s.) yeye alikuwa mkweli wa ahadi pia alikuwa akiwaamrisha watu wake swala na kutoa zaka. Soma Surat Maryam aya ya 54 hadi 55. Sasa huu ni mfano mmojawapo wa kutuonyesha jukumu letu kwa watu wetu wanaotuzunguka. Ni kuwahimiza juu ya suala zima la kumcha Mwenyezi Mungu. Jambo la pili ambalo litaathiri tabia ya mtoto ni kumlea kwa kufuata mwenendo wa Kiislamu. Mfano kwenda naye Msikitini, kumzoesha tabia (Akhlaq) za Kiislamu kama kusalimia Kiislamu, kula vyakula halali, michezo mizuri iliyoruhusiwa katika Uislamu, adabu za kula n.k. Kwa kumzoesha haya, ni wazi kuwa mtoto atakuwa na malezi mazuri yanayoendana na mafundisho ya Uislamu. Pia ni vizuri haya yote yakaendana na kumpa mawaida (nasaha) nzuri watoto (rejea Qur’an surat Luqman aya ya 13), wazazi wamtahadharishe mwanao wao juu ya hatari atakayoipata kwa Mola wake atakapokuwa na tabia mbaya. Wazazi pia wasisitize kumtia adabu pindi anapokosea. Yapo makosa ambayo wazazi hawana budi kuyakemea kwa mtoto wao pale wanapogundua kuwa amefanya makusudi. Mfano anajua kuwa ni lazima awaheshimu wakubwa ikiwa ni pamoja na kuwatolea salam ya Mwenyezi Mungu. Asipofanya hivyo aonywe haraka iwezekanavyo. Ni vipi tutaweza kuwalea watoto wetu wafikie kuwa na tabia njema: Tutaweza kufikia lengo hili kwa kuwapa au kuwafundisha itikadi sahihi ya maisha. Itikadi ambayo baadaye akishakuwa mkubwa haitamvuruga akili akachanganyikiwa. Bali kadri anavyokuwa mkubwa itikadi hiyo imsaidie kupanua mawazo na kipaji chake awe Muislamu safi anayetegemewa na jamii ya Kiislamu. Vile vile mtoto apewe mawazo sahihi ambayo hayapotoshi ukweli wa mambo ulivyo. Kwa mfano kumwambia kwamba zamani babu zetu walikuwa ni nyani wakitembea miguu miwili na waliishi porini kama nyani wa karne hii walivyo. Haya ni mawazo potofu kabisa sawa na kumpotezea kumbukumbu ili baadaye upachike za kwako kisha umtumie kwa malengo uyatakayo. Wazazi wanatakiwa wamfahamishe mtoto umuhimu wa kuwa na rafiki mwema ambaye tabia zake ni nzuri hazipingani na mafundisho ya Uislamu. Ikibidi hapa mzazi afuatilie kwa karibu sana mwenendo wa rafiki au marafiki wa kijana wake. Mtoto afundishwe michezo mizuri ambayo inamjenga kiafya, kiakili na ambayo inaendana na mwenendo wa Kiislamu. Ahadharishwe na michezo haramu kama kamari n.k. Mtoto ahadharishwe na shirki na mambo mengine ya uzushi. Vile vile mtoto asipewe fursa ya kuangalia sinema na picha nyingine ambazo si za maadili ya Kiislamu. Mwisho wazazi wahakikishe kwamba mtoto wao anajengewa hisia za kujiona
kwamba analazimika kuwa Khalifa wa Allah (s.w.) katika kusimamisha ujumbe
wa Allah (s.w.) (Uislamu) hapa duniani
Ijue Madrasatul-Qaadiriya Sokoni I Arusha. Na Habiba Swedi, Arusha MADRASA hii ipo nje kidogo ya mji wa Arusha, muasisi akiwa ni Maalim (Khalifa) Takdiri Haji Mohammed pamoja na mdhamini wa madrasa hiyo na Msikiti wake hapo Sokoni ni mzee Ismail Ulomi. Ilianzishwa mwaka 1991 ikiwa na wanafunzi 15 tu, muda mfupi baadaye idadi ya wanafunzi iliongezeka hadi kufikia 50. Hivi sasa madrasa ina wanafunzi 120 ambao kati yao ni watoto wadogo 50, kinamama 45 na vijana wa umri wa kati wako 25, vijana hawa wanatoka sehemu mbalimbali nchini kuja kutafuta elimu. Madrasatul Qaadiriya kama jina linavyoonyesha ni tawi la vyuo vya jumuiya ya Zawiya el-Qadiriya ambayo ilianzishwa miaka ya 1985 hapa Arusha. Makao Makuu ya Jumuiya hii yako Dar es Salaam na mlezi wake ni Sheikh Mohammed Nassor Abdallah al-Qadiriya. Masomo yafundishwayo madrasani hapo ni pamoja na Qur’an na tafsiri yake, Fiqh, Sira, Lugha ya Kiarabu na Kiingereza, Swarfa, Hadith, Tawhiid, Tasaufi tukiyataja kwa uchache tu. Mafanikio ya kujivunia ya madrasa hii ni kwamba imeweza kutoa vijana kwenda sehemu mbalimbali kufundisha na kujiendeleza zaidi kimasomo. Kadhalika eneo la Sokoni ni limeweza kuonyesha nuru ya Uislamu baada ya kuwa ni eneo la vurugu katika siku za nyuma. Pia madrasa ina matawi zaidi ya matatu Sokoni I nayo yakichangia maendeleo ya dini ya Allah (s.w.). Kwa upande wa malengo ya baadaye, madrasa hii ina mipango ya maendeleo mingi sana, lakini tukiyataja machache tu ni kujengwa kwa shule ya ufundi, shule ya msingi na ya sekondari. Tayari wanayo shule ya Chekechea kwa ajili ya watoto wa Kiislamu. |
YALIYOMO
Tahariri Onyesheni ushujaa wa Badri Daniel kuwatimua waumini Msikitini Waislamu Moshi: Wadai kulishwa nguruwe, vibudu Dondoo za Kisakolojia
Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) - 2 MASHAMBULIZI YA MAREKANI NCHINI IRAQ Njia bora zitakazotusaidia kuwalea
watoto
Ijue Madrasatul-Qaadiriya Sokoni
I Arusha.
Tutafute kwanza ufalme wa Allah (s.w.)
Chuo cha Kilimo Ukiriguru kupata
Msikiti mpya
Huduma za maji Kondoa haziridhishi
Mnyororo wa imani
Je, Yesu alibatizwa?
Kufuatia Waislamu kuritadishwa Merela Morogoro: Masheikh wa mjini watupiwa lawama Abiria walaani kumwagiwa pombe Kondoa Sheikh Bafadhil ateuliwa
kudhamini waandishi wa habari Morogoro
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|