Barua
 

Je, ni kweli Mh. Rais wetu hajui matatizo au vilio vya Waislamu?

Ndugu Mhariri

KWANZA kabisa ningependa kuwapongeza Kamati, Masheikh na wote waliofanikiwa kufanyika kwa Baraza la Idd katika Msikiti wa Mtambani Kinondoni kwani uliendeshwa kwa amani ya hali ya juu mbali ya amani hiyo kutaka kutibuliwa na polisi lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema mambo yote yalikwenda kama yalivyopangwa.

Pili, ningependa pia kuwapongeza BAKWATA, viongozi mbalimbali wa dini, viongozi wa madhehebu mbalimbali waliofanikisha kufanyika kwa Baraza la Idd lililofanyika Diamond Jubilee.

Niliguswa sana na hotuba au risala iliyosomwa kwa Rais, kubwa zaidi ikiwa ni kilio cha Waislamu hususan uonevu tunaofanyiwa na serikali yetu. Cha kushangaza ni kauli ya Mh Rais kusema kwamba ndio kwanza anasikia malalamiko au kilio chetu sisi Waislamu. Je, hii inaingia akilini kweli?

Au ndio kusema kuwa Rais wetu yuko mbali na mtandao wa vyombo vya habari? Vilio vya Waislamu vilitawala sana vyombo vya habari kama magazeti na televisheni.

Na je ile piga yule ongeza tena yeye hakuiona? Basi kama ni kweli Rais wetu hana habari na vilio au ndio kwanza aliyasikia siku ile basi hii inaonyesha ni jinsi gani Rais wetu alivyokuwa mbali na jamii ya Kiislamu.

Ally Sadiki,
Mbezi Beach,
Dar es Salaam.



Mh. Sumaye tueleze wapi malalamiko ya Waislamu yapelekwe?

Ndugu Mhariri

WAZIRI Mkuu aeleze wapi Waislamu tukapate nusra? Kazi za Wabunge ni zipi? Kama hakuna hoja ya Wabunge kuwawakilisha wananchi basi wateue Wabunge wa kuitetea serikali bungeni. Huu ni udikteta.

Waislamu wanalalamika kwa sababu wanadhulumiwa haki zao. Yule na yeyote asiyelalamika naona anapewa haki yake ipasavyo ndio maana hata kwenye Baraza la Idd tulitoa baadhi tu ya matatizo.

Tunataka matatizo yetu wananchi wote wayaelewe maana Ikulu kuna kitulizo. Na matatizo ya Waislamu yasitatuliwe kwenye faragha.

S.R. Mghuna,
Dar es Salaam.


Vielelezo vya dhulma nchini

Ndugu Mhariri

NI HALI ya kusikitisha kuona zinafanywa jitihada za makusudi na wahusika kulidhoofisha kundi moja la wapiga kura na walipa kodi.

Baada ya kuua, kudhaElilisha mama zetu watukufu, kuwafunga watoto wadogo na vikongwe na kuwasababishia maradhi mbalimbali na wengine kupoteza maisha yao, sasa wanaendelea kuwashika viongozi wetu na kuwafungulia mashitaka bandia yasiyokuwa na ukweli wowote ila ni chuki zao tu.

Hawakutosheka piga yule! Mwongeze! Waliendelea kuwasaka Masheikh wetu na kuwatisha hata kuwavunja miguu na kuwatia mahabusu.

Hivi vyote ni vielelezo vinavyothibitisha dhulma inayofanywa na serikali kwa kisingizio cha kulinda amani. Lakini kwa sisi tunaodhulumiwa tunaona dalili za kuchoka kuishi kwa amani, upendo na mshikamano.

Abdul Rawf Bashiri,
Box 157,
Moshi - Hai.



Pongezi gazeti la ANNUUR

Ndugu Mhariri

KWA mara ya kwanza najitokeza katika gazeti lako kuungana na wenzangu ambao tayari ni wenyeji. Niweke katika safu ya wapenzi wa gazeti lako ambalo kwa sasa limejichukulia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi.

Kwanza habari zinazochapishwa humu zina uhakika 100% kutokana na kufanyiwa uchunguzi wa kina na inatokana na umahiri mkubwa wa waandishi wake, hongereni sana.

Nashangaa kuona gazeti hili lipo huru kwa wasomaji wa madhehebu yote kutoa maoni yao n.k. kinyume na magazeti mengine ambayo hayaandiki habari inayohusu Uislamu ila kwa uchochezi na kutia chuki kati ya Waislamu. Wenyewe wanajijua. Basi na waache kutuzulia.

Hashim Ismail NKY
P.O. Box 441,
Morogoro.


Muadhama Pengo anzia ngazi za juu

Ndugu Mhariri

UPO usemi mashuhuri unaosema "Ili tuendelee tunahitaji mambo manne, watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora". Watu wapo haina shaka, ardhi ipo ila maendeleo kwa Tanzania yanakwamishwa na vitu viwili kukosekana siasa safi na uongozi bora.

Tukianzia na siasa safi, siasa ya Tanzania ni ya kibaguzi, mkubwa kumbagua mdogo, mtu wa dini moja kumbagua wa dini nyingine japokuwa kinadharia inaonyesha kana kwamba ni ya ushirikiano na haki sawa kwa wote. Lakini kivitendo ni tofauti kwani ubaguzi umeenea toka ngazi za juu hadi chini.

Tukija katika uongozi bora, vile vile Watanzania tunakosa uongozi bora, uongozi uliopo na uliokuwepo toka mwanzo sio mzuri. Kwa kawaida sifa mojawapo ya uongozi bora ni uadilifu na kuwa na ujuzi (elimu) wa juu zaidi ili kuleta ufanisi katika kazi.

Hivi karibuni imeripotiwa kwenye gazeti moja Kadinali Polycarp Pengo akisema kuwa, mpaka mwaka 2000 atahakikisha wakuu wote wa mikoa wawe na shahada (digrii). Kauli ya "nitahakikisha" inamaanisha kuwa zipo mbinu na mikakati ya makusudi kabisa kuhakikisha ifikapo mwaka 2000 wakuu wote wa mikoa wawe na digrii.

Hii inaonyesha Kadinali Pengo ana nafasi kuwa katika serikali hii.

Inawezekana kabisa mkakati huo ukawa ni mzuri ili kuleta ufanisi katika kazi na maendeleo ya nchi hii, kwani viongozi ndio watendaji wakuu, hivyo wakiwa na elimu ya kutosha na muafaka wataweza kusababisha maendeleo ya kweli katika Tanzania.

Lakini tusije tukaharakisha kuwa na wakuu wa mikoa wenye digrii huku tukawa na Waziri Mkuu mwenye Diploma!

Ukhti Mwema,
Dar es Salaam.



Hongera Baraza la Idd Mtambani

Ndugu Mhariri

NATOA pongezi zangu kwa viongozi wetu walioandaa Baraza la Idd Mtambani na Waislamu wote waliohudhuria Baraza hilo. Mungu awe pamoja nao amin.

Tumeshuhudia Mtambani wakitoa sauti kwa niaba ya umma wa Kiislamu wa Tanzania na ulimwengu wa Kiisamu kutokana na matatizo wanayoyapata Waislamu wa nchi hii yanayofanywa na serikali ya Tanzania.

Je, Waislamu ambao mlihudhuria Baraza la Iddi kule Diamond Jubilee mna imani gani kumpa matatizo yenu Mh. Rais Mkapa kwani kuna tatizo kubwa kama la Mwembechai na yeye hajachukua uamuzi wowote.

Hata mliposoma risala yenu hakutoa hata pole kwa wafiwa au kuonyesha huzuni na masikitiko. Rais akiwa mpenda amani, haki na uadilifu alipaswa atuombe radhi Waislamu kutokana na vitendo vya mauaji yaliyofanywa na serikali yake, lakini hilo halikutokea.

Bibi Salum Fakhi Mjaka,
S.L.P. 80,
Kilwa Masoko.
 
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook