KATIKA uongozi wa nchi yoyote ile chombo kikubwa cha kujadili na kusikiliza matatizo ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi ni Bunge. Na ndio maana katika muda wa hivi sasa Bunge la Marekani lilikaa kwa muda mrefu na kujadili masuala ya kesi ya ngono, ya Rais wa nchi hiyo Bill Clinton.
Hii ina maana kuwa mahali ambapo masuala yote nyeti yahusuyo maendeleo, na mustakbali wa nchi yoyote ile ni Bunge.
Tunaona na kusikia masuala mengi nyeti yahusuyo nchi yanajadiliwa na kutolewa ufumbuzi Bungeni. Mfano suala la kesi ya ubakaji, kwa vile ni tatizo kubwa katika nchi limejadiliwa na matokeo yake ufumbuzi umepatikana sheria kali imewekwa kwa yeyote atakayejihusisha na jambo hilo.
Ili kuleta uhuru, umoja, ustawi na ushirikiano katika nchi ni lazima wananchi wote waangaliwe na kupewa haki sawa. Isiwe raia mmoja awe na haki mwingine awe raia wa daraja la pili.
Tatatizo la raia mmoja lionekane ni tatizo na tatizo la raia mwingine lisiwe tatizo. Ikiwa hivi raia mmoja atajiona yuko juu (superior) kuliko raia mwingine. Na raia mwingine akajiona yeye ni mnyonge akajenga chuki ndani ya nafsi yake kuwa anaonewa hilo si suala zuri katika ustawi wa nchi na inaleta ubaguzi na kudharauliana baina ya raia.
Katiba ya Tanzania inasema kila raia ana haki ya kuabudu anachokitaka ili mradi asivunje sheria ya nchi. Kipengele hiki cha Katiba kinatumika vibaya hata wale wenye dhamana ya kuilinda Katiba hiyo pia wanaitumia vibaya. Waislamu katika Tanzania hawana haki wala uhuru wa kuabudu, kwani wanapofanya mambo ambayo kwao ni ibada kama jambo hilo linapingana na imani za viongozi wa nchi (Wakristo) basi wataambiwa wana kashifu na matokeo yake ni Mwembechai.
Hivi karibuni, Mbunge wa Kigamboni Mheshimiwa Kitwana Kondo (KK) alisimama Bungeni na kuliambia Bunge kuwa upo upendeleo na ubaguzi wa wazi katika masuala mbalimbali kama vile elimu na masuala mengine ya ibada kama hijab na swala ya Ijumaa.
Matokeo yake kilichotokea kimenikumbusha usemi maarufu usemaowatu wenye akili/fikra pevu hujadili hoja zilizotolewa na watu, na watu wenye fikra finyu hujadili watu waliotoa hoja .
Kwani badala ya kujadiliwa hoja za KK alianza kujadiliwa KK mwenyewe, kwa kuambiwa ni mdini na mtu anayependelea dini yake badala ya kuipendelea nchi.
Mbali na hivyo, Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto (CCM) alisema bungeni sio mahali pa kuzungumzia masuala ya dini na hata baadhi ya wabunge hawana dini. Alishauri masuala hayo yamalizwe chini ya miti, makanisani na Misikitini.
Pia Waziri Mkuu Mh. Frederick Sumaye alisema masuala ya dini ni masuala nyeti na waheshimiwa wabunge wawe waangalifu kuyazungumza.
Sasa kama dini ni suala nyeti, na masuala nyeti ndio yanayojadiliwa bungeni, suala hili likajadiliwe wapi? Inabidi watueleze vizuri kwani kufumbia macho tofauti za kidini na uonevu wa wazi wa kidini, ndio kusababisha yanayotokea Bosnia, Chechnya, Kosovo n.k. na ndio yanayoiumiza vichwa vya wengi hivi sasa ulimwenguni.
Kama Mh. Sumaye anakubali kuwa ni masuala nyeti basi bungeni ndio mahali muafaka pa mambo hayo kuzungumziwa, na lisipoangaliwa inaweza kuleta mfarakano mkubwa sana katika jamii.
Miongoni mwa mambo ambayo KK amehoji ni kuhusu ruhusa ya Waislamu siku za Ijumaa kazi zisitishwe saa sita ili wapate kwenda kuswali, ikiwa jambo hili ni haki yao ya kikatiba.
Mwandishi Mayage S. Mayage akitoa wazo lake binafsi katika gazeti moja la kila wiki juu ya kichwa cha habari "KK matatizo ya Waislamu siyo kupumzika Ijumaa", alisema kitendo hicho ni kukiuka misingi ya dini na ni kufru mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani vitabu vyote vimeandika kwamba baada ya sala tawanyikeni mkatafute rizki.
Hajamuelewa KK, KK hajasema watu wasifanye kazi siku ya Ijumaa ila muda wa swala ya Ijumaa uchungwe, ili Waislamu wakafanye ibada yao hiyo kwa wasaa, kisha waendelee na kazi zao kama kawaida.
Vile vile wapo Maprofesa wa Chuo Kikuu, waliosema suala hili halihitaji mjadala kwani sheria ipo inayoruhusu watu saa 6 kwenda kuswali. Lakini ili kuthibitisha chuki zao za dini, wao wenyewe wanaendelea kufundisha mpaka saa 7 siku za Ijumaa. Vikao vya bodi vinaendelea mpaka saa saba, masomo mashuleni yanaendelea mpaka saa 7. Hivyo kumfanya mwanafunzi achague ima kuendelea na masomo akose swala au akawali akose masomo na hiyo ni kwa kila Ijumaa. Vile vile mfanyakazi (mwanabodi) aamue kukosa kikao akaswali au aache kuswali akahudhurie kikao. Hivyo ni wajibu kwa Mh. KK kulikumbusha Bunge na kuhoji masuala kama haya.
Halikadhalika japokuwa hijabu imeruhusiwa sehemu za kazi na mashuleni, lakini baadhi ya viongozi kwa chuki zao binafsi, wanazuia watoto wa shule kuvaa hijab, na wanaovaa hunyanyaswa, wakati hijab ni haki ya Muislamu mwanamke na mwanaume. Sasa vipi udini kwa KK kuzungumzia masuala haya, au wao kuzuia na kuwanyanyasa wafanyaji.
Hivi karibuni Rais Benjamin William Mkapa alifikishiwa madai ya Waislamu, katika Baraza la Idd el Fitr na kuahidi kuyashughulikia na kuyapatia ufumbuzi unaostahiki. Kabla ya siku kupita anatokea mtu kusema maswala hayo ni nyeti hayafai kuzungumzwa. Sasa tushike lipi la Rais au Waziri Mkuu, ukizingatia kuwa wote ni viongozi wa nchi.
Wakati sasa umefika, kuachana na porojo na kujadili hoja zinazotolewa na sio kumjadili anayetoa hoja, kwani hii ni tabia sugu ya viongozi wa Tanzania.
|
|