AN-NUUR 
Na.183 Ramadhan 1419, Januari 8 - 14, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kona ya WachaMungu 

Udugu wa kweli huja pale ... 

NAJARIBU kufikiria hatua ambazo ningechukua kuuimarisha udugu wetu wa imani kama ambavyo Allah(s.w) anavyotuhimiza katika Qur’an. 

Udugu ninaouona hapa si ule ambao wengi wangeudhani. Ni udugu unaokuja baada ya kutekelezwa masharti kadhaa pia kuzingatia miiko yake. 

Kwa mujibu wa mafunzo ya Mtume(s.a.w) Waumini tunajifunza baadhi ya yanayoweza kujenga udugu wa kweli wa kiimani na pia kuyajua yanayotishia udugu huo. 

Mtume (s.a.w.) amesema peaneni salamu mtapendana. Pia amehimiza kutembeleana, kualikana, kuandaliana vyakula. Hili Waislamu wengi wamekuwa wakitekeleza Alhamdulillah! 

Hata hivyo, Salaam na kutembeleana ni makapu yaliyokusanya mambo mengi ndani yao. Uhakika ni kwamba haiyumkini ibakie salaam iliyosisitizwa na Mtume; wakati ameficha chuki, choyo, utesi, masengenyo, majivuno, kashfa, dharau na kero nyingine. Na hakuyumkini kutembeleana kulikohimizwa na Mtume (s.a.w.) ilhali kumeandamana na husda, wivu, ria, kukogana na mengine yaliyojificha katika mitihani ya kupata na kukosa. 

Hayupo katika udugu wa Kiislamu yule ambaye atatoa "salaam alaykum" kwa "nduguye" Muislamu kwa dakika hii kisha dakika nyingine akae na kumzungumza vibaya nduguye huyo, iwe chemba na wale wa karibu zaidi nae au na mke au mumewe nyumbani kwani huu unaangukia kwenye usengenyi na utesi ambayo ni kansa inayoozesha viungo vya mafungamano ya Uislamu. Wengi tunaopanga safu za jamaa Misikitini tulio mstari wa mbele katika makundi na "harakati", tunaugua ugonjwa huu! 

Hayupo katika udugu wa Kiislamu yule ambaye "asalam alaykum" imetawala kinywa chake wakati nduguze katika imani wanaendelea kutaabika kwa hali ngumu kimaisha ilhali anao wasaa ... Si katika salamu iliyohimizwa na Mtume (s.a.w.) ile inayotoka katika kinywa cha asiyeguswa na matatizo ya wengine. 

Tushindane kuyafikia mambo ya kheri yanayoboresha udugu miongoni mwetu yasiyotoa mianya kwa mashetani wanaoweza kujipenyeza kwa sura tofauti kihali na kimali. Na tukumbuke kuwa udugu wa kweli miongoni mwa waumini ni Faradhi: 

"Hakika waumini wote ni ndugu". (49:10) 



Jicho la Uzalendo 

Ukombozi umeegemea kwenye kafara! 

MALALAMIKO na vilio vya wananchi Waislamu wa nchi hii juu ya kero mbalimbali zinazowakabili, vimekuwa vikiambulia patupu mara kadhaa. Hii si kwamba wahusika hawaoni au kusikia, la hasha! Wanasikia na kukiri ukweli wa hayo, lakini jambo moja laelekea kuwa ndio ni kwamba kwa kuwa katiba si zao la muafaka, hukuwepo wewe, mimi wala yule wakati "ikitengenezwa", kwa hiyo, huwezi kumfanya lolote anayekutenda visivyo katika walio juu kinchi. Labda utumie mbavu zako. 

Wakati Katiba ikiwa katika mazingira ya "mizengwe" kiasi hicho, pia kuna wale waliokosa uzalendo unaojali ustawi wa wote! Hawa wamekosa shukrani na uungwana baada ya kutua kivulini. Hawataona haya kufanya yao pasi na kuzingatia uwepo wa wengine. 

Kinadharia hula kiapo kuwa watendaji chini ya Katiba, kiutendaji mara kadhaa hutenda kwa mujibu wa maelekezo yasiyo rasmi ya watakatifu wao. Kibaya zaidi, kwa hawa, huwa watiifu kwa asilimia mia moja! 

Kukaa na kuamua kumsaka Ponda au kuwashitaki walioko mahakamani hivi sasa kuhusu Mwembechai huku ukimwacha , mchochezi Paroko wa Mburahati ni katika hayo tunayodhani ya kutekeleza maagizo yasiyo rasmi. 

Kuahirisha mitihani au matokeo ili kusherehekea vyema Krismasi huku ukiwasahau wanaofunga na kutarajia kusherehekea Idi ni katika hayo ya Katiba kutokuwa na wajibu wowote katika jamii yetu. 

Na haya yanakuja kwa sababu walioko juu hawategemei wala hawatokani na nguvu ya wananchi (kura). Uwachague watakuwepo, usiwachague watakuwepo.  

Mataifa ambayo wananchi wake huwa na kauli, tunayaona yaking’ara kisiasa. Viongozi huheshimu maamuzi ya Wananchi, husikiliza malalamiko na vilio vyao. Hujibu tuhuma dhidi yao na hutatua shida zao. Upendeleo, chuki, mizengwe ya udini, dharau na ubabe havina nafasi. 

Huku kwetu haya ni ndoto kwa baadhi ya wananchi kwa sababu viongozi wana uhakika wa kushinda hata kama nchi nzima hawatapiga kura! 

Katika hali na mazingira haya ya kutotendewa haki kwa baadhi ya wananchi, ufumbuzi utapatikana pale tu hawa wanyonge watakapojiona wanastahiki kupata kila kilicho chao kwa gharama yoyote!  

Mimi sikubaliani na wale wanaohimiza "utangamano" katika mazingira haya. Huo ni unafiki, huko ni kulinda maslahi ya waporaji wachache wa haki za wengi. Naona ukombozi umeegemea zaidi kafara ya damu. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Onyesheni ushujaa wa Badri 

Daniel kuwatimua waumini Msikitini 

Waislamu Moshi: Wadai kulishwa nguruwe, vibudu 

Dondoo za Kisakolojia 
Na. Abu Halima Sachangwa 

Kona ya WachaMungu  

Jicho la Uzalendo 

Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) - 2 

Vipi umoja wetu uwe hatari ? 

MASHAMBULIZI YA MAREKANI NCHINI IRAQ  

Marekani si rafiki mwema  

Tunahitaji UN ya Waislamu - 2  

Njia bora zitakazotusaidia kuwalea watoto 
Na Ust. Hashim Rusaganya, Mombasa 

Ijue Madrasatul-Qaadiriya Sokoni I Arusha. 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tutafute kwanza ufalme wa Allah (s.w.) 
Na Mwapwani Mohammed 

Sheikh Kisiwa atunuku zawadi 

Chuo cha Kilimo Ukiriguru kupata Msikiti mpya  
Na Mwandishi Wetu, Mwanza  

Huduma za maji Kondoa haziridhishi 
Na Abu Zuberi, Kondoa  

Mnyororo wa imani 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Je, Yesu alibatizwa? 
Na Muhibu Said  

Kufuatia Waislamu kuritadishwa Merela Morogoro: Masheikh wa mjini watupiwa lawama  

Abiria walaani kumwagiwa pombe Kondoa 

Sheikh Bafadhil ateuliwa kudhamini waandishi wa habari Morogoro 
Na Mussa Ally, Morogoro 

Sayansi na Teknolojia 
[Tatizo la mwaka 2000] 

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Chakula na lishe 
[Mlo wa siku ya Idd] 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita