Ulaji wa ‘Kiti Moto’ hadharani
 
Umoja wa Kitaifa wafikia hatma yake
  UMOJA wa Kitaifa Tanzania inaojivunia upo mbioni kuporomoka tena kwa kasi kubwa kutokana na mwelekeo wa Wakristo kulazimisha mazingira ya kujitenga.

Hayo ni maoni ya watu kadhaa waliohojiwa na gazeti hili kufuatia tarifa za vyombo vya habari kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Jiji Bw. Charles Keenja ametoa agizo kwamba ulaji wa nyama ya nguruwe sasa uwe hadharani.

Akitoa maoni yake kufuatia taarifa hizo, Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mwinshehe Ng’amba alisema kwamba inavyoonekana Wakristo wa nchi hii wanapata tabu sana kuchanganyika na Waislamu. Na kwa kuwa kisiasa hawawezi kutangaza hadharani kwamba wanajitenga. Wameamua kujenga mazingira ya kufikia lengo hilo.

Amesema kwamba Tume ya Jiji isiishie tu kujenga mazingira ya ‘kuhalalisha’ nyama ya nguruwe hadharani bali pia ianze mpango kabambe wa mipango miji ambapo Wakristo watakuwa na mitaa yao mbali na Waislamu.

Aidha, amesema isije ikawa ni jambo la kushangaza tena kuona watu wakisusiana yale mambo yaliyozoeleka ya ujirani mwema ikiwa ni pamoja na watoto kucheza pamoja, kushirikiana katika mazishi, harusi n.k.

Mzee Mwinshehe ambaye amejitambulisha kwamba anatoka Rufiji, amesema kwamba zamani kulikuwa na kitabu kinasema "Paulo usicheze nasi una mikono michafu", lakini kikafutika; pengine kutokana na ujumbe usiokubalika, unaojengwa na kitabu hicho.

Lakini akasema kwa "kuhalalisha" nguruwe aliwe hadharani ni kwamba wenye kula nguruwe wanajitangaza hadharani na hivyo kujitenga wenyewe, nyumba zao zisitembelewe, maduka yao yasusiwe na watoto wao watengwe wasicheze na wenzao.

Alisema hii ni kutokana na ukweli kwamba nguruwe kwa Muislamu ni uchafu mkubwa (najisi kubwa) isiyoondoka ila mpaka kwa kusafishwa mara saba moja ikiwa kwa mchanga.

Mzee mwingine wa Mabibo aliyefika katika ofisi za gazeti hili kutoa maoni yake amesema kwamba anasikitika umoja wa kitaifa ambao Mwalimu Nyerere amekuwa akijinasibu nao na kuuhesabu kama moja ya mafanikio ya uongozi wake unabomoka akiwa angali hai.

Amesema kwamba Waislamu toka ukoloni wamekuwa wakifanya kila juhudi kujali umoja huu wa kitaifa, lakini kwa bahati mbaya wenzao kama alivyosema Dk. Sivalon wakiingia Bungeni wamekuwa wakijihesabu si kama Wakristo tu lakini huenda mbali zaidi kuangalia Wakatoliki wangapi.

Mzee huyo ambaye amejitambulisha kwa jina moja la Mkopi amesema kwamba zamani huko Kisiju palikuwa na Mtungi na kopo pekee la kuwapea wasio Waislamu maji na kopo hilo haliingizwi ndani bali hukaa nje tena mbali watoto wasichezee.

Akipita mpita njia asiyekuwa Muislamu na kuomba maji ya kunywa hupewa kwa kutumia kopo hilo. Hiyo ilikuwa ni tahadhari ya kujitenga na najisi (uchafu) ambao ingesambazwa na mtu huyo kwani ilidhaniwa kwamba kila asiye Muislamu ni mla nguruwe.

"Kwa mtindo huu anaokuja nao Bw. Keenja", alisema Mzee Mkopi itakuwa ama turejeshe makopo ya kuwapea maji Wakristo au tuanze kuwaelimisha watoto wetu wasinywe maji kwa Mkristo na wao wasiwape maji kwani watatia najisi gilasi zao.

Hata hivyo, Waislamu wengine waliotoa maoni yao kwa njia mbalimbali wamesema kwamba inavyoelekea inaonekana umoja wa Kitaifa umeshapoteza umuhimu wake. Kwamba baadhi ya watu wanadhani wanajitosheleza kwa kila kitu na hawahitaji msaada wala mahusiano mazuri na watu wa imani tofauti na wao.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook