|
|
|
BIASHARA ya utalii , kwa kiwango fulani imechangia mmomonyoko wa maadili mema kwa baadhi ya vijana huko Zanzibar. Hivi sasa limeibuka wimbi la vijana wanaoitwa papasi, wanaong’ang’ania kutembeza watalii kwa tamaa ya kupewa "kitu kidogo". Lakini Ustadh Faridi, wakati vijana wengiwe wanawafuata watalii kwa ajili ya kuwaomba omba, yeye amekuwa akiwaandama ili awape Da’awa juu ya Uislamu. Mwandishi Maalim Bassaleh anaelezea zaidi. Papasi wengi ni vijana wasio na mwelekeo katika maisha. Wanaishi maisha ya kihuni na yasiyokuwa na uhakika. Ni maisha ya kubahatisha bahatisha tu. Watalii wanapokuwa wengi, papasi huwa na uhakika wa kupata kula yao; lakini wanapokuwa wachache, huanza kuwagombania kila mmoja akitaka aajiriwe yeye. Baadhi ya watalii hao ni watu waliokosa maadili mema. Hujishughulisha na vitendo vya ufuska na hata madawa ya kulevya. Papasi wengine, kwa tamaa ya kujipatia pesa, hushawishika kushiriki katika vitendo hivyo viovu. Vijana wengi wamekwishaharibika. Na kama hatua za makusudi hazitachukuliwa kudhibiti hali hiyo, vijana wengi zaidi wataharibika. Watu wengi wamekuwa wakiilalamikia hali hiyo, lakini wameshindwa la kufanya. Naona kana kwamba Ustadh Farid amekuja na jibu. Yeye ameamua kuwapa Da’awa watalii wanaoingia visiwani, pamoja na kujaribu kuwakusanya vijana wa Kizanzibari kuwafunza maadili mema. Ninahisi kwa kiwango fulani amefanikiwa. Kazi anayoifanya ni ngumu na yenye usumbufu. Inahitaji moyo wa kujitolea na uvumilivu wa hali ya juu sana. Inaonekana Ustadh Farid anazo sifa zote hizo. Huenda ikawa amerithi sifa hizi toka kwa babake mzazi, marehemu Maalim Himidi. Babake alikuwa ni mwalimu wa Qur’an na Fiqh ya Kiislamu Msikiti Baraza, Zanzibar. Ni mwalimu maarufu sana na watu wengi wa Unguja walisomeshwa na yeye. Basi kama watu walizoea kurithi mali kutoka kwa wazazi wao, naona Ustadh Farid amerithi juhudi za babake za kufunza wengine maadili ya Kiislamu. Ustadh Farid huwafuata watalii akawagaia vijarida na vijitabu vinavyoeleza juu ya Uislamu. Vijarida hivyo huwa vina maudhui tofauti, kama "Nini Uislamu", "Utume katika Uislamu", "Haki za binadamu katika Uislamu", "Yesu katika Uislamu", na vingi vinginevyo. Yeye huvipata vijarida hivyo kutoka katika tawi la Africa Muslim Agency lililopo Mwanakwerekwe, Zanzibar. Wakishavisoma kama wanakuwa na maswali Ustadh Farid huyajibu. Uzoefu umemwonyesha kuwa watalii wengi huvutiwa na mada zinazohusu Haki za Binadamu katika Uislamu, hasa kuhusu haki za mwanamke na nafasi yake katika jamii. Aidha, hupenda kujua mchango wa Uislamu katika elimu, ustaarabu na maendeleo ya ulimwengu. Amekuwa akiifanya kazi hii ya Da’awa kwa kipindi cha miaka miwili sasa. Alianza mwaka 1997, baada tu ya kurudi kutoka Arabuni alipokuwa akiishi. Amekwisha silimisha jumla ya watalii 18, kwa nyakati tofauti. Katika mwaka 1997 alisimilisha watalii 6 na mwaka 1998 walisilimu watalii 12 kupitia mikononi mwake. Miongoni mwao walikuwamo Waingereza, Wacanada, Waustria na baadhi ya Wazungu wengine. Ama Mataliana, ameniambia ni wagumu sana, hawana hamu ya kujifunza chochote juu ya Uislamu. Mmoja kati ya wale aliowasilimisha mwaka jana, hivi karibuni amekuja kutembea Zanzibar pamoja na mamake. Hivi sasa yuko Unguja na anafunga Ramadhani kama Waislamu wengine. Yeye ni kijana wa Kibelgiji, alikuwa akiitwa Ben na sasa anaitwa Karimu. Huenda akaisherehekea Idd - el- Fitr hapo hapo Zanzibar. Ustadh Farid amejijengea umaarufu mkubwa kwa watalii. Anajulikana mpaka Ulaya. Mwaka jana walifika Zanzibar watalii kutoka Norway, wakawa wanaliulizia jina la Ustadh Farid. Wamesema wamepata habari zake huko huko Ulaya, kutoka kwa wenzao waliowahi kutembelea Zanzibar. Walitaka awaeleweshe zaidi mambo mbalimbali juu ya Uislamu na pia walivihitajia vile vijarida anavyovigawa. Ustadh Farid kwa moyo mkunjufu aliwatimiza haja zao. Mbali na kuwapa Da’awa watalii, Ustadh Farid pia hujishughulisha na kuwapatia vijana mafunzo juu ya maadili mema ya Kiislamu. Kipindi cha jioni huwakusanya vijana kwenye Msikiti Maamur, uliopo eneo la Hurumzi kwa ajili ya kuwadarisisha. Kuna kijana mwingine anayeitwa Ustadh Salim ambaye ndiye anayesimamia mafunzo ya vijana hao. Mimi mwenyewe niliwahi kuombwa kutoa waadhi katika Msikiti huo. Jambo lililonitia moyo ni kuona takriban wasikilizaji wote walikuwa ni vijana. Jumla yao ilikuwa haipungui aroboini. Watu wazima waliokuwepo hawakuzidi watano. Lakini wote ni vijana baina ya miaka 18 na 30. Kati ya vijana hao kuna wengine waliokuwa wakijishughulisha na vitendo vya kihuni pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya, Alhamdu Lilah, Mwenyezi Mungu amewaongoa, wameacha. Katika jitihada za kuwaunganisha vijana hao wawe na maingiliano na umoja baina yao, Ustadh Farid amewaundia timu ya mpira wa miguu. Siku za Jumapili hutembelea sehemu za mashamba kwenda kucheza mechi na timu za huko. Lakini timu hiyo haina jezi wala vifaa vya michezo. Nilipomwuliza kama anapata msaada kutoka popote pale, alinijibu kuwa hawapati msaada wowote. Nilimshauri Ustadh Farid aanzishe maktaba itakayokuwa na vitabu mbalimbali vya Kiislamu. Itasaidia sana katika kazi yake ya Da’awa. Kwanza vijana watapata sehemu ya kuweza kujiongezea maarifa na pili wale watalii watakaotaka kujua zaidi juu ya Uislamu watapata fursa ya kujisomea wenyewe. Aidha, maktaba kama hiyo inaweza kutumiwa kuandaa semina na warsha. Kimsingi amekubaliana na rai yangu. Amenifahamisha kuwa idara ya Wakfu Zanzibar iko tayari kumpa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Maktaba, lakini tatizo hana nyenzo za ujenzi. Kwa hivyo lengo la kuandika makala haya ni kuielezea jamii ya Kiislamu juu ya harakati za Da’awa zinazofanywa na Ustadh Farid; pamoja na kuwaomba Waislamu na taasisi za Kiislamu kusaidia katika kufanikisha ujenzi wa maktaba hiyo. |
YALIYOMO
Tahariri Baada ya futari nzuri: Tuwatupie macho wenye njaa Rais Mkapa kuwa mgeni rasmi Baraza la Idd Waumini, Masheikh Arusha wasutana kwa futari ya Mrema Dondoo za saikolojia
MSADAT yazidi kutia moyo Tanga MAFUNZO KUHUSU FUNGA YA RAMADHANI Michezo isiyoruhusiwa katika Uislamu Ustadh Farid: Kijana aliyejitolea kuwapa Da'awa watalii Hakuna Magharibi wala Mashariki:
Uislamu ni ubinaadamu
Ijue madrasati Mar-wa ya Dodoma
mjini
Ijue Madrasat Jadidul Fiqhyyat
- Tabata Kimanga
Madrasat Hidayatul Muumini Mwadui Washindi wa mashindano ya Hadithi za Mtume (s.a.w.) wapatikana Madrasa Shafii Ujiji Kigoma yaonyesha umahiri wake Waanzisha mifuko kusaidia wagonjwa Dodoma Waislamu Kondoa waomba msaada kumalizia Msikiti Mnyororo wa imani-2
Kutoka magazeti ya zamani:
Jengo la Waislamu Moshi lageuzwa
Kanisa la Walokole
Masjid Nurania yaswaliwa
Ijumaa
Jabal Hira kutoa mafunzo
ya Kompyuta Morogoro
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|