AN-NUUR 
Na.183 Ramadhan 1419, Januari 8 - 14, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Tutafute kwanza ufalme wa Allah (s.w.)
 
Na Mwapwani Mohammed
 

NIMEKUWA nikufuatilia makala za Alhaj Yusuf Kalala katika gazeti hili zikituhimiza Waislamu wa Tanzania tutafute kwanza ufalme wa kisiasa na kuwa silaha yetu kuu ni kuwa pamoja (block vote). Ni nzuri kwa mtazamo fulani, lakini ningependa kuchukua fursa kutoa maoni yangu ili lengo na madhumuni ya Uislamu yabaki yale yale yaliyokusudiwa na Allah (s.w.). 

Kimsingi dhana "tafuteni kwanza ufalme wa kisiasa" itakuwa sahihi kama italenga kwenye kazi ya Mitume na Manabii wote wa Allah (s.w.) (kumtii Allah (s.w), kusimamisha sheria na ufalme wa Allah hapa duniani kama ilivyo mbinguni.). 

Mtume Issa (a.s.) anasema: "Msisimbuke basi, mkisema tule nini? Au tunywe nini? Au tuvae nini? Kwa maana hayo yote hayatafuta; kwa sababu baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake na hayo yote mtazidishiwa". (Mathayo 6:31 - 33). 

Mitume, Manabii na wacha Mungu wote harakati na siasa zao zote kimaneno (mahubiri) na kimatendo (vita) zililenga kusimamisha ufalme wa Allah (s.w.), kwanza kabisa katika kila nyoyo (nafsi) ya mtu, kisha kwa jamii nzima. Hii ni kwa kuwa Allah (s.w.) ameahidi utawala wa haki wenye amani na ustawi mkubwa ni ule tu ulio chini ya viongozi na watendaji walio chini ya Katiba ya dola ya Allah (s.w.) kama isemavyo katika Kumb. 17:14-20. 

Nayo Katiba mpya (Qur’an) inasema: "Hakika tuliteremsha Taurati yenye uongozi na nuru; ambayo kwayo Manabii waliojisalimisha (kwa Mwenyezi Mungu) waliwahukumu Mayahudi na watawa na maulamaa pia (waliwahukumu kwa hiyo Taurati); kwa sababu walitakiwa kuhifadhi kitabu (hicho) cha Mwenyezi Mungu; nao walikuwa mashahidi juu yake. Basi nyinyi (Waislamu) msiwaogope watu, bali niogopeni (Mimi). Wala msibadilishe aya zangu kwa thamani chache (ya duniani). Na wasiokuwa kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri. (Qur’an 5:44). 

Inasisitiza zaidi inasema: "Na wahukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao. Nawe jihadhari nao wasiye kukugeuza na baadhi ya yale aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu. Na kama wakikengeuka basi jua kwamba hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwafanikishia (adhabu) kwa baadhi ya dhambi zao. Na bila shaka wengi katika watu ni maasi. Je, wao wanataka hukumu za kijahili (za siku zile za ujinga kabla ya kuletwa Mtume)? Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu - (yanafahamika haya) kwa watu wenye yakini". (Qur’an 5:49-50) 

Vile vile Allah (s.w.) aliahidi tangu katika katiba ya kale kuwa, pale Waislamu watakaposhikamana barabara na katiba yake watapata amani na ustawi mkubwa (Kumb 28:1-4), na wakiitupa na kushikamana na Katiba za kigeni au walizojitungia wenyewe watapata mateso, hofu na kudhalilishwa na makafiri (Kumb. 28:15-68). Ukweli wa ahadi hizo ulijidhihirisha tangu zamani, kwa mfano; dola ya Kiislamu ya Samaria (Israel Kaskazini) ilipomwasi Allah (s.w.), mfalme Sargono wa Ashuru aliivamia na kuitawala mwaka 721 KK. 

Nayo dola ya Yuda (Israel Kusini) alipoasi na kukataza kutubu mfalme Nebukadneza wa Babeli aliivamia na kuitawala. Na walipoasi ili kujirejeshea utawala wa kisiasa bila kutubu walipata madhara makubwa ya kuteketezwa mji mkuu wao (Jerusalem), (Yeremia 39:1-10) na baadaye kuteketezwa Msikiti mkuu (Hekalu) wa Jerusalem, baada ya uasi wa tatu. 

Mateso ya kutisha dhidi ya Waislamu yaliyofanywa na mfalme Mgiriki aitwaye Antioko Epifani aliyetawala Palestina (Uyahudi) katika mwaka 175 - 163 KK. Chanzo cha mateso hayo wanakielezea Wayahudi (Waislamu) wenyewe kama ifuatavyo: 

"Lakori Selenko alipokufa na Antioko aitwaye Epifani alipopokea ufalme wake; Yasoni (Muislamu) nduguye Onia (aliyekuwa Kuhani/Sheikh Mkuu) alimnyang’anya nduguye cheo chake cha Kuhani Mkuu akaahidi katika (barua ya) maombi yake kwa mfalme kutoa talanta za fedha mia tano na sitini, na talanta themanini katika akiba nyingine. 

Zaidi ya hizo, aliahidi kutoa nyingine mia na hamsini iwapo atapewa ruhusa ya kujenga kiwanja cha michezo ya Kiyunani (Kigiriki) na chama chake cha vijana na kuwaandika wenyeji wa Yerusalem kuwa raia wa Antikia. 

Mfalme alipokubali ombi hilo, Yasoni aliposhika kazi, akaanza kushawishi (makuhani) wenzake wazikubali kawaida za Kiyunani (Kigiriki). Aliziachilia mbali sharti za kifalme zilizotolewa kwa ajili ya Wayahudi (kufuata sheria za Kiislamu - Torati), alizozipata Yohana, baba wa Eupolemo, alipotumwa kwa Wanini kutaka urafiki na kufanya mapatano, akazivunja kawaida za halali za maisha akaingiza desturi mpya zilizokatazwa na sheria. 

Alifurahi kuweka kiwanja cha michezo ya Kiyunani chini ya ngome yenyewe; akawashawishi vijana walio bora wavae kofia za Kiyunani. Tamaa ya kufuatisha desturi za Kiyunani na mila za kigeni ilizidi mno kwa sababu ya ukufuru wa Yasoni - si kuhani kabisa huyu! 

Hata Makuhani (Masheikh/Maimamu) hawakufurahia tena ibada ya madhabahuni; bali walilidharau hekalu na kuziacha dhabihu ili kukimbilia mambo ya haramu kiwanjani. Mara michezo ya kutupa, disko ilipotangazwa (kilipolia kipenga). Hivyo walizifanya desturi zilizoheshimiwa na baba zao kuwa si kitu wakahesabu mambo ya Kiyanuni tu kuwa ndio bora. 

Kwa hiyo misiba mikubwa iliwapata, maana watu wale wale ambao walipenda sana kuzifuata desturi zao na kutaka kufanana nao sawasawa, hao waligeuka kuwa adui zao na kuwatesa. Kuzihalifu amri za Mungu si jambo dogo; haya yataonekana wakati wake". (2Makabayo 4:7-17). 

Katika kilele cha mateso, Antioko Epifani aliwachukua wacha Mungu saba na mama zao waliokataa kutii sheria za Kigiriki na kuwakataka viungo vyao wakiwa hai kisha kuwakaanga mmoja mmoja ili waikane torati, lakini wao walisema hivi: "Na baada yake walimchukua wa sita. Naye alipokuwa kufani alisema, wasidanganyike bure, sisi tunateswa hivi kwa sababu ya dhambi zetu wenyewe, kwa kuwa sisi tumemkosa Mungu wetu. Ndiyo sababu mambo haya ya kutisha yametupata". (2 Makabayo 7:18) 

Tukizingatia sababu hizo zilizopelekea Waislamu wenzetu wa zamani waadhibiwe vikali, sisi bado tunazitenda tena kwa kiwango kikubwa zaidi. Tumeacha na kujiweka mbali kabisa na Qur’an na Sunnah na kung’ang’ania sheria tulizozitunga wenyewe, huku tukijipinga kufuata "maendeleo" na "ustaarabu" wa Kizungu, kimchezo, kimavazi, kiutamaduni, kistarehe (mabaa, madisko, dansi, taarab n.k.) tukidharau kabisa nyakati na umuhimu wa sala, funga n.k. 

Japo hayajatufika yaliyowafika wenzetu, lakini tusipojirekebisha yatatufika tena zaidi ya hayo. Wenzetu waliendelea kuadhibiwa hali walipotubu na kuanzisha vita vitakatifu vya ukombozi chini ya uongozi wa Kuhani Matathia na baadaye mwanaye Yuda Makabayo na kupata ushindi mkubwa kwa muda mfupi. (1 Makabayo sura ya pili hadi ya nne). 

Hivi sasa dunia inashuhudia baadhi ya dola zinazoongozwa na Waislamu zikiwatendea unyama wa hali ya juu Waislamu wenzao. Na hata pale "demokrasia" (kura) inapoonekana kuweka viongozi wenye nia ya kusimamisha ufalme wa Allah (s.w.) (mfano mzuri ni Algeria), uchasguzi unakuwa batili na kufutwa. Inatupasa kufahamu kuwa "demokrasia" na "uchaguzi" ni mbinu nyingine za mabeberu kuendelea kutawala kwa namna waipendayo. 

Mbinu pekee itakayotuletea amani na ustawi mkubwa Waislamu na wasio Waislamu ni ile ile iliyotumiwa na Mitume na Manabii. Kwanza kufanya harakati (mahubiri) za kusimamisha ufalme wa Allah (s.w.) kwenye nyoyo za viongozi wa Misikiti (Maimamu) na taasisi za Kiislamu ili kufukuza utawala wa shetani unaoweka woga nyoyoni mwao. Baada ya kuondoa woga nyoyoni mwao, wafanye harakati kwa nguvu na uwezo wao wote ili kuondoa utawala wa shetani katika nyoyo za waumini wao (woga, ulevi, uzinifu, wizi, kuacha sala, funga n.k.). 

Baada ya kusimamisha barabara ufalme wa Allah (s.w.) nyoyoni mwa viongozi na Waislamu wote (au wale watakaopatikana) ndipo tutakapoweza kusimamisha barabara ufalme wa Allah (s.w.) katika nyanja zote za maisha (siasa, uchumi, sayansi n.k.) na kuleta amani, haki na ustawi kwa Waislamu na wasio Waislamu. Mbinu yeyote kinyume na hiyo ni kumuasi Allah (s.w.), kujidanganya wenyewe na kupoteza muda bure. "Tutafute kwanza ufalme wa Allah (s.w.) na falme zingine zote zitafuata". 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Onyesheni ushujaa wa Badri 

Daniel kuwatimua waumini Msikitini 

Waislamu Moshi: Wadai kulishwa nguruwe, vibudu 

Dondoo za Kisakolojia 
Na. Abu Halima Sachangwa 

Kona ya WachaMungu  

Jicho la Uzalendo 

Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) - 2 

Vipi umoja wetu uwe hatari ? 

MASHAMBULIZI YA MAREKANI NCHINI IRAQ  

Marekani si rafiki mwema  

Tunahitaji UN ya Waislamu - 2  

Njia bora zitakazotusaidia kuwalea watoto 
Na Ust. Hashim Rusaganya, Mombasa 

Ijue Madrasatul-Qaadiriya Sokoni I Arusha. 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tutafute kwanza ufalme wa Allah (s.w.) 
Na Mwapwani Mohammed 

Sheikh Kisiwa atunuku zawadi 

Chuo cha Kilimo Ukiriguru kupata Msikiti mpya  
Na Mwandishi Wetu, Mwanza  

Huduma za maji Kondoa haziridhishi 
Na Abu Zuberi, Kondoa  

Mnyororo wa imani 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Je, Yesu alibatizwa? 
Na Muhibu Said  

Kufuatia Waislamu kuritadishwa Merela Morogoro: Masheikh wa mjini watupiwa lawama  

Abiria walaani kumwagiwa pombe Kondoa 

Sheikh Bafadhil ateuliwa kudhamini waandishi wa habari Morogoro 
Na Mussa Ally, Morogoro 

Sayansi na Teknolojia 
[Tatizo la mwaka 2000] 

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Chakula na lishe 
[Mlo wa siku ya Idd] 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita