Maofisa Ubalozi, Wizara watuhumiwa kufitini mwanafunzi
 

UBALOZI wa Tanzania nchini Urusi na baadhi ya maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini wametuhumiwa kufitini na kuchochea hadi kusitishwa udhamini wa serikali kwa mwanafunzi mmoja aliyekuwa akisoma Chuo cha Urafiki wa Kimataifa (Lumumba) Moscow.

Akizungumza na gazeti hili mwanzoni mwa wiki hii, mwanafunzi muathirika Bwana Athman Duday amedai anautuhumu Ubalozi na Wizara ya Mambo ya Nje kumfitini kwa sababu hadi sasa haijaelezwa ni kwa nini amerejeshwa nchini na kwamba amekuwa akiambiwa nenda huku na kule kuulizia suala hilo.

Akielezea mkasa anaodhani ni chimbuko la kuondolewa chuoni hapo; mwanafunzi huyo wa mwaka wa pili Kitivo cha Uhandisi alisema maafisa wa Ubalozi hasa aliyekuwa Mwambata wa Elimu (1997) walianza kumuandama baada ya yeye kuongoza wanafunzi wenzake kuhoji juu ya posho zao Ubalozini hapo.

Bw. Duday ameliambia gazeti hili kuwa mwezi Februari 1997 yeye akiwa Katibu wa Jumuiya ya wanafunzi wa Tanzania (TSU) na viongozi wengine wa jumuiya hiyo walikwenda Ubalozini kuulizia kuchelewa kwa posho za wanafunzi ambazo kikawaida zilipaswa kuwafikia Januari 16 (1997) badala ya tarehe 14 ya mwezi Februari waliyokuja kupokea.

"Tuliuliza kwanza huku nyumbani kama pesa hizo zilishatumwa, tukahakikishwa kuwa tayari ilikwishafanyika hivyo, tukashangaa ni kwa vipi Ubalozi haujatukabidhi posho hizo hadi tarehe ile", ameeleza Bw. Duday.

Hata hivyo, alisema walipofika Ubalozini aliyekuwa Balozi Bwana James Kateka aliwaeleza kuwa pesa hizo zimecheleweshwa na urasimu wa kibenki.

"Hatukuridhika na jibu hilo kwani tulifahamu utendaji wa benki za Urusi usingechukua muda mrefu kiasi kile", amedai mwanafunzi huyo ambaye pia alikuwa Katibu wa Vijana wa Kiislamu chuoni hapo.

Amesema tangu kutokea kadhia hiyo hapakuwa na mawasiliano mazuri baina yake na Balozi James Kateka ambaye amedai alidiriki hata kumfukuza ofisini kwake wakati akiwasilisha baadhi ya masuala Ubalozini.

Kuhusu Ubalozi kufanya njama dhidi yake, Bw. Duday amesema mwezi Machi (1997) alilazimika kuahirisha baadhi ya mitihani kwa sababu ya ugonjwa. Hata hivyo, amedai alikamilisha mitihani hiyo muda mfupi baadaye.

Amesema wakati akikamilisha mitihani hiyo zikatolewa taarifa kuwa amefukuzwa chuo kufuatia maendeleo duni ya kimasomo.

"Jumuiya yetu ilikanusha taarifa hizo kwa barua ya Mei 13, 1997", amedai mwanafunzi huyo.

Sehemu ya barua hiyo inasema: TSU - Russia baada ya uvumi wa kusikia kuhusu kufukuzwa kwa mwanafunzi huyo (Duday) ilifuatilia kwa makini pamoja na kuonana na Dean of the faculty of Engineering na kupata habari kuwa mwanafunzi huyo amemaliza mitihani yake vizuri na wanamtambua kama mwanafunzi. Na taarifa hizi TSU - Russia ilizitoa kwenye mkutano wa Moscow tarehe 27, Aprili mbele ya Mwambata wa Elimu.

Hata hivyo, imedaiwa kuwa Mwambata baada ya kupata habari hizo, Aprili 29, 1997 alimwandikia barua Rector wa chuo kumjulisha kuwa mwanafunzi huyo ameombewa hati ya PTA (Post Telegraphic Air Ticket) kurudishwa nyumbani.

"Barua hiyo ya Rector ilizua maswali mengi miongoni mwa wanafunzi chuoni", ameeleza Bw. Duday.

Amesema baadhi ya masuala yalihoji jinsi ubalozi ulivyoweza kuomba tiketi ya PTA kwa siri bila ya kuonana na mwanafunzi kwanza.

Tangu arejeshwe nchini Bw. Duday amekuwa akifuatilia suala baina ya Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Elimu ya Juu hata hivyo sehemu zote hizo amedai amekuwa akipokea maelezo ya juu juu au kuambiwa "njoo kesho" yapata mwaka sasa.

Gazeti hili lilipowasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje, msemaji wa Wizara hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Bw. Ilete alidai hana taarifa zozote na kwamba angewasiliana na ofisi husika kupata taarifa juu ya suala hilo.

ANNUUR itaendelea kulitafiti suala hili na taarifa za zaidi huenda zikachapishwa katika matoleo yajayo

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook