BAADA ya kuangalia maradhi ya kisaikolojia ya aina ya Paraphilia (ambayo husababishwa na kukithiri kwa zinaa katika jamii), nimeamua leo kugusia gonjwa jingine kubwa la kisaikolojia ambalo mara nyingi wanalipata watu wenye maradhi ya Multiparaphiliasis (yaani mchanganyiko wa maradhi mengi ya kisaikolojia aina ya Paraphilia. Ugonjwa huu unaitwa Islamophobia. (Hatujazimaliza Paraphilia, Insha-Allah tutazichambua nyingine katika matoleo yajayo)
Neno - Phobia ni kinyume cha neno Philia. Neno Philia lina maana ya hali ya kupenda kitu fulani kusiko kwa kawaida. Kwa mfano neno Aelurophilia ni hali ya mtu kupenda sana paka. Ndio maana katika matoleo yaliyopita tuliona Paraphilias, maradhi ya kupenda kufanya jambo fulani kinyume na maadili, kama vile kupenda kukodolea macho watu walio kuwa wazi (Voyeurism), au kupenda kuacha wazi sehemu nyeti za mwili (ExhIbitionism) n.k.
Kwa hiyo neno - Phobia lina maana ya kuogopa mno, au kutokupenda kitu au jambo fulani. Kwa mfano watu wenye Claustrophobia ni watu wenye kuwa na hofu wanapokuwa kwenye chumba kilichofungwa au sehemu (uchochoro) mwembamba. Photophobia pia ni tatizo la kisaikolojia la mtu kutokupenda mwanga. Yaani ni hali ambayo mtu akiwepo kwenye hali hiyo ya Pressure (presha) inampanda. Kwa hiyo basi, Islamophobia ni hali ya mtu kuuogopa Uislamu, na hivyo chochote kinachohusiana na Uislamu basi kinampa msisimko hasi, yaani msisimko usiopendeza, na anaingiwa na hofu na tafarani ya moyo.
Kuna wagonjwa wa aina mbili wa Islamophobia. Kundi la kwanza ni wale wanaopewa maelezo ya uongo kuhusu Uislamu na Waislamu. Hawa hupewa picha ya Waislamu kuwa ni watu wakatili, wauwaji, mara nyingi wanaume hunasibishwa na majambia, vilemba (hasa vyekundu) pamoja na madevu. Pia hutajiwa sheria kali za Kiislamu kama ile ya kumkata mwizi mkono, kumtandika bakora mlevi, na mzinifu kupigwa mawe hadi kufa. Kwa hiyo mtu huyu hukua na picha hii ya "ukatili" wa Uislamu. Kwa hiyo akimuona Muislamu basi anapata picha ya chinja chinja.
Kundi la pili ni lile ambalo lina maradhi ya kisaikolojia, hasa yale ya Ukozimeni (Voyeurism), wendauchi (Exhibitionism) n.k. Kwa vile Uislamu ni dini ambayo inapiga vita mambo ambayo wao wanayapenda, basi wanatokea kuuchukia Uislamu, na wanapokuwa katika mazingira ya Kiislamu yasiyo na zinaa, basi wanajisikia kama samaki aliyetolewa kwenye maji akawekwa nchi kavu. Hawa ndio hupambana kiasi wanachoweza kuhakikisha kwamba katika eneo walipo hakuna athari ya Uislamu.
Ndipo kwa mfano, mwalimu anamzuia binti wa Kiislamu kuingia darasani kwa vile amevaa gauni refu linalomstiri, na kwa vile amevaa ushungi unaoziba kifua chake, vitu ambavyo katika jamii ya wendawazi havitakiwi. Uniform nzuri kwake ni ile inayoacha miguu (ikiwezekana mapaja) na hata makwapa wazi. Cha kushangaza, baadhi ya walimu ni wanawake. Ukimuuliza anasema, "hatutaki udini". Yeye kuruhusu mabinti wavae kama dini yake inavyoruhusu, yaani visketi na viblauzi huo sio udini!
Kundi la tatu la wenye maradhi ya Islamophobia ni la mifumo ya kiutawala ya Kitwaghuti. Hawa wamaejaa dunia nzima. Husema kwamba serikali zao hazina dini, lakini utakuta Uislamu unapotangazwa kama unavyotakiwa uwe, wale watangazaji huitwa magaidi, wachochezi, wavunja amani, basi tafarani ndogo tu ya Msikitini itatulizwa na mabomu. Waislamu wa kweli wataitwa Siasa kali n.k. Uislamu wanaotaka wao ni ule wa siasa poa! Yaani wewe ujue lako, uwaache wenzio waendelee na yao, waendelee tu kuchafua mazingira ya jamii kwa ulevi, uzinzi, wizi, ujambazi, uafriti, dhulma n.k. Ukae kimyaa na tasbihi. Hapo utakuwa rafiki yao, na futari watakupikia.
Uislamu usiosafisha jamii na maovu ni mpya. Uislamu niujuao mimi ni ule unaotokana na maneno ya Muumba wa Ulimwengu:
"Hawawi sawa Waislamu wanaokaa tu bila ya dharura (ya kuwakalisha) (kuwa sawa) na wale wanaofanya juhudi katika njia ya Mwenyezi Mungu..." (4:95).
Tunatakiwa tuufuate Uislamu wetu bila ya kuogopa chuki ya yeyote mwenye Islamophobia, na wakitokea kupata uchungu kwa kuufuata kwetu Uislamu vilivyo, tunaambiwa tuwaeleze:
"Kufeni kwa uchungu wenu..." (3:119)
|
|