Umuhimu wa huduma kwa jamii na matokeo yake
 
Na Kawela Saidi, Dodoma
 

KATIKA gazeti la ANNUUR namba 187 ukurasa wa 11, ilichapishwa makala iliyohusu "Mashirika ya Dini yaekeleze misaada vijijini". Kwa leo makala hii itahusu umuhimu wa huduma kwa jamii na matokeo yake. Mwandishi kwa leo anatathmini matokeo yaliyojitokeza pale aliposhiriki katika kusambaza chakula cha misaada toka shirika moja la Dini ambalo lilitoa misaada ya chakula na madawa ya binadamu katika vijiji saba vya Dodoma hivi karibuni.

SHIRIKA moja la Kimataifa la Kiislamu na Uenezaji wa Dini na Huduma za Kibinadamu (World Islamic Propagation and Humanitarian Services (WIPHAS) ilitoa misaada ya chakula na madawa ya binadamu katika vijiji vya Chamwino Masjid Taq’wa (Ikulu), Msanga, Magereko, Chalinze, Mahito, Babayu, Mbande na Dodoma Vijijini.

Kwanza nalipongeza shirika hilo kwa kutoa kipaumbele huduma zake kwa muda muafaka kabisa kwa walengwa na usimamizi mzuri pamoja na uadilifu kwa viongozi hao ambao ni wawakilishi wa WIPHAS Dk M. Shareef alinijulisha kuja kwake Dodoma kumetokana na kupatikana kwa taarifa za njaa zilizotangazwa na vyombo vya habari vya serikali na watu binafsi kama Radio na Magazeti.

Dk. Shareef alisema "Tuliamua kuja kutoa misaada hii bila kusubiri na kujua yupi anastahili na asiyestahili, kama suala la utafiti tutalifanya huku huku kwa kukutana na viongozi wa vijiji husika, kwani tabia ya urasimu (red tapes) mara nyingi husababisha hisia za rushwa na hata maafa, fundisho tunalolipata katika saumu ya Ramadhani inatosha kuwa na huruma pale tunaposikia watu fulani hawana chakula huhangaika huku na kule na kuharibu mustakabali wa uzalishaji wa uchumi", alisema Dk. Shareef.

Safari yetu ilianzia kijiji cha Chamwino (Ikulu) katika Masjid Taq’wa. Kijiji cha Chamwino (Ikulu) kimegawanyika sehemu mbili, moja ni ile sehemu ya watumishi wa serikali, kama Ikulu, Elimu, Polisi, Posta, Mahakama n.k. Sehemu ya pili ambayo ndiyo kubwa zaidi ni ya wana kijiji ambao wameathiriwa sana na njaa.

Kufika kwetu hapo tulikutana na uongozi wa Masjid Taq’wa ambao ulituomba chakula hicho kipewe wanakijiji ambao wameathirika sana na njaa, Bwana Hamis ambaye ni Mwenyekiti wa Masjid Taq’wa alizungumza kwa niaba ya uongozi wa serikali ya kijiji ambao nao walithibitisha hali hiyo mbaya.

Alisema Mwenyekiti wa Kijiji hicho kuwa "Sisi ni wafanyakazi wa Idara mbalimbali za serikali hivyo tuna uwezo wa kubajeti pindi tupatapo mishahara yetu na angalau tunaweza kuishi bila ya matatizo, ni lazima tuonyeshe huruma kwa wanachi wenzetu ambao hawana kipato chochote", alisema Mwenyekiti huyo wa kijiji. Kitendo walichokifanya viongozi hao kilionyesha huruma na mapenzi waliyonayo baina ya viongozi wa serikali ya kijiji na wanakijiji hao walioathirika kwa njaa.

Kijiji cha Msanga ambacho kipo kaskazini mwa Chamwino (Ikulu) nacho kimeathiriwa na njaa kiasi cha baadhi ya watu walishindwa kusimama (foleni) ili waweze kupokea msaada wa chakula hicho, baadhi yao walishangaa kupata msaada huo wa ghafla (bila ya kuhesabiwa).

"Tumeshaandikishwa zaidi ya mara mbili na kamati inayohusika na ugawaji wa chakula cha serikali cha bure na nguvu kazi lakini hatujakipata hadi sasa (Januari 24, 1999) na sasa hivi tunatoka katika mkutano wa viongozi hao husika, lakini urasimu unaofanyika unazidi kutuumiza", alisema Bwana mmoja ambaye alijitambulisha kuwa ni Mwalimu Khalifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mwalimu mmoja wa shule ya msingi ya Msanga ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema "mahudhurio ya wanafunzi yamefikia 43% katika shule ya Msanga watu wanakula zambarau na hata kufikia kula mihogo ya mikahewa (kisamvu mpira)".

Tulipofika kijiji cha Mageleko (km 60) toka Dodoma Mjini au (km 20) kutoka Chamwino (Ikulu) wananchi wa kijiji hicho hawakuonyesha furaha kwani walihisi ni yale yale ya kuandikishana kila mara na kufanya vikao mfululizo huku watu wakiathirika na kuathiri hata shughuli zao.

 
Juu RUDI

Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook