|
|
|
TUMEISIKIA kauli ya serikali wakati Mh. Rais alipokuwa akijibu Risala ya Waislamu katika Baraza la Eid el Fitr hivi karibuni. Hizi ni zama za ukweli na uwazi, Mh. Rais alikubali na kuipokea risala iliyojaa malalamiko ya Waislamu. Hakuishia hapo, lakini akaahidi kuyashughulikia akishirikiana na Baraza lake la Mawaziri. Aidha, aliwaomba Waislamu wamsaidie kwa kuyachambua matatizo hayo na kuyafanyia utafiti wa kisayansi. Lililo muhimu zaidi ni kwamba Mh. Rais Benjamin William Mkapa aliyapokea malalamiko hayo kwa furaha na moyo mkunjufu huku akiwashukuru sana Waislamu kwa kuwa wazi kwake. Hakuwakemea wala kutoa onyo kwamba wamezungumza mambo nyeti. Akifunga hoja yake ya kujadili hotuba ya Mh. Rais Bungeni Waziri Mkuu Mh. Frederick Sumaye alisema kwamba masuala ya dini ni nyeti na hapana budi kuwa waangalifu katika kuyazugumza. Pamoja na kukiri kwamba kuna kutokulingana kwa Waislamu na Wakristo katika mashule yetu lakini akasema kwamba hilo halipo kwa Waislamu na Wakristo tu. Amesema upo upogo pia kwa wanawake, wafugaji na wakulima, ambapo watoto kutoka makundi hayo hawapati fursa ya kusoma sawa na wengine. Aidha, Mh. Waziri Mkuu akionyesha kuwa tatizo la maendeleo hasa katika elimu halipo kwa Waislamu tu alisema kwamba yapo baadhi ya makabila ambayo bado yapo porini wakila mizizi na matunda. Na kwamba kinyume na Waislamu watoto kutoka makabila hayo hawajui hata ilipo shule. Mh. Waziri Mkuu Bw. Frederick Sumaye alitoa maelezo hayo kama kielelezo cha kuonyesha kwamba Waislamu hawabaguliwi katika elimu kutokana na dini yao bali kutokana na sababu nyingine kama ilivyo kwa makabila yaliyo porini yakila mizizi na matunda. Aliyosema Mh. Rais Mkapa tumeyaelewa. Hatuna la kuhoji zaidi ila kumsaidia katika utekelezaji. Ila tumetatizika na haya yaliyosemwa na Mh. Sumaye, lakini hata hivyo, tusingependa kupambanisha kauli ya Mh. Sumaye na ile ya Mh. Rais Mkapa. Tunajizuia na yanayotugusa zaidi. Awali ya yote, tungependa tuseme kwamba ni kweli Waislamu wamekuwa wakidhulumiwa na kuonewa kutokana na dini yao. Pili, kufanya malalamiko ya Waislamu jambo nyeti ni kuficha ukweli kwa lengo la kuendeleza dhulma iliyopo sasa. Tatu, ukurasa wa kuyafanya malalamiko ya Waislamu suala nyeti ulifungwa Januari 19, 1999 Mh. Rais Benjamin William Mkapa alipoyapokea rasmi malalamiko ya Waislamu na kuahidi kuyashughulikia akisaidiana na Baraza lake la Mawaziri. Nne, tunahisi Waislamu hawakutendewa haki na kwa kweli yaweza kuwa ni dharau na pia kejeli iliyopindukia mipaka kwa matatizo yao kutizamwa sawa na ya wale walio porini wakila mizizi na matunda. Walio porini bila nguo ila ngozi au magome ya miti wakila mizizi, nyama na asali ni kutokana na uoni wao juu ya uhai, lengo la kuumbwa kwao, tafsiri ya maendeleo na ustaarabu na kubwa zaidi nini hadhi yao hapa duniani ikilinganishwa na viumbe wengine. Kabla Muislamu hajaelezwa Mungu ni nani anaamrishwa asome. "Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba". (96:1) Japo Mh. Waziri Mkuu si bingwa na Profesa wa historia, lakini hakosi kujua habari za Ibn Sina, Ibn Khaldun asili ya neno kemia , aljebra ... n.k. Aidha Mh. Waziri Mkuu hakosi kujua habari za Chuo Kikuu na Maktaba kuu kongwe ya Cordova. Na kwa mfano wa karibu huko si kuwa na kumbukizi kwamba wakoloni wa Kijerumani walipoingia nchini waliwatumia Waislamu kama makarani kwani ndio waliokuwa wakijua kusoma na kuandika. Ni vizuri tukakumbusha kuwa wakati Wazungu wa kwanza wakiingia nchini kupitia Arusha na Kilimanjaro mnamo karne iliyopita, walifika Sambaa na kukuta watoto wa Chifu Kimweri waliokuwa Waislamu wakiandika kumbukumbu za kesi alizokuwa akihukumu baba yao mahakamani. Wazungu hao Krapf na Rebman, hawakuyaona hayo kwa watu wa maeneo hayo ya Kaskazini waliokuwa wakiishi maisha ya ujima. Vipi leo utawafananisha Waislamu na watu hao. Lakini pia atakumbuka jinsi Waislamu walivyojenga shule za Muslim kwa nguvu zao na kuziendesha wenyewe bila ya mfadhili huku Wakristo wakipewa ruzuku iliyotokana na kodi za wananchi. Vipi leo, tatizo la elimu kwa Waislamu litazamwe sawa na linavyotizamwa tatizo la walio porini wasiojua hata shule ipo wapi. Pamoja na hayo tuchukulie mtizamo huo huo wa Mh. Waziri Mkuu kwamba matatizo ya Waislamu ni sawa na yale ya wanawake, wafugaji na Wamang’ati. Lakini serikali inao mkakati maalum wa kuwaendeleza wanawake na huko porini kwa Wamasai, Wabarbaig na Wamang’ati hujengewa shule rasmi za bweni kwa ajili ya watu hao. Na kampeni kubwa hufanywa kutoa motisha na vishawishi vya kila namna ili mradi tu kuhakikisha kwamba watoto kutoka makabila hayo wanapata elimu. Pengine Mh. Waziri Mkuu atueleze serikali ina mkakati gani kwa ajili ya Waislamu! Wakati wa ukoloni Waislamu sawa na wananchi wengine walilipa kodi, lakini ni mashirika ya Kikristo pekee yaliyoruhusiwa kuanzisha shule na kupewa fedha za serikali. Hata pale ambapo Waislamu waliruhusiwa kuanzisha shule walinyimwa ruzuku iliyokuwa inajulikana kama Grant in Aid. Pale ilipotolewa ilitolewa kwa uchache sana ikilinganishwa na ile waliyopewa Wakristo. Hali hiyo ilipelekea Waislamu kuilalamikia serikali ya kikoloni kama tunavyolalamika leo. Si mahala pake kunukuu malalamiko hayo; yataenda kwa Rais kupitia kamati ya Alhaj Madabida. Baada ya mashule ya dini kutaifishwa, mashule ya seminari za Kikristo ziliendelea kusajiliwa wakati Waislamu waliwekewa vikwazo. Aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu Almaruhumu Profesa Kighoma Ali Malima mwaka mmoja alibadili utaratibu uliokuwa ukitumiwa kutahini na kuchagua wanafunzi kwenda kidato cha kwanza. Kwa kauli yake aliyowahi kuitoa hadharani katika uhai wake ni kuwa kutokana na juhudi iliyokuwa imefanyika kuzuia mianya ya upendeleo, idadi ya wanafunzi Waislamu waliochaguliwa iliongezeka kwa takriban asilimia arobaini ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Sote tunakumbuka zogo lililotokea dhidi yake akatolewa Wizara ya Elimu na utaratibu aliokuwa ameanzisha ukafutwa. Tunayo mifano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu ambao waliwahi kuhojiwa juu ya dini zao na endapo wao ni siasa kali au la. Matokeo yake wakanyimwa nafasi ya kuendelea kuwa Wahadhiri chuoni hapo japo kimasomo walikuwa wakiongoza. Bw. Jan Pvan Bergen katika kitabu chake "Development and Religion in Tanzania" ameeleza jinsi viongozi wa serikali ya awamu ya kwanza walivyotumia Ukatoliki wao kuupa nguvu Ukristo. Aidha, ameeleza pia jinsi Wakristo walivyokuwa wakijenga udini wakati Waislamu wakiangalia utaifa na maslahi ya nchi kwanza. Leo ni mwaka wa 18 toka kitabu hicho kichapishwe hakuna Mkristo yeyote aliyesimama kuyakanusha hayo. Lakini Dk. John Sivalon wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kitabu chake mashuhuri "Kanisa Katoliki na Siasa Tanzania mwaka 1953 hadi 1984", ameeleza kwa urefu jinsi Kanisa lilivyomtumia Mwalimu Nyerere kulilinda na wakati huo huo kuzipiga vita taasisi za Kiislamu. Kitabu hicho kimechapishwa na Kanisa lenyewe pengine katika kusherehekea kufanikiwa kwa mikakati yake ya kuitumia serikali kuwakandamiza Waislamu. Kwa taarifa tulizo nazo Dk. John Sivalon ashakutana na Mwalimu Nyerere takriban mara tatu toka kitabu hicho kitoke mwaka 1992 na Mwalimu hajamwuliza chochote juu ya yale aliyoandika. Lakini lipo lingine ambalo linamhusu Mh. Sumaye zaidi. Yeye amehusika sana kuivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuunda Tume ya Jiji hilo. Aidha, mwaka jana akapeleka hoja bungeni tume hiyo iongezewe muda baada ya muda wake wa awali kumalizika. Wakurugenzi wote wa Tume hiyo, wakuu wa kanda pamoja na Mwenyekiti wao, hakuna Muislamu hata mmoja. Waislamu wameambualia kazi za kufagia, "uaskari" na makarani wa kupewa amri na kutumwa. Pengine tuelezwe wakurugenzi hao sifa gani wanapaswa kuwa nazo ambapo amekosekana Muislamu hata mmoja aliyenazo! Tunaamini ushahidi wote huu na mengine mengi ambayo hatuwezi kuyataja hapa yamefika kwa Mh. Rais Mkapa. Na hakukurupuka tu kuyapokea malalamiko ya Waislamu ya kuonewa na kutokutendewa haki na serikali, bali ni baada ya kuiona hali halisi na kuzingatia maslahi ya muda mrefu ya nchi hii. Kama alivyoahidi kusaidiana na Baraza la mawaziri kulishughulikia suala hili, tunahisi msaada anaohitaji Mh. Rais si kurejesha tena unyeti. Bali kulijadili suala hili kwa uwazi na kulifanya utafiti, huru na wa kina. Mfano Mh. Kitwana Kondo amedai kwamba watoto Waislamu waliofanya mtihani kwa mkoa wa Dar es Salaam ni 71%, Wakristo ni 29%, lakini Wakristo wakachaguliwa asilimia 79 (79%) na Waislamu 21%. Badala ya kuonya kuwa masuala haya ni nyeti au kuyalinganisha sawa na suala la wala mizizi porini iundwe tume ya wataalamu ya uchungzi kwa uwiano sawa Wakristo na Waislamu ipitie karatasi za mitihani darasa la saba mwaka jana. Lengo likiwa kuona kama waliochaguliwa wanastahiki kutokana na walivyofaulu. Kwani hatutarajii japo ni kuchaguliwa achaguliwe aliyepata alama 70 aachwe aliyepata 80. Mh. Waziri Mkuu amesema kwamba vyombo vya dola havifanyi kazi kwa kumwangalia huyu ni Mohammed au Frederick. Masheikh na Waislamu kwa ujumla wamekuwa wakilalamika juu ya nguruwe wanaoranda randa na kuingia Misikitini. Katika Msikiti wa Ubungo Darajani nguruwe aliingia na kufia ndani ya Msikiti. Nguruwe pia aliingia Msikti wa Ubungo External na Tabata. Taarifa zilipelekwa polisi na serikalini, wahusika hawakupigwa kirungu wala kukamatwa. Sheikh Nurdeen Hussein Shadhly ni Amir Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu. Ni kiongozi Mkuu wa Twaikat Shadhly kwa nchi nzima. Sheikh Nurdeen aliwahi kulalamika mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Ali Ameir mwaka 1998kwamba kuna Wakristo wanaukashifu Uislamu kwa kusema "Mtume (S.A.W.) kafa kwa ukimwi". Hakuna hatua zilizochuliwa. Lakini muda mfupi baadaye Padri Lwambano akadai kwamba Yesu anatukanwa. Vyombo vya dola vikahamanika watu wakakamatwa zogo likawa kubwa na baadhi ya Waislamu wakauliwa. Wanawake Waislamu wamevuliwa nguo wakapekuliwa tupu zao na wanaume, Mkristo gani aliyewahi kufanyiwa hivyo. Kama si Uislamu nini kilichofanya mzee Chata (Mungu amrehemu) na Mzee Katambo wawekwe ndani na kunyimwa dhamana. Lipi lilikuwa kosa lao. Lilipotokea tatizo la Arumeru na Wakristo kuuana hatukusikia polisi wakipewa amri "piga yule" lakini juhudi zilifanyika kutatua mgogoro ule kwa njia ya mazungumzo. Mbona lalamiko la Paroko limejibiwa kwa amri za kamata kamata, kuvamia Msikiti hadi kufikia kuua? Kama Simbaulanga aliyesema "Mtume (s.a.w.) kafa kwa ukimwi" aliingizwa rumande mlango wa mbele akatolewa ule wa nyuma wakati kina Mzee Chata wakiteseka kwa kunyimwa dhamana ni wazi kama waliouliwa pale Mwembechai wangekuwa Wakristo Tume ya uchunguzi ingekwisha undwa. Aidha polisi wahusika wangekwishafikishwa mahakamani na pengine wangelishapewa adhabu. Kama alivyosema Mh. Kitwana Kondo, tunawaomba viongozi wa serikali hasa Mawaziri wamsaidie Mh. Rais Mkapa kuyaangalia malalamiko haya ya Waislamu kwa maslahi yetu sote na nchi yetu. Mh. Sumaye udini upo wa kuwapendelea Wakristo na kuwadhulumu Waislamu. |
YALIYOMO
Tahari
Matokeo ya mitihani darasa la saba serikali ieleze: Je, Waislamu ni taahira au kuna agenda ya siri Wenye siasa za kikaburu wasimyumbishe Rais Hatuko tayari kuruhusu viwanja viporwe - Manyema Maoni yetu
DONDOO ZA KISAIKOLOJIA: PEDOPHILIA Uislamu na Mazingira katika
Umoja wa Mataifa
Barua za Mtume (s.a.w.) za Jihad katika
Internet
Rais Mkapa atekeleze hadi yake
kwa hadhari
Mashirika ya Dini yaelekeze
misaada vijijini
Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni Dodoma Ni serikali ipi anayoiwakilisha
Sumaye
Sehemu ya maelezo ya Waziri Mkuu bw. Frederick Sumaye bungeni Zanzibar ni nchi au mkoa?.
Sheikh Bafadhil aamuru kusimamishwa shughuli za African Muslim Agency Moro Vijana Arusha njooni mnione - Alhaj Mollel Waislamu Korelo wazama kwenye ushirikina Waislamu Hanang’ wajenga Msikiti Sayansi na Teknolojia
Chakula na Lishe
|