AN-NUUR 
Na.183 Ramadhan 1419, Januari 8 - 14, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Mnyororo wa imani
 
  
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

NIMEKUWA nikisoma katika magazeti, majarida, vitabu n.k. kwa uchungu mkubwa, matusi, kejeli, dhihaka n.k. dhidi ya baadhi ya Mitume na Manabii wa Mwenyezi Mungu (s.w.). Tatizo kubwa linalowakabili waandishi hao ni kutojua "mnyororo wa imani" (Believing Chain). Hivyo wanadhani kwa kumtukana Mtume fulani, wanamtukuza Mtume wanayempenda na kumfurahisha Mwenyezi Mungu (s.w.). Katika makala hii nitajaribu kuwasaidia wapendwa hao katika Bwana, kwa kuwafafanulia mpango kamili wa Mwenyezi Mungu (s.w.) kuhusu Mitume na Manabii wake. Ili nieleweke kirahisi, nimegawa somo hili katika maeneo mawili ya Mwenyezi Mungu ni nani kwa Mitume na Manabii, na vipi Nabii au Mtume anakuwa mkuu kuliko wenzake. 

Mwenyezi Mungu na Mitume: 

Pamoja na kuwa Mwenyezi Mungu ni MUNGU na BWANA wa Mitume na Manabii, kiutendaji Yeye ni Waziri wa Elimu, Mkuu wa taasisi ya Mitaala (mikakati), Mkaguzi wa elimu na mwalimu mkuu. Manabii wao ni waalimu wa kawaida. Hivyo mipango yote ya kufikisha elimu kwa walengwa (binadamu) kuanzia waalimu (Mitume), silabasi (mwongozo), mitaala (vifaa) na mbinu za kufundishia hupangwa na Yeye mwenyewe. Kwani ndiye peke yake anayejua elimu sahihi ya walengwa. Hivyo Manabii hupewa elimu kubwa zaidi, miongozo bora zaidi, nyenzo bora zaidi na mbinu bora zaidi kulingana na ile jamii wanayotumwa. 

Tuangalie mifano ya Manabii Musa (a.s), Yesu (a.s.) na Muhammad (s.a.w.). Wakati wa Nabii Musa (a.s.) kulishamiri sana elimu ya uchawi. Waganga wa Misri na kwingineko waliweza kufanya mazingaombwe ya ajabu sana, hivyo wengine wakaonekana ni miungu kwa hiyo Mwenyezi Mungu alipomtuma Musa (a.s.) alimpa uwezo mkubwa zaidi na kuweza kuzima mazingaombwe ya waganga. 

Wakati wa Nabii Yesu (a.s.) elimu ya kifikra (falsafa) ilishamiri. Tayari kulikuwa na fikra za Mafilosofa akina Socrates (B.C 484 - 399), Plato (B.C 427 - 348), Aristotle (B.C 384 - 322) N.K. Aidha elimu ya udaktari ilishamiri sana. Hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.) akampa Nabii Yesu (a.s.) falsafa ya juu sana na kufundisha kwa mifano na mafumbo (tazama Mathayo 13:34, Marko 4:33-34) ili kuwaponda wanafalsafa na akapewa miujiza mikubwa ya uponyaji n.k. ili kuwaponda madaktari. 

Wakati wa Nabii Muhammad (s.a.w.) akili za watu ziliisha chemka sana. hivyo wakawa wanathibitisha na kukanusha mambo kwa ushahidi wa kuona, rejea za vitabu na majaribio ya kisayansi. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akateua Mtume asiyesoma kabisa, tena kutoka jamii iliyobobea katika ujinga, na kumpa elimu iliyowazidi wasomi wote. Hadi leo bado watalaamu hawajamaliza kuthibitisha yaliyo katika Qur’an na Sunnah. Hizi zote ni njia za kufundisha za Mwenyezi Mungu (s.w.) zenye kuonyesha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.) yuko juu ya kila kitu (Almighty - Alla kulli shay-in Qadiir). 

Hivyo Mitume tofauti, mbinu tofauti, nyenzo tofauti n.k. yote hufanywa na Mwenyezi Mungu ili kumsaidia mwanadamu amkubali Mwenyezi Mungu (s.w.) na Mtume wake anayehusika (aliyepo wakati huo) na kuishi kama atakavyo Mwenyezi Mungu kulingana na mazingira na wakati wanaoishi. 

Nabii Mkuu: 

Kiubora na kiheshima, Mitume na Manabii wote wako sawasawa. Lakini kiutendaji lazima awepo Nabii Mkuu au kiongozi wao, ili kurahisisha utendaji kazi na kuepusha migongano. Watu wengi wanadhani Nabii Mkuu ni yule aliyefanya miujiza mingi au kuzaliwa tofauti na wenzake. Ili kupata ukweli wa jambo hili, nitanukuu aya ya Qur’an iliyo maalum kwa Manabii, kisha nitathibitisha utekelezaji wake katika Biblia. 

"Na (kumbukeni) alipochukua Mwenyezi Mungu ahadi kwa Manabii (akawaambia): "Nikishakupeni kitabu na hikima, kisha akakujieni Mtume msadikishaji wa yale yaliyo pamoja nanyi, ni juu yenu kumwamini na kumsaidia". Akasema: (Mwenyezi Mungu) "Je, mmekiri na mmekubali kushika agizo langu juu ya hayo?" Wakasema: "Tumekubali". Akasema: "Basi shuhudieni, na mimi ni pamoja nanyi katika mashahidi". (Qur. 3:81). 

Akifafanua aya hiyo, Nabii Yesu (a.s.) anasema: "Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona Nabii. Naam, nawaambia na aliye mkuu zaid ya Nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, tazama namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, atakayeitengeneza njia yako mbele yako". (Mathayo 11:9-10). 

Aya hii haionyeshi Nabii maalum aliyeandikiwa hayo, bali Nabii yeyote anayekuja nyuma ya mwenzake anakuwa mkubwa kuliko yule aliyetangulia. Hapa ieleweke wazi kuwa katika Qur’an 3:81, Mwenyezi Mungu anaongea na roho za manabii tu kabla hazijapewa nchi (kuja duniani). Hivyo manabii kabla hawajapewa rasmi unabii, hawajui kama walitoa kiapo hicho mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.). 

Sasa tuone Manabii wamekiheshimu vipi kiapo hicho cha kiroho. Nabii Daud (a.s.) anasema: "Neno la BWANA kwa Bwana wangu, uketi mkono wangu wa kuume. Hata niwafanyapo adui zako kuwa chini ya miguu yako". (Zaburi 110:1. 

Na Nabii Yesu (a.s.) akitamba na filosofia yake ya juu, anawajaribu wasomi wa Kiyahudi kwa kuwaambia: "Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akasema, mwaonaje katika habari za Kristo? Ni mwana wa nani? Wakamwambia, ni mwana wa Daud. Akawauliza, imekuwaje basi Daud katika Roho kumwita Bwana, akasema, Bwana alimwambia, Bwana wangu umeketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako kuwa chini ya miguu yako. Basi Daud akamwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe? Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu yeyote tangu siku ile kumwuliza neno tena". (Mathayo 22:41-46). 

Wanatheolojia wa sasa wakijaribu kujibu swali hilo, nao wanavurunda kabisa kusema: "22:45 Masiya, ingawa ni nasaba ya Daud kadiri ya ukoo wake wa kibinadamu (1:1-17), alikuwa na tabia ya kimungu pia iliyomfanya awe juu ya Daud. Na hali hiyo Daud alikwisha isema mbele. Hilo ndilo jibu walilopaswa kumpa Yesu". (Biblia takatifu Tabora Uk. 901). 

Nabii Yesu (a.s.) akimtukuza Nabii Yohana (a.s.) kuliko Manabii wote waliokuwa kabla yake anasema "Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji ..." (Mathayo 11:11). Lakini akilimlinganisha na yeye (Yesu a.s.) anamalizia kwa kusema "... walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye (Yohana a.s.). Akithibitisha hilo, Yohana (a.s.) anasema "kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba, bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto". (Mathayo 3:11). Yohana (a.s.) alimwogopa Yesu (a.s.) hata kabla Yesu hajapewa utume. "Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordan kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, kubali hivi sasa, kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali (Mathayo 3:13-15) na Mtume atakayekuja baada yake, alisalimu amri na kusema "Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja MKUU wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu". (Yohana 14:30). 

Tazama pia Mathayo 12:31-32. Hapa napenda niweke wazi kuwa, neno "ulimwengu" hapo halimaanishi milki ya shetani. Kwani shetani anaimiliki dunia tangu enzi za Adam na Hawa. Hivyo Yesu (a.s.) asingetumia neno "yuaja" kama angemaanisha shetani. Neno "ulimwengu" limefasiriwa na wanatheolojia kama ifuatavyo: "1:9 "Ulimwengu" kadri ya Yohana una maana au ya viumbe vyote au ya dunia au binadamu au wale wote wanaomkataa Mungu na kumdhulumu Yesu Kristo na wafuasi wake (7:7; 18:19; 17:14). Anaposema "ninyi ni wa ulimwengu huu" au kitu kama hicho Yohana anatumia maana hiyo ya mwisho ya ulimwengu (8:23) Biblia Takatifu Tabora Uk. 967. Hivyo neno "mkuu wa ulimwengu" linamaanisha mkuu wa dunia yote na vilivyomo. Yaani Nabii Mkuu. 

Ili mtu ajue Mwenyezi Mungu anataka nini na kwa utaratibu gani katika wakati uliopo, lazima akubali kufanya "kazi ya Mungu". "Basi wakamwambia, tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndio kazi ya Mungu, mwaminini Yeye aliyetumwa na Yeye". (Yohana 6:28-29). 

Kutokumwamini Mtume aliyetumwa katika wakati unaohusika ni kumchukiza sana yule Mtume unayemwamini. Hili limewekwa wazi na Mtume Yesu (a.s) "Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba, yuko anayewashitaki, ndiye Musa mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini na mimi, kwa sababu yeye aliandika habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini wapi maneno yangu". (Yohana 5:45-47). 

Hivyo, kumkataa, kumdharau, kumtukana Mtume aliyekuja baada ya Mtume unayemwamini ni madhambi makubwa sana. Jitihada yoyote mtu atakayofanya ili kuhalalisha matusi yake, inathibitisha uduni wake wa fikra na kubobea kwa kiasi kikubwa katika fani ya upuuzi, uzushi na porojo. Na jinsi mtu atakavyokazana kufanya juhudi hiyo, ndivyo anavyodhihirisha ubingwa wake katika fani hiyo. Cha kushangaza sana waliobobea sana katika fani hiyo ni Maprofesa. Katika kuthibitisha ubingwa wao, wanatuletea kitabu kiitwacho "Allah wa kwenye Qur’an siye Yehova". Mimi kabla sijasoma kitabu hicho, nacho nakiita cha upuuzi (Rejea makala yangu "Msiiparamie ovyo Biblia" katika ANNUUR Na. 169). 

Ndugu msomaji hebu fuatilia maelezo ya Kamusi zifuatazo nadhani nawe utaniunga mkono. Katika Kamusi iitwayo "Alqamus al Madrasi - The Dictionary". Arabic - English, English - Arabic ya Bwana Elias A. Elias, 1984, Karachi Pakistan ikifasiri neno "Mwenyezi" katika Uk. 10 inasema "Almighty - Alqadiir Alqadiiru alaa kullli shay-in" (yaani, mwenye uwezo. Mwenyezi uwezo wa kila kitu). Ikifasiri neno "Mungu" katika uk. 131 inasema "God - Allah. Ilaaha, Rabbbu" (yaani, Mwenyezi Mungu. Mungu Bwana). Hapa tuzingatie kwamba; neno "Jehova" ni neno la Kiebrania. Hivyo halimo katika kamusi ninazotumia hapa za Kiingereza, Kiarabu na Kiswahili. Badala yake tunatumia neno lililo sawa nalo la "Mwenyezi Mungu" (tazama Biblia Uk. VI). 

Sasa tuzingatie kamusi nyingine iitwayo "A Standard Swahili - English Dictionary" ya iliyokuwa Inter-territorial Language Committee for the East African Dependencies chini ya Katibu wake Mkuu Frederick Johnson iliyotolewa na Oxford University Press, Ely House, London W.I., mwaka 1939. Kamusi hii imepata baraka za Askofu Thomas wa Zanzibar na ndiye aliyeiandikia neno la awali (fore word). 

Pamoja na maneno mengine ya kuisifu anasema: "It is a matter of good fortune that the revision of these two dictionaries (Za steere na Madan) was placed in the capable hands of the late Frederick Johnson, formerly Secretary of the Inter-territorial Language (Swahili) Committee, which has done so much so standardize the language and to preserve its orthography from confusion (kama hizi za Maprofesa). Anamalizia kwa kusema "This conspectus of the Swahili language neill there fore help us all to find that the language is more worthy of our serious study than perhaps we had previously considered". 

Katika ukurasa wa 9-10 tunakuta maneno "Allah - n. God. Seldom used except in Arabi expressions and formulas, such as: Allah Akbar, God is great. La illahi ila Allah, there is no God but God, the first clause of Muhammadan creed, which is song over and over again by the funeral procession on its way to the grave ... (cf. Rasi, Mola, Mungu. Ar.). Katika ukurasa wa 315 tunakuta maneno "Mungu, n. (miungu). (1) God, a god; (2) Providence, luck, accident - used to describe anything unccountable or unexpected. Words connected with Mungu are Mwenyezi Mungu, i.e. Mwenye enzi Mungu, Almighty God... Mola is sometimes used for God, but Seldom Allah ... (cf. Mola, Allah, Rabi, and various titles of God)" 

Ili nami nitoe mchango wangu wa "kufanikisha" kitabu hicho (Allah sio Yehova), naona nimwongezee Profesa wangu maneno Kristo, Isa, Nabii na Mtume kwa mujibu wa kamusi hizo. 

Katika kamusi ya Elias A. Elias Uk. wa 49 tunakuta maneno "Christ - Assayyidul Masiihu. Isa" (Kristo - Bwana masihi. Isa). Na katika kamusi ya Frederick Johnson Uk. 143 tunakuta maneno "Isa, n. a Proper name. Also the name for Jesus Christ known to Muhammadas - often with addition bin Mariam. Katika Uk. 328 tunakuta maneno "Nabii, n. ma- a Prophet, a preacher of righteousness, one who foretells the future. Used of Adam, Noah, Abraham, Jesus, and others as well as Muhammad. (cf. bashiri, tabiri, sibu. 

Na katika ukurasa wa 477 tunakuta maneno "... Mtume, n. one who is employed or sent, a messenger, an emissary, but esp. Muhammad. i.e. Apostle, and also of the chief characters of the old testament, Moses, Job, and others. It is the word adopted for Christian Apostles also ... used like Mtume, of Muhammad, as Apostle of God...". 

Namalizia kwa kusema, ninakisubiri kitabu hicho kwa hamu. 


Je, Yesu alibatizwa?
 
  
Na Muhibu Said

KWA kusoma peke yake maelezo yaliyo kwenye Mathayo 3:13-17 na Marko 1:9-11, imekuwa ikidaiwa na rafiki zangu Wakristo kuwa Nabii Isa ama Yesu (a.s.) akiwa na umri usiopungua miaka thelathini alibatizwa na Nabii Yahya au Yohana Mbatizaji (a.s). kwa kuzamishwa kwenye maji ya mto Jordani. 

Kufuatia dai hilo, dhana ya "ubatizo" imejengeka kiasi cha kufanywa kuwa ni nguzo muhimu na ya lazima ambayo "uumini wa mtu kwa Mungu", kuanzia mtoto mchanga hadi kabla ya kufa kwake hauhesabiwi kuwa ubatizo kamili hadi hapo atakapokuwa ameitekeleza "nguzo hiyo". 

Aidha, dhana hiyo imeshamiri, licha ya kuibuka mgawanyiko miongoni mwao kwa kuwepo makundi mawili tofauti, la Wakristo wanaofuata ubatizo wa kuzamishwa kwenye maji mengi na wale wanaoamini ubatizo wa kuzamishwa kwenye maji machache. 

Hata hivyo, pamoja na kutokuwepo maelezo ya wazi ya maandiko ya Biblia yanayofafanua hasa lengo la mantiki ya "Yesu kuzamishwa (kubatizwa) ndani ya maji ya mto Jordani na Yohana", kwanza kuna utata mkubwa wa kuthibiti (kuwepo) kweli kwa tukio hilo. Na ndio maana pamoja na kufanikiwa kutunga masikukuu kadhaa, lakini wameshindwa kabisa kubuni "sikukuu ya kubatizwa Yesu" au angalau kutaja japo kumbukumbu tu ya siku ambayo tukio hilo "muhimu " lilifanyika. 

Ubatizo wa Yohana haukumstahili Yesu 

Biblia inafundisha dhahiri kuwa ubatizo wa Nabii Yohana (a.s.) ambao ni wa maji ulikuwa ni kwa ajili ya utakaso wa kumwondolea mtu dhambi, kama tunavyosoma katika aya zifuatazo: 

"Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi. Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto Yordani, wakiziungama dhambi zao". (Marko 1:4-5). 

Kwa maandiko hayo, ni wazi kuwa ubatizo huo wa Yohana kamwe haukumstahili Yesu kwani kama Manabii wengine, Yesu hakuwa na dhambi hata astahili kubatizwa na Yohana, kama mwenyewe (Yesu) anavyosema: 

"Nami kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki. Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki? (Yohana 8:45-46). 

Kama wanadamu wengine, Yesu naye hakurithi dhambi ya asili 

Katika kushikilia msimamo wao, rafiki zangu Wakristo hudai kwamba sababu ya msingi ya wao kutilia mkazo "ubatizo" ni kutaka kuwasafisha wanaadamu ili waondokane na dhambi ya asili waliyoirithi kutoka kwa Adamu na Hawa ya kula tunda walilokatazwa na Mungu kulila. Na kwa vile Yesu naye ni mwanaadamu basi naye pia atakuwa ameirithi dhambi hiyo na kwa hiyo ubatizo wa Yohana kwake wa kuziungama dhambi pia ulimstahili kama wanaadamu wengine wanavyotakiwa kubatizwa kwa ajili hiyo. 

Hata hivyo, dai la kwamba mtu anaweza kurithi dhambi ya mtu mwingine kwa kweli lilikwishapingwa vikali na Mungu katika Biblia Takatifu. Maandiko yafuatayo yanathibitisha ukweli huu: 

"Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe". (Kumbukumbu la Torati 24:16). 

Aidha, suala la mtu kurithi kosa la mtu mwingine yeyote ijapokuwa ni baba yake, Mungu alilipinga vikali kwa kusema: 

"Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayo kufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe; haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake". (Ezekieli 18:20). 

Kufuatana na maelezo hayo ya Mungu, ni dhahiri kuwa kosa lile la Adamu (a.s.) kama baba yetu haliwezi kamwe likatuhusu kwa kuwa sisi, Yesu akiwemo kama wanawe, siyo tuliolitenda. Hivyo ni wazi kuwa kama binadamu wengine Yesu naye hakurithi "dhambi hiyo ya asili" hata uhitajike kwake ubatizo wa Yohana ambao ulikuwa ni ungamo na ondoleo la dhambi. 

Yohana hakuwahi kumbatiza Yesu 

Kinyume na maelezo ya Mathayo 3:13-17 na Marko 1:9-11, maandiko mengine ya Biblia yanaonyesha wazi kuwa Nabii Yohana (a.s.) hakuwahi kabisa kumbatiza Bwana Yesu (a.s.). Na hiyo ni kutokana kwamba muda mchache baada ya kuzaliwa katika nchi ya Israeli, Yesu akiwa yu mtoto mdogo, Yusufu ambaye ameelezwa na Biblia kama mlezi alipewa amri na Mungu ya kumwondoa mtoto Yesu na mamaye hapo Israeli na kukimbilia nchini Misri. 

Uamuzi huo wa Mungu wa kumhamishia mtoto Yesu na mamaye kwa muda nchini Misri kama Biblia inavyoeleza, ulifuatia azma ya mfalme Herode aliyekuwa akiitawala Israeli zama hizo kutaka kumwangamiza mtoto Yesu. (Mathayo 2:13-15). 

Aidha, Biblia inaonyesha wazi kuwa mtoto Yesu alipokimbilia Misri alimwacha Yohana akiendelea kuhubiri na kubatiza hapo nchini Israeli chini ya utawala wa mfalme Herode. 

Mtoto Yesu akiwa Misri, Herode amchinja Yohana Israeli 

Biblia inaonyesha pia kwamba wakati mtoto Yesu akiwa bado nchini Misri, huko Israeli mfalme Herode alimchinja Nabii Yohana kwa vile Yohana alimwambia mfalme Herode kuwa "si halali kwake kuwa na mke wa nduguye". 

Herode naye afariki, mtoto Yesu arejea Israeli na kumkuta mfalme mpya aitwaye Arkelao, mtoto wa Herode 

Maandiko ya Biblia yanabainisha wazi kuwa baada ya kukaa kitambo kidogo nchini Misri, hatimaye Mungu alimwamuru Yusufu amrejeshe mtoto Yesu na mamaye nchini Israeli baada ya mfalme Herode kufariki na nafasi yake kuchukuliwa na mwanawe aitwaye Arkelao, kama tunavyosoma katika maandiko yafuatayo: 

"Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa BWANA alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri. Akasema, ondoka, umchukue mtoto na mamaye ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya". (Mathayo 2:19-22). 

Kwa maandiko hayo na mengine niliyoyataja hapo awali, kinachodhihirika hapa ni kwamba: 

Kati ya mfalme Herode na Nabii Yohana (a.s.) aliyetangulia kufa ni Nabii Yohana (a.s.). 

Yesu (a.s.) alirejea Israeli baada ya mfalme Herode aliyemwua Yohana kufariki. 

Na ndio kama Biblia inavyoeleza, aliporejea Israeli alikuta mtawala mpya aitwaye Arkelao aliyerithi kiti hicho kwa baba yake Herode. Hivyo hakumkuta Herode wala Yohana. 

Zaidi ya hivyo, Yesu alirejea Israeli akiwa bado yu mtoto mdogo. 

Maandiko ya Biblia yanapingana wazi kama tulivyoona maelezo yale ya Mathayo Mtakatifu 3:13-17 na Marko 1:9-11 na shuhuda nilizoziainisha katika makala yangu hii. 

Ikiwa ukweli ni huo, hapa ninashawishika kuhoji, ni Yohana gani aliyembatiza Yesu akiwa na umri wa miaka thelathini? Na nini lengo la ubatizo huo? 

Ubatizo wa maji uliishia kwa Yohana 

Tumekwishaona sababu tofauti za msingi zinazoonyesha utata juu ya kuwepo kwa tukio la Yohana (a.s.) kumbatiza Yesu (a.s.) katika mto wa Jordani. 

Pamoja na utata huo, ni vyema hapa pia nikaweka bayana jambo lingine muhimu la kuzingatia kwa waumini wote. Ni kwamba kwa mujibu wa maandikio ya Biblia Takatifu, ubatizo wa maji unaotumiwa hadi leo na rafiki zangu Wakristo kwa kweli uliishia kwa Yohana. Aidha ubatizo unaotakiwa utumiwe hivi sasa badala ya huo wa maji ni wa Roho Mtakatifu na moto, kama Nabii Yohana (a.s.) mwenyewe anavyothibitisha hilo katika maandiko yafuatayo: 

"Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto". (Mathayo 3:11). 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Onyesheni ushujaa wa Badri 

Daniel kuwatimua waumini Msikitini 

Waislamu Moshi: Wadai kulishwa nguruwe, vibudu 

Dondoo za Kisakolojia 
Na. Abu Halima Sachangwa 

Kona ya WachaMungu  

Jicho la Uzalendo 

Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) - 2 

Vipi umoja wetu uwe hatari ? 

MASHAMBULIZI YA MAREKANI NCHINI IRAQ  

Marekani si rafiki mwema  

Tunahitaji UN ya Waislamu - 2  

Njia bora zitakazotusaidia kuwalea watoto 
Na Ust. Hashim Rusaganya, Mombasa 

Ijue Madrasatul-Qaadiriya Sokoni I Arusha. 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tutafute kwanza ufalme wa Allah (s.w.) 
Na Mwapwani Mohammed 

Sheikh Kisiwa atunuku zawadi 

Chuo cha Kilimo Ukiriguru kupata Msikiti mpya  
Na Mwandishi Wetu, Mwanza  

Huduma za maji Kondoa haziridhishi 
Na Abu Zuberi, Kondoa  

Mnyororo wa imani 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Je, Yesu alibatizwa? 
Na Muhibu Said  

Kufuatia Waislamu kuritadishwa Merela Morogoro: Masheikh wa mjini watupiwa lawama  

Abiria walaani kumwagiwa pombe Kondoa 

Sheikh Bafadhil ateuliwa kudhamini waandishi wa habari Morogoro 
Na Mussa Ally, Morogoro 

Sayansi na Teknolojia 
[Tatizo la mwaka 2000] 

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Chakula na lishe 
[Mlo wa siku ya Idd] 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita