|
|
|
IPO kauli maarufu toka pande zote za wananchi na viongozi wa serikali kwamba serikali haina dini lakini wananchi wake wana dini zao. Na kwamba serikali inaheshimu dini za wananchi. Kauli hii asili yake si maneno ya kustarehesha jukwaa au baraza. Ni kauli inayotokana na kutambua msingi asilia wa historia ya mwananchi tangu alipoamua kuunda serikali. Kiasili wananchi walianza hatua ya kuunda serikali kwa kuunda Katiba ya nchi, na ndani ya Katiba hiyo wakaonyesha aina ya serikali waitakayo, namna ya kuwapata viongozi na watendaji wa serikai hiyo na namna wananchi watakavyosimamia utendaji kazi wa serikali na viongozi wake juu ya yale yanayowawajibikia. Ndiyo maana viongozi wanaochaguliwa kuongoza serikali, hulazimika kula kiapo cha kuilinda na kutekeleza wajibu wao kwa kufuata katiba. Kama katiba imetamka kutambuliwa na kuheshimiwa kwa dini ya mwananchi, serikali na watendaji wake huwa hawana hiyari ya kufanya au kutamka vinginevyo. Na ni jukumu la wananchi kuona serikali na watendaji wake wanatekeleza wajibu wao. Wananchi huifanya kazi hiyo kupitia wawakilishi wao ambao huwachagua kuwapeleka bungeni ambako kwa mujibu wa katiba, wanayo haki ya kuihoji serikali kuhusu utekelezaji wa yale yaliyokwishawekwa na wananchi katika katiba ya nchi yao. Na hiyo ndiyo haki, wajibu na kazi za Wabunge kama Mh. Kitwana Kondo. Kiongozi wa serikali kumbeza Mbunge wa aina hiyo ni sawa na kuwabeza wananchi waliounda katiba iliyozaa serikali, kisha wakapiga kur kuchagua viongozi watakaoiongoza serikali hiyo. Inapodhihiri kuwa wale waliochaguliwa kuongoza serikali kinyume na matakwa ya wananchi, kazi ya wananchi huwa moja tu, kuwang’oa madarakani kwa kutowapigia kura pindi uchaguzi mkuu unapowadia. Februari 2, 1999 Mh. Kitwana Kondo alisimama Bungeni kutoa hoja ya kuitaka serikali iondoe kero zinazowasibu wananchi wa Kiislamu. Lakini majibu yaliyotolewa na kiongozi wa serikali bungeni Mh. Frederick Sumaye yamekuwa ya kushangaza kwa sababu hayakusema wala kufafanua kama serikali inawajali wananchi hao na ipo tayari kuondoa kero hizo. Moja ya hoja ya Mh. Kondo ilihusu kero wanayofanyiwa wananchi wa Kiislamu hususan waajiriwa na wanafunzi kwa kukoseshwa haki yao inayotambuliwa na katiba ya kufanya ibada ya sala ya Ijumaa kwa wasaa wakati Wakristo wana siku mbili za Jumamosi na Jumapili kufanya ibada zao. Jibu la Mh. Sumaye likawa la kukemea hoja hiyo kwamba ni ya udini! Hebu tujiulize, lipi lenye udini, kuhoji dhulma wanayofanyiwa wananchi wa Kiislamu au serikali kuwapa Wakristo siku mbili nzima za Jumamosi na Jumapili kufanya ibada zao na kuwanyima Waislamu japo nusu siku ya Ijumaa? Suala lingine alilohoji Mh. Kondo ni kuhusu elimu, kwamba inakuwaje idadi kubwa sana wa wanafunzi wa Kiislamu miaka yote washindwe mitihani ya kuingia sekondari na vyuo vya juu tofauti na Wakristo? Lakini badala ya Mh. Kondo kupewa sababu za hali hiyo alilaumiwa kwa kutowafikiria wananchi wengine. Laiti huo ndiyo ungelikuwa mwenendo wa majibu na mtazamo wa serikali dhulma wanayofanyiwa Waislamu katika elimu ingelikwisha zungumzwa siku nyingi na kupatiwa ufumbuzi miaka mingi iliyopita tangu hoja za kuwafikiria wanawake kuachwa nyuma kielimu zilipofikishwa bungeni. Hata hivyo, ndiyo tuseme Waislamu wanatakiwa waikubali dhulma katika elimu kwa sababu wapo pia wananchi wengine wanaodhulumiwa? Kwani dhulma ikienea hugeuka haki? Hatuelewi kwa nini serikali inadhani Waislamu hawastahili majibu yaliyochambuliwa kisayansi kila wanapohoji dhulma wanzofanyiwa. Katika hali ya kawaida serikali yoyote yenye kutambua wajibu wake kwa wananchi walioipigia kura, haiwezi kuona hali ya dhulma katika jamii au ikaona kuna jambo jema linalostahili kufanya wananchi, ikakaa kimya kufanyiwa mpaka wananchi hao walalamike. Lakini upo ushahidi kwamba serikali yetu inayajua hayo na inawajibika ipasavyo. Tatizo ni kwamba haioni vibaya kuwajibika kwa Wakristo na kuwapuuza wananchi wa Kiislamu. Tunashindwa kuelewa vipi kiongozi wa serikali ya aina hii anaweza kumlaumu Mh. Kondo kwa udini kwa kutoa hoja zilizo wazi na halali lakini asiuone udini huu uliopo serikalini. Mfano wa karibu juu ya udini wa serikali dhidi ya Waislamu ni kauli ya serikali iliyoitoa mwezi Desemba 1998 kwamba iliahirisha kutangazwa matokeo ya mtihani wa darasa la saba nchini ili kuepuka watakao kuwa wameanguka mtihani huo kushindwa kusherehekea vyema sikukuu yao ya Krismasi. Serikali haikuwasubiri wala hatukusikia Wakristo wakiwasilisha malalamiko ya kupinga kutangazwa kwa matokeo ya mtihani huo na serikali kuwataka wawasilishe hoja zilizochambuliwa kisayansi! Na wakati ikichukua hatua hizo za kuwaandalia furaha ya Krismasi watoto wa Kikristo walioshindwa mtihani wa darasa la saba, serikali hiyo hiyo haikuona ubaya wowote kuwalazimisha watoto wa Kiislamu kufanya mtihani wakiwa katika saumu na ibada ya mwezi wa Ramadhani na ikaona ni stahili yao wanafunzi wa Kiislamu kufanya mtihani siku ya sikukuu yao ya Eid el Fitr. Mpaka wazazi wa Kiislamu walipolalamika kuhusu watoto wao kufanyishwa mtihani mwezi wa Ramadhani na siku ya Eid ef Fitr ndipo serikali ilipotangaza kusimamisha mitihani hiyo siku ya Eid! Na si ajabu kama serikali ingeliamua kwanza kulipeleka suala hilo kwenye Baraza la Mawaziri ili kulijadili na kuona kama lina mashiko yoyote yenye uchambuzi wa kisayansi. Tunashindwa kuelewa kwa nini serikali haioni vibaya kuwatizama wananchi wa Kiislamu sawa na wengine. Wapo Wabunge waliwahi kusimama na kudai kwamba Adhana inawakera. Hatukuisikia serikali ikiikemea kauli hiyo iliyojaa chuki ya kuhoji haki ya Waislamu kutekeleza ibada. Ni tafsiri gani inayotumiwa na serikali katika kutambua masuala ya udini na yale ya kawaida yanayohusu haki ya msingi ya wananchi? Kwanini serikali haioni vibaya kuipa tafsiri isiyo sahihi hoja ya Mh. Kitwana Kondo? Dhulma yoyote inayojengeka kwa misingi ya kiubaguzi kati ya wananchi wa nchi mmoja ni hatari sana. Hayo ndiyo yaliyofikisha wananchi wa Rwanda, Burundi na Congo hapo walipo. Hatuelewi ni vipi serikali inadhani watu wenye kuitakia mema nchi hii wanaweza kuinyamazia dhulma ya ubaguzi wa kidini inayotaka kupewa sura ya haki nchini! Ni jambo la kusikitisha sana kwamba majibu yale ya Mh. Waziri Mkuu kwa Mh. Kitwana Kondo yamekuja katika muda wa wiki mbili tu tangu Mh. Rais Mkapa ayapokee vema na kuyapa ahadi njema na yenye matumaini malalamiko ya wananchi wa Kiislamu ambayo hayana tofauti na yale aliyoyatolea hoja Mh. Kondo. Mwananchi yeyote hawezi kuwa na tatizo la kuielewa hoja ya Mbunge inayokwenda sambamba na malalamiko ya wananchi; kwa sababu ni wajibu wa Mbunge kuwawakilisha wananchi. Lakini ni vigumu kwa mwananchi kuielewa kauli ya serikali inayotolewa na Waziri Mkuu inapopigana na kauli ya Rais wake katika suala lile lile. Ni dhahiri katika hali hiyo, mwananchi anaweza kushangazwa na pengine kujiuliza; ni serikali ipi anayoiwakilisha Waziri Mkuu! "MIMI ningependa kusema maswala haya ni nyeti na kwa kweli waheshimiwa Wabunge tuwe waangalifu kuyazungumza. Tutakapozungumza kana kwamba tunadhani ni sawa sawa na serikali inaonea kundi fulani. Ni lazima tuelewe ukweli na tuzungumze kweli. Sasa mimi nakubali kwamba kuna kutokulingana kwa dini hizi kubwa mbili katika shule zetu ... jinsi unavyokwenda juu. Lakini hiyo haiko kwa Waislamu na Wakristo tu. Iko kwa wanawake na wanaume. Sio kwao hao tu. Ungelienda kwa watoto wa wakulima na wafugaji hali hiyo ipo. Ndio nasema hali za namna hii tusije tukaziingiza katika hali ya kuwafanya wananchi wetu wasielewe nini kinachotokea. Maana ukisema Magerezani wapo Waislamu kwa wingi, unataka kusema kana kwamba polisi wanapokamata wanakuuliza jina lako nani ukisema Mohammed ndani, ukisema Frederick ah huyo hapana. Sasa mimi nasema masuala ya dini tunapoyazungumza lazima tuwe waangalifu sana. Kinachotakiwa, tusema jamani hapa pana tatizo, sasa namna ya kulitatua, lakini si kwamba kuna watu wanaonewa makusudi. Wanafunzi hawachaguliwi kwa majina ya Kikrsto na Kiislamu hata kidogo. Lakini tukubali kuna tatizo tulifanyie kazi. Watoto wa wafugaji hawa hawaendi shule tufanyeje, watoto wa kike hawapati nafasi za kutosha. Hakuna anayewazuia, lakini ni kweli hawapati nafasi, sasa tufanyeje. Waislamu hakuna anayewazuia, lakini kweli hawapo wengi, tufanyeje. Haya ndiyo mambo yanayotakiwa katika kujenga nchi. Ndugu Spika wapo hata watoto wa makabila mengine bado yapo porini wanakula
mizizi na matunda. Hata shule hawajui ipo wapi. Haya ndiyo mambo ambayo
kama taifa tunatakiwa tuweke vichwa vyetu pamoja tuone tuyatatue namna
gani. Tusitafute mchawi maana hayupo"
|
YALIYOMO
Tahari
Matokeo ya mitihani darasa la saba serikali ieleze: Je, Waislamu ni taahira au kuna agenda ya siri Wenye siasa za kikaburu wasimyumbishe Rais Hatuko tayari kuruhusu viwanja viporwe - Manyema Maoni yetu
DONDOO ZA KISAIKOLOJIA: PEDOPHILIA Uislamu na Mazingira katika
Umoja wa Mataifa
Barua za Mtume (s.a.w.) za Jihad katika
Internet
Rais Mkapa atekeleze hadi yake
kwa hadhari
Mashirika ya Dini yaelekeze
misaada vijijini
Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni Dodoma Ni serikali ipi anayoiwakilisha
Sumaye
Sehemu ya maelezo ya Waziri Mkuu bw. Frederick Sumaye bungeni Zanzibar ni nchi au mkoa?.
Sheikh Bafadhil aamuru kusimamishwa shughuli za African Muslim Agency Moro Vijana Arusha njooni mnione - Alhaj Mollel Waislamu Korelo wazama kwenye ushirikina Waislamu Hanang’ wajenga Msikiti Sayansi na Teknolojia
Chakula na Lishe
|