UMOJA wa Waislamu mkoani Kigoma unaelekea kurudi katika hali yake ya kawaida baada ya vurugu za Msikiti wa Kibondo (Kitongoni) zilizofanyika siku kadhaa zilizopita na kusababisha Waislamu kugawanyika ndani ya Msikiti huo na kuwa makundi mawili.
Hayo yamesemwa na Sheikh wa Mkoa wa Kigoma Alhaj Tofiki Ibrahim Malilo, wakati akiongea na Waislamu waliohudhuria katika sherehe yandoa ya Bwana Yamungu Mustafa na Bi Vumilia bint Rashid ndani ya Msikiti wa Mwanga Majengo mkoani hapa.
Sheikh Tofiki aliwaasa Waislamu kuacha tabia ya kuitana makafiri kwa sababu ya tofauti ndogo za kimadhehebu ili hali wote ni Waislamu.
Wakati huo huo, Sheikh wa Mkoa Alhaj Tofiki Ibrahimu Malilo alichangisha mchango wa ujenzi wa darasa moja katika sekondari ya Kiislamu iliyoko Ujiji Jihad Secondary School.
Aidha, Sheikh Tofiki amewahimiza Waislamu kujitolea kukamilisha ujenzi wa shule hiyo na nyingine pia.
WAZAZI wa Kiislamu wa mjini Dodoma wameahidi kutoa ushirikiano wa dhati kuwafichua Wakuu wa Shule/Vyuo watakaokiuka agizo la Waziri wa Elimu na Utamaduni Mheshimiwa Juma Kapuya juu ya agizo la serikali la kuwataka Wakuu wa Shule na Vyuo kuwaruhusu wanafunzi wa kike wa Kiislamu kuvaa Hijabu.
Waraka huo ambao ulitolewa na Kamishna wa Elimu mwaka 1995; EDC/10/62/Vol.1/147 ya 28/8/1996 umeonekana kupuuzwa kwa idadi kubwa ya Wakuu wa Shule na Vyuo mkoani Dodoma.
Katibu wa kikundi cha akina mama wa Kiislamu cha Bi Khadija, Bi Mwanaisha Mwinchumu alisema, tamko la Mheshimiwa Kapuya limewapa ari kubwa hasa pale jitihada zao binafsi kutofanikiwa kwa Wakuu wa Shule hizo.
Akifafanua zaidi, Bi Mwinchumu alisema: " Tulifuatilia suala hili kwa jitihada kubwa hata kuingia gharama za kutayarisha nguo hizo, lakini baadhi ya wakuu wa shule hawakukubali, hasa shule ya Central, hakika tumefarijika kwa agizo hilo alilolitoa Bungeni Februari 2, 1999 alasiri, pale alipojibu taarifa ya Mheshimiwa Kitwana Kondo.
Naye Mzazi Bwana Kawela Saidi ambaye ni Mkuu wa Da’awah katika umoja wa vijana wa Kiislamu (UVK) alisema, walikuwa wakipata malalamiko mengi sana toka kwa wanafunzi wa Central jinsi Mkuu wa Shule hiyo alivyopuuzia agizo la Kamishna wa Elimu, juu ya wanafunzi kuvaa hijabu.
Bwana Kawela alisema "tunao ushahidi wa risala zao zilizokuwa zikitolewa katika mahafali za kuagana".
"Walishatuma barua kwa Mkuu huyo (Central) ili awaruhusu wanafunzi kuvaa hijabu kwa mujibu wa agizo la serikali, lakini hadi sasa hajatujibu", alisema Katibu wa U.V.K. Ustadh Kamana.
Aidha, mwanafunzi mmoja anayechukua Diploma (stashahada) ya Ualimu katika Chuo kimoja cha Ualimu Mjini Dodoma Ustadh Athmani alisema kuwa yeye binafsi alishamuona Mkuu wa Shule ana kwa ana kuzungumzia suala la hijabu, jibu la Mkuu huyo lilikuwa "Shule itakuwa na sare ngapi? Sintaruhusu wala nisisikie tena suala hilo", alijibu Mkuu huyo wa shule.
Bi Halima Kalaghe mkazi wa Airport Mjini Dodoma alisema kuwa "umefikia muda kwa Waislamu kutojinyongesha kwa watendaji wasiotii amri za Wakuu (waajiri) wao. Serikali yetu ni nzuri lakini inaharibiwa na watendaji wake wa chini, ambao kwa namna moja au nyingine ndiyo wanaoweza kuwa chimbuko la kuhatarisha amani", alisema Bi Halima.
"Sasa tutawavalisha hijabu binti zetu kisha tuone ukaidi wa hao watendaji, aidha tutawafichua kwa Waziri wa Elimu na Utamaduni kama alivyotoa wito Bungeni" alimalizia kusema Bi Halima.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii kuwa Mkuu wa shule ya Central alishapata unaonyesha barua kadhaa za kumtaka awaruhusu wanafunzi wa kike wa Kiislamu wavae hijabu lakini zote hazikujibiwa.
Barua hizo ni pamoja na ile ya BAKWATA Wilaya DIST/BKT/DO/1/191 ya Februari 26, 1996, na umoja wa vijana wa Kiislamu UVK/DOM/11/65/89 ya Desemba 10, 1998.
WALIMU wa taaluma wa shule tatu za sekondari za mjini Tanga wameshutumiwa kwa kutokuwa waadilifu katika kazi zao , hasa kwa jinsi wanavyowashughulikia wanafunzi wa Kiislamu.
Shutuma hizo zimetolewa na wanafunzi kadhaa wa Kiislamu waliomaliza kidato cha nne hivi karibuni.
Katika shutuma zao hizo zenye kufanana, wamesema walimu hao ambao wote ni Wakristo walikuwa na njama za kupunguza idadi yao katika kufanya mtihani wa somo la elimu ya dini ya Kiislamu.
Wanafunzi wa shule ya Mkwakwani wamesema kati ya wanafunzi 20 waliosajiliwa kufanya somo hilo, ni saba tu miongoni mwao walioruhusiwa mwanzoni kufanya mtihani.
Hata hivyo, kwa mujibu wa wanafunzi hao, baada ya mvutano wa muda mrefu na kuitwa kwa Mwalimu wa taaluma Bw. Bendera ilibidi wote wafanye, kwani karatasi za maswali zilikuwa sawa na idadi yao, na fomu za usajili zilionyesha saini za wanafunzi kamili.
Tatizo kubwa lilitokea shule ya Galanos ambako mvutano katika ukumbi wa mitihani ulipelekea mtihani wa karatasi ya mwanzo kuanza saa 11 badala ya saa 8 pale mwalimu mkuu, Bw. Kinala alipoingilia kati kufuatia kugoma kwa wanafunzi kutoka ndani ya chumba cha mitihani ambapo ilibidi karatasi zaidi zitafutwe kwa ajili yao.
Kwa upande wa Usagara, wanafunzi 5 walizuiliwa moja kwa moja kati ya 43 kufanya mtihani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu hapo Februari 9, 1999, Mwalimu Mkuu wa Galanos alikanusha kuzuiliwa kwa wanafunzi wa Kiislamu kufanya mitihani yao, hata hivyo alikiri kutokea kasoro za kiutendaji siku ya mwanzo.
Mwalimu Kinala alizungumza baada ya mwalimu wa taaluma Bw. Mzee kukataa kusema lolote.
Akitabasamu, Bw. Kinala alimuhakikishia mwandishi kuwa tayari ameandika barua ili karatasi zote zisahihishwe kikawaida.
Mwalimu wa taaluma wa Mkwakwani alisisitiza kwa njia ya simu kuwa madai ya wanafunzi si ya kweli na kwamba yeye hakuhusika kumzuia yeyote. Papo hapo akataka habari hizi ziwekwe vizuri ili zisieleweke vibaya.
Alitaja kutokujazwa vyema kwa fomu za "Entry" na "CS" kuwa ndiko kulikopelekea hali hiyo. Alipoulizwa iwapo kosa kama hilo lilitokea kwa masomo mengine, alikiri kuwa ni kwa somo hili moja tu.
Juhudi za kumpata Mwalimu Shao wa Usagara aliyelalamikiwa hazikufanikiwa.
Shule nyingine kadhaa za mjini Tanga zimeelezwa kufanya mtihani huo, hata hivyo hakuna malalamiko yoyote yaliyopokelewa kutoka kwa shule hizo.
Wakati huo huo, mwandishi wetu kutoka Morogoro anaripoti kwamba walimu wa taaluma wamechangia kiasi kikubwa kuwafanya wanafunzi wa kidato cha nne wasifanye mitihani ya dini ya Kiislamu.
Imeelezwa kuwa walimu wa taaluma hutumia mbinu mbalimbali kuwazuia vijana wa Kiislamu wasifanye mtihani wa somo la dini ikiwa ni pamoja na kuwaambia kuwa somo hilo halipo katika masomo yanayofanyiwa mitihani.
HUDUMA za chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa mjini hapa ni mbaya kutokana na ubovu wa majokofu yake.
Uchunguzi wa hivi karibuni wa gazeti hili umegundua kuwa maiti huifadhiwa hivyo hivyo licha ya athari hiyo huku harufu kali ikihatarisha afya za watu.
Wakiongea na ANNUUR mwishoni mwa wiki, baadhi ya wakazi wa mji huo walionya kwamba hatua za haraka zisipochukuliwa mambo yataharibika zaidi.
Aidha, baadhi ya wakazi waliilaumu serikali kwa uhodari wa kuwakamua kodi huku wakiwa dhaifu katika utoaji huduma bora kwa jamii husika.
Wakati huo huo, Waislamu wa mjini hapa waliokuwa wakitoa huduma za usafi, vyakula, madawa na kufariji wagonjwa hospitalini hapo wamewekewa ngumu hivyo kusimamisha shughuli hizo kwa zaidi ya miezi miwili sasa.
Kwa mujibu wa kiongozi mwandamizi wa tamasha hilo Bw. Shaban Viguro, uongozi wa hospitali hiyo umewataka waandike barua wajiegemeza kwa taasisi yoyote ya Kiislamu, jambo ambalo Waislamu hao hawakubaliani nalo.
"Tulipoomba mwanzoni tuliwaambia kuwa sisi hatufungamani na taasisi yoyote, wakakubaliana nasi na tukaanza kazi huku wakitupa pongezi kwa msaada wetu kwao na kwa wagonjwa, sasa vipi leo watugeuke? Bila shaka ipo namna", alisema kiongozi huyo.
Tamasha la wagonjwa Morogoro liliasisiwa na Daruweshi Kazimoto wa Tabora akisaidiana na Sheikh Mussa Kariati wa Mwembesongo katikati ya mwaka jana, na kuanza kuwekewa ‘mizengwe’ na uongozi wa hospitali hiyo mwishoni mwa mwaka jana.
Mwandishi wa habari hizi alikwenda mara kadhaa katika ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa kujua kadhia zote mbili bila ya mafanikio, zaidi ya lugha za kawaida za ‘hayupo’ na ‘katoka kidogo’ au ‘ana kazi nyingi’.
|
|