Ndugu Waislamu,
Assalaam alaykum warahmatullah wabarakatuh,
Tunapenda kuchukua fursa hii kushukuru kwa kupewa nafasi ya kutoa maoni yetu kwenye maadhimisho haya ya mauaji ya Mwembechai. Itakumbukwa kwamba Februari 12 na 13 mwaka 1998 jeshi la polisi lilivamia Msikiti wa Mwembechai na kukamata, kudhalilisha akinamama, kupiga watu risasi za moto mpaka kumpelekea Chuki Athumani kulazwa katika Hospitali ya Muhimbili hali ya kuwa na pingu bila ya kupata matibabu hali ambayo ilimpelekea kupooza na watu wengine kuuliwa kwa risasi hizo za moto.
Katika matukio hayo kulionekana uonevu dhahiri ukifanywa dhidi ya Waislamu. Uonevu wa dhahiri kutoka kwa askari polisi, matumizi ya risasi za moto zilizopigwa kwa dhamira ya kuua. Polisi hao wakipokea amri ya piga yule, ongeza, kukamatwa ovyo kwa viongozi wa Kiislamu, kunyanyaswa na kudhalilishwa kwa akinamama kwa kisingizio cha kutafuta mabomu katika sehemu zao za siri, ni baadhi tu ya mifano inayoonyesha dhulma iliyofanywa dhidi ya Waislamu. Isitoshe walio tenda matendo hayo ya kinyama walipewa pongezi kutoka kwa viongozi wa serikali na baadhi yao kupandishwa vyeo.
Baada ya hayo yote kufanyika, Waislamu walipata fursa ya kutoa malalamiko yao mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo Mh. Rais Mkapa aliyajibu kwa kutoa ahadi ya kuyashughulikia katika Baraza la Mawaziri. Kwa mantiki hiyo hivi sasa malalamiko ya Waislamu yamekwisha fika katika meza ya Ikulu, picha inayopatikana nikuwa ukurasa mpya umefunguliwa katika utatuzi wa matatizo ya Waislamu.
Hizi ahadi za Mh. Rais ni nzuri lakini kuna watu wenye roho mbaya ambao wanaona matatizo ya Waisalmu ni nyeti hawa wanamtia Rais fitna na kuwafananisha Waislamu sawa na wavaa magome, yaani wasubiri matatizo yao yatakapotatuliwa basi na ya Waislamu nao yatatuliwa. Hii siyo sahihi kwani Waislamu ndio ambao waliondoa dhulma ya mkoloni hapa Tanganyika, kwa maana hiyo viongozi kama hawa (wakina Waziri Mkuu Frederick Sumaye) wana roho mbaya hivyo Rais ni lazima uwaangalie sana kwani huenda wakapelekea kuvuruga amani hapa nchini kwetu.
DAMUSSA tunapenda kuikumbusha serikali Chuki Athumani amepata kilema cha kudumu mikononi mwao na hivi sasa anahitaji matibabu ya haraka kwa gharama za waliomlemaza.
Pili swala la wanafunzi Waislamu kutochaguliwa lichunguzwe na serikali na taarifa ya kitalaam itolewe.
(a) Ubora wa shule na vifaa pamoja na walimu katika maeneo yenye Waislamu wengi, utazamwe mfano shule kama Mlimani Primary, Upanga Primary, Muhimbili Primary, ukizingatia shule hizi ni bora zaidi na haya ni maeneo ambayo hawaishi Waislamu wengi, huwezi kulinganisha na shule kama za Tandika, Tabata, Magomeni n.k., hizi ni sehemu ambazo zina Waislamu wengi lakini utakuta shule hizo sio bora na walimu sio wakutosha.
(b) Uwezekano wa udanganyifu katika mitihani nao utazamwe.
(c) Upendeleo wa uchaguzi wa kuingia kidato cha kwanza.
Mwito kwa Waislamu wote uchaguzi ujao Waislamu wasiwachague wale wote wanaoonekana na nia mbaya katika dini yao.
•Wanaotaka kuihujumu ahadi ya Rais wakidai nyeti.
• Wanaoficha nyaraka za serikali mfano:
• Waraka wa hijabu kwa shule za msingi
• Kufunga masomo kwa muda wa saa sita mpaka saa nane mchana siku ya Ijumaa.
Mwisho ni wajibu wetu Waislamu kupigania dini ya Allah (s.w.) kwa hali na mali na kusimama kidete dhidi ya dhulma inayoelekezwa kwetu Waislamu. Tukumbuke kuwa Mtume (s.a.w.) anasema "Muislamu haumwi na ng’e katika shimo mara mbili".
WABILLAHI TAWFIQ
|
|