AN-NUUR 
Na.184 Ramadhan 1419, Januari 15 - 21, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Internet ni nini?
 

Na Hassan Omar 

Neno ‘Internet’ (linaloanza na herufi kubwa ‘I’) ni jina linalowakilisha utando (network) wa mamia ya maelfu ya kompyuta zilizounganishwa pamoja duniani kote. Kompyuta hizo zimeunganishwa kwa kutumia njia za mwasiliano ya kasi kubwa sana ili kuwezesha watumiaji kompyuta hizo wapelekeane barua-umeme (‘electronic mail’ au kwa ufupi ‘e-mail’) na pia kuweza kupata taarifa mbali mbali kwa njia za haraka sana. 

"Internet’ (kwa ufupi ‘Net’) imekuwa maarufu sana duniani kote sasa hivi kutokana na huduma kadhaa ambazo zinaweza kupatikana kupitia njia hiyo. Watu wengi wanaitumia ‘Internet’ kupelekea na kupokelea barua-umeme (‘e-mail’). Barua-umeme ni njia moja maarufu na ya haraka sana ya kumtumia ujumbe (barua) mtu aliye mbali. Kinachohitajika ni kwa mtumaji kujua anuani ya barua-umeme ya mtu anayetaka kumpelekea barua hiyo. 

Ni kama vile unapotaka kutuma fax ni lazima uijue nambari ya fax ya mtu unayependa aipokee hiyo fax, au unapotuma barua ya posta (siku hizi barua ya posta imebatizwa jina ‘snail-mail’, yaani ‘barua-konokono’ kwa vile inachukua muda mrefu kufika) ni lazima uijue anuani ya posta ya unayetaka kumpelekea barua - na kwa barua-umeme ni hivyo hivyo. 

Kwa mfano, anuani yangu ya barua-umeme ni: hassan@glcom.com ikionesha kuwa kisanduku changu (akaunti) cha barua-umeme kina jina ‘hassan’ na kipo kwenye kompyuta yenye jina ‘glcom.com’. Kila kompyuta iliyoungwa au yenye uwezo wa kuunganishwa na ‘Internet’ ina jina maalum mfano wa hilo ‘glcom.com’. Kompyuta zote zilizoko kwenye Internet zinafahamu jinsi ya kufikisha barua-umeme kuja kwenye kompyuta yenye kisanduku changu cha barua-umeme. (ANGALIA: Anuani ya barua-umeme inaweza kuandikwa kwa herufi kubwa au ndogo au kwa mchanganyiko, na zote hizo ni sawa. Kwa mfano, ni sahihi kuiandika anuani yangu kama: Hassan@GLCOM.com). 

Mtu yeyote yule ambaye anatumia kompyuta iliyounganishwa na ‘Internet’ anaweza kunitumia barua-umeme na ikanifikia baada ya sekunde au dakika chache tu. Kutegemeana na wapi ujumbe wa barua-umeme ulipotokea, na njia iliyotumiwa mpaka kuufikisha ujumbe huo kwenye kisanduku changu cha barua-umeme, inaweza kuchukua zaidi ya dakika chache. 

Ili kuweza kutuma barua-umeme, unahitaji kuwa na kompyuta ambayo ina uwezo na programu ya kukuwezesha kuitayarisha barua-umeme na kuituma kwa unayemtaka. Kompyuta na programu za aina mbali mbali zinatumika kupelekea barua-umeme. Kompyuta (PC) yako ya kawaida inatosha kabisa kuweza kuitumia kupelekea barua-umeme. Unachokihitaji ni kampuni (Internet Service Provider au kwa kifupi ISP) itakayokupatia kisanduku cha barua-umeme na programu kama vile Eudora, Microsoft Outlook, Netscape Mail, Pegasus Mail, n.k., za kukuwezesha kuandikia na kusomea hizo barua-umeme. 

Pamoja na PC utahitaji kitu kinachoitwa ‘modem’ ambacho tumekizungumza kwenye makala zetu zilizopita. ‘Modem’ itakuwezesha kuiunganisha PC yako na kompyuta ya kampuni inayokupatia huduma za ‘Internet’ kwa kupitia njia ya simu moja kwa moja ukiwa nyumbani au ofisini kwako. Kwa hivyo, ili kuweza kuunganisha kompyuta yako na Internet, ni lazima uwe na line ya simu. 

Kikawaida njia ya barua-umeme hutumiwa kupelekea ujumbe wenye matini (text) tupu. Yaani ujumbe wenye herufi za kawaida tu bila ya madoido mengine kama herufi nzito (bold), za mlalo (italic), zilizopigiwa mistari, n.k. Lakini unaweza pia kumpelekea mtu makala ulioiandika, kwa mfano, kwa kutumia MS-Word au Excel, WordPerfect, au hata jalada lenye picha kama lilivyo. 

Kutuma barua-umeme ni rahisi sana (kwa bei) ukilinganisha na njia nyingine, kwa mfano fax. Kwa mfano, wanaotoa huduma za Internet Tanzania wengi wao wanalipisha $50 kwa mwezi kwa idadi yoyote ile ya barua-umeme utakazozipeleka na kuzipokea. Lakini fedha hizo zitakuwezesha kutuma fax chache tu nje ya Tanzania. 

Hata hivyo, barua-umeme haziondoi kabisa kabisa haja ya kutumia fax hasa unapotaka kumpelekea mtu wa mbali maandishi yenye picha ndani yake. Na zaidi ni kuwa si watu wote wana anuani za barua-umeme wakati matumizi ya fax ni maarufu na watu wengi wanaweza kuwa na mahali wanapoweza kupokelea fax kwa namna fulani. 

Lakini pamoja na hayo, ni rahisi zaidi kutuma fax moja kwa moja kutoka kwenye kompyuta kwa kutumia njia ya barua-umeme inayogeuzwa kuwa fax. Kwa njia hii mtu anatuma barua-umeme kama kawaida na barua yake inatumwa kama fax kwa mtu ambaye hana kisanduku cha barua-umeme lakini anayo nambari ya fax. Ukimuuliza ISP wako bila shaka atakujuilisha jinsi ya kutuma fax hata nchi za nje kwa kutumia njia ya barua-umeme (yaani e-mail). 

Siku hizi pia kuna namna ya kumtumia mtu ujumbe kwa njia ya barua-umeme, na ukamfikia kwenye simu yake ya mkononi (cellular phone). Au pia unaweza mtu kumtumia ujumbe kwa njia ya barua-umeme ukamfikia kwenye pager yake. 

Kitu kimoja kizuri sana kinachopatikana kutokana na huduma ya barua-umeme ni kuwapa watu uwezo wa kushiriki kwenye kumbi mbali mbali za majadiliano (mailing-lists) ambazo ndani yake kunafanywa majadiliano ya mambo mbali mbali wanayoyapendelea. Kwa mfano, wafanyakazi wa hospitali wanaweza kujiunga na ukumbi wa kujadili mambo ya afya na walimu nao wakajiunga na ukumbi wa kujadili mambo yao ya elimu nchini na hata kimataifa. 

Kuna ukumbi wa majadiliano unaoitwa TANZANET ambao una wajumbe zaidi ya 300, wengi wao wakiwa Watanzania walio nje ya nchi. Ukumbi huo ni kwa madhumuni ya kujadili mambo mbali mbali yanayohusu Tanzania na watu wake. Ikiwa tayari una anuani ya e-mail, unaweza kuomba kujiunga na ukumbi huo kwa kupeleka ujumbe kwenda kwenye anuani: LISTSERV@SMTP.PARRETT.NET na ndani ya ujumbe wako uandike maneno yafuatayo: SUBSCRIBE TANZANET 

Pia kuna ukumbi wa majadiliano unaoitwa ZANZINET ambao unakusanya Wazanzibari wasiopungua 200 wanaojadili mambo yanayohusu Zanzibar na watu wake. Wazanzibari wanaweza kujiunga na ukumbi huo kwa kupeleka ujumbe kwenda kwenye anuani: ZANZINET@ZANZINET.ORG na ndani ya ujumbe waandike maneno yafuatayo: JOIN ZANZINET 

Huduma nyengine ya ‘Internet’ ambayo ni maarufu sana ni huduma inayoitwa ‘World-Wide Web’, au ‘WWW’ au kwa kifupi ‘Web’. Huduma hii imekuwa maarufu sana kiasi cha watu kufikiria kuwa ‘Internet’ ni sawa na ‘Web’. Na ndio maana unawasikia watu wakisema wanataka kuingia kwenye ‘Net’ huku wakimaanisha kuwa wanataka kutumia huduma ya ‘Web’. 

WWW inamruhusu mtumiaji kuangalia mambo yalioko kwenye kompyuta mbali mbali zilizoko kwenye Internet. Mambo hayo, huwa yamewekwa kwenye mafaili maalum na kwa mtindo maalum ili kwa makusudi kuruhusu watu wengine waweze kuyaona. Watumiaji wengi wa ‘Internet’ wameyatayarisha mafaili yao kwenye kompyuta zao na kufanya kitu kinachojuilikana kama "kurasa" za WWW au ‘WWW pages’. Kila ‘ukurasa’ wa WWW una anuani yake inayojuilikana kwa Kiingereza "Uniform Resource Locator" au kwa kifupi "URL". Kwa mfano, URL ya "ukurasa" wangu wa Web ni kama ifuatavyo: http://www.glcom.com/hassan 

Hebu jaribu kuingia kwenye ukurasa huo uone picha yangu na maelezo mengine kadhaa. Wengine kurasa za Web huziita "home pages" au hata "web sites". 

Kurasa za WWW za watu mbali mbali zina mambo mbali mbali kuhusiana na kila kitu unachoweza kukifikiria. Kurasa hizi zinakuwa na maandishi, picha na hata sauti ili kuwezesha kufikisha kikamilifu taarifa zinazokusudiwa. Takriban kurasa zote hizo zinaweza kusomwa na mtu yeyote yule mradi awe na programu inayoweza kusoma kurasa za WWW. 

Programu za namna hiyo huitwa ‘Web browsers’. ‘Browser’ maarufu ni ile yenye jina Netscape. Nyingine ni ‘Internet Explorer’ ya kampuni ya Microsoft. 

WWW ina utajiri mkubwa sana wa taarifa na hasa kuhusiana na mambo ya kujielimisha na kujifurahisha. Wanaotoa huduma za ‘Internet’ Tanzania pia wanaweza kukuwezesha kupata huduma ya WWW. Kuna hata huduma za namna hiyo ambazo unalipa kama Sh. 2000 kwa saa moja kuweza (kama wengi wanavyokuita) ‘ku-surf’ kwenye ‘Net’. 

Insha-Allah tutaendelea kuziangalia huduma nyingine zinazopatikana kwenye ‘Internet’ kwenye makala ijayo. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Baada ya futari nzuri: Tuwatupie macho wenye njaa 

Rais Mkapa kuwa mgeni rasmi Baraza la Idd 

Ubungo yakumbwa na ukame 

Waumini, Masheikh Arusha wasutana kwa futari ya Mrema 

Dondoo za saikolojia 
Na. Abu Halima Sa Changwa 

Waislamu turejee kwa Allah 

MSADAT yazidi kutia moyo Tanga 

Mjue Usama bin Ladin 

MAFUNZO KUHUSU FUNGA YA RAMADHANI 

Michezo isiyoruhusiwa katika Uislamu 

Ustadh Farid: Kijana aliyejitolea kuwapa Da'awa watalii 

Hakuna Magharibi wala Mashariki: Uislamu ni ubinaadamu 
Na Abubakari S. Marwillo 

Ijue madrasati Mar-wa ya Dodoma mjini 
Na Abu Zuberi, Dodoma 

Ijue Madrasat Jadidul Fiqhyyat - Tabata Kimanga 
Na B. Mwakangwale 

Madrasat Hidayatul Muumini Mwadui 

Washindi wa mashindano ya Hadithi za Mtume (s.a.w.) wapatikana 

Madrasa Shafii Ujiji Kigoma yaonyesha umahiri wake 

Waanzisha mifuko kusaidia wagonjwa Dodoma 

Waislamu Kondoa waomba msaada kumalizia Msikiti 

Mnyororo wa imani-2 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Kutoka magazeti ya zamani: 
Wanaoshitakiwa kwa uhaini kortini leo 

Jengo la Waislamu Moshi lageuzwa Kanisa la Walokole 
Na Mwandishi Wetu, Moshi 

Masjid Nurania yaswaliwa Ijumaa 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Jabal Hira kutoa mafunzo ya Kompyuta Morogoro 
Rajab Rajab na Mussa Ally, Morogoro 

Sayansi na Teknolojia 
[Internet ni nini?] 

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Thamani ya mlo wa Uyoga] 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita