AN-NUUR 
Na.185 Shawwal 1419, Januari 29 - Februari 4 , 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
PELEKA FAX NCHI ZA NG’AMBO BURE! – (2)
 
Hassan Omar
 

Wiki iliyopita tulizungumza kwa urefu utaratibu wa kufuata ili kuweza kutuma fax (ufupisho wa neno fascimile) kwenda nchi za ng’ambo bila malipo yoyote. Utaratibu tuliouzungumza, hata hivyo, ni wa kuweza kutuma fax yenye matini (text) tu kwa kutumia huduma za bure za email-to-fax zinazotolewa na TPC.INT. Kama tulivyoahidi, kwenye makala ya leo, tutazungumzia utaratibu wa kufuatwa kuweza kutuma fax yenye matini (text) pamoja na picha (image) kupitia huduma hiyo ya TPC.INT. 

Huduma ya TPC.INT kwa ujumla inakuruhusu kutuma e-mail kwenye mitambo yake na kuweza kuipeleka e-mail hiyo kwa njia ya fax kwenye nambari ya fax uliyoiainisha. E-mail unayoituma inaweza kuwa ama yenye matini tu, au ikawa na matini na kufunganishwa na jalada (file) la kompyuta lenye picha iliyo kwenye mfumo (image file format) wa TIFF (Tagged Image File Format) au mfumo wa Postscript 

Mfumo wa TIFF ndio maarufu zaidi unaotumiwa na mashine za fax za Group III. Ukiingiza ukurasa wenye maandishi kwenye mashine ya fax ukurasa huo unachukuliwa picha yake na kugeuzwa kuwa msururu wa binary data yaani bits "1" na "0". Kwa lugha nyengine, ukurasa huo unakuwa digitized. Baada ya hapo, inatumika mbinu maalum kupunguza ukubwa wa data za picha iliyochukuliwa – matokeo yake ni kupatikana faili lenye data za mfumo wa TIFF. Data hizo ndizo zinazopelekwa kwenye mashine nyengine ya fax kwa kutumia utaratibu maalum kama unavyoelezwa kwenye protokali (protocol) ya Group III inayotumiwa na takriban mashine zote za fax zinazotumika hivi sasa. 

Mfumo wa picha wa Postscript sio mfumo halisi unaotumia na mashine za fax, lakini mfumo huo unapendwa sana kwa sababu unatambulikana na programu na mashine nyingi. Kwa mfano, printa nyingi zinaelewa jinsi ya kuichapa picha iliyo kwenye mfumo wa Postscript. Na uzuri zaidi, si kazi kubwa kuigeuza picha iliyo kwenye mfumo wa Posctscript kuwa kwenye mfumo mwengine wowote ukiwemo wa TIFF. 

Ili kuweza kutuma e-mail iliyofunganishwa faili lenye picha, huna budi kuwa na programu ya kupelekea e-mail ambayo ina sifa ya kuwa MIME-aware. MIME (Multipurpose Internet Mail Extensions) ni mfumo maalum (standard) wa kuweza kutuma faili lolote la kompyuta kwa njia ya e-mail na kuweza kupokelewa na kueleweka ipasavyo likifika linakotakiwa.  

Ujumbe wa e-mail unaposafirishwa, unatakiwa uwe na text tu, yaani herufi za kawaida kama unavyoziona kwenye keyboard ambazo zinajuilikana kama ASCII characters. (ASCII ni ufupisho wa American Standard Code for Information Interchange). Lakini, faili lenye picha (kwa mfano) ni binary file lenye mambo zaidi ya herufi za kawaida unazoziona kwenye keyboard, kwa hivyo haziwezi kama zilivyo kusafirishwa kwa njia ya e-mail. Inabidi kwanza zibadilishwe kuwa text kwa mtindo fulani maalum – yaani inabidi ziwe encoded. Zikifika zinakotakiwa inabidi zirudishwe kama zilivyokuwa kabla – yaani inabidi ziwe decoded. MIME ni utaratibu maalum wa kusaidia ku-encode na ku-decode e-mail kuweza kwa urahisi kabisa kusafirishika bila matatizo yoyote. Programu ya kutuma/kupokea e-mail yenye uwezo wa kutumia utaratibu wa MIME ndio inasemwa kuwa yenyewe ni MIME-aware. 

Program maarufu na inayotumiwa na wengi ni Eudora. Hiyo kwa bahati nzuri ni MIME-aware. Pegasus Mail, Netscape Mail, Microsoft Outlook, na nyingi nyenginezo, zote ni MIME-aware. Lakini kwa bahati mbaya, mara nyengine programu hizo huwa hazikujuilishwa namna ya kutuma faili la picha ya TIFF au Postscript, kwa hivyo inabidi uzisaidie kidogo. Hapa chini tutaelezea jinsi ya kuifanya Eudora iweze kutuma e-mail iliyofunganishwa na faili la TIFF au Postscript kwa ajili ya kupelekwa kwenye mitambo ya TPC.INT. 

Kama huna Eudora, unaweza kuipata Eudora Lite, ambayo ni bure, kutoka kwenye anuani ya web ifuatayo: 

http://www.euodora.com/ 

Baada ya kuiweka Eudora kwenye kompyuta yako, tumia Notepad, fungua fiaili lenye jina Eudora.ini na ongeza maneno yafuatayo (kama hayapo tayari) kwenye sehemu ya Mappings. 

[Mappings] 

out=rp,,,application,remote-printing 
out=tif,,,image,tiff 
out=ps,,,application,postscript 

Utahitaji kuiweka picha yako kwenye mfumo wa TIFF au Postscript. Kwa kutumia scanner unaweza kuigeuza picha yoyote ile kuwa faili ambalo unaweza kulifungua kwa kutumia programu za picha (graphics editors) mbali mbali. Unaweza ukaitumia scanner kuhifadhi picha yako kwenye mfumo wa TIFF au Poscript moja kwa moja. Lakini kama haiwezi kufanya hivyo, unaweza kuiweka kwenye mfumo wowote ule na baadaye unaweza kuigeuza kuwa faili la Postscript kwa kufuata hatua zifuatazo. 

Kama hujaiweka tayari, weka (install) printa yenye jina Apple LaserWriter kwa kutumia CD za Windows 95. Hatua za kufanya hivyo ni chache tu. Bonyeza Start -> Settings -> Printers -> Add Printer. Bonyeza Next mara mbili na utapata dirisha la Add Printer Wizard ambapo upande wa Manufactures changua Apple na upande wa Printers chagua Apple LaserWriter, kisha bonyeza Next. Mara tatu. Kwenye dirisha unaloulizwa "Would you like to print a test page" chagua No kisha bonyeza Finish. Kama ikihitajika isaidie kompyuta kujua mahali ilipo CD au mafaili ya Windows 95. 

Baada ya kuiweka printa hiyo, kwa kutumia programu yoyote ile inayoweza kulisoma faili lenye picha unayoitaka kuituma kwa fax, lifungue faili hilo na uli-print kama kawaida kwa kutumia File -> Print. Kwenye dirisha la Print, chagua Apple LaserWriter kwenye sehemu ya Printer Name, na hakikisha kuwa umeweka tiki kwenye sehemu ya Print to File kama inavyoonekana kwenye Picha 1. Ukibonyeza OK utapata dirisha ambalo utahitajika kuandika jina la faili lenye picha yako. Tumia jina lolote lile lakini hakikisha kuwa lina extension .ps, yaani linamalizikia na .ps 

Ukishalitengeneza faili lako la Postscript, tumia njia za kawaida unazozitumia kuli-attach yaani kulifunganisha na ujumbe wako wa e-mail ambao utautuma kama ilivyoelezwa kwenye makala iliyopita. Kwa mfano, ukitaka kumpelekea fax rafiki yako Akili Mali aliye London, Uingereza (Country Code "44"), kwenye eneo lenye Area Code "181", na mwenyewe nambari yake ya fax ni 123-4567, utatumia programu yako ya kawaida ya kupelekea e-mail, kwa mfano Eudora, Netscape Mail, Microsoft Outlook, n.k, kupeleka ujumbe wako kwenda kwenye anuani ya e-mail ifuatayo: 

remote-printer.Akili_Mali@441811234567.iddd.tpc.int 

Kama umeweza kuiweka picha yako katika mfumo wa TIFF kwa kutumia njia yoyote ile, basi utaweza moja kwa moja kui-attach kwenye ujumbe wako wa e-mail na kuipeleka unapotaka itumwe kwa njia ya fax. Unaweza kutumia programu inayoitwa BliceFax, ambayo ni ya bure, kutoka kwenye anuani ifuatayo ya web: 

http://www.faxaway.com/user_guide/tiffconvert.html 

ambayo itakusaidia kuigeuza picha yoyote ile kuwa katika mfumo wa TIFF ulio mzuri zaidi kwa ajili ya kupelekwa kwa njia ya fax. 

Kuna programu nyengine kadhaa ambazo unaweza kuzitumia moja kwa moja kutuma picha kwa kutumia huduma ya e-mail-to-fax inayotolewa na TPC.INT. Kwa mfano, unaweza kutumia programu inayoitwa ScanFax inayopatikana kwenye anuani ifuatayo ya web: 

http://madhaus.cns.utoronto.ca/tpc/clients/files/pc/SCNFAC95.ZIP 

Kama unatumia kompyuta inayotumia UNIX, basi kuna programu moja safi sana inaitwa FaxMail ambayo binafsi nimeshaijaribu kwenye kompyuta yangu inayotumia Linux, na kuona inafanya mambo vizuri sana. Kwa kutumia FaxMail, unaweza moja kwa moja ukapeleka fax yenye picha kupitia mitambo ya TPC.INT. Uzuri wake ni kuwa, wakati ScanFax inakuja kwenye faili lenye ukubwa wa kama 1.2MB, FaxMail inakuja kwenye faili dogo sana la ukubwa wa 37KB tu na inafanyakazi vizuri sana. 

Natumai baada ya kusoma maelezo haya utaweza kutuma sio tu fax yenye text tupu, bali pia fax yenye picha kwa kupitia mitambo ya bure ya TPC.INT ya kutuma fax kwa njia ya e-mail. 

Juu 
 

YALIYOMO 
 

Tahari 
Kama hakuna haki watu watachukua sheria mkononi  

Kupokelewa kwa malalamiko ya Waislamu: Masheikh wasubiri ukweli wa Mkapa  

Afariki baada ya kutokwa damu nyingi: Yadaiwa hakuwa na sh. 4,000  

Nyumba ya Wakfu iliyoporwa yarejeshwa  

Kamanda Gewe atakiwa amkamate Daniel  

Sheikh awasambaratisha walevi Liwale  

Msikiti wavamiwa na kuvunjwa milango, madirisha  

Mjue Usama bin Ladin -2  

Msikiti wa Mwinyimkuu wafanya sensa  

Njaa hakuna, tunategemea kula silaha  

Parole kwa mbinde!  

Mabaraza yawatetee Waislamu - Sheikh Bafadhil  

Hali ya Uislamu Lukulunge, Kongwa inatisha  

Waislamu Kondoa waagizwa kuyatunza magazeti ya ANNUUR  

I.P.C yatakiwa kujitangaza  

Kutoka magazeti ya zamani  

Sabato ni ya Waisraeli, Mungu alikwishaiondoa  
Na Muhibu Said  

Waislamu wachoma moto nguruwe  

Tume ya kubadili Katiba Kenya: Waislamu kuwakilishwa  

Waislamu Msonge waomba wanusuriwe  

Sayansi na Teknolojia  
[PELEKA FAX NCHI ZA NG’AMBO BURE! – (2)]  

Masomo ya Kiislam  

Barua za Wasomaji  

Mashairi  

Chakula na Lishe  
[Mwongozo wa mlo wa kila siku]  
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita