AN-NUUR 
Na.183 Ramadhan 1419, Januari 8 - 14, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Sayansi na Teknolojia 

Tatizo la mwaka 2000 

Na Hassan Omar 

Nadhani tayari umeshasikia watu au vyombo vya habari vikizingumzia "Tatizo la Mwaka 2000" (Year 2000 Problem) ambalo pia linajuilikana kama "The Millenium Bug", "Y2K Problem", na majina mengine kadhaa. Hilo ndilo litakalokuwa mada ya makala hii. Itakapofika siku ya Ijumaa, tarehe 31 Desemba 1999, saa 5, dakika 59 na sekunde 59 za usiku, ulimwengu utakuwa tayari kuingia katika karne ya 21, lakini kompyuta nyingi duniani zitadhani ndio kwanza karne ya 20 inataka kuingia. Yaani badala ya kuifanya tarehe ya siku ya kwanza ya mwaka mpya kuwa Jumamosi, 01 Januari 2000, kimakosa zitaifanya kuwa Jumatatu, 01 Januari 1900! 

Kosa hilo litatokeaje? Sababu kuu ni kawaida yetu ya kuandika tarehe. Tuna kawaida tarehe kuiandika kwa kutumia nambari sita tu, kwa mfano tarehe ya leo tunaiandika 08/01/99, tukimaanisha tarehe 8 Januari 1999, badala ya kutumia nambari nane, 08/01/1999. Sehemu ya mwaka tunaiandika kwa kutumia nambari mbili tu tukitaraji kuwa nambari mbili za mwanzo za mwaka "tayari" zinajuilikana kuwa ni ‘19’. 

Tunafanya hivyo hata kwenye fomu na risiti mbali mbali. Watengenezaji wa kompyuta na waandishi wa programu mbali mbali za kompyuta nao walikumbwa na kawaida hiyo ya kutumia herufi mbili tu za kutambulisha mwaka, kiasi kwamba mwaka 2000 utakapofika, mwaka huo ndani ya kompyuta itauandika ‘00’. 

Kwa vile herufi mbili za mwanzo za mwaka zinachukuliwa kuwa ni ‘19’ basi mwaka mpya, ndani ya baadhi ya kompyuta utachukuliwa kama kwamba ni mwaka 1900! 

Sasa ilikuwaje hata watengenezaji wa kompyuta na waandishi wa programu mbali mbali za kompyuta, kama kweli ni watu wenye akili, wakakumbwa na mughafala huo? Kuna sababu mbili kuu. Ya kwanza ni kwa minajili ya kupunguza ukubwa wa data za kuhifadhiwa - tarehe yenye nambari sita inahitaji nafasi ya hifadhi (storage memory) ndogo zaidi kwa asilimia 25 ukilinganisha na tarehe yenye nambari nane. 

Enzi hizo za miaka ya 60 na 70 matumizi ya kompyuta yalipoanza kushamiri hifadhi ya kompyuta (computer memory) ilikuwa ghali sana na kwa hivyo lilikuwa jambo la maana sana kufanya kila njia kupunguza ukubwa wa data za kuhifadhiwa. Sababu ya pili ni kuwa, waandishi wa programu mbali mbali katika miaka hiyo ya 60, 70 na hata 80, hawakudhani kuwa programu zao walizoziandika zitadumu na kuendelea kutumika bila ya kurekebishwa mpaka kufikia mwaka 2000. Kwa hivyo hawakuona hasara ya kutumia tarehe ya nambari sita. 

Lakini hasara imethibitika kuwa kubwa sana! Kwa bahati mbaya programu nyingi za zamani hasa zile kubwa na zinazotumiwa na makampuni makubwa makubwa kama vile mabenki, na makampuni ya kutoa huduma kama simu, umeme, maji, n.k., zimedumu kwa muda mrefu mpaka hivi leo. Zimekuwa zikifanyiwa marekebisho mengine tu lakini suala la tarehe limebakizwa hivyo hivyo. 

Sasa chukulia kwa mfano mtu mmoja ameweka pesa benki Sh. 10,000 kwenye "fixed deposit" 03 Januari 1999 kwa makubaliano ya riba (interest) ya asilimia 10, (simple interest). Akienda benki Jumatatu, 03 Januari 2000 na kuomba apewe fedha zake, kompyuta inaweza kutoa jibu kwamba kwa kweli riba yake ni (Mtaji x Riba% x Idadi ya miaka)/100 = (Mtaji x riba% x (tarehe ya leo - tarehe ya kuweka mtaji))/100 = (10,000 x 10 x (03/01/1900 - 03/01/1999))/100 = Sh. -99,000 (angalia alama ya kutoa hapo) na hivyo ataelezwa kuwa kwa kweli atatakiwa ailipe benki jumla ya (Mtaji + Riba) = (10,000 + (-99,000)) = Sh. 89,000! 

Akiambiwa hivyo bila shaka atashangaa na atakuja juu, lakini hiyo ni hasara ya "The Millenium Bug" au "Year 2000 Problem" au kwa Kiswahili, "Tatizo la Mwaka 2000"! 

Mifano ya namna hiyo ipo mingi. Kwa mfano ukipiga simu ya mbali siku ya mkesha wa mwaka mpya na mwaka mpya ukaanza bado uko kwenye simu, si hasha ukaambiwa kuwa hukupiga simu kabisa, au pengine ukahesabika kuwa umepiga simu kwa urefu wa miaka 99 na bili itakayokujia mbwa hairuki! Kuna matajuri (safes) ya benki na ofisi mbali mbali hujifungua yenyewe kila siku ya kazi na kutokana na tatizo hilo la mwaka 2000, kuna matajuri yatakayojifungua yenyewe yakidhani kuwa hiyo ni siku ya kazi ya Jumatatu, 01 Januari 1900! Wafagizi wanaosafisha mwisho wa wiki 

naona siku hiyo watafaidi! 

Kutokezea makosa ya namna kama hizo ni moja kati ya athari za Tatizo la Mwaka 2000 lakini kuna kompyuta kadhaa zitakazogoma kabisa kufanyakazi! Mbali ya programu, kuna kompyuta za kale ambazo tarehe ya nambari sita imejengewa hasa kwenye kompyuta yenyewe yaani kwenye kitu kinachoitwa BIOS. Hizo hapana shaka zitaleta purukushani. 

Ni nani hasa kwa uhakika ataathirika na Tatizo la Mwaka 2000? Wa kwanza ni hao wenye mabenki na vyombo vyengine vya fedha kama Bima, Malipo ya Uzeeni (Pension Fund), n.k; wanaotoa huduma za umeme (akina TANESCO hao), wanaotoa huduma za simu (akina TTCL, Mobitel, Tritel), maji (NUWA), na yeyote yule ambaye anatumia programu za zamani zinazotumia tarehe ya nambari sita. 

Njia nzuri ya kutambua kama utaathirika na Tatizo la Mwaka 2000 ni kuangalia kama programu yako unayoitumia inayo sehemu ya kuingizia tarehelakini sehemu hiyo inahitaji nambari mbili tu za mwaka. Ukiwa na programu ya namna hiyo unaweza kuathirika na Tatizo la Mwaka 2000. Programu hiyo inaweza kuwa ni programu kamili au hata "macro" tu kwenye "spreadsheet" kama vile Excel, Lotus 123, Quattro, n.k. 

Kompyuta za kupigia hesabu za mishahara, na nyenginezo hasa zenye programu zilizoandikwa kwa kutumia lugha ya kompyuta ya COBOL ni kati ya programu zitakazoathirika na Tatizo la Mwaka 2000. Hata mashine za mauzo (cash registers) za zamani zinaweza kukumbwa na tatizo hilo. Na kama mtu ana data ambazo amezitengeneza kwa kutumia tarehe za nambari sita nazo data hizo zitakuwa na muhkeli hasa kwenye programu za kwenye "spreadsheet" na "database". 

Sasa mtu afanyeje kujinusuru na athari za Tatizo la Mwaka 2000? Kuna njia mbili. Kwa wale wenye mabenki na makampuni makubwa, inaonekana ni jambo la busara kukodi wataalamu na kuzirekebisha programu zao kuweza kuwa "Year 2000 compliant", yaani zenye kuepukana na Tatizo la Mwaka 2000. Kazi hiyo si rahisi na ni ghali mno na inahitaji muda ambao haupo wa kutosha. 

Njia ya pili ni kununua kompyuta na programu za kisasa ambazo tayari zimetengenezwa kukabiliana na Tatizo la Mwaka 2000. Na hilo pia si rahisi na kila ikikaribia mwaka 2000 utatuzi utakuwa ghali zaidi. Hivi sasa inakisiwa kuwa gharama za kukabiliana na Tatizo la Mwaka 2000 duniani kote zitafikia jumla ya dola za Kimarekani bilioni elfu moja (trilioni moja)! Hivi sasa wataalamu wa kutatua tatizo hilo wanalipwa $500 kwa siku na ikikaribia mwaka 2000 watataka kulipwa zaidi ya $2,000 kwa siku! 

Mambo mengine muhimu ya kuyajua ni pamoja na ukweli kwamba hivi sasa makampuni hayana budi kujitayarisha na kesi za madai zitakazoambatana na upotefu wa mali kuhusiana na Tatizo la Mwaka 2000. Baadhi ya Mashirika ya bima yameshaanza kusema kuwa yatakataa kulipia upotefu wowote utakaosababishwa na Tatizo la Mwaka 2000. 

Hii ni kuwalazimisha wateja wao wajitayarishe vyema. Wakaguzi (auditors) wa makampuni mbali mbali hivi sasa wameanza kusisitiza na kuhakikisha kuwa kuna jitihada zinazofanywa kukabiliana na tatizo hilo. Shirika la ndege la KLM tayari limeshatangaza kuwa siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 2000, baadhi ya safari za ndege zake zitasimamishwa kwa kuhofu matatizo hasa yatakayotokana na mitambo ya ardhini ya kuongozea ndege. 

Je Tanzania tumejitayarisha vya kutosha kukabiliana na Tatizo la Mwaka 2000? Nchi nyingi zilizoendelea zimeunda tume maalum kukabiliana na tatizo hilo na kutoa ushauri kwa serikali na vyombo vyake na hata mashirika ya watu binafsi na kusimamia mpango mzima wa kuhakikisha kuwa nchi hizo haziathiriwi na Tatizo la Mwaka 2000. Wakati tukiwa ndio kwanza tumeanzisha DSE (Dar es Salaam Stock Exchange) hatuna budi kuwa macho na suala hili la sivyo litakuja kutukuta tumelala usingizi na matokeo yake yatakuwa mabaya sana. 

Wanaotaka taarifa zaidi za "Tatizo la Mwaka 2000" waangalie kurasa za Web zifuatazo: 

http://www.year2000.com 
http://www.y2knews.com 
http://www.microsoft.com.technet/topics/year2k 
http://www.s390.ibm.com:80/stories/tran2000.html 
http://www.itaa.org/year2000.htm 

Unaweza kupata baadhi ya programu za kucheki kama kompyuta yako ni Y2K-compliant (yaani haitakumbwa na Tatizo la Mwaka 2000) kutoka kwenye website ifuatayo: http://www.vendor2000.com/ 

Utapata taaifa nyingi kwa kufanya web-search kutafuta maneno yafuatayo: "Year 2000", "Y2K", "Millenium Bug". 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Onyesheni ushujaa wa Badri 

Daniel kuwatimua waumini Msikitini 

Waislamu Moshi: Wadai kulishwa nguruwe, vibudu 

Dondoo za Kisakolojia 
Na. Abu Halima Sachangwa 

Kona ya WachaMungu  

Jicho la Uzalendo 

Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) - 2 

Vipi umoja wetu uwe hatari ? 

MASHAMBULIZI YA MAREKANI NCHINI IRAQ  

Marekani si rafiki mwema  

Tunahitaji UN ya Waislamu - 2  

Njia bora zitakazotusaidia kuwalea watoto 
Na Ust. Hashim Rusaganya, Mombasa 

Ijue Madrasatul-Qaadiriya Sokoni I Arusha. 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tutafute kwanza ufalme wa Allah (s.w.) 
Na Mwapwani Mohammed 

Sheikh Kisiwa atunuku zawadi 

Chuo cha Kilimo Ukiriguru kupata Msikiti mpya  
Na Mwandishi Wetu, Mwanza  

Huduma za maji Kondoa haziridhishi 
Na Abu Zuberi, Kondoa  

Mnyororo wa imani 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Je, Yesu alibatizwa? 
Na Muhibu Said  

Kufuatia Waislamu kuritadishwa Merela Morogoro: Masheikh wa mjini watupiwa lawama  

Abiria walaani kumwagiwa pombe Kondoa 

Sheikh Bafadhil ateuliwa kudhamini waandishi wa habari Morogoro 
Na Mussa Ally, Morogoro 

Sayansi na Teknolojia 
[Tatizo la mwaka 2000] 

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Chakula na lishe 
[Mlo wa siku ya Idd] 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita